Monday, March 28, 2016

Picha Yangu Kwenye Jalada la Kitabu

Jana jioni nilivyokuwa ninachapisha kitabu changu kipya mtandaoni, nilijipiga picha kwa ajili ya kuiweka kwenye jalada la nyuma la kitabu. Nilikuwa nimetumia masaa yapata manne katika kuweka marekebisho ya ziada ya mswada na pia katika hatua za kwanza za kuuweka mswada mtandaoni.

Picha niliyojipiga inaonyesha dalili za uchovu niliokuwa nao baada ya kufanya kazi ya kufikirisha. Sikujali. Niliamua kuitumia picha hiyo hiyo, nikamalizia shughuli ya kuchapisha kitabu.

Tukijiuliza kwa nini tunaweka picha kwenye jalada la kitabu, tutakumbana na masuala na masuali. Suali pana zaidi ni kwa nini tunajipiga picha. Picha kama hii niliyojipiga jana itakaa kwenye jalada hivyo ilivyo, pamoja na kwamba inaleta taswira yangu ilivyokuwa kwa sekunde ile moja ilipopigwa.

Baada ya sekunde ile moja, uso wangu haukubaki hivyo. Huenda nilitabasamu au kununa. Baada ya muda, sikuwepo humu ofisini, na vitabu nyuma yangu, wala sikuvaa nguo zinazoonekana pichani.

Tunaweza kusema kuwa picha ni udanganyifu. Inatuaminisha kuwa huyu ni fulani, lakini fulani huyu si mtu hai. Hapumui wala haongei. Angalia hata macho. Yatabaki hivi kwa miaka na miaka, bila kuyapepesa. Angalia nywele na ndevu. Baada ya muda, mvi zitakuwa zimetanda. Cha zaidi ni kuwa siku chache zilizopita, kinyozi alizipunguza. Kama tunapenda kuwa wakweli, labda tuwe tunajipiga video muda wote, maisha yote, bila kuacha hata sekunde moja.

Udanganyifu wa picha hauishii hapo. Kwa ujumla, watu wanajiandaa kabla ya kupigwa picha. Wanajiweka katika hali ya unadhifu. Wengi wanaamini ni muhimu kutabasamu wakati wa kupigwa picha, hata kama moyoni kuna machungu.

Masuala na masuali ni mengi, yanayogusa nyanja mbali mbali, kama vile saikolojia, falsafa na sanaa ya upigaji na upigwaji picha. Hata namna tunavyoziangalia na kuzielewa picha ni suala linalofungamana na misingi kama utamaduni na saikolojia. Wataalam wanayatafakari masuala hayo, na wameyaandikia makala na vitabu, kwa mfano Photography Theory in Historical Perspective cha Hilde Van Gelder na Helen Westgeest.

Sunday, March 27, 2016

Nimechapisha Mwongozo wa "Song of Lawino"

Leo nimechapisha kitabu ambacho ni mwongozo wa Song of Lawino, utungo maarufu wa Okot p'Bitek. Kitabu hiki, Notes on Okot p'Bitek's Song of Lawino, ni zao la miaka mingi ya kutafakari utungo huu maarufu katika fasihi ya Afrika.

Nimejitahidi kuandika mwongozo ambao unaichambua Song of Lawino katika mkabala wa fasihi ya Afrika, kwa maana ya mtazamo wa fasihi linganifu, na masuala ya itikadi. Vile vile, nimetumia dhana za nadharia ya fasihi, ambazo zina umuhimu katika kuuelezea utungo wa Song of Lawino.

Uandishi wa miongozo ya kazi za fasihi nilianza zamani. Mwongozo wa kwanza kabisa nilioandika ni juu ya tamthilia ya Arthur Miller, A View From the Bridge, ambao niliuandika kwa ajili ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Tanzania, miaka ya sabini na kitu. Niliwahi pia kuandika mwongozo juu ya The African Child, utungo wa Camara Laye. Mwongozo wangu ambao unajulikana zaidi ni Notes on Achebe's Things Fall Apart, ambao historia yake niliielezea katika blogu hii.

