Wednesday, August 29, 2012

Rais Mkapa na Vitabu

Nimeiona picha hii kwenye blogu ya Michuzi. Inamwonyesha karani wa sensa akiwa na rais mstaafu Benjamin Mkapa. Wako katika shughuli ya sensa.

Kitu kilichonifanya niandike ujumbe huu ni vitabu vinavyoonekana hapo pichani. Daima nimekuwa nikijiuliza je, mawaziri, wabunge, wakurugenzi, na wengine wote ambao tunawaita viongozi, wana vitabu majumbani mwao, na je, wanavisoma?

Ni faraja na heshima kuwa na viongozi wanaosoma vitabu. Ingekuwa jambo jema iwapo watu wanapogombea ubunge au nafasi nyingine ya uongozi, tungewauliza kama wana vitabu, kama wanasoma vitabu, na kwa muda huu wanapogombea wanasoma vitabu vipi. Hapo tungeweza kuwabaini watu makini na mavuvuzela pia.

Lakini tatizo ni kuwa utamaduni wa kusoma vitabu haupo Tanzania. Kwa hivyo, mavuvuzela nao wanaingia katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wakiwa na uhakika kuwa hakuna atakayewauliza kuhusu masuala ya vitabu.

2 comments:

Fadhy Mtanga said...

Nimefurahi sana kumwona Mkapa na lundo la vitabu na magazeti.

Mbele said...

Hapo pichani vinaonekana vile vilivyokuwepo sehemu hiyo wakati picha inapigwa. Sina shaka kuwa ana utitiri wa vitabu kwenye maktaba yake.

Mwalimu Nyerere nadhani alitia fora kwa kusoma vitabu. Alikuwa pia mhimizaji mkubwa wa usomaji wa vitabu, na hivi karibuni nimeona habari ya kusisimua kuhusu hilo katika kitabu kiitwacho Africa Writes Back, kilichoandikwa na James Currey. Iko siku nitaandika kuhusu hilo, Insh'Allah.

Lakini jingine la msingi na kushtua ni kuwa maktaba binafsi ya Mwalimu Nyerere kule Butiama ina vitabu zaidi ya 8000. Soma hapa. Sijui kama wabunge wetu wakikusanya vitabu vyao vyote (kama wanavyo) vinaweza kufikia 2000.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...