Thursday, August 9, 2012

Tamasha la "Afrifest 2012" Minnesota

Wikiendi hii kutafanyika tamasha jingine la Afrifest hapa Minnesota. Tamasha hili hufanyika kila mwaka, na huu ni mwaka wa tano. Lengo ni kuwakutanisha wa-Afrika, watu wenye asili ya ki-Afrika, na wengine wote, kwa ajili ya kujionea na kuelimishana kuhusu mambo mengi ambayo watu weusi wamefanya katika historia, katika nyanja mbali mbali. Ni fursa ya kusherehekea mafanikio yao katika fani mbali mbali, na pia kubadilishana mawazo kuhusu changamoto zilizopo, kwa lengo la kujipanga kwa mshikamano na maendeleo siku za usoni.

Nafurahi kuwa nimekuwa mshirika katika shughuli za Afrifest tangu mwanzo, kama mwanabodi wa Afrifest na sasa mwenyekiti wa bodi. Kesho, tarehe 10 jioni, tutafanya ufunguzi wa tamasha. Nitaongea machache kuhusu Afrifest na kisha watu watapata fursa ya kujumuika na kufahamiana.

Keshokutwa, Jumamosi, na hadi Jumapili, tutakuwa na maonesho ya aina aina. Nami nitakuwa na meza yangu, nikiwa na vitabu na machapisho mengine. Kwenye shughuli hizi napata fursa ya kuongea na watu wengi kuhusu shughuli zangu katika utafiti, ufundishaji, mipango ya kuwapeleka wanafunzi Afrika. Ni fursa ya pekee kuongea na watu kuhusu ninayoandika katika nyanja za fasihi na tamaduni za wa-Afrika na Wamarekani, kama inavyodhihirika katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Afrifest imeshakuwa tukio muhimu hapa Minnesota, na kadiri miaka inavyopita, watu wengi zaidi na zaidi wanahamasika kuhudhuria au kushiriki kwa namna moja au nyingine. Kuna vivutio vingi, kama vile muziki, michezo, maonesho ya mitindo, kumbukumbu za historia, na burudani mbali mbali kwa watu wazima na watoto. Kwa taarifa zaidi, soma hapa.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...