Showing posts with label shukrani. Show all posts
Showing posts with label shukrani. Show all posts

Monday, August 7, 2017

Global Minnesota Wameniletea Kifuta Jasho

Juzi, tarehe 5, niliandika katika blogu hii kwamba nilikuwa nimepata barua ya shukrani kutoka Global Minnesota, kufuatia mhadhara niliotoa. Leo, bila kutegemea, nimepata cheki kutoka kwao, kama kifuta jasho.

Sikutegemea, kwani tangu mwanzo waliponialika kutoa mhadhara na hata baada ya mhadhara, sikuwa na hata fununu kwamba kuna kifuta jasho. Nami sikufikiria wala kutegemea. Nilichojali ni kufanya kazi waliyoniomba kufanya, yaani kujadili mada ya "African Folktales to Contemporary Authors."

Ninaongozwa na nasaha ya wahenga kwamba tenda wema nenda zako; usingoje shukrani. Kama nilivyosema katika blogu hii, mengine ni matokeo. Sijawahi kukataa mwaliko wa kwenda kutoa mhadhara kwa sababu ya malipo.

Watu wanaonihimiza nisitoe huduma bila malipo ninawaambia kuwa kuna baraka katika kuwasaidia watu. Fursa ya kutoa mhadhara ni ya manufaa kwangu, kwani inaniongezea uzoefu na kuniwezesha kujitathmini ufahamu wangu, hasa katika kipindi cha masuali na majibu. Vile vile matangazo ya mhadhara yanayoandaliwa na kusambazwa na wale wanaonialika yananiongezea kufahamika.

Mara nyingi, huwezi kujua watu unaowahutubia ni akina nani katika jamii. Nimeshuhudia baada ya mhadhara watu wakijitokeza na kujitambulisha kwangu na kuniuliza iwapo nitakuwa tayari kuhutubia kwenye taasisi au jumuia zao. Mwaliko moja unazaa mialiko mingine. Ninasema hayo ili kuwashawishi wale wanaosita kutoa huduma bila kuahidiwa malipo. Hakuna hasara, bali ni faida.

Saturday, August 5, 2017

Shukrani ya Global Minnesota kwa Mhadhara Wangu

Tarehe 12 Julai, nilitoa mhadhara Global Minnesota, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Nimepata barua ya shukrani kutoka Global Minnesota, iliyoandikwa tarehe 20 Julai, ambayo ni kumbukumbu nzuri kwangu. Imeandikwa:

Dear Dr. Mbele

On behalf of Global Minnesota, I would like to thank you for speaking at the Global Conversations program on "African Folktales to Contemporary Authors" at the Minneapolis Central Library on July 12.

Your extensive knowledge and skillful storytelling captured and kept our audience's attention throughout the program. The program was both informative and entertaining, and the feedback we received from the attendees and our partners was extremely positive.

We were also so pleased that you brought your daughters to the program and rekindled an old MIC/GLobal Minnesota connection.

Thank you for partnering with us on this program and helping us in our mission to bring greater awareness and appreciation of African culture to the general public in Minnesota. We look forward to engaging with you again on future Global Minnesota programs!

Kwanza kabisa, mimi nina tabia ya kujitathmini mwenyewe. Pamoja na kusikiliza namna watu wengine wanavyotathmini kazi zangu, tathmini yangu mwenyewe ndiyo inayonisukuma zaidi. Kuna wakati ambapo watu wanaweza kusifia kazi yangu lakini mimi mwenyewe nikawa na mtazamo tofauti.

Pamoja na sifa nilizomwagiwa na Global Minnesota, mimi mwenyewe niliona kuwa muda wa mhadhara ulikuwa mfupi. Kwa hivyo, nilishaamua kuwafahamisha wanipangie siku nyingine na mada nyingine, niweze kuteremsha nondo za kufa mtu, kama wasemavyo wa-Tanzania vijiweni. Sasa, kwa kuwa katika barua yao nao wanapendekeza tuendelee kushirikiana katika programu zao, fursa hiyo sitailazia damu.

