Sunday, October 11, 2020

Tamasha la Kimataifa Faribault, Minnesota

Jana, tarehe 10, nilishiriki tamasha la kimatafifa mjini Faribault, Minnesota. Tamasha hilo huandaliwa kila mwaka na Faribault Diversity Coalition. Miaka iliyopita, nilikuwa mjumbe wa bodi wa hiyo Coalition.

Tamasha hujumuisha maonesho ya tamaduni za watu wa mataifa mbali mbali waishio Faribault na maeneo ya jirani. Nimeshiriki tamasha hili Miata iliyopita, na daima inakuwa ni fursa nzuri ya kukutana na watu na kubadilishana uzoefu na mawazo kuhusu mambo mbali mbali ya dénia yetu ya utandawazi wa leo. Ninashiriki kama mwandishi na mtoa ushauri katika masuala ya taamaduni. Ninaonesha vitabu vyangu. Hii jana nilionesha pia vitabu via Bukola Oriola na mtoto wake wa miaka kumi na tatu Samuel Jacobs.

Saturday, October 3, 2020

Sunday, August 16, 2020

Tundu Lissu, Serikali ya CCM, na Ushoga

Kwa kuzingatia kuwa kuna upotoshaji mwingi kuhusu msimamo wa Tundu Lissu juu ya ushoga, napenda kusema kuwa msimamo wake unafanana na msimamo wa serikali ya CCM kuhusu ushoga.

Katika mahojiano kwenye kipindi cha "Hard Talk," yaliyotumia lugha ya kiIngereza, ambacho waTanzania wengi hawakijui, Tundu Lissu aliulizwa msimamo atakaochukua kuhusu ushoga endapo atakuwa na mamlaka. Alijibu kuwa hatajishughulisha na kupekua nini kinaendelea vyumbani mwa watu. Alimaanisha ataheshimu haki ya "privacy." Ikumbukwe kuwa haki hiyo imo katika katiba ya Tanzania pia.

Kwa upande wa serikali, baada ya kushambuliwa sana kutoka ndani na nje ya nchi kufuatia kauli za Makonda, wizara ya mambo ya nje ilitoa ufafanuzi kwamba kauli za Makonda si msimamo wa serikali ya Tanzania.

Wizara ilisema kuwa Tanzania inaheshimu mikataba yote ya kimataifa iliyosaini juu ya haki za binadamu. Tamko hilo lilitosha kuzimisha mashambulizi. Nami nilitamka na bado ninatamka kuwa serikali ilifanya busara kutoa hilo tamko la jumla, bila kuingia katika "details." Niko tayari kuelezea kwa nini ninasema kuwa serikali ilifanya busara kutoa hilo tamko la jumla.

Jambo la msingi ni je, hiyo mikataba ya kimataifa juu ya haki za binadamu ni ipi? Ni wazi kuwa muhimu zaidi ya yote na msingi wa yote ni tangazo la kimataifa la haki za binadamu. Haki ipi inayohusika hapa? Ni ile ile aliyoitaja Tundu Lissu, yaani haki ya "privacy."

Msimamo wa Tundu Lissu kuhusu ushoga unafanana na msimamo wa serikali ya CCM. 

Wednesday, August 12, 2020

Duka Jipya la Vitabu Vyangu

Vitabu vyangu viwili, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na Matengo Folktales sasa vinapatikana katika duka la taasisi iitwayo Planting People Growing Justice.

Mwanzilishi na mwendeshaji wa taasisi hiyo, Dr. Artika Tyner, ni profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha St. Thomas hapa Minnesota. Aliniuliza iwapo nitaridhia vitabu vyangu kuuzwa na taasisi hiyo.

Alianza kukifahamu kitabu changu mwaka juzi, baada ya kununua nakala kadhaa kwa ajili ya watu aliowapeleka Ghana katika safari ya kielimu akishirikiana na Monica Habia,  mwanazuoni mwenzake kutoka Ghana. Baada ya safari hiyo, Monica alinielezea jinsi kitabu kilivyowasaidia waMarekani kuyaelewa mambo waliyokutana nayo Ghana.

Unaweza kutembelea tovuti ya Planting People Growing Justice. Vitabu hivi viwili vinapatikana Tanzania, katika maduka ya Soma Book Cafe na A Novel Idea.