Kwa kadiri ninavyokumbuka, sijawahi kufundisha Song of Lawino. Kazi ya kuandaa mwongozo huu ilikuwa ni ya kujitakia tu, kutokana na kuupenda kwangu utungo huu maarufu. Kadiri nilivyokuwa naendelea kusoma fasihi za ulimwengu na nadharia za fasihi nilivutiwa na wazo la kuuchambua utungo wa Song of Lawino. Nilitaka nitoe mchango kwa wanafunzi na wasomaji katika kuutafakari utungo huu.

Kwa sababu hii, nimeweka pia maswali mwishoni mwa Notes on Okot p'Bitek's Song of Lawino. Ninategemea masuali haya yatakuwa changamoto ya kufikirisha kwa wasomaji wa Song of Lawino.

Saturday, March 26, 2016

Wasomaji Wangu: Akina Mama wa ki-Afrika, Marekani

Leo napenda kuendelea na jadi ya kuwakumbuka wasomaji wangu, kwa moyo wa shukrani. Kwa kuwa ninaandika katika magazeti, majarida, blogu zangu na za wengine, Facebook, na pia naandika vitabu, nina wasomaji wengi sehemu mbali mbali za dunia.

Hapa nimeamua kuwakumbuka wasomaji wa vitabu vyangu ambao ni wanawake wenye asili ya Afrika na nimefahamiana nao Marekani. Kwa kuwa nao ni wengi, na wengi siwafahamu, nitawataje wachache tu.


Huyu hapa ni Shannon, m-Marekani Mweusi anayeishi Minnesota. Ni profesa na mwandishi ambaye amekuwa akijijengea umaarufu. Kitabu chake cha kwanza, See No Color, kimewavutia wasomaji na wahakiki.

Shannon alikuwa mhakiki wa kwanza kuchapisha uhakiki wa kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Niliwahi kuandika habari zake katika blogu hii.

Huyu hapa ni Maimouna, mzaliwa wa Ivory Coast, anayeishi Minnesota. Yeye ni
mmoja wa wasomaji wa mwanzo kabisa wa Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nilifarijika sana aliponiambia kuwa amekipenda  kitabu hiki, na kwamba kitumiwe na wanafunzi wa ki-Marekani wanaokwenda Afrika. Kwa kuwa huyu mama na mume wake ambaye ni rafiki yangu ni wa-Islamu, kukipenda kwake kitabu changu kulinipa faraja ya pekee, kwani sikuwa na uhakika kuwa mambo ninayosema kitabu yameendana na maisha kama anavyoyafahamu yeye.Huyu ni Latonya, m-Marekani Mweusi. Anaishi Minnesota. Tunakutana katika matamasha. Anapenda maandishi yangu, na aliwahi kunielezea hisia zake pale ninapoandika kwa ki-Swahili. Aliniuliza kwa nini ninawaweka kando ndugu zangu wa-Marekani Weusi. Nilijisikia vibaya, nikamwahidi kuwa nitajitahidi kuzingatia kauli yake.


Huyu ni Nalongue, mzaliwa wa Togo anayeishi Minnesota. Ni kati ya watu ambao wamekuwa wakifanya bidii sana kukitangaza kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Huyu ndiye ambaye niliwahi kumtaja katika blogu hii hapa, hapa na hapa.


Huyu hapa ni Rita, kutoka Sierra Leone. Anaishi Minnesota. Ni mwanzilishi na mkurugenzi wa jumuia ya wanawake iitwayo African Women Connect.

Baada ya yeye kusoma kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, tulikutana mjini Minneapolis tukakiongelea kwa karibu saa mbili. Alikuwa na hamu ya kuandika uhakiki wa kitabu hiki.


Huyu ni Leah, mzaliwa wa Kenya. Ni profesa, ambaye alipokuwa anafundisha katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Iowa, alikisoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, akaamua kukitumia alipowapeleka wanafunzi Rwanda na Tanzania mwaka 2008 katika safari ya masomo.Huyu ni Eli, mzaliwa wa Togo. Anaishi Minnesota. Anavyo na amevisoma vitabu vyangu vya ki-Ingereza. Anaponikuta kwenye matamasha au mijumuiko mingine, anakuwa na dukuduku ya kujua kama nimeshaandika kitabu kingine.  Ninahamasika kwa moyo huu wa ufuatiliaji.