Napenda nihitimishe ujumbe wangu kwa kuelezea falsafa inayoniongoza. Jambo la msingi ni kwamba Global Minnesota waliponiuliza kama nitaweza kwenda kutoa mhadhara, nilikubali bila kusita. Ninatambua kuwa mimi ni mwalimu, na ufundishaji hauishii darasani bali unahitajika pia katika jamii nje ya chuo. Vipaji nilivyo navyo nilipewa na Mungu kwa ajili ya wanadamu, si kwa ajili yangu.

Sijivunii vipaji hivyo, bali ninamshukuru Mungu na kumwomba anisaidie kuvitumia kwa namna anavyotaka. Kwamba ninaamka kila asubuhi nikiwa mzima na akili timamu, ni baraka ya Mungu, kuniwezesha kufanya wajibu wangu. Ndio maana, sitilii maanani suala la malipo ninapoalikwa kwenda kutoa mhadhara, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii. Ninazingatia ufanisi wa hali ya juu katika shughuli ninazofanya. Mengine ni matokeo.

Friday, January 6, 2017

Namshukuru Mteja

Leo nimepita kwenye mtandao wa Amazon kuangalia vinapopatikana vitabu vyangu, nikaona ujumbe ulioandikwa jana na mteja kuhusu kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Ni mmoja wa wateja ambao baada ya kununua na kusoma kitabu, huweka maoni yao kuhusu kitabu hapo mtandaoni.

Ninaguswa na wateja hawa na ninapenda kuwashukuru. Ninazingatia kuwa hela walizotumia kununulia kitabu changu wangeweza kuzitumia kwa mahitaji mengine. Halafu, ninawashukuru kwa kitendo chao cha kuandika maoni. Wananitangazia kitabu bila malipo bali kwa hisani yao.

Huyu mteja aliyeandika jana, anaonekana ni m-Marekani, na amesema:

Great book to compare things we do in the United States and how it differs in Africa. Some of the differences would be insulting to Africans and I would not have known it Highly recommend this book if you are traveling to Tanzania as author is from there. It is a short, easy read.

Natafsiri

Kitabu bora kwa ajili ya kufananisha mambo tufanyayo Marekani na yalivyo tofauti kwa Afrika. Baadhi ya tofauti hizo zingetafsiriwa kama utovu wa heshima kwa vigezo vya wa-Afrika, nami nisingejua. Ninakipendekeza sana kitabu hiki iwapo unasafiria Tanzania, kwani mwandishi anatoka kule. Ni kitabu kifupi, rahisi kusomwa.

Ninamshukuru mteja huyu kwa moyo wake wa kutaka kuwasaidia wengine wawe katika mstari sahihi wakiwa wageni Afrika.

Thursday, September 8, 2016

Wasomaji Wangu Wa Nebraska Waendao Tanzania

Nina jadi ya kuwaongelea wasomaji wangu katika blogu hii, kama njia ya kuwaenzi. Ni jambo jema kwa mwandishi kufanya hivyo. Leo ninapenda kuwakumbuka wasomaji wangu wa sinodi ya Nebraska ya Kanisa la Kiluteri la Marekani, ambao tangu zamani wamekuwa na programu ya kupeleka watu Tanzania kuendeleza uhusiano baina yao na wa-Luteri wa Tanzania.

Hao wasafiri, sawa na wenzao wa sinodi zingine za Marekani, wamekuwa wakitumia kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences katika kujiandaa kwa safari, ili kuzielewa tofauti za tamaduni za Marekani na Afrika. Ni elimu muhimu katika ulimwengu wa utandawazi wa leo, ambayo nje ya ufundishaji wa darasani, ninashughulika nayo.


Wakati huu ninapoandika, waumini wa Nebraska wanajiandaa kwa safari ya Tanzania, ambayo itafanyika mwezi Februari mwaka 2017. Wameitangaza safari hii mtandaoni, na mratibu mojawapo wa safari, Martin Malley, ameniandikia ujumbe leo akisema, "We still recommend your book." Katika ukurasa wa 16 wa chapisho la maelezo na maandalizi ya safari, kitabu hicho kimetajwa.