Thursday, July 23, 2020

Kitabu Muhimu kwa Wageni Marekani

Tarehe 11 mwezi huu, nilipata ujumbe kutoka kwa jamaa aishiye eneo la kati la jimbo hili la Minnesota. Anasema kuwa wana jumuia yao ambayo inawakaribisha na kuwasaidia wahamiaji na wakimbizi kimaisha. 

Anasema kuwa wanatumia kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na wanakiona ni bora sana kwa malengo yao. Kauli kama hizi si ngeni kwangu. Nimezisikia tangu mwaka 2005 nilipochapisha kitabu. Sehemu ya ujumbe ni hii hapa:

I  have been involved with a local organization in St. Joe that works to help refugees and immigrants adjust to and succeed in central Minnesota. Our group is called Cultural Bridges. 

I have been sharing your book, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, with members of our group. Everyone who has read it has really enjoyed it and we see it as an excellent resource as we work to fulfill our mission as an organization.

Friday, July 17, 2020

Yatokanayo na Picha ya Msomaji Nami

Picha hii ilipigwa tarehe 27 Julai, 2019, Soma Book Cafe, Dar es Salaam. Wadau wa vitabu, yaani waandishi, wachapishaji, wauzaji, na wasomaji wa vitabu, tulikusanyika kuongelea masuala yanayotuunganisha.

Huyu ninayeonekana naye pichani ni Chiombola Joseph ambaye nilimfahamu siku hiyo. Nilikuwa nimetoa mhadhara kuhusu "Writing About Americans," naye akawa mmoja wa wale walionunua vitabu vyangu vilivyokuwa vikiuzwa na Soma Book Cafe. Napenda kusema neno juu ya hilo na mengine yatokanayo.

Uamuzi wa kununua kitabu si wa kawaida na si rahisi katika jamii yetu waTanzania. Huyu ndugu alinunua viwili. Sikumbuki wanauzaje, lakini lazima nusu laki au zaidi ilimtoka. Zingatia kuwa vitabu vyangu si udaku na haviko katika orodha ya vitabu vinavyofundshwa mashuleni na vyuoni nchini. Anayeamua kununua vitabu vyangu Tanzania ninamwona kama mtu wa pekee. Najiuliza, ni nini kinachomtuma kufanya hivyo? Bila shaka ni hamu tu ya kutaka kujua mambo. Mimi mwenyewe niko hivyo. Sichoki kununua na kusoma vitabu.

Kwa upande wangu kama mwandishi, na ili kuwajuza wasomaji wangu, napenda niseme kwamba kitu kimojawapo kilichonisukuma kuandika hivi vitabu viwili ni kule kutoridhika kwangu na vitabu vya wengine nilivyovisoma.

Nilikuwa ninafundisha "Oral Literature" (fasihi simulizi) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1976. Mwaka hadi mwaka, sikuona kitabu cha nadharia kilichoniridhisha kwa kufundishia somo hilo.

Jawabu likawa kwamba kulalamika kuhusu hali hakutoshi. Ni lazima kutafuta suluhu. Nikaamua kuanza kuandaa kitabu ambacho kingeniridhisha. Baada ya miaka 23 nilichapisha kitabu cha "Matengo Folktales." Hadi sasa ninaridhika nacho, na waalimu wengine wanakitumia kufundishia, kama vile hapa Marekani na Uingereza.

Habari ni hiyo hiyo kuhusu kitabu cha "Africans and Americans: Embracing Cultural Differences." Tangu kuja kwangu kufundisha hapa Marekani, mwaka 1991, nilihusika kama mshauri katika programu za ushirikiano baina ya vyuo vya Marekani na nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania.

Nilikuwa mtoa ushauri katika masuala ya tofauti za tamaduni, ili kuwaandaa wanafunzi kabla hawajaenda Afrika, na pia baada ya wao kurejea tena Marekani, kujibu masuali yao kuhusu yale waliyoyashuhudia Afrika.

Niliona mapema kuwa hapakuwa na kitabu cha kuniridhisha kuhusu masuala hayo. Suluhisho likawa kuandaa kitabu changu, kazi iliyonichukua muda mrefu, hasa mwaka 2005 ambapo nilizama katika kazi hiyo tu kwa miezi yapata mitano. Ninaridhika na kitabu hiki, na maelfu hapa Marekani wamekisoma na wengi wanakisoma.

Hata hivi, ninaandika kitabu kingine juu ya mada hii ya tofauti za tamaduni, ili kufafanua zaidi mawilii matatu niliyoongelea au kugusia, na pia kuleta mapya.