Huyu ni Julia, mzaliwa wa Kenya. Ni mwandishi katika magazeti hapa Minnesota anayejituma sana. Ni mmoja kati ya wasomaji wangu wa mwanzo, ambaye tangu mwanzo alijitosa katika kukitangaza kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Niliwahi kumtaja katika blogu hii, nilipoongelea juhudi za wa-Kenya katika masuala ya elimu na vitabu.


Huyu ni Nneka. Baba yake ni kutoka Nigeria na mama yake ni m-Marekani Mweusi. Nilifahamu jina lake kutokana na shughuli zake katika taasisi ya African Global Roots, inayoshughulika na utamaduni na elimu kwa waAfrika na wana-Diaspora wa ki-Afrika.

Wiki chache zilizopita nilikutana naye kwa mara ya kwanza, nikaelewa habari zake kama mtoto wa tamaduni mbili tofauti. Alipotambua kuwa ninashughulika na masuala hayo, aliniuliza masuali kadhaa. Baadaye nilimpelekea kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Baada ya siku chache aliniletea ujumbe akielezea jinsi alivyokipenda. Ninategemea kuendelea mawasiliano naye, angalau kumpa mwanga kuhusu masuala anayokabiliana nayo.

Wednesday, March 23, 2016

Watu Wanaofanikiwa na Wale Wasiofanikiwa

Katika vitabu vinavyohusu mafanikio na maendeleo binafsi na pia kuinufaisha jamii, kuna mambo yanayoelezwa tena na tena. Mambo hayo tunaweza kuyaita mbinu au siri za mafanikio.

Picha nilizoweka hapa zinaorodhesha mambo hayo. Kwa upande mmoja kuna mambo wanayofanya watu wenye mafanikio au wanaotaka mafanikio. Ni mambo ambayo ni sehemu ya tabia ya watu hao.

Kwa upande wa pili, yanatajwa mambo wafanyayo watu wasio na mafanikio, au wasiofahamu njia au siri ya mafanikio. Hao ni watu wa kushindwa.

Mambo wanayofanya watu wenye mafanikio au wanaotaka mafanikio ni kama kusoma kila siku, kuwa wepesi wa kuyapokeo mabadiliko, wepesi wa kuwasamehe wenzao, wanaongelea fikra na mawazo, wanajifunza muda wote, ni wenye shukrani, wanajiwekea malengo na wanayatekeleza, wanawatakia wenzao mafanikio, wanayasifia mafanikio ya wenzao.

Watu wasio na mafanikio au wasiofahamu siri ya mafanikio ni wakosoaji wakubwa na walalamishi,  wanaogopa mabadiliko, wana visirani, wanawaongelea watu, wanajiona wajuaji, wanawalaumu wengine kwa lolote, wanadhani wanastahili kila watakacho, hawajiwekei malengo, hawakiri udhaifu wao au makosa yao, hawatambui mazuri ya wenzao, wanataka sifa hata wasipostahili, wanaangalia televisheni kila siku.

Katika kuyatafakari mambo hayo, nimeona wazi matatizo ya wa-Tanzania wengi. Wengi wamo katika hili kundi la wasiofanikiwa. Tabia ya kukaa vijiweni na kulumbana kuhusu vilabu vya mpira vya Ulaya, kuhusu vituko vya mastaa, kulalamikia hili au lile, ni tabia iliyoshamiri. Muda wanaokaa vijiweni wangeweza kuutumia kwa kusoma vitabu. Lakini huwaoni wakifanya hivyo, wala nyumbani, wala maktabani. Wasipofanikiwa, hawajitathmini na kutambua dosari zao, bali wanatafuta visingizio na wachawi.

