Friday, August 31, 2012

Kumbukumbu ya Johannesburg: Mwanamuziki Moeketsi

Nilikuwa Johannesburg, Juni 14 hadi 18 mwaka huu, kama nilivyoandika hapa.

Tarehe 17 nilikuwa katika ziara ya sehemu kadhaa za mji wa Johanneburg. Sehemu moja tuliyotembelea inaitwa Newton, na hapo ndipo nilipopiga picha inayoonekana hapa. Nimekaa pembeni ya sanamu ya Kippie Moeketsi, mpiga saksofoni maarufu, aliyezaliwa mwaka 1925 na kufariki mwaka 1983.

Mwenyeji wetu aliyekuwa anatuongoza katika ziara hii alisema kuwa Kippie aliamua kubaki nchini Afrika Kusini pamoja na matatizo yote ya utawala wa makaburu.

Leo nimeangalia taarifa za mwanamuziki huyu mtandaoni, nikagundua kuwa huenda nilishasikia na kupendezwa sana na muziki wake. Hebu msikilize:


Thursday, August 30, 2012

Uzinduzi wa Mzunguko wa Tano wa Mashindano ya Uandishi





 Mwenyekiti wa Bodi ya Mradi wa Vitabu vya Watoto Tanzania (CBP), Abdullah Saiwaad (kushoto), akimkabidhi Mkama Mwijarubi, hundi ya dola za kimarekani 2000 Dar es Salaam jana, baada ya kitabu chake alichoandika cha Kiss Kiddo: The birthday party kuchaguliwa kuwa moja ya kitabu bora ambacho kitaingia katika mzunguko wa nne wa mashindano ya uandishi wa riwaya za kiingereza kwa ajili ya vijana. Katikati ni Katibu Mtendaji wa Mradi huo Pilli Dumea.
Katibu Mtendaji wa Mradi wa Vitabu vya Watoto Tanzania (CBP), Pilli Dumea (katikati), akiwaonesha waandishi wa habari Dar es Salaam jana, moja ya vitabu vilivyo ingizwa katika muhutasari wa vitabu bora vilivyoandikwa kwa lugha ya kiingereza chini ya mradi huo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya (CBP), Abdullah Saiwaad na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Tuzo ya Burt Adam Shaffi.
--
Na Mwandishi Wetu
Tuzo ya Burt ya Fasihi ya Kiafrika ni Mradi ulioanzishwa na Shirika la Kimataifa la Elimu, CODE kwa ufadhili wa Bwana Bill Burts ambaye ni Mkanada.
Madhumuni makubwa ya Mradi huu ni kuwezesha upatikanaji wa vitabu vya kujisomea vitakavyowasaidia wanafunzi walioko katika shule za msingi kujifunza Kiingereza ili kujiandaa kwa elimu ya sekondari ambayo inatolewa kwa Kiingereza.
Aidha vitabu hivyo vinalenga katika kuhamasisha usomaji miongoni kwa vijana, pamoja na kukuza uchapishaji na fasihi ya Kiafrika. Zaidi ya hayo, Mradi unalenga katika kutambua waandishi bora wa Afrika na vitabu bora kutoka Afrika.
Hadi  sasa Mradi umeweza kuchapisha vitabu aina 9 ambavyo ni:
1.      Tree land: The Land of Laughter
2.      The Best is Yet to Come
3.       A Hero’s Magic
4.      Face Under the Sea
5.      Living in the Shade
6.      In the Belly of Dar es Salaam
7.      Close Calls
8.      Lesssilie the City Maasai
9.      The Choice
Miswada bora ya mzunguko wa nne ni:
1.      Run Free - Richard Mabala
2.      Tears From Lonely Heart - Israeli Yohana
3.      Kiss Kiddo: The birthday party - Mkama Mwijarubi.
Hivi sasa miswada hiyo inachapishwa na wachapishaji waliowasilisha miswada hii ambao ni: E& D Vision Publishing, Mkuki na Nyota na Aidan Publishing
Mashindano ya mzunguko wa tano yataanza leo tarehe 29 Agosti, 2012 hadi Machi, 30, 2013, ambapo wachapishaji watatakiwa kuwasilisha miswada yao katika ofisi za Mradi.
Mafaniko ya Tuzo ya Burt ya Fasihi  ya Kiafrika
1.      Tuzo ya Burt imeweza kuchapisha aina tisa (9) za vitabu ambazo ni sawa na nakala 30,000. Vitabu hivi vimesambazwa katika shule 146 zilizoko katika Programu ya Usomaji, maktaba za jamii, na nakala 300 maktaba zilizoko mikoani.
2.      Vitabu hivyo vimeongeza uwepo wa vitabu vya kujisomea shuleni katika lugha ya Kiingereza.
3.      Baadhi ya wachapishaji wameweza kuuza vitabu vyao katika nchi jirani za Afrika Mashariki.
4.      Tuzo hii imewezesha kutambua waandishi mahiri wa lugha ya Kiingereza.
5.      Tuzo hii inaunga mkono Mkukuta kwa kutoa mafunzo kwa wadau na kutoa zawadi nono kwa washindi.
6.      Kwa kupitia Tuzo hii waandishi wa Kitanzania wamehamasika kuandika miswada ambayo inahaririwa  na kuchapishwa kwa ubora wa hali ya juu.
7.      Warsha za waandishi zimewawezesha kujifunza mbinu za uandishi wa riwaya kwa Kiingereza.
8.      Serikali imeweza kuutambua Mradi na kumshukuru mfadhili wa Mradi, jambo linaonyesha heshima kwa mfadhili huyo.
9.        Aina 3 za vitabu chini ya Mradi vimeteuliwa kutumika kama vitabu vya fasihi ya kiingereza kwa madarasa ya kidato cha 3-4 na 5-6 kuanzia Julai 2012. Vitabu hivyo ni Face Under the Sea, The Best is Yet to Come na Tree Land the Land of Laughter.
Changamoto
-          Wachapishaji wengi wa vitabu wako katika miji mikubwa na hasa Dar es Salaam. Mikoani kuna wachapishaji wachache sana. Hali hii inawafanya waandishi chipukizi kutoka mikoani kushindwa kushiriki katika mashindano.
-          Waandishi wengi hawana mafunzo ya kutosha na mbinu mbali mbali za uandishi kuwawezesha kuandika miswada iliyo bora.
-          Tuzo hii inapata ugumu wa kuwafikia waandishi wengi zaidi hasa walio pembezoni mwa nchi.

