Tuesday, December 25, 2012

Milima Haikutani

Wa-Swahili husema, milima haikutani bali binadamu hukutana. Hayo yalinipata mjini Karatu mwaka 2008 nilipokutana na mzee ambaye anaonekana nami pichani.

Siku hiyo ilikuwa siku ya mnada mjini Karatu, siku ambayo hutokea mara moja kwa mwezi. Katika umati mkubwa wa watu, yeye na mimi tulijikuta uso kwa uso. Yeye alinitambua mara moja, akauliza: "Profesa Mbele?" Nilimwambia ndio mimi. Tulifurahi sana, tukaanza michapo.

Mzee huyu nilimfahamu mwaka 1996 wakati nafanya utafiti wa masimulizi ya jadi kuhusu shujaa wa wa-Iraqw aitwaye Saygilo Magena. Utafiti huu ulinipeleka kwenye miji na vijijini kama vile Mbulu, Mamaisara, na Karatu.

Kati ya watu walionisaidia sana ni huyu mzee ambaye jina lake ni John Qamlali. Baada ya kufahamiana kule Mbulu, tulikutana tena mjini Arusha, tukaongea sana. Anajua sana habari za wa-Iraqw na ameshawasaidia watafiti wengine wa mataifa mbali mbali. Ninazo kanda za maongezi yetu.

Kukutana tena mwaka 2008, miaka zaidi ya kumi tangu tulipokutana mara ya kwanza, ilikuwa ni ajabu na pia jambo la kushukuru.

Maaskofu Watoa Tamko Juu Ya Masuala Mbali Mbali

TANZANIA CHRISTIAN FORUM (TCF) MKUTANO MKUU WA NNE WA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA (TCF)

TAMKO RASMI “ATUKUZWE MUNGU JUU MBINGUNI, NA DUNIANI IWE AMANI KWA WATU ALIOWARIDHIA”

Utangulizi Katika Mkutano Mkuu wa Nne wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, Tanzania Christian Forum – TCF, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano na Mafunzo cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Kurasini jijini Dar es Salaam, tarehe 6 Desemba, 2012; Wajumbe walitafakari kwa undani juu ya kuzorota kwa mahusiano baina ya Dini mbili za Ukristo na Uislamu nchini Tanzania, pamoja na kutathmini juu ya wajibu wa Kanisa na Utume wake wa Kinabii kwa taifa letu.

Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) linajumuisha taasisi kuu za Umoja wa Makanisa nchini kama ifuatavyo;- Jumuiya ya Kikristo Tanzania - CCT Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania - TEC Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania - PCT Kanisa la Waadventisti Wasabato – SDA (observers)

Tafakari Tafakari yetu ilianza kwa kujiuliza yafuatayo:

1. Ni mwenendo gani uliotusibu hivi karibuni kusababisha kukutana kwetu hapa? Vikundi vya kihalifu vikiongozwa chini ya mwavuli wa waamini wa Kiislamu vimekuwa vikishambulia kwa ukali na kikatili sana imani, mali, majengo na makanisa ya Wakristo kwa jeuri na kujiamini.

2. Kwa mwenendo huo ni kitu gani kilicho hatarini? Vitendo na mienendo yote ya namna hiyo inahujumu sana Amani, Mapatano na Uelewano kati ya watu wote nchini mwetu. Tunaelewa kwamba ni waamini wachache tu wenye kutenda maovu hayo, lakini mienendo ya kikatili ya namna hii huchochea shari miongoni mwa walengwa wa ukatili husika na kutaka kulipiza kisasi hata kusababisha uvunjifu wa amani.

3. Ni athari gani kwa nchi, katika muda ujao, iwapo mienendo hiyo haitadhibitiwa na kukomeshwa kabisa?

Katika nyakati zetu hizi, tunashuhudia fadhaa na migogoro mingi ya kijamii. Kuna hasira kubwa ya chinichini inayotokana na kasoro nyingi za kiutendaji katika mihimili mikuu ya uongozi na utando mkubwa wa ufukara wa kutupwa kwa wananchi wengi usio na matumaini ya kumalizika hivi karibuni. Hatari ya hali hii ni dhahiri kwamba makundi nyemelezi (kisiasa, kiuchumi na kidini), kwa kutumia vikundi halifu vilivyo katika hali ya ufukara na migogoro, yatavielekeza kimapambano na kiharakati kutetea kijeuri ajenda hasimu za wale walio madarakani au washindani wao kwa maslahi ya wanyemelezi. Hali tunayoelezea sio ya kufikirika kwani ndiyo inayotokea huko nchini Nigeria, Kenya na nchi za Afrika ya Kaskazini hivi sasa. Tanzania haina kinga ya kipekee kuiepusha kukumbwa na maovu ya namna hiyo bila utaratibu na vyombo thabiti kuhimili mienendo hasi kama hii. Kutokana na matukio na kauli zinazotolewa na watu mbalimbali hapa nchini, inawezekana tayari wanyemelezi wako kazini wakiongoza vikundi kusukuma ajenda za kutekeleza maslahi yao.