Ninapowakumbuka wasomaji wangu wa Nebraska, ninakumbuka nilivyokutana katika uwanja wa ndege wa Amsterdam na kikundi cha watu wa Nebraska waliokuwa wanakwenda Tanzania, tukasafiri pamoja. Mimi sikuwajua, ila wao walinitambua, kama nilivyoelezea katika blogu yangu ya ki-Ingereza.


Wednesday, March 23, 2016

Watu Wanaofanikiwa na Wale Wasiofanikiwa

Katika vitabu vinavyohusu mafanikio na maendeleo binafsi na pia kuinufaisha jamii, kuna mambo yanayoelezwa tena na tena. Mambo hayo tunaweza kuyaita mbinu au siri za mafanikio.

Picha nilizoweka hapa zinaorodhesha mambo hayo. Kwa upande mmoja kuna mambo wanayofanya watu wenye mafanikio au wanaotaka mafanikio. Ni mambo ambayo ni sehemu ya tabia ya watu hao.

Kwa upande wa pili, yanatajwa mambo wafanyayo watu wasio na mafanikio, au wasiofahamu njia au siri ya mafanikio. Hao ni watu wa kushindwa.

Mambo wanayofanya watu wenye mafanikio au wanaotaka mafanikio ni kama kusoma kila siku, kuwa wepesi wa kuyapokeo mabadiliko, wepesi wa kuwasamehe wenzao, wanaongelea fikra na mawazo, wanajifunza muda wote, ni wenye shukrani, wanajiwekea malengo na wanayatekeleza, wanawatakia wenzao mafanikio, wanayasifia mafanikio ya wenzao.

Watu wasio na mafanikio au wasiofahamu siri ya mafanikio ni wakosoaji wakubwa na walalamishi,  wanaogopa mabadiliko, wana visirani, wanawaongelea watu, wanajiona wajuaji, wanawalaumu wengine kwa lolote, wanadhani wanastahili kila watakacho, hawajiwekei malengo, hawakiri udhaifu wao au makosa yao, hawatambui mazuri ya wenzao, wanataka sifa hata wasipostahili, wanaangalia televisheni kila siku.

Katika kuyatafakari mambo hayo, nimeona wazi matatizo ya wa-Tanzania wengi. Wengi wamo katika hili kundi la wasiofanikiwa. Tabia ya kukaa vijiweni na kulumbana kuhusu vilabu vya mpira vya Ulaya, kuhusu vituko vya mastaa, kulalamikia hili au lile, ni tabia iliyoshamiri. Muda wanaokaa vijiweni wangeweza kuutumia kwa kusoma vitabu. Lakini huwaoni wakifanya hivyo, wala nyumbani, wala maktabani. Wasipofanikiwa, hawajitathmini na kutambua dosari zao, bali wanatafuta visingizio na wachawi.

Wednesday, March 11, 2015

Video ya Kumbukumbu ya Miaka Kumi ya Kitabu

Jana, binti yangu Zawadi na mimi tulirecodi video ya kumbukumbu ya miaka kumi tangu nilipochapisha kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Hatukuwazia tungefanya shughuli hiyo jana. Tulijishitukiza bila maandalizi. Tulitayarisha kompyuta nami nikaanza kuongea. Zawadi alifanya shughuli yote ya kiufundi hadi kuiweka video katika
mtandao wa You Tube.

Katika kumbukumbu hii ya miaka kumi ya kitabu changu, napenda kuwashukuru wasomaji wangu, familia, na marafiki na wengine wote walionihamasisha kwa namna moja au nyingine.

Kwa mwezi huu wote, yeyote anayetaka kitabu hiki, popote duniani, ataweza kukipata kutoka kwangu kwa bei nafuu ya dola 12. Awasiliane nami kwa barua pepe, africonexion@gmail.com au simu (507) 403 9756. Mwisho wa fursa hii ni tarehe 31.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...