Wito unatolewa kwa wachapishaji walioko mikoani kutafuta waandishi chipukizi na kuwasaidia ili waweze kushiriki.

CHANZO: Blogu ya Hakingowi  

Wednesday, August 29, 2012

Rais Mkapa na Vitabu

Nimeiona picha hii kwenye blogu ya Michuzi. Inamwonyesha karani wa sensa akiwa na rais mstaafu Benjamin Mkapa. Wako katika shughuli ya sensa.

Kitu kilichonifanya niandike ujumbe huu ni vitabu vinavyoonekana hapo pichani. Daima nimekuwa nikijiuliza je, mawaziri, wabunge, wakurugenzi, na wengine wote ambao tunawaita viongozi, wana vitabu majumbani mwao, na je, wanavisoma?

Ni faraja na heshima kuwa na viongozi wanaosoma vitabu. Ingekuwa jambo jema iwapo watu wanapogombea ubunge au nafasi nyingine ya uongozi, tungewauliza kama wana vitabu, kama wanasoma vitabu, na kwa muda huu wanapogombea wanasoma vitabu vipi. Hapo tungeweza kuwabaini watu makini na mavuvuzela pia.

Lakini tatizo ni kuwa utamaduni wa kusoma vitabu haupo Tanzania. Kwa hivyo, mavuvuzela nao wanaingia katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wakiwa na uhakika kuwa hakuna atakayewauliza kuhusu masuala ya vitabu.

Saturday, August 25, 2012

Mwanaanga Neil Armstrong Amefariki

Mwanaanga Neil Armstrong alikuwa binadamu wa kwanza kutua na kutembea mwezini, Julai 20, 1969. Dunia nzima ilisisimka kutokana na tukio hilo. Wakati ule nilikuwa shuleni, kidato cha tatu.

Tulifuatilia kwa makini habari nzima za shirika la NASA hadi kufikia hatua ile ya kihistoria. Hayo nayakumbuka vizuri sana. Nakumbuka pia kuwa sheikh moja wa Tanzania alitoa tamko kuwa haiwezekani binadamu kwenda mwezini, kwani Quran haiafiki.

Kwetu sisi, Neil Armstrong alikuwa shujaa, pamoja na wenzake Edwin Aldrin na Michael Collins waliosafiri naye kwenye chombo chao, Apollo 11. Nakumbuka kuwa katika Tanzania, kuna watu waliviita vyombo vyao vya usafiri, kama vile magari, Apolo 11.

Neil Armstrong amefariki, akiwa na umri wa miaka 82. Mungu amweke mahali pema Peponi. Amina.

Thursday, August 23, 2012

"The Satanic Verses:" Kitabu Kigumu Kukielewa



The Satanic Verses, kitabu cha Salman Rushdie,  ni kitabu ambacho nimekiona kigumu kukielewa. Nilinunua nakala miaka mingi kidogo iliyopita, nikaanza kusoma, lakini sikufika mbali.

