Tuesday, May 19, 2020

Utalii wa Utamaduni Wilayani Kwetu

Kwa miaka na miaka nimekuwa nikiongelea masuala ya utamaduni na utandawazi pia utamaduni na utalii au utili wa utamaduni.  Nimewahi kuhusisha vitabu na utalii. Nimesema kuwa watalii wengi kutoka huku ughaibuni, kama vile Marekani, hupenda kusoma vitabu, na sisi tutahitaji kuwa na maduka ya vitabu.

Napenda kujielekeza wilayani kwetu: wilaya ya Mbinga, lakini Nyasa pia. Tunatakiwa kuandika vitabu kuhusu historia, utamaduni, na mambo mengine ya kwetu. Watalii wakija, wakute maduka ya vitabu, vitabu kuhusu historia ya miji kama Mbambabay, Liuli, Lituhi, Mbinga, Kigonsera na kadhalika pia taasisi kama hospitali ya Litembo. Wakute vitabu kuhusu vivutio kama jiwe la Mbuji.

Tuwe na hifadhi ya vitu mbali mbali vya kitamaduni, kama vile mitumbwi, nyavu za kuvulia samaki, ala za muziki, kama vile ngoma, "ngwaja," "sekatela," "mapenenga," na "nkwendakwenda." Katika jumba la hifadhi, ziwepo video za ngoma, na masimulizi ya hadithi. Ziwepo picha za vivutio na watu mbali mbali wakiwa katika shughuli kama kulima, uvuvi, kusuka vikapu, kufinyanga vyungu,  na kadhalika.

Watalii watafurahi kuangalia ngoma na vivutio, lakini wakipata vitabu, watajielimisha kuhusu waliyoyaona. Vitabu vinawezesha elimu endelevu. Kwa njia ya vitabu hivi, tutauelimisha ulimwengu. Vijana wetu nao wataelimika kwa kusoma vitabu hivi.  




No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...