Friday, January 17, 2020

Mwaliko wa African Travel Seminars

Nimepata mwaliko kutoka African Travel Seminars wa kushiriki shughuli itakayofanyika tarehe 22 Februari. Mada siku hiyo itakuwa "Celebrating Black Culture Through Travel." Kutakuwa na chakula, maonesho na michezo mbali mbali kuhusu Afrika.

Nimealikwa kuongelea kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho African Travel Seminars hutumia kwa watalii wanaoenda Afrika.

African Travel Seminars inaelimisha na kujenga mahusiano baina ya watu kupitia utalii. Hivi karibuni, tumeamua kushirikiana. Malengo ya kampuni hiyo yanafanana kwa namna fulani na ya kampuni yangu ndogo ninayojaribu kuikuza iitwayo Africonexion: Cultural Consultants.

Monday, January 6, 2020

Kitabu Kimeingia Kwenye Maktaba ya Peace Corps

Kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kimeingia kwenye maktaba ya Peace Corps iliyoko Washington DC. Mkurugenzi ameniandikia, na sehemu ya ujumbe ni hii:

We will add it to the Peace Corps library where our staff and visitors can enjoy it.

I look forward to reading more of it as I find the topic to be very relevant and important to our work. I have already begun reading it, and it has reminded me of my own experiences in Togo, West Africa. As I was reading, I was struck by the section on eye contact. I really love the verses you included from the poem by Sufi poet Ibn ‘Arabi about the veiled woman and eye contact, and I got a good chuckle at your stories of misunderstandings—as I, as well surely all of us, have had many such experiences and misunderstandings.

Kauli za mkurugenzi za kukumbuka aliyoona Afrika na kufananisha na yaliyomo kitabuni, zinafanana na kauli za waMarekani wengine waliosoma kitabu hiki baada ya kuishi Afrika. Afrika kwenyewe, kwa sasa, kitabu kinapatikana Tanzania na Kenya. Tanzania kinapatikana kutoka duka la Soma Book Cafe, lililoko Dar es Salaam, na pia duka liitwalo A Novel Idea, lililoko Dar es Salaam na Arusha. Kenya kinapatikana katika duka la Bookstop katika Yaya Center Mall, Nairobi.

Tuesday, December 17, 2019

Kofia ya CCM Nchini China

Naleta picha ya ujumbe wa CCM kwenye kikao na wenyeji wao mjini Shanghai, China, mwaka 2018. Hapo mezani upande wa kushoto kuna kofia ya CCM. Yawezekana walikwenda ziarani na magwanda yao na vikofia. Je, kuna sababu gani mimi kuandika ujumbe kuhusu kofia? Sina jambo la maana zaidi la kuongelea? Kwa nini nisiongelee madhumuni ya ziara na mafanikio yake?

Ninaandika ujumbe huu kama mtafiti, mwandishi, na mtoa ushauri juu ya masuala ya utamaduni na utandawazi. Nimekuwa nikifanya shughuli hizo hapa Marekani na Tanzania pia, ambako nimeendesha warsha mara kadhaa kuanzia mwaka 2008 katika miji ya Arusha, Tanga, na Dar es Salaam.

Ninajaribu kuwaelewesha watu kuwa tofauti za tamaduni zina athari kubwa, hasa katika dunia ya utandawazi wa leo. Tunapokutana na watu wa tamaduni tofauti na wetu, tuwe makini. Tunaweza tukaelewana vibaya, au tunaweza tusielewane. Ni muhimu tujielimishe kuhusu tofauti hizo kabla hayajatupata hayo.

Kofia ya CCM ni sehemu ya vazi rasmi la wana CCM. Ni utambulisho wao. Hata mimi ambaye sina chama ninawatambua kwa mavazi yao. Vyama vingine navyo vina mavazi yao. Kwa hapa nchini Tanzania, hakuna utata juu ya hayo mavazi. Lakini je, hali ni hiyo hiyo nje ya Tanzania kwenye tamaduni tofauti?

Nchini China, kofia ya kijani ni mkosi. Mwanaume kuvaa kofia ya kijani maana yake anatangaza kwamba mke wake ni mzinzi.

Kuhusu asili ya tafsiri hii ya waChina kuhusu kofia ya kijani, maelezo yanatofautiana. Baadhi ya maelezo ni kwamba zamani za kale, ndugu wa malaya walilazimishwa kuvaa kofia ya kijani wabebe aibu. Maelezo mengine ni kwamba zamani za kale, wahudumu katika madanguro walikuwa wanavaa kofia za kijani. Lakini kama nilivyogusia, maelezo yanahitilafiana. Ila jambo ambalo halina utata ni kwamba katika utamaduni wa China, kofia ya kijani ni mkosi kwani inatangaza habari ya uzinifu wa mke.

Sasa fikiria hiyo ziara ya ujumbe wa CCM China. Wafikirie wako sehemu mbali mbali kama wageni rasmi, wamevalia kofia za kijani. Bila shaka, wenyeji wao walifanya ukarimu na heshima kama ilivyo desturi. Lakini bila shaka, makada hao wa CCM watakuwa wameacha gumzo na taswira ambayo hawakutegemea.

Katika warsha ambazo nimeandaa Tanzania tangu mwaka 2008, waTanzania wachache sana wamekuwa wakihudhuria. Mbali ya warsha, nimekuwa nikielezea katika blogu zangu masuala ya athari za tofauti za tamaduni katika dunia ya utandawazi wa leo. Nimeandika hata kitabu, kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho kinapatikana Tanzania pia, kutoka katika maduka ya Kimahama (Arusha), Soma Book Cafe (Dar es salaam), na A Novel Idea (Arusha na Dar es Salaam).

Pamoja na kujaribu njia zote hizo, nimeona kuwa labda, kwa kuandika ujumbe huu kuhusu kofia ya CCM nchini China, waTanzania watanielewa vizuri na watachukua hatua stahiki katika masuala yote husikka, iwe ni mahusiano binafsi, biashara za kimataifa, utalii, diplomasia na kadhalika.

Thursday, December 5, 2019

Maongezi Kuhusu Fasihi Simulizi ya Africa

Jana jioni, kwa mwaliko wa chama cha wanafunzi kiitwacho Karibu, nilitoa mhadhara hapa chuoni St. Olaf kuhusu fasihi simulizi ya Afrika. Tuna wanafunzi wachache kutoka Afrika, lakini wanajitahidi kuitangaza Afrika kwa namna mbali mbali, kama vile mihadhara, filamu, ngoma, muziki, michezo ya kuigiza, na maonesho ya mavazi.

Mara kwa mara wananialika kuelezea utamaduni wa Afrika, hasa unavyojitokeza katika fasihi simulizi. Nami hupenda kufanya hivyo. Ninauenzi mchango wa Afrika duniani. Afrika ni chimbuko la binadamu. Ni chimbuko la tekinolojia, sayansi, lugha, fasihi, falsafa, na kadhalika.

Hiyo jana nilelezea hayo, nikaleta methali kadhaa kuthibitisha uzito wa falsafa ya wahenga wetu kuhusu masuala ya maisha na maadili. Tulitafakari methali hizo, na mwishoni nilisimulia hadithi iitwayo "The Donkey Who Sinned," iliyomo katika kitabu cha Harold C. Courlander kiitwacho A Treasury of African Folklore. Nayo tuliitafakari, kwa jinsi inavyoonyesha athari za ubabe kwa wale wasio na nguvu. Katika hadithi hiyo, wenye mabavu wanaogopwa hata pale wanapokosea, na asiye na nguvu anadhulumiwa.

Saturday, November 30, 2019

Wadau wa Utalii wa Kielimu Tumekutana

Tarehe 2 Novemba nilikutana na mama Georgina, ambaye anatoka Ghana na ni mmiliki wa kampuni iitwayo African Travel Seminars. Anapeleka wasafiri kwenda nchi za Afrika, kuanzia kaskazini, hadi kusini, mashariki hadi magharibi, na Tanzania imo. Mbali ya kuwaonesha vivutio vya utalii, anawaelimisha kuhusu maisha na tamaduni za waAfrika.

Niliifahamu kuhusu kampuni yake kuanzia miaka ya tisini na kitu, nikaona jinsi shughuli zake zinavyofanana na zangu, ambazo zimeelezwa katika tovuti ya Africonexion. Hivi karibuni nilianza kuwasiliana na huyu mama, na tukapanga kukutana.

Kabla hatujakutana, mama huyu alisoma kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Ameamua awe anawapa wageni anaowapelea Afrika. Yeye nami tunafahamu kuwa hii itawawezesha wageni kuelewa mwenendo na tabia za waAfrika na pia kujielewa namna wao wenyewe wanavyoeleweka kwa mtazamo wa waAfrika.

Tumejithibitishia kuwa malengo yetu yanafanana. Tunapenda kuendeleza elimu kuhusu Afrika kwa waMarekani na tunapenda kujenga maelewano baina ya waMarekani na waAfrika. Yeye nami tuna uzoefu wa kuongelea masala haya hapa Marekani, kwa wanafunzi na walimu, watu wanaoenda Afrika kwa shughuli za kujitolea, watalii, nakadhalika.

Thursday, November 14, 2019

Kijana Msomali Amekipenda Kitabu Hiki

Jana, nilikuwa posta hapa chuoni nikipata huduma. Ghafla nikasikia kwa nyuma ninaitwa, "Professor Mbele!" Nilipinduka nikamwona kijana mmoja, mwanafunzi wetu mSomali ananisogea. Aliniambia amesoma kitabu changu, akimaanisha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Nilifurahi, ila sikujua nimwambie nini, ila aliongezea kuwa alitamani kipatikane kama "audio book" ili mama yake aweze kusikiliza. Niliguswa sana, kwa sababu ninaelewa hali ya waSomali hapa Minnesota na Marekani kwa ujumla.

Wako wengi sana, wakimbizi au wahamiaji kutoka nchini kwao. Jimbo hili la Minnesota lina idadi kubwa ya waSomali kuliko sehemu nyingine duniani ukiachilia mbali Somalia yenyewe.

Ninafahamu pia kuwa waSomali hawakuwa na jadi ya maandishi. Utamaduni wao ni wa masilimuzi. Walipata mwafaka wa namna ya kuandika lugha yao mwaka 1972. Watu wazima wengi hawajui kuandika na kusoma, na wazee ndio kabisa.

Wote hao wako hapa Marekani, ambapo utamaduni ni wa maandishi. Ninafahamu changamoto zinazowakabili, kwani nina uzoefu katika masuala yao, ikiwemo fasihi simulizi na elimu. Kijana huyu alivyoniambia kuhusu mama yake, niliguswa sana. Nimeshampelekea ujumbe rafiki yangu mSomali kumwelezea suala hilo. Huyu tulishaongelea kutafsiri kitabu changu kwa kiSomali. Nimemwambia kuwa kutokana na kauli ya huyu kijana ya kutaka mama yake asome kitabu hiki, inabidi tukamilishe tafsiri halafu irekodiwe kama "audio book." Itachukua muda, lakini hii si hoja.