Mtindo aliotumia Rushdie katika kuandika kitabu hiki unahitaji msomaji awe amesoma sana vitabu vingine. Inatakiwa msomaji awe anajua mambo mengi, kuanzia yale ya falsafa hadi ya hadithi na dini. Vinginevyo, ni rahisi kutoka kapa unapojaribu kusoma The Satanic Verses.

Mwandishi maarufu Nadine Gordimer wa Afrika Kusini, ambaye alipata tuzo ya Nobel mwaka 1991, amegusia suala hili alipoandika kwamba "anyone who actually has read, and been sufficiently literate fully to understand, this highly complex, brilliant novel knows that dominant among its luxuriant themes is that of displacement." Hayo ameyaandika katika insha yake, "Censorship--the Final Solution, the Case of Salman Rushdie," Telling Times, Writing and Living, 1954-2008, uk. 448.

Mimi ni profesa wa masomo ya ki-Ingereza na fasihi yake. Ninasoma na kufundisha maandishi ya waandishi mbali mbali. Hata maandishi mengine ya Rushdie nimesoma, bila tatizo. Lakini, pamoja na uzoefu na ujuzi wangu, kitabu cha The Satanic Verses kimekuwa changamoto kubwa kwangu, kwa jinsi Rushdie anavyoimudu lugha ya ki-Ingereza, na kuiingiza katika ubunifu, mbwembwe, na madoido mbali mbali kama mchawi mahiri wa lugha. Kwa kiasi fulani, nakifananisha kitabu chake hiki na maandishi ya Derek Walcott, mwandishi kutoka St. Lucia, sehemu za Caribbean, ambaye alipata tuzo ya Nobel mwaka 1992. Huyu naye amejikita sana katika historia ya maandishi na anatawala uwanja mkubwa wa waandishi kuanzia wa kale hadi wa leo. Kwa hivi, kuyaelewa maandishi yake, kunahitaji mtu uwe umesoma sana.

The Satanic Verses ni kama mtihani. Sitakubali kushindwa, ingawa ni mtihani mgumu. Pole pole nitafanikiwa kuelewa, kwa namna yangu, alichoandika Rushdie. Msomaji makini yeyote ana uwezo wa kuelewa andiko, kwa namna yake. Ndivyo nadharia ya fasihi inavyofundisha.

Utamaduni wa Kusoma Vitabu

Picha hii nimeiona kwenye mtandao wa VOA NEWS. Ilipigwa ufukweni Ziwa Nyasa, upande wa Malawi.

Nimevutiwa na huyu mtalii anayejisomea kitabu. Ninafahamu manufaa ya kusoma vitabu; navisoma kila siku. Nafahamu faida ya kuwa na vitabu, kwani ninavyo zaidi ya 3000.

Kama ninavyoandika mara kwa mara katika blogu hii na sehemu zingine, utamaduni wa kusoma vitabu uko sana miongoni mwa wa-Marekani. Ni kawaida kwa wa-Marekani kuwanunulia wenzao vitabu kama zawadi, kwa mfano kwenye nyakati muhimu kama Krismasi.

Wa-Marekani wanapokwenda nchi yoyote kama watalii, ni kawaida kwao kutafuta vitabu kuhusu nchi ile, wavisome kabla ya kusafiri, wakishafika kwenye nchi ile, au wakisharudi kwao. Ndio maana watalii hao hupenda sehemu zenye maduka ya vitabu.

Wa-Tanzania wangekuwa makini wangetambua na kuitumia fursa hiyo, kama nilivyoelezea katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Lakini lazima nikubali kuwa kuweka mawazo na mawaidha katika kitabu haiisaidii jamii ambayo haina utamaduni wa kusoma vitabu.

Tuesday, August 21, 2012

Kufungiwa kwa Gazeti la MwanaHalisi


Watetezi wa haki za binadamu, asasi za kijamii na wadau wakuu wa habari nchini, leo wameipa serikali siku saba kufungulia gazeti la MwanaHALISI, vinginevyo wataitisha maandamano ya kupinga hatua ya serikali kufungia gazeti hilo kwa muda usiojulikana, kuminya uhuru wa habari, haki za binadamu na utesaji wa wanaharakati. 

Tamko la asasi hizo ni kama ifuatavyo hapa chini:

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 22 Agosti 2012
YAH: KUFUNGIWA KWA GAZETI LA MWANAHALISI
 
KWA mara nyingine tena, tumewaiteni hapa kuwaomba mtufikishie ujumbe wetu huu kwa watawala. Ujumbe wenyewe unahusu kufungiwa kwa gazeti la kila wiki la MwanaHALISI na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda aliyoitoa bungeni, Alhamisi tarehe 16 Agosti 2012. Kama mnakumbuka vema, wakati akijibu swali bungeni siku hiyo, Waziri Mkuu Pinda alisema, “Serikali imechukua wajibu wake kulifungia gazeti hilo, na kwamba kama wahusika hawakuridhika na hatua iliyochukuliwa na serikali wana haki ya kukata rufaa kwa mamlaka za juu.”
 