Kwa hiyo, utaona kwamba kwa kiasi fulani, vitabu ninaandika kujiridhisha mimi mwenyewe, ingawa nina lengo la kuelimisha wengine pia. Ni kazi ngumu inayohitaji ustahimilivu mkubwa. Kama unawazia hela, utaona kuwa ni kazi isiyolipa. Ukitaka hela, achana na wazo la kitabu, uende Mererani ukatafute mawe ya tanzanite.

Mtu anayenunua kitabu changu namwona kama ameanzisha uhusiano fulani nami. Anaingia katika nafsi yangu na kujionea, angalau kwa kiasi fulani. Uhusiano huo ni wa kudumu, kwani si rahisi mtu kusahau kila alichosoma kitabuni, hasa pale anapokutana na jina la mwandishi au taarifa yoyote juu yake.

Thursday, July 16, 2020

Sasa Nimesoma "The Comedy of Errors" (Shakespeare)

Jana nilimaliza kusoma "The Comedy of Errors," tamthilia mojawapo ya Shakespeare, ambaye alliandika tamthilia 37, na labda zaidi kidogo. Katika ulimwengu wa fasihi, Shakespeare ni kinara. Wanafasihi wanaweza kuhoji kwa nini ninatumia neno fasihi kuziongelea tamthilia. Malumbano huenda yasiishe.

"The Comedy of Errors" ni tamthilia inayoelezea matatizo na mikanganyiko itokanayo na uwepo wa watu kadhaa katika jamii ambao wanafanana maumbile na sura kiasi kwamba ukikutana na mmoja, halafu baadaye ukakutane na mwingine, hutajua hata kidogo kuwa ni mwingine. Tamthilia hii inaonyesha migogoro, kutoelewana, na magomvi kwa sababu hiyo.

Kusoma maandishi ya Shakespeare kunahitaji mwendo wa taratibu. KiIngereza chake ni cha zamani, miaka mia tano iliyopita, na utamaduni ni vile vile. Ni chemsha bongo kwa sisi watu wa leo, sawa na kusoma tungo za zamani za kiSwahili kama vile "Al Inkishafi" au "Utenzi wa Rasi 'lGhuli." Kwa mtazamo wangu, chemsha bongo hii ina manufaa kwa afya ya akili, sawa na mazoezi ya mwili yalivyo na manufaa kwa afya zetu.

Shakespeare ni mwandishi wa waandishi. Alitambuliwa na anaendelea kutambuliwa hivyo na waandishi wakuu duniani. Shaaban Robert, mwandishi wetu maarufu kuliko wote, alisema kuwa akili ya Shakespeare ni kama bahari kubwa sana, ambayo mawimbi yake yalitua kwenye fukwe zote za dunia.

Saturday, July 4, 2020

Tunasoma Fasihi ya Afrika

Baada ya muhula wa masomo kwisha hapa chuoni St. Olaf, mwezi Mei, sasa ninafundisha kozi maalum ya fasihi ya Afrika. Kwa miaka, nimefundisha kozi hiyo. Ni fursa kwa watu kuufahamu mchango wa waAfrika katika kutafakari masuala ya maisha ya binadamu (kwa maana ya kifalsafa ya "the human experience" na "the human condition") kwa njia ya fasihi.

Ninapofundisha fasihi ya Afrika, ninaanza kwa kuielezea Afrika kama chimbuko la binadamu, tekinolojia, lugha, fasihi, falsafa, na yengine yite ambayo binadamu anahusika nayo.

Safari hii ninafundisha Changes: A Love Story, Maru, Season of Migration to the North, na Woman of the Ashes.

Nimesoma baadhi ya vitabu vya waandishi wote wanne na caribou vyote nilivyovisoma nilivbsoma katika kufundisha. Naweza kusema ninafahamu zaidi kazi za Ama Ata Aidoo na Mia Couto.

Hata hivyo, vitabu hivi ninavyofundisha sikuwahi kuvisoma. Kila mara ninapofundisha kozi hii, au nyingine yoyote ya fasihi, nina jadi hiyo ya kufundisha angalau baadhi ya vitabu ambavyo sijasoma kabla. Ninajua kuwa kuna waandishi wengi maarufu tangu karne zilizopita na wengine wanaendelea kujitokeza. Kwa hiyo, nami ninataka kujiongezea upeo muda wote.

Tuesday, May 19, 2020

Utalii wa Utamaduni Wilayani Kwetu

Kwa miaka na miaka nimekuwa nikiongelea masuala ya utamaduni na utandawazi pia utamaduni na utalii au utili wa utamaduni.  Nimewahi kuhusisha vitabu na utalii. Nimesema kuwa watalii wengi kutoka huku ughaibuni, kama vile Marekani, hupenda kusoma vitabu, na sisi tutahitaji kuwa na maduka ya vitabu.

Napenda kujielekeza wilayani kwetu: wilaya ya Mbinga, lakini Nyasa pia. Tunatakiwa kuandika vitabu kuhusu historia, utamaduni, na mambo mengine ya kwetu. Watalii wakija, wakute maduka ya vitabu, vitabu kuhusu historia ya miji kama Mbambabay, Liuli, Lituhi, Mbinga, Kigonsera na kadhalika pia taasisi kama hospitali ya Litembo. Wakute vitabu kuhusu vivutio kama jiwe la Mbuji.

Tuwe na hifadhi ya vitu mbali mbali vya kitamaduni, kama vile mitumbwi, nyavu za kuvulia samaki, ala za muziki, kama vile ngoma, "ngwaja," "sekatela," "mapenenga," na "nkwendakwenda." Katika jumba la hifadhi, ziwepo video za ngoma, na masimulizi ya hadithi. Ziwepo picha za vivutio na watu mbali mbali wakiwa katika shughuli kama kulima, uvuvi, kusuka vikapu, kufinyanga vyungu,  na kadhalika.

Watalii watafurahi kuangalia ngoma na vivutio, lakini wakipata vitabu, watajielimisha kuhusu waliyoyaona. Vitabu vinawezesha elimu endelevu. Kwa njia ya vitabu hivi, tutauelimisha ulimwengu. Vijana wetu nao wataelimika kwa kusoma vitabu hivi.  
Friday, May 1, 2020

Mhadhara Wangu wa Kwanza Kwa Zoom

Tarehe 28 mwezi huu, nilitoa mhadhara kwa wanachuo wa chuoni St. Olaf na wasikilizaji walikuwa Mankato. Mada ilikuwa Understanding Each Other: Brothers and Sisters From Two Continents.

Nimeshahutubia wanachuo wa South Central College mara kadhaa, na ninafurahi kuwa wanaendelea kuwa na hamu ya kunisikiliza, kama inavyoelezwa hapa. Kivutio kimojawapo ni kitabu changu

Hii tarehe 28 ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuhutubia kwa kutumia Zoom. Changamoto ya kuhutubia bila kuiona hadhira kiuhalisia haikosi kuathiri mhadhara. Lakini ripoti nilizopata kutoka kwa mratibu wa mhadhara ni kwamba watt waliufurahia mhadhara wangu, ambao ni huu hapa.

Sunday, April 19, 2020

Ninaupenda Ualimu

Ndoto yangu tangu ujana wangu ilikuwa ni kuwa mwalimu. Nilihitimu chuo kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1976, nikateuliwa kuanza kufundisha pale, katika idara ya "Literature." Ndoto yangu ikawa imetimia. Ninaipenda kazi yangu na ninawapenda wanafunzi wangu. 
Tangu mwaka 1991, ninafundisha katika idara ya kiIngereza hapa katika chuo cha St. Olaf, jimbo la Minnesota. Naleta picha kutoka miaka michache iliyopita nikiwa na wanafunzi wangu wa somo la kuandika kiIngereza. Hili ni moja kati ya masomo ninayofundisha.
Inapendeza kuwasaidia wanafunzi kujifunza matumizi ya lugha rasmi kwa nidhamu na usahihi kabisa. Lugha ina mitego na changamoto nyingi. Tuchukulie mfano wa mwanafunzi wa kubuniwa ambaye jina lake ni Mark. Tuchukulie kuwa Mark ameandika, "The reason why I spoke that way was because I was not feeling well." 
Hapa Marekani, jamii ambayo kiIngereza ni lugha mama yao, watu wengi huandika kwa kiwango hicho, na wengi hawafikii kiwango hicho, kwani hutumia maneno, misemo, na miundo isiyo rasmi, ambayo wameizoea tangu utotoni, tofauti au kinyume na itakiwavyo katika lugha rasmi.
Kwa kuwa lengo langu ni kufundisha matumizi ya lugha rasmi iliyo bora kabisa, namshinikiza na kumwelekeza mwanafunzi Mark kurekebisha sentensi yake. Namwambia kuwa ametumia maneno mengi mno na asirudie neno au dhana katika sentensi. Anajikuna kichwa, anajitahidi, na hatimaye anaandika hivi: "The reason I spoke that way was that I was not feeling well" 
Hiyo sentensi ni afadhali kuliko ilivyoandikwa mwanzo, kwa sababu angalau ameondoa neno "why" na neno "because," ambayo ni marudio ya "the reason." Lakini, ingawa rekebisho lake limeboresha sentensi, haijafikia kiwango cha juu kabisa cha ubora. Kwa hiyo ninaendelea kumshinikiza Mark atafakari zaidi. Labda, hatimaye anaandika hivi: "I spoke that way because I was not feeling well"
Hiyo ni bora zaidi, lakini si mwisho wa safari. Ninaendelea kumshinikiza Mark hadi aandike: "I spoke that way because I was unwell." Hapo niko tayari kumwachia, ingawa naweza kumshauri pia kuwa hilo neno "unwell" linaweza kutafutiwa neno tofauti na sentensi ikawa na ladha zaidi. Lakini hili badiliko si muhimu.
Ninajisikia raha sana kumfikisha mwanafunzi kwenye hatua hiyo, na ninajisikia raha kumwona mwanafunzi mwenyewe anavyofurahi kutokana na kutambua makosa na mitego aliyopitia. Hiyo furaha ninayopata haielezeki. Ndio siri ya mimi kuupenda ualimu namna hiyo. Sitaacha ualimu kamwe, labda nitakapokuwa sina tena uwezo wa kufundisha.