Sunday, March 20, 2016

Tukio Katika Nyumba ya Hemingway, Oak Park

Tarehe 27 Februari, nilizuru nyumba alimozaliwa mwandishi Ernest Hemingway, na pia jumba la kumbukumbu ya Hemingway, kama nilivyoandika katika blogu hii na blogu ya ki-Ingereza. Ilikuwa ni siku ya pekee, siku ambayo ndoto yangu ya miaka ilitimia.

Kati ya watu niliokutana nao katika nyumba ya Hemingway, ambao nao walikuwa wamekuja kuitembelea, ni binti aliyejitambulisha kuwa ni wa ukoo wa Hemingway. Alinipa kadi yake, iliyoonyesha kuwa jina lake ni Laura Hemingway.

Nilishangaa na kufurahi, nikaanza kuongelea namna ninavyomwenzi Hemingway. Niliongelea kozi yangu ya Hemingway, na jinsi ninavyowasiliana na mzee Patrick Hemingway. Binti huyu na wengine tuliokuwa tunasubiri kuanza ziara walivutiwa na taarifa hizo. Ninajitambua kuwa siwezi kuiachia fursa yoyote ya kuongelea habari za Hemingway.

Kwa bahati mbaya, niliporejea kutoka Chicago, niligundua kuwa nilikuwa nimepoteza anwani ya binti huyu. Leo amejitokeza katika facebook kuanzisha mawasiliano nami. Baada ya kuweka uhusiano huo, nimeweza kuipata picha tuliyopiga siku tulipokutana, ambayo inaonekana hapa juu.

Saturday, March 19, 2016

Bill Gates: Msomaji Makini wa Vitabu

Bill Gates, tajiri mkubwa kuliko wote duniani, ni msomaji makini wa vitabu. Anasoma vitabu yapata 50 kwa mwaka. Anaviona kuwa njia bora ya kujipatia elimu, hata kwa yule ambaye hakusoma sana shuleni. Yeye mwenyewe alijiunga kama mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Harvard, lakini alijiondoa bila kuhitimu.

Kwa maelezo yake mwenyewe, Bill Gates anasema kuwa tangu alipokuwa mtoto, alikuwa na ndoto nyingi kuhusu maisha yake ya baadaye. Anashukuru kwamba wazazi wake walimpa fursa tele za kusoma vitabu, ambavyo vilistawisha ndoto zake.

Sasa, katika utu uzima wake, anaendelea kusoma vitabu vya aina mbali mbali, ingawa anapenda zaidi vitabu vinavyoelimisha, kama vile vitabu vinavyoelezea mabadiliko ya dunia, sayansi, tekinolojia, na jamii, na namna binadamu anavyoweza kuchangia mabadiliko chanya. Anapenda vitabu vinavyohusu namna ya kutatua matatizo kama vile magonjwa.

Unaweza kujionea jinsi Bill Gates anavyovithamini vitabu ukitembelea blogu yake. Ziko pia video ambamo anaongelea vitabu, kwa mfano hii hapa.

Friday, March 18, 2016

Mwandishi Unapoigusa Mioyo ya Wasomaji

Ukimwuliza mwandishi kwa nini anaandika, anaweza kukuelezea msukumo, sababu, na malengo yake. Nami kuna mambo yanayonisukuma niandike, hasa hamu ya kuwafikishia watu fikra na mitazamo yangu kuhusu masuala mbalimbali. Nina hamu ya kujieleza kwa namna ya kuwagusa wasomaji, na ninapoona nimefanikiwa, ninafurahi. Wasomaji hao wananipa motisha ya kuendelea kuandika.