Awali ya yote, tuseme wazi, kuwa hatukuridhika na majibu ya Waziri Mkuu kuhusu kufungiwa kwa MwanaHALISI. Majibu ya Waziri mkuu Pinda yamelenga kuahirisha tatizo, siyo kutatua. Kwanza, Waziri Mkuu anatetea uamuzi huo uliofanywa na sheria katili na kandamizi ya magazeti. Sheria inayonyang’anya uhuru wa kufikiri, uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa kuwasiliana.  Pili, Mheshimiwa Pinda anatumia sheria hiyo kutaka kuliangamiza gazeti hili ambalo limesifiwa kwenye ripoti mbalimbali za ndani na nje ya nchi ikiwamo ile iliyotolewa majuzi na Baraza la Habari Tanzania (MCT) inayochambua Mwenendo wa vyombo vya Habari nchini kwa mwaka 2011 inayosema katika ukurasa wa tisa:
 
 “Pamoja na kusakamwa na serikali, MwanaHALISI limesimamia uandishi wake wa kuikosoa serikali.”
 
Serikali imelituhumu gazeti hili kwa kuchapisha habari ambazo inasema “zinakiuka” vifungu 32(1) (a), (c) – (d); 32(1)(c) na 36(1) vya Sheria ya Magazeti Na. 3 ya 1976. Habari hiyo inahusu kutekwa, kuteswa kinyama na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande kwa kiongozi wa madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka. Hii ndiyo habari ambayo serikali inaita ya “uchochezi.” Yaani badala ya serikali inayojigamba ina mkono mrefu wa kumfikia yeyote kuutumia mkono huo kutafuta watuhumiwa waliotajwa na gazeti kuwa walifanikisha kutekwa kwa Dk. Ulimboka, imeamua kutumia mabavu kulifungia MwanaHALISI huku wakiacha maisha ya Dk. Ulimboka na wanaharakati wengine njia panda.
 
Serikali imechukua hatua hiyo, huku wakijua kuwa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Mabadiliko ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (2005), ilipanua haki ya kutoa, kutafuta, kupokea, na kusambaza habari. Mabadiliko hayo yaliondoa kivizo cha “kwa mujibu wa sheria” Kila mtu- anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi; anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake.
 
Aidha, mabadiliko hayo yanatoa haki kwa kila raia ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio muhimu mbalimbali kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.  Hivyo basi haki na uhuru wa kujieleza, kupokea na kutoa habari haina vipingamizi ambavyo serikali inadai kuwamo katika Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976.
 
Vilevile, kuwekwa kwa Vipengele vya Haki za Msingi na Wajibu wa Mwanadamu (Bill of Rights) katika Katiba ya nchi yetu kulibadilisha sheria zote ambazo zinakiuka haki za binadamu. Vifungu vyote tulivyovitaja hapo juu viliguswa moja kwa moja na Vipengele vya Haki za Msingi na Wajibu wa Mwanadamu. Ibara ya 14 ya Katiba inalinda haki ya kuishi na inaitaka jamii kutoa hifadhi ya maisha kwa kila mtu. Kana kwamba hiyo haitoshi, Ibara ya 26(1) na (2) zinataka kila mtu na serikali kutii Katiba ya nchi na vilevile kuchukua hatua za kuheshimiwa haki na sheria za nchi.
 
Waziri mkuu anayajua haya vizuri. Anafahamu kuwa sheria iliyotumiwa kufungia gazeti, ni sheria katili na imepitwa na wakati. Kuitumia sheria hii kunaendeleza dhana ya kuwa serikali hii inatumia udhaifu wa Katiba na baadhi ya sheria kukandamiza Haki za Binadamu na Uhuru wa Habari! Mambo haya hayakubaliki.
 
Kutokana na hali hiyo, sisi watetezi wa haki za binadamu na asasi nyingine za kiraia:
1.      Tunarejea wito wetu wa kuitaka serikali kulifungulia mara moja na bila masharti, gazeti hili ambalo limekuwa kipenzi cha wananchi. Tunaitaka serikali ndani ya siku saba (7) kutekeleza hilo kwa kuangalia maslahi mapana ya jamii badala ya kuangalia maslahi ya baadhi ya viongozi wenye maslahi fulani katika kutimiza malengo yao binafsi.
 
Serikali itekeleze takwa hili haraka iwezekanavyo, na kwamba asasi za kijamii hazikubaliani na kauli ya Waziri Mkuu ya kutaka wahusika waende kwenye vyombo vya juu kwa sababu tatu zifuatazo:
 
Kwanza, sheria ya magazeti hairuhusu ukataji wa rufaa kwa waziri wa Habari ambaye ndiye aliyetuhumu na kuhukumu gazeti bila kutoa nafasi kwa wahusika kusikilizwa. Pili, Waziri Mkuu Pinda pamoja na sheria hiyo kutomtaja, hakueleza kuwa yuko tayari kupokea malalamiko ya MwanaHALISI. Hivyo kutoelekeza kwake tunakuchukulia kama njia ya kukwepa wajibu wake.
 
