
Alikuja kwenye meza yangu mama mmoja. Katika maongezi nilitambua kuwa ni m-Marekani mweusi. Tuliongelea kuhusu shughuli zangu za ufundishaji, na pia alipenda kujua mada za vitabu vyangu, nami nikamwelezea. Alichukua vitabu vifuatavyo: Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, Africans in the World, na Matengo Folktales. Kisha, alipoona kitabu cha ki-Swahili, CHANGAMOTO: Insha za Jamii, alikichukua.
Nilishangaa kidogo kuona anachukua kitabu cha ki-Swahili, wakati haijui lugha hiyo. Aliniambia kuwa mume wake ni m-Somali kutoka Kenya, ambaye anajua ki-Swahili. Akaendelea kunieleza kuwa anamnunulia hicho kitabu. Kisha akaniomba nikisaini, nami nilifanya hivyo, nikaandika na salaam kwa ki-Swahili.
Niliwahi kuandika katika blogu hii kuwa hapa Marekani nimeona tabia aliyoonyesha huyu mama. Watu wanafurahi kuwanunulia wenzao vitabu. Watu wanaona kitabu ni zawadi bora. Nilijiuliza iwapo kwetu Tanzania unaweza kumpa mtu kitabu kama zawadi ya Krismasi au Iddi el Fitri. Soma hapa.
Kwenye matamasha kama haya ya Afrifest, huwa nachukua nakala mbili tatu za kitabu hiki cha ki-Swahili, kwani sitegemei kama atapatikana mtu atakayevihitaji. Lakini, mambo hutokea, kama nilivyoeleza hapa juu.
No comments:
Post a Comment