Hapa kushoto niko na mama Kandie, m-Marekani. Alikuwa mfanyakazi katika Chuo cha St. Olaf nilipoajiriwa mwaka 1991, tukawa tunafurahi na kuongea kila tulipokutana. Ni msomaji wa vitabu vyangu tangu zamani. Baadaye alistaafu kazini. Picha hii tulipiga mjini Faribault, mwaka jana. Tunapokutana tunajiona kama ndugu.
Hapa kushoto niko na wadau wawili. Huyu wa katikati ni bwana Richard, kutoka Sierra Leone. Baada ya kununua na kusoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, alinunua vingine akawapelekea marafiki sehemu mbali mbali hapa Marekani. Hii picha tulipiga katika tamasha la utamaduni Brooklyn Park. Richard alimleta huyu mwenzake, mzaliwa wa Sudan, kumtambulisha kwangu ili naye ajipatie kitabu. Richard mwenyer ameshika kijitabu changu kingine, Africans in the World, ambacho alikinunua siku hiyo.

Pichani hapa kushoto niko na dada Latonya, m-Marekani Mweusi. Tulipiga picha hii katika tamasha la Afrifest mjini Brooklyn Park, baada ya yeye kununua kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho anaonekana amekishika. Latonya hataki kukosa ninachoandika, hata mitandaoni. Tunafurahi kila tunapokutana.

Kuhitimisha ujumbe wangu, napenda kusema kwamba habari kama hizi nilizoleta hapa ni za maana sana kwangu. Sio siri kwamba kuna watu wanaoandika vitabu kwa mategemeo ya kupata fedha. Lakini kwa upande wangu, kuwagusa watu kwa maandishi yangu ni tunu isiyo kifani, yenye thamani kuliko fedha. Maisha yangu, sawa na ya binadamu mwingine yeyote, ni mafupi, lakini maandishi yangu yatadumu.

Thursday, March 17, 2016

Ninafurahia Kuendesha Blogu

Ingawa kuendesha blogu kuna magumu, ninatambua faida zake. Faida kubwa kabisa kwa upande wangu ni uhuru wa kujieleza. Hakuna yeyote anayenizuia kuandika chochote nitakacho, kwa namna nitakayo.

Ninaifurahia hali hii nikizingatia jinsi vyombo vya habari vinavyotawala uhuru wa watu. Wahariri na wamiliki wa vyombo hivyo wana uwezo wa kulikubali au kulikataa andiko wanaloletewa. Waandishi wanakosa uhuru nilio nao kama mmiliki wa blogu. Ninaamini kuwa baadhi ya mambo ninayoandika katika blogu yangu hayangechapishwa kwingineko. Mfano ni mada za dini.

Mimi ni mtetezi wa uhuru wa watu kujieleza. Nikianzisha mada hapa katika blogu, ninamkaribisha yeyote kuchangia. Ninafurahi kuona hoja zikipambanishwa. Ninafurahi kuwapa watu fursa ambayo ni finyu au inakosekana mahali pengine.

Msimamo huo nimekuwa nao tangu zamani. Siafiki kupigwa marufuku vitabu, magazeti, au njia zingine za watu kujieleza na kusambaza mawazo na mitazamo. Kuunga mkono upigaji marufuku wa maandishi au aina zingine za watu kujieleza ni kujichimbia kaburi. Kama unatetea vitendo hivyo, usilalamike endapo maandishi yako au yale unayoyathamini yatapigwa marufuku. Usilalamike ukihujumiwa haki na uhuru wako wa kujieleza.

Kumiliki na kuendesha blogu kumeniunganisha na wasomaji sehemu mbali mbali za dunia. Ninaangalia takwimu na kujionea idadi ya watu wanaotembelea blogu na mahali waliko. Baadhi yao wananiandikia ujumbe binafsi. Kwa mfano, mwanahabari wa kituo cha televisheni maarufu Tanzania aliniandikia kwamba anafuatilia blogu yangu na inamsaidia katika kuandaa vipindi. Ni faida nyingine na motisha ya kuendesha blogu.