Tatu, hatukubaliani na kauli ya Waziri Mkuu na wengine wanaoitaka MwanaHALISI waende mahakamani kutafuta haki yao kwa kuwa serikali yenyewe haikutumia njia ya mahakama kufungia gazeti. Serikali inataka kuitumia mahakama ili kuchelewesha MwanaHALISI kupata haki yake. Nyote mnajua jinsi mahakama zetu zinavyokabiliwa na gonjwa kubwa la ucheleweshaji wa kesi.
 
2.      Serikali, baadala ya kushughulika na watetezi wa haki na wanahabari wanaofichua uovu, ishughulike na wahalifu waliomteka, kumtesa na hatimaye kumtelekeza Dk. Ulimboka. Ushahidi uliobainishwa na gazeti hili haukuacha shaka yeyote juu ya waliohusika na sakata hili, na kama serikali au watendaji wake waliotajwa (na waliohusishwa) wana mashaka wangetumia ushahidi na taarifa zile kutafuta haki zao: kwanini wasiende mahakamani au wajitokeze na ushahidi wa kukanusha yaliyobainishwa?
 
3.      Serikali iachane kabisa na ukandamizaji huu wa haki na uhuru wa habari. Matendo aliyofanyiwa Ulimboka, habari zilizobainishwa na MwanaHALISI juu ya sakata hili na kufungiwa kwa gazeti hili kunaonesha mtiririko wa matukio ya serikali kuminya uhuru na haki.
 
Ikumbukwe pia kuwa, Kesi Na. 34/2009 iliyofunguliwa tangu 2009 kupinga sheria ya magazeti ya mwaka 1976 iliyotumika kuwafungia MwanaHALISI haijasikilizwa mpaka sasa. Hii inaenda sambamba na serikali kufumbia macho mahitaji ya sheria ya uhuru wa habari na kudharau mapendekezo ya muswada wa habari tangu 2007 bila kupeleka Bungeni.
 
Kwa hoja hizo, sisi watetezi wa haki za binadamu, asasi za kijamii na wadau wakuu wa habari nchini, tunaendelea kusisitiza kuwa serikali itimize wajibu wake kwa kulifungulia mara moja gazeti hili na kufanyia kazi yaliyobainishwa. Kama ikishindwa kufanya hivyo, tutaitisha maandamano ya kupinga hatua ya serikali kufungia gazeti hili, kuminya uhuru wa habari, haki za binadamu na uteswaji wa wanaharakati na watetezi wa haki na kwamba tukifika hapo tunawaomba waandishi wa habari mtuunge mkono kwa yafuatayo.
 
i.        Msichapishe habari yoyote inayomhusu Waziri wa Habari, Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, na pia Mkurugenzi wa Maelezo. Tunawasihi wahariri wasiwatume waandishi katika Ukumbi wa Habari Maelezo kwa ajili ya kuchukua habari kama ilivyo kawaida na badala yake Watanzania wote wahakikishiwe kupata habari kwa njia nyingine mbadala.
ii.           Tunawasihi wadau wote wanaoweza kutuunga mkono mara tutakapohitaji msaada wao ikiwa ni pamoja na kushiriki kwenye maandamano na kupata mawakili ambao watasaidia katika uendeshaji wa shauri letu mahakamani.
iii.        Tunawasihi wanaharakati wote wasichoke wala wasirudi nyuma katika azma hii ya kutetea haki, uhuru na ulinzi kwa haki na watetezi wake. 
 
Marcossy Albanie
Mwenyekiti wa Kamati

mwisho


  
 
Ndimara Tegambwage
Information and Media Consultant
P.O. Box 71775, Dar es Salaam
Tel: 255 (0)713614872
e-mail: ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

Ziarani Israel

Mwishoni mwa Desemba, mwaka 1992, nilikwenda Israel kuhudhuria mkutano wa Israeli Folklore Society, ambao ulifanyika mjini Nazareth. Tulihudhuria watafiti kutoka nchi mbali mbali. Tulipata pia fursa ya kutembelea sehemu mbali mbali, kama vile Jericho, Jerusalem na Bethlehem.

Hapa pichani naonekana nikiwa Jerusalem. Ilikuwa tarehe 29 Desemba. Huyu mzee aliye kushoto alikuwa akijaribu kuniuzia hilo vazi nililovishwa kichwani. Wachuuzi wa Jerusalem ni mahiri sana, wenye ushawishi mkubwa. Kwa ushawishi wao, na ucheshi, mtu unaweza kujikuta unanunua bidhaa ambazo hukutegemea.

Kususia Sensa ni Kujihujumu

Sensa ni muhimu kwa nchi yoyote kwa maana kwamba ni sherti serikali ijue idadi ya watu wake na mahali wanapoishi.

Takwimu na taarifa hizo ndio msingi wa upangaji wa mipango yoyote ya huduma na maendeleo. Kwa akili yangu finyu, huu ni ukweli usiopingika.

Kama kuna sehemu ambapo watu hawajahesabiwa, sehemu hiyo itaonekana iko wazi; haina watu. Kwa maana hiyo, hakutakuwa na msingi wowote wa kuiingiza sehemu hiyo katika mpango wa huduma au maendeleo.

Sehemu itakayoonekana haina watu itawekwa kando katika mipango hiyo ya huduma na maendeleo. Sasa basi, endapo kulikuwa na watu sehemu hiyo, ambao walisusia sensa, wasije wakajitokeza baadaye na kulalamika kuwa wanaonewa.

Saturday, August 18, 2012

Salamu za Idd Mubarak

Kwa siku hii tukufu ya Idd Mubarak, napenda kutoa salam kwa ndugu zetu wa-Islam waliotimiza majukumu ya Mwezi Mtukufu hadi kumaliza vizuri. Naamini kuwa baraka za Muumba zitokanazo na ibada hizi zinatuneemesha sote.

Pia naomba Muumba atusaidie kujenga mshikamano na undugu miongoni mwetu wanadamu wote, kwani hili ni fundisho la msingi la dini zetu. Fundisho hili nimeliona katika picha hii ninayoibandika hapa, ambayo nimeikuta Facebook.

Friday, August 17, 2012

Leo Ninatimiza Miaka 61

Leo ninatimiza miaka 61 ya maisha yangu. Pamoja na kumshukuru Mungu kwa kuniweka hai hadi leo, ni lazima nijiulize: nimetumiaje fursa hii aliyonijalia Mungu ya kuwepo duniani miaka yote hiyo?

Mungu ametuweka hapa duniani kwa sababu gani? Maisha yetu yana faida gani kwa wanadamu wenzetu? Tuna malengo gani yenye manufaa kwa wanadamu wengine siku hadi siku, mwezi hadi mwezi, mwaka hadi mwaka?

Miaka hii ninamwazia na kumsoma sana Ernest Hemingway. Alifariki akiwa na umri unaofanana na huu niliofikia leo. Tangu akiwa kijana, na miaka yote ya maisha yake, alitoa mchango mkubwa kwa walimwengu kwa uandishi wake. Alipokuwa na miaka 53, alitunukiwa tuzo ya Nobel katika fasihi. Je, nikijifananisha na watu kama Hemingway, mimi nimeshafanya nini?

Masuali haya ni magumu. Siku ya leo, pamoja na kumshukuru Mungu, pamoja na kujiuliza kuhusu wajibu wangu hapa duniani, nawajibika kuwakumbuka wenzetu wengi ambao hawakupata fursa ya kuishi miaka niliyoishi. Wengi wamefariki wakiwa wachanga, wengine vijana. Kwa nini Mungu kaniweka hadi leo? Hilo liwe suali la kujiuliza muda wote, liwe mwongozo wa maisha yangu yaliyobaki.




Wednesday, August 15, 2012

Matukio Afrifest 2012

Kama ilivyo katika matamasha mbali mbali ninayohudhuria, katika tamasha la Afrifest lililofanyika siku chache zilizopita, kulikuwa na matukio mengi ya kukumbukwa, na nilipata bahati ya kukutana na watu wengi. Napenda kuongelea tukio moja.

Alikuja kwenye meza yangu mama mmoja. Katika maongezi nilitambua kuwa ni m-Marekani mweusi. Tuliongelea kuhusu shughuli zangu za ufundishaji, na pia alipenda kujua mada za vitabu vyangu, nami nikamwelezea. Alichukua vitabu vifuatavyo: Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, Africans in the World, na Matengo Folktales. Kisha, alipoona kitabu cha ki-Swahili, CHANGAMOTO: Insha za Jamii, alikichukua.

Nilishangaa kidogo kuona anachukua kitabu cha ki-Swahili, wakati haijui lugha hiyo. Aliniambia kuwa mume wake ni m-Somali kutoka Kenya, ambaye anajua ki-Swahili. Akaendelea kunieleza kuwa anamnunulia hicho kitabu. Kisha akaniomba nikisaini, nami nilifanya hivyo, nikaandika na salaam kwa ki-Swahili.

Niliwahi kuandika katika blogu hii kuwa hapa Marekani nimeona tabia aliyoonyesha huyu mama. Watu wanafurahi kuwanunulia wenzao vitabu. Watu wanaona kitabu ni zawadi bora. Nilijiuliza iwapo kwetu Tanzania unaweza kumpa mtu kitabu kama zawadi ya Krismasi au Iddi el Fitri. Soma hapa.

Kwenye matamasha kama haya ya Afrifest, huwa nachukua nakala mbili tatu za kitabu hiki cha ki-Swahili, kwani sitegemei kama atapatikana mtu atakayevihitaji. Lakini, mambo hutokea, kama nilivyoeleza hapa juu.

Monday, August 13, 2012

Afrifest Twin Cities 2012

Kwa mara nyingine tena, tamasha la Afrifest limefanyika hapa Minnesota. Tamasha hili hufanyika mara moja kwa mwaka, na huu ni mwaka wa sita. Kulikuwa na shughuli mbali mbali, kuanzia tarehe 10, hadi 12. Hapa naleta picha chache za shughuli ya jana, yaani tarehe 12.

Kama kawaida, wauza bidhaa mbali mbali walikuwepo. Hili banda lilikuwa na kaseti za hotuba za wanamapinduzi mbali mbali waliojihusisha na harakati za wa-Marekani Weusi. Kulikuwa pia na t-shirts na vitu vingine, vyenye picha za watu maarufu kama Marcus Garvey, Bob Marley, na Malcolm X. Hapa nilinunua t-shirt yenye picha ya Bob Marley.
Hao jamaa, wenye asili ya Jamaica, walikuwa wanauza chakula.
Tamasha la Afrifest ni fursa ya wafanya biashara kuleta bidhaa au huduma zao. Hapa kushoto kabisa ni banda la benki ya Wells Fargo. Tamasha kama hili kwa vile ni fursa ya kuwapata wateja wapya.
Hapa ni wachezaji wa soka wakiingia.
Shughuli za Afrifest ni kwa ajili ya watu wa kila rika. Watoto nao hushiriki.
Hapo ni uwanjani, timu za soka zilipokuwa zinachuana.

Hapa ni meza ya vitabu na machapisho yangu mengine. Nilishinda hapo nikiongea na wadau. Kama kawaida, nilipata fursa ya kufahamiana na watu ambao sikufahamiana naoHiyo hapa ni meza ya vitabu na machapisho yangu mengine. Nilishinda hapo nikiongea na wadau. Kama kawaida, nilipata fursa ya kufahamiana na watu ambao sikufahamiana nao.







Hapa naonekana na mdau.

Hao jamaa ndio walikuwa wanaburudisha umati kwa muziki, siku nzima. Wako hapa na mitambo yao.

Friday, August 10, 2012

Maprofesa Wanakipenda Kitabu Hiki

Siku chache zilizopita, nimeona makala ya Elizabeth M. Cannon na Carmen Heider ambao ni maprofesa wa Chuo Kikuu cha Wisconsin-Oshkosh. Wameelezea jinsi kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kilivyowasaidia katika ufundishaji wa wanafunzi waliowaleta Tanzania kimasomo. Makala yenyewe ni "A Study Abroad Program in Tanzania: The Evolution of Social Justice Action Work," Humboldt Journal of Social Relations, 34 (2012), 61-84

Maprofesa hao waliwaleta wanafunzi Tanzania mwaka 2008, 2010 na 2012. Pamoja na mambo mengine, wameelezea matatizo waliyoyapata katika kuwahamasisha wanafunzi kwenye vipengele kadhaa vya masomo yao. Hatimaye walitafuta njia ya kukitumia kitabu cha Africans and Americans katika mijadala darasani, kwa kuwapangia wanafunzi sehemu za kusoma ili waongoze majadiliano darasani. Mkakati huu ulileta mafanikio mazuri, kama wanavyoeleza hapa:

We also thought carefully about how to design our on-site class sessions to reflect our commitment to active, student-centered learning and provide general guidance to our students. We decided to focus these classes on Mbele's Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, on of our readings from 2008, because this Tanzanian author challenges stereotypes through the presentation of his cultural experiences. Before we left the United States, we divided students into four groups and assigned each a section of this text on which they would lead one of four on-site class sessions. On-site discussions focused on comparisons between Mbele's views on Tanzanian life and students' interactions with the people they met and the places they visited. Frustration was replaced with excited conversations. These classes shifted from tense obligations where learning was stifled to an exciting component of the trip where insights flourished. (uk. 68)

Sina la kuongeza. Namshukuru Mungu kwa kunijalia fursa na uwezo wa kukiandika kitabu hiki kwa namna nilivyokiandika, hadi kimekuwa msaada kwa walimu, wanafunzi, na jamii kwa ujumla. Mungu bado ameniweka hai. Wajibu wangu ni kuendelea kujielimisha kwa bidii na kuandika.

Thursday, August 9, 2012

Tamasha la "Afrifest 2012" Minnesota

Wikiendi hii kutafanyika tamasha jingine la Afrifest hapa Minnesota. Tamasha hili hufanyika kila mwaka, na huu ni mwaka wa tano. Lengo ni kuwakutanisha wa-Afrika, watu wenye asili ya ki-Afrika, na wengine wote, kwa ajili ya kujionea na kuelimishana kuhusu mambo mengi ambayo watu weusi wamefanya katika historia, katika nyanja mbali mbali. Ni fursa ya kusherehekea mafanikio yao katika fani mbali mbali, na pia kubadilishana mawazo kuhusu changamoto zilizopo, kwa lengo la kujipanga kwa mshikamano na maendeleo siku za usoni.

Nafurahi kuwa nimekuwa mshirika katika shughuli za Afrifest tangu mwanzo, kama mwanabodi wa Afrifest na sasa mwenyekiti wa bodi. Kesho, tarehe 10 jioni, tutafanya ufunguzi wa tamasha. Nitaongea machache kuhusu Afrifest na kisha watu watapata fursa ya kujumuika na kufahamiana.

Keshokutwa, Jumamosi, na hadi Jumapili, tutakuwa na maonesho ya aina aina. Nami nitakuwa na meza yangu, nikiwa na vitabu na machapisho mengine. Kwenye shughuli hizi napata fursa ya kuongea na watu wengi kuhusu shughuli zangu katika utafiti, ufundishaji, mipango ya kuwapeleka wanafunzi Afrika. Ni fursa ya pekee kuongea na watu kuhusu ninayoandika katika nyanja za fasihi na tamaduni za wa-Afrika na Wamarekani, kama inavyodhihirika katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Afrifest imeshakuwa tukio muhimu hapa Minnesota, na kadiri miaka inavyopita, watu wengi zaidi na zaidi wanahamasika kuhudhuria au kushiriki kwa namna moja au nyingine. Kuna vivutio vingi, kama vile muziki, michezo, maonesho ya mitindo, kumbukumbu za historia, na burudani mbali mbali kwa watu wazima na watoto. Kwa taarifa zaidi, soma hapa.

Thursday, August 2, 2012

Kwenye Baa Hakuna Udini

Katika wiki sita zilizopita, nimepata fursa ya kuichunguza nchi yangu kwa karibu. Kitu kimoja kilichonigusa, ingawa sio kigeni, ni kwamba kwenye baa hakuna udini. Niliamua niandike makala hii kuhusu jambo hilo, kwani naona linasisimua.

Nimezunguka Dar es Salaam, Tanga, Arusha na Songea, na kwa vile baada ya shughuli zangu za mchana napenda jioni kuvinjari baa, nimejikuta nikijumuika na wa-Islam na wa-Kristu katika baa kwenye miji hiyo. Kilichobadili hali hiyo ni ujio wa Mwezi Mtukufu.

Lakini kabla ya hapo wa-Islam na wa-Kristu tulikuwa tunajumuika vizuri kabisa huko baa. Hatubaguani bali tunakaribishana. Tunaongea; tunapiga soga; tunajenga mahusiano mema. Kwenye baa moja Tanga, nilipata fursa ya kuongea na meneja, ambaye ni mu-Islam. Mada yetu ilikuwa ulabu.

Nilianza mimi, kwa kusema kuwa katika dini yetu, hatukatazwi kunywa pombe. Tunakatazwa kulewa. Meneja naye akaionyesha kidole bia yangu na kuniambia kuwa kwa mu-Islam, ile bia yangu ni haram. Muislam haruhusiwi kuinywa hata kidogo.

Tuliongelea mitazamo ya dini zetu kwa ustaarabu na kuheshimiana hadi mwisho. Tulielimishana. Maongezi yale yalitufanya tuelewane na kufahamiana. Kwenye baa hakuna udini.

Kinachoshangaza ni kuwa katika nchi hii hii kwenye nyumba za ibada hatujumuiki watu wa dini mbali mbali. Tunatengana kabisa. Ni ajabu. Lakini je, Mungu amewakataza wa-Islam wasihudhurie ibada za wa-Kristu? Je, Mungu ametukataza wa-Kristu tusihudhurie ibada za wa-Islam?

Sio hilo tu. Kuna nyumba za ibada nchini mwetu ambako wahubiri wanaeneza udini na wanakazana kukashifu dini za wengine. Je, Muumba anayakubali hayo? Inakuwaje kwenye baa kuwe ndiko sehemu tunakoheshimiana watu wa dini mbali mbali, wakati kwenye hizo nyumba za ibada mafundisho ni ya kujenga chuki na uhasama? Inakuwaje kwamba kwenye baa ndiko kuna busara kuliko kwenye hizo nyumba za ibada? Ni ajabu kweli kwamba ni bora mtu aende baa, kuliko kwenye hizi nyumba za ibada. Tulifikaje hapo?

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...