Sunday, March 8, 2020

Vitabu Nilivyonunua Leo

Ni muda mrefu umepita, nami sijaandika kuhusu vitabu nilivyonunua kama nilivyokuwa naandika miezi iliyopita. Leo nimeona nifanye hivyo.

Nilienda Apple Valley kukutana na mkurugenzi wa African Travel Seminars ambaye tunafanya shughuli za kutangaza utalii Afrika. Baada ya kikao, nilienda katika duka la Half Price Books, ambalo nimelitembelea mara nyingi. Kama kawaida, nilikwenda kwanza kuona vitabu vya Hemingway. Nilichagua Paris Without End: The True Story of Hemingwahy's First Wife na Ernest Hemingway: Artifacts From a Life.

Nilichagua Paris Without End kwa sababu nilitaka kujua zaidi juu ya Hadley Richardson, mke wa kwanza wa Hemingway. Nimesoma habari zake hapa na pale, lakini si kwa undani. Ninafahamu jinsi anavyoelezwa na Hemingway katika riwaya ya A Moveable Feast. Vile vile niliguswa sana na barua alizoandika Hemingway kwa mke wake huyo pale alipokuwa ameanzisha uhusiano na mwanamke mwingine, Pauline. Hemingway anaelezea namna alivyosongwa na mawazo kuhusu tatizo hilo. Kwa hivyo, ninataka kufahamu undani wa maisha ya mama huyu.

Nilichagua Ernest Hemingway: Artifacts from a Life kwa kuwa nilishaona baadhi ya vitu vya Hemingway katika ziara yangu nyumbani alikozaliwa, katika kitongoji cha Oak Park, karibu na Chicago. Nilishaona vitu vingine vya Hemingway katika maktaba ya J.F. Kennedy mjini Boston. Kitabu hiki kitaniwezesha kufahamu mengi zaidi, kwani kina picha na maelezo.

Baada ya hapo, nilienda sehemu ambapo huwekwa vitabu vya bei rahisi zaidi. Nilichagua Anna Karenina, riwaya ya Leo Tolstoy, kwa sababu sijisikii vizuri kwamba sijasoma riwaya za mwandishi huyu maarufu wa uRusi. Ninatamani hapa nilipo ningekuwa nimesoma War and Peace na Anna Karenina. Nimechukua hatua kuelekea kwenye lengo hilo.

Monday, February 24, 2020

Sherehe ya African Travel Seminars

Juzi tarehe 22, Ilifanyika sherehe mjini Minneapolis ya kutimiza miaka 24 ya kampuni ya African Travel Seminars. Niliwahi kuandika taarifa katika blogu hii. Waalikwa walikuwa watu waliowahi kusafiri na kampuni hii ya utalii ambayo hupeleka watu kwenye nchi kama vile Ghana, Senegal, Gambia, Morocco, Misri, Ethiopia, Kenya, Tanzania, Afrika Kusini, Cuba na na Brazil. Walialikwa pia marafiki wa kampuni.  Nilipata fursa ya kusema machache, nikaongelea utalii kama nyenzo ya elimu na ujenzi wa mahusiano baina ya mataifa na tamaduni.