Tuesday, March 15, 2016

Kutana na Fundi Abdallah Ramadhani

Leo ninapenda kumtambulisha Abdallah Ramadhani, ambaye nimefahamiana naye siku chache tu zilizopita katika mtandao wa Facebook. Ilikuwa bahati tu kuwa nilianzisha mawasiliano naye, na ndipo nikaweza kujua habari zake. Nilivutiwa na shughuli za ufundi anazofanya.
Nilimwambia kuwa ningeweza kuzitangaza shughuli zake katika blogu yangu. Nilitambua tangu miaka iliyopita kuwa ninaweza kuitumia blogu yangu hii kutangazia shughuli za wa-Tanzania ninaokutana nao au ninaopata habari zao na kuvutiwa na namna wanavyojishughulisha. Ninawaunga mkono. Kwa mfano, niliwahi kuandika juu ya wajasiriamali wa Duka Asili na Super Muhogo.Abdallah Ramadhani alizaliwa Temeke, Dar es Salaam, mwaka 11 Mei,1979.  Anatengeneza viatu vizuri kama inavyoonekana pichani katika ukurasa huu. Ufundi huu alijifunza kwa baba yake, ambaye alijifunza kwa wa-Hindi.

Wa-Tanzania tujijengee utamaduni wa kuvithamini vipaji vya wa-Tanzania wenzetu, na huduma wanazotoa. Tuwe na utamaduni wa kuzithamini kazi zao. Tuzithamini bidhaa zinazozalishwa nchini mwetu, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii, na katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Manufaa yake ni kwa hao wahusika na kwa Taifa.

Unaweza kuwasiliana na Abdallah kwa simu, namba  255-682-588-583 au 255-719-588-583


Sunday, March 13, 2016

Piano Katika Nyumba ya Hemingway, Oak Park

Wanasema tembea uone. Ni njia ya uhakika ya kujipatia elimu. Tarehe 26 Februari, nilifika Oak Park, Illinois, kutembelea nyumba alimozaliwa mwandishi Ernest Hemingway na pia jumba la kumbukumbu juu yake. Niliandika kuhusu ziara hii katika blogu hii na katika blogu yangu ya ki-Ingereza.

Mimi kama msomaji wa maandishi na habari za Ernest Hemingway nilifurahi kufika eneo hilo ambalo habari zake nilikuwa nimezifahamu kwa miaka mingi. Kabla ya kuisogea nyumba, nilimwomba dreva wa teksi, mzaliwa wa Nigeria, anipige picha.Humo ndani, baada ya kukaribishwa sehemu ya mapokezi na kulipia, nilijumuika, na wageni wengine, tukaanza ziara. Katika chumba cha kwanza, kuna viti, meza, na vitu vingine, na vile vile piano kama inavyoonekana pichani.

Mama ya Ernest, Grace Hall Hemingway, alikuwa mpenda muziki na uimbaji, na aliwahamasisha wanafamilia katika fani hizo. Mtoto Ernest hakupenda, lakini alilazimika.  Nilijifunza mengi. Nitajitahidi kuyaelezea kidogo kidogo siku za usoni.

Friday, March 4, 2016

Dini ni Siasa Tu, Asema Mwandishi Nawal el SaadawiKatika kozi yangu ya Muslim Women Writers, tunajiandaa kusoma The Fall of the Imam, riwaya ya Nawal el Saadawi wa Misri. Nimeshawapa wanafunzi maelezo kuhusu historia ya fasihi andishi Misri, ambayo imekuwepo tangu miaka yapata elfu saba iliyopita. Hii ni kwa mujibu wa maandishi ya kale yaliyogundulika, kama vile hadithi na mafundisho ya dini, hasa The Egyptian Book of the Dead.

Miaka ilivyopita, fasihi ya Misri ilitajirika kwa kutokana na mikondo ya ndani na nje, na hiyo ya nje ni kutoka sehemu kama Mashariki ya Kati na Uarabuni, pande zingine za Afrika, na Ulaya. Kwa karne moja na kidogo iliyopita, wamejitokeza waandishi wengi maarufu nchini Misri. Mifano ni Naguib Mahfouz, Taha Hussein, Tawfiq al Hakim, Yusuf Idris, Nawal el Saadawi, Sonallah Ibrahim,  na Alifa Rifaat. Kwa ujumla wao, waandishi hao wametumia mikondo niliyoitaja.

