Thursday, December 21, 2023

"Chickens in the Bus" Kusomwa Shuleni Cameroon

Leo, tarehe 21 Desemba, 2023, nimepata habari ya pekee kuhusu kitabu cha Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences. Mama mmoja kutoka Cameroon aishiye hapa Minnesota, na ni mmoja wa wale ambao wamafahamu kazi zangu miezi ya karibuni, ameniambia kuwa anahitaji nakala za Chickens in the Bus kwa ajili ya kuzipeleka kwenye shule Cameroon, ambayo yeye mi mmoja wa wahusika. Amesema wanahitaji nakala 20 ili kila darasa liwe na angalau nakala tatu. 

Taarifa hii imenifanya nirudie kukipitia kwa uangalifu kitabu hiki, nijiridhishe hakina kosa lolote. Naogopa kuwapa watoto wa shule kitabu chenye kosa. Kwa mtazamo wangu, kusambaza kitabu chenye makosa ni uhalifu. Kuwapa watoto kitabu cha namna hiyo ni kosa la jinai.

Saturday, October 7, 2023

KIKAO MJINI MAPLE GROVE, MINNESOTA


Tarehe 30 Septemba, 2023, nilikwenda Maple Grove, Minnesota, kuongelea kitabu changu cha Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences. Kikao kilifanyika katika maktaba ya Maple Grove. Tulitambulishana na wale ambao hatukufahamiana. Tulibadilishana uzoefu na mawazo. 

Aliyeandaa na kuendesha kikako ni Samba Fall wa Senegal aonekanaye kulia kabisa kwenye hii picha. Yeye ni mratibu wa Multicultural Kids Network pia mjumbe katika Hennepin County Race Equity Advisory Council. Yeye na mimi tumefahaiana kwa miaka kadhaa.

Wadau walipata fursa ya kununua vitabu vyangu. Hii itachangia tafakari na maongezi yetu kuwa endelevu. Papo hapa, ndugu Samba Fall anataka vikao vya aina hii vifanyika katika maktaba zote za Hennepin County. Tumekubaliana hivyo.




Saturday, May 27, 2023

Kijitabu Hiki Kiuzwe Angalau Shilingi Milioni Moja

WaTanzania wenzangu, nimechapisha kijitabu, "Notes on 'Song of Lawino'" na sasa naleta hoja kuhusu bei yake.
Kijitabu hiki nimekiandika kutokana na jinsi ninavyoipenda fasihi. Nilipenda kuandika uchambuzi wa "Song of Lawino." Nimetumia miaka mingi kutafakari na kuandika. Ingekuwa ninalipwa kwa kila saa na siku niliyofanya hiyo kazi, ningekuwa tajiri.
Kwa maneno mengine, ingekuwa masaa yale yote na siku zile zote nimetumia kutengeneza na kuuza mkaa au kwenye ajira katika ofisi fulani, ukizingatia elimu yangu, ningekuwa nimeingiza mfukoni mamilioni ya shilingi.
Sasa kumbe matokeo ya shughuli yote hii ni kijitabu cha kurasa 70 tu. Watu watauliza bei yake ni shilingi ngapi. Ni dola 12, ambayo ni karibu shilingi 28,000. Najua kuwa wako watakaoshangaa bei hiyo kwa kijitabu cha kurasa chache.
Je, bei ya kitabu inawakilisha nini? Ndio thamani ya kitabu? Yaani tafakari yote na mawazo yote yaliyomo humu thamani yake ni hii shilingi 28,000? MTanzania akienda baa na hizi hela, atakunywa bia ngapi? Je kitabu hiki thamani yake ni sawa na hizi bia chache?
Binafsi, nakataa. Inatakiwa kitabu hiki kiuzwe angalau shilingi milioni moja. Angalau milioni moja, ukizingatia jasho nililotoa, na mikwamo niliyopitia. Niliyoandika humu nayaona kuwa ya thamani kubwa. Angalau kiuzwe milioni moja. Shilingi 28,000 ni dhuluma tupu, mchana kweupe.
Halafu, hiki ni kitabu ambacho hakitanunuliwa, labda na watu wachache sana. Huenda zisiuzwe nakala 10. Kingekuwa kitabu cha udaku, kingeuzika kwa kiasi fulani. Lakini hiki ni kitabu kikavu cha kitaaluma. Kitasota bila wateja. Hakitaniletea hela, labda visenti vichache. Ni kazi isiyo na ujira.
Mimi siandiki vitabu kwa ajili ya kupata hela. Nilitumia muda wangu wote huu kuandika hiki kitabu nikijua kuwa hakitauzika, labda nakala chache sana. Kinachonifanya niandike si pesa bali kuipenda kwangu fasihi. Nitaendelea kuandika.

 

Sunday, February 26, 2023

Mdau Kajipatia Vitabu

Jana ndugu aitwaye John Oketch kaweka picha katika ukurasa wa Facebook uitwao Africans in the United States, akiwa ameshika kitabu changu Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences. Ameambatanisha ujumbe akiwahimiza watu wajipatie nakala ya kitabu hiki. Picha hii imenivutia sana. Naona imepigwa kwa ustadi mkubwa.

>

Baadaye, ndugu Oketch aliweka hii picha nyingine, na ujumbe huu: thank you professor. I am grateful for your writing especially for my 4 kids who are born and raised in America. I have added your books to our African collection. Would you be kind to please share the link again in the reply just incase someone would like a copy.

Tafsiri: asante profesa. Nashukuru kwa uandishi wako hasa kwa ajili ya watoto wangu wanne ambao wamezaliwa na kulelewa hapa Marekani. Nimeviweka vitabu vyako katika maktaba yetu ya vitabu kuhusu Afrika. Je, unaweza, tafadhali, kuweka tena linki ya vitabu endapo kuna atakayehitaji nakala?

Nami nimeweka linki hii kwenye ukurasa ule wa Facebook.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...