Mmiliki na mkurugenzi wa African Travel Seminars, Georgina Lorencz, aliniagiza nipeleke nakala za kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho siku za karibuni ameanza kukipendekeza kwa wadau naowapeleka Afrika. Nilipeleka pia nakala za Matengo Folktales kuwa kuwa nilijua kuwa katika hotuba yangu ningetaja umuhimu wa kuelewa misingi ya utamaduni na falsafa ya wahenga wetu wa Afrika.


Kulikuwa pia na vyakula vha kiAfrika. Baadhi ya mambo yaliyofanyika katika sherehe ni zoezi la kujibu maswali mbali mbali kuhusu Afrika. Watu walivutiwa na zoezi hili lililokuwa ni chemsha bongo. Baadhi ya masuali ninayoyakumbuka ni haya: kiSwahili ni lugha ya taifa ya chi zipi? Nchi ipi imetoa washindi wengi zaidi wa tuzoya Nobel? Mama yupi pekee duniani amewahi kuwa "First Lady" wa nchi mbili?Washindi walipewa zawadi, zikiwemo nakala za kutabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Georgina alikuwa ameagiza kuwa kilt mtu agenda akita ameba vazi la kiAfrika. Nami nilijiandaa kwa kununua shati siku mbili kabla ya tukio, kwa sababu mashati yangu mengine nimeshayavaa mara kwa mara miaka iliyopita.
Palifanyika mashindano ya mavazi kwa lengo la kumtambua mtu aliyetia fora kwa vazi la kiume na hivyo hivyo kwa vazi la kike. Nilipata fursa ya kuongea na watu kadhaa, nikajionea wnavyipenda kampuni ya African Travel Seminars.


Niliona pia watu walivyovutiwa na yale niliyosema, kwa jinsi walivyochangamkia vitabu vyangu na kuvinunua. Mwishoni mwa sherehe, Georgina alitabgaza mipango ya safari zijazo mwaka huu mwezi Septemba na mwakani kwenda Afrika Kusini na Brazil.

Friday, January 17, 2020

Mwaliko wa African Travel Seminars

Nimepata mwaliko kutoka African Travel Seminars wa kushiriki shughuli itakayofanyika tarehe 22 Februari. Mada siku hiyo itakuwa "Celebrating Black Culture Through Travel." Kutakuwa na chakula, maonesho na michezo mbali mbali kuhusu Afrika.

Nimealikwa kuongelea kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho African Travel Seminars hutumia kwa watalii wanaoenda Afrika.

African Travel Seminars inaelimisha na kujenga mahusiano baina ya watu kupitia utalii. Hivi karibuni, tumeamua kushirikiana. Malengo ya kampuni hiyo yanafanana kwa namna fulani na ya kampuni yangu ndogo ninayojaribu kuikuza iitwayo Africonexion: Cultural Consultants.

Monday, January 6, 2020

Kitabu Kimeingia Kwenye Maktaba ya Peace Corps

Kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kimeingia kwenye maktaba ya Peace Corps iliyoko Washington DC. Mkurugenzi ameniandikia, na sehemu ya ujumbe ni hii:

We will add it to the Peace Corps library where our staff and visitors can enjoy it.

I look forward to reading more of it as I find the topic to be very relevant and important to our work. I have already begun reading it, and it has reminded me of my own experiences in Togo, West Africa. As I was reading, I was struck by the section on eye contact. I really love the verses you included from the poem by Sufi poet Ibn ‘Arabi about the veiled woman and eye contact, and I got a good chuckle at your stories of misunderstandings—as I, as well surely all of us, have had many such experiences and misunderstandings.

Kauli za mkurugenzi za kukumbuka aliyoona Afrika na kufananisha na yaliyomo kitabuni, zinafanana na kauli za waMarekani wengine waliosoma kitabu hiki baada ya kuishi Afrika. Afrika kwenyewe, kwa sasa, kitabu kinapatikana Tanzania na Kenya. Tanzania kinapatikana kutoka duka la Soma Book Cafe, lililoko Dar es Salaam, na pia duka liitwalo A Novel Idea, lililoko Dar es Salaam na Arusha. Kenya kinapatikana katika duka la Bookstop katika Yaya Center Mall, Nairobi.