Katika kozi hii ya Muslim Women Writers, nimemchagua mwandishi mmoja tu kutoka Misri, ambaye ni huyu Nawal el Saadawi. Na nimechagua riwaya yake moja tu. Ningeweza kuchagua riwaya tofauti ya mwandishi huyu, au ningeweza kufundisha hadithi za Alifa Rifaat, Distant View of a Minaret.

Nawal el Saadawi si tu mwandishi, bali ni daktari na mwanaharakati maarufu. Amekuwa akipambana na mfumo wa kijamii wa nchi yake, ambao unawakandamiza wanawake. Anazikosoa na kuzipiga vita itikadi zozote, zikiwemo dini, zinazohalalisha ukandamizaji wa wanawake. Nawal el Saadawi ni mama shujaa ambaye anajiamini na hatishiki, kama inavyonekana katika video niliyoweka hapa ambayo nitawaonyesha wanafunzi wangu kama maandalizi ya kujadili The Fall of the Imam.

Wednesday, March 2, 2016

Picha za Mtoto Ernest Hemingway

Tarehe 27 Februari, nilitembelea Oak Park, pembeni mwa Chicago. kwa ajili ya kuzuru nyumba alimozaliwa mwandishi Ernest Hemingway na nyumba ya kumbukumbu, Hemingway Museum, kama nilivyoripoti katika blogu hii na blogu ya ki-Ingereza.

Katika Hemingway Museum, ambayo picha yake inaonekana hapa kushoto, niliona picha nyingi, zikiwemo za mtoto Ernest Hemingway.


Hapa kushoto anaonekana babu wa Ernest kwa upande wa mama yake, akiwa na wajukuu. Kushoto kabisa ni Ernest, na hao watoto wengine ni dada zake.
Hapa kushoto anaonekana mtoto Ernest, akiwa na bunduki na zana ya kuvulia samaki. Tangu utotoni, Ernest alifundishwa kuvua samaki na kuwinda.Hapa kushoto, mtoto Ernest anaonekana akimlisha mnyama ambaye kwa ki-Ingereza huitwa squirrel. Nimeangalia mtandaoni nikaona kuwa mnyama huyu anaitwa kindi kwa ki-Swahili.

Nilipoiona picha hii nilivutiwa kuona mnyama ametulia namna hii, lakini nilipoisogelea na kusoma maelezo yanayoonekana chini kushoto, nilitambua kuwa huyu si mnyama hai. Ni mzoga ambao umekarabatiwa na kufanywa uonekane kama mnyama hai.

Hata hivyo picha inanivutia, kwa namna inavyowasilisha ukweli muhimu juu ya Hemingway, jinsi maisha yake na hisia zake zilivyofungamana na maisha ya viumbe kama wanyama, samaki na ndege.

Mtoto Ernest alipokuwa shuleni aliandika kuwa ndoto yake maishani ilikuwa ni kuwa mwandishi na pia mtu wa kusafiri. Ilikuwa kama amejitabiria, kwani akiwa kijana wa miaka 18, alipelekwa Kansas City ambako aliajiriwa kama ripota wa gazeti la Kansas City Star.

Katika kipindi hicho yeye na waandishi wengine wa gazeti hili waliwajibika kufuata orodha ya amri kali kuhusu uandishi uliotakiwa. Watafiti wote wanakubaliana kwamba kufanya kwake kazi katika Kansas City Star kulimjenga Hemingway katika aina ya uandishi aliyotumia maisha yake yote.

Hapa kushoto Ernest anaonekana akiwa ameshika bunduki na ndege. Sikuona maelezo juu ya picha hii, ila ninahisi ilipigwa baada ya Hemingway kumpiga huyu ndege kwa risasi.

Jadi ya kupiga picha ya mwindaji na mnyama au ndege aliyemwua imekuwepo tangu zamani. Kuna picha kadhaa za Hemingway za miaka ya baadaye akiwa na wanyama aliowaua, si tu huku Marekani, bali pia sehemu zingine, ikiwemo Afrika Mashariki. Wachambuzi wa saikolojia wanaweza kuelezea vizuri maana ya jadi hii ya kuthamini hiki kinachoitwa "trophy" kwa ki-Ingereza.