4. Masuala yanayotakiwa kufafanuliwa na kudhibitiwa na Dola mapema ili yasiendelee kupotoshwa:

Hali ya mahusiano kuzorota pamoja na kashfa dhidi ya Kanisa.

Huu ni wakati wa kukubali kwamba misingi ya Haki, Amani na Upendo katika Taifa letu imetikiswa kwa kiwango kikubwa. Uchochezi, kashfa, matusi na uchokozi wa wazi na makusudi unaofanywa na baadhi ya waamini wa dini ya Kiislamu, ukiendeshwa na kuenezwa kupitia vyombo vyao vya habari vya kidini (redio na magazeti) mihadhara, kanda za video, CD, DVD, vipeperushi, makongamano, machapisho mbalimbali na kauli za wazi za viongozi wa siasa na hata viongozi wa dini husika (ushahidi wa mambo yote haya tunao) pasipo Serikali kuchukua hatua yeyote huku bali imekuwa ikibakia kimya tu. Ukimya huu unatoa taswira ya Serikali kuunga mkono chokochoko hizi. Jambo hili linavyoendelea kuachwa hivi hivi linaashiria hatari kubwa ya kimahusiano siku zijazo.

Hadhi ya Baba wa Taifa kuhifadhiwa.

Huyu ni kiongozi aliyetoa maisha yake kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu akitetea Watanzania wote bila ubaguzi wowote, akiimarisha umoja wa Kitaifa, amani na upendo kwa watu wote. Kashfa, kejeli na habari za uongo dhidi yake ni kukipotosha kizazi hiki na hata vizazi vijavyo kwa kuondoa moja ya alama muhimu ambazo kiongozi huyo alisimamia kwa ajili ya umoja wa kitaifa.

“Memorandum of Understanding” (M.o.U) ya mwaka 1992, kwa ajili ya huduma za kijamii zitolewazo na Makanisa kwa Watanzania wote, ikiwa ni pamoja na huduma za hospitali, vituo vya afya na zahanati na shule mbalimbali zinazoendeshwa na Makanisa nchini kote. Ni vema ikaeleweka wazi kwamba makubaliano hayo (M.o.U) yalikuwa ni kati ya Makanisa ya Tanzania na Makanisa ya nchini Ujerumani ambapo Serikali ya Tanzania ilihusishwa tu, kwa vile raia wake ndio wangenufaika na misaada hiyo ambayo nchi ya Ujerumani ingeitoa kupitia Makanisa hayo. Kanisa limeendelea kujishughulisha na huduma hizi kwa jamii hata kabla ya uhuru na baada ya uhuru pasipo ubaguzi. Ikibidi ni vema kuondoa hali hii, ya Kanisa kuendelea kutukanwa, chuki na kukashifiwa viongozi wake kutokana na huduma hizi kwa jamii yote. Jukwaa la Wakristo Tanzania tunaitaka Serikali itoe tamko la ufafanuzi juu ya M.o.U hiyo, maana yake, makusudi yake na manufaa yake kwa Watanzania wote.

Hujuma ya kuchomwa Makanisa na mali za Kanisa, ni tukio la uvamizi na uchokozi wa wazi, ulioyakuta makanisa yetu na waamini wake wakiwa hawana habari na bila maandalizi yoyote. Ni muhimu kuanzia sasa, Wakristo wote wakae macho na wawe waangalifu zaidi.

Dhana ya kuwa Tanzania inaendeshwa kwa mfumo Kristo ni potofu na potevu.

Maneno hayo ni ushahidi wa uwepo wa ajenda za waamini wenye imani kali na waliojiandaa kwa mapambano maovu kutetea dhana potovu kinzani na misingi ya demokrasia na haki za binadamu kama ilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa na kuridhiwa na Serikali yetu. Jukwaa la Wakristo nchini tunakanusha wazi wazi na kueleza bayana kuwa, nchi hii haiongozwi kwa mfumo Kristo!. Kwa watu walio makini hakuna kificho kuwa viongozi wote waandamizi wa ngazi ya juu Serikalini awamu ya sasa, asilimia 90 ni Waislamu (Rais wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu, Makamu wa Rais, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Jaji Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi). Kwa mantiki hiyo haiingii akilini kueleza watu kuwa nchi hii inaendeshwa kwa mfumo Kristo! Kwa upande wa Zanzibar asilimia 100 ya viongozi ngazi za juu Serikalini ni Waislamu, na sio kweli kwamba Zanzibar hakuna Wakristo wenye sifa za kuongoza. Kisha, hata uwakilishi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, theluthi mbili ya wajumbe wake ni Waislamu. Tunayo mifano mingine mingi iliyo wazi, na hii ni baadhi tu. Watanzania wanapaswa kuelewa wazi kuwa, nchi hii inaongozwa kwa misingi ya Utawala wa Kisheria na sio vinginevyo.

Matumizi hasi ya Vyombo vya Habari vya Kidini:

Vyombo vya habari vya kidini vinatumiwa na viongozi wa dini ya Kiislam kuukashifu Ukristo na kuwachochea Waislamu hadharani kupitia vyombo hivyo wakiwataka wawaue Maaskofu na Wachungaji, iwe kwa siri au hadharani. Japo Serikali imesikia kashfa na uchochezi huo hatarishi, imendelea kukaa kimya, na kuwaacha wachochezi hao wakiendelea kuhatarisha amani bila kuwadhibiti. Jambo hili linatia mashaka makubwa juu ya umakini wa Dola kuhusu usalama wa wananchi nchini mwao. Imani kali za namna hii huchochea vitendo viovu vya uasi na hujuma sio tu dhidi ya waamini na viongozi wa dini fulani, bali hata na kwa Serikali na viongozi waliopo madarakani, endapo waamini wa dini fulani katika taifa kama Tanzania lililo na waamini wa dini nyingi tofauti, hawataheshimu na kutendeana kiungwana baina yao na wale wasio wa dini na mapokeo yao. Hali hii inapelekea kujiuliza kama je,huu ni wakati mwafaka kwa kila raia au kiongozi wa dini kujilinda yeye mwenyewe na waamini wake dhidi ya wenye imani kali?

Matukio yanayosababisha hasira na kutenda maovu:

Tumejionea matukio kadhaa ambayo kwayo vikundi vya watu wenye hasira vilisababisha hujuma na uharibifu mkubwa wa mali za watu wengine. Hivyo ni viashiria tosha vya uchovu na unyonge mkubwa katika jamii yetu, ambamo jambo dogo tu na hata la kupuuzwa, likitendwa na afikiriwaye kuwa hasimu wa watu fulani, wahalifu hujipatia fursa ya kuonesha hasira yao kwa vitendo vya hujuma na shari, wakiharibu hata kuteketeza mali na nyenzo za maisha ya jamii. Suala hili lataka uchambuzi yakinifu na wa kiroho ili kupata majibu na maelezo sahihi na wala sio kwa kutumia nguvu za ziada za kijeshi au kwa majibu mepesi ya kisiasa. Hili ni suala lihusulo tunu na maadili ya jamii yote ya Watanzania katika ujumla wao. Kila mmoja wetu ni mhusika na sote tukitakiwa kuwajibikiana katika ujenzi wa amani iletayo mapatano na uelewano kati yetu.

Mapendekezo: Kutokana na muono wetu huo tunapendekeza yafuatayo:

Tabia na mienendo ya kukashifiana ikomeshwe kabisa na badala yake tujengeane heshima/staha tukizingatia utu wa kila mmoja katika utofauti wetu.

Tumwendee Mungu wetu na kumwomba atuongoze sote kufuata utashi wake tukitafuta huruma yake iliyo sheheni upendo wake mkuu, ili atujalie umoja wa kuishi pamoja kwa amani nchini mwetu.

Tunaitaka Serikali yetu na vyombo vyake vya usalama, sheria na amani kutenda mara moja na bila kuchelewa, katika nyakati ambazo vikundi halifu kisiasa au kidini vinapoanza uchochezi ili kupambanisha wanajamii. Tabia ya kuachia uchochezi wa kidini kuendelea pasipo hatua mathubuti kuchukuliwa na Dola ni udhaifu mkubwa wa uongozi na uwajibikaji. Ikithibitika kwamba uharibifu uliofanywa ulitokana na kikundi mahususi chini ya uongozi wa dini au chama cha kisiasa au asasi isiyo ya kiserikali, basi taasisi husika iwajibishwe na kulipa fidia kwa uharibifu uliofanywa.

Lianzishwe Baraza mahsusi lililo huru lisiloegemea chama chochote cha kisiasa wala dini yoyote na litamkwe na kuwezeshwa kikatiba likiwa na dhumuni kuu la kuilinda na kuiongoza Serikali kuto fungamana na dini yoyote na kuhakikisha kwamba dira na dhana ya utu katika mfumo wa uchumi wenye kujali maslahi ya wote havipotoshwi. Baraza hilo liwe na uwezo wa kuvichunguza vyombo vya sheria na usalama itokeapo matatizