Friday, August 17, 2012

Leo Ninatimiza Miaka 61

Leo ninatimiza miaka 61 ya maisha yangu. Pamoja na kumshukuru Mungu kwa kuniweka hai hadi leo, ni lazima nijiulize: nimetumiaje fursa hii aliyonijalia Mungu ya kuwepo duniani miaka yote hiyo?

Mungu ametuweka hapa duniani kwa sababu gani? Maisha yetu yana faida gani kwa wanadamu wenzetu? Tuna malengo gani yenye manufaa kwa wanadamu wengine siku hadi siku, mwezi hadi mwezi, mwaka hadi mwaka?

Miaka hii ninamwazia na kumsoma sana Ernest Hemingway. Alifariki akiwa na umri unaofanana na huu niliofikia leo. Tangu akiwa kijana, na miaka yote ya maisha yake, alitoa mchango mkubwa kwa walimwengu kwa uandishi wake. Alipokuwa na miaka 53, alitunukiwa tuzo ya Nobel katika fasihi. Je, nikijifananisha na watu kama Hemingway, mimi nimeshafanya nini?

Masuali haya ni magumu. Siku ya leo, pamoja na kumshukuru Mungu, pamoja na kujiuliza kuhusu wajibu wangu hapa duniani, nawajibika kuwakumbuka wenzetu wengi ambao hawakupata fursa ya kuishi miaka niliyoishi. Wengi wamefariki wakiwa wachanga, wengine vijana. Kwa nini Mungu kaniweka hadi leo? Hilo liwe suali la kujiuliza muda wote, liwe mwongozo wa maisha yangu yaliyobaki.




5 comments:

Yasinta Ngonyani said...

HONGERA SANA KWA KUTIMIZA MIAKA 61 YA MAISHA YAKO. NATUMAINI UIMEKUWA NA SIKU NJEMA KATIKA KUTAFAKARI NA PIA KUFURAHIA SIKU HII. NAMI NASEMA MWENYEZI MUNGU NA AKUZIDISHIA 61 TENA ILI UWEZE KUFANYE VILE ULIVYOKUSUDIA AMBAVYO HUJAFANYA. AKANONO!!!

Rachel Siwa said...

Hongera sana kwa kufikia hapo,MUNGU Azidi kukubariki na kukupa Umri zaidi.
Uzidi kuwa Bararaka kwa Familia na Jamii Pia.

Emmanuel Turuka said...

Hongera sana na Mwenyezi Mungu aendelee kukujalia afya njema ili uweze kuendelea kuelimisha jamii kwa namna hii; nafikiri umeweza kufanya mambo mengi umeweza kutumia talanta yako ya elimu katika kuelimisha jamii ya Tanzania.Huu ni wajibu mkubwa ambao umefanikiwa kuufanya kwa jinsi Mwenyezi Mungu alivyo kujalia; Basi nakutakia baraka za Mungu na uweze kuishi miaka 120 kulingana na maandiko. Hongera sana;

PBF Rungwe Pilot Project said...

Hongera sana kwa kutimiza miaka 61,na kisha kwa kuibua mjadala muhimu wa kifalsafa- kuwa mwisho mwishoni kila mtu atatakiwa kuleta hesabu ya kuwa amefanyia nini hii dunia ambayo imemhifadhi kwa kipindi cha maisha yake.
Nakushukuru sana.

Mbele said...

Asanteni sana kwa dua zenu na mawaidha murua. Nimeona kuwa kadiri umri wangu unavyosonga mbele, nimefikia hatua ya kulenga zaidi kwenye maana ya maisha, nikizingatia kuwa maisha haya ni dhamana tu ambayo Mungu ametupa ili tufanye mambo ya maana kwa walimwengu.

Tena basi, katika kutafakari hilo, nimekumbuka kuwa Yesu alituambia kuwa tunapaswa kushikamana na watu wasiotuhusu, yaani watu baki. Huko ndiko tunapata thawabu nzito. Lakini tukizingatia kushikamana na ndugu tu na marafiki, hatutimizi amri ya Mungu ipasavyo.

Kwa hivi, pamoja na kushirikiana na watu wetu wa karibu, yaani ndugu, jamaa, na marafiki, kazi inayobaki ni kutafuta njia ya kuwa karibu na watu baki. Kama wewe ni muumini wa dini fulani, kwa mfano, nenda nje ya dini yako, kajumuike na watu wa dini zingine, wapinzani wa dini yako, na watu wasio na dini. Yesu alituamuru kumpenda Mungu kwa moyo wetu wote na uwezo wetu wote, na kuwapenda watu wote, wakiwemo maadui zetu. Hapo ndipo tutapata thawabu tele.

Ni mtihani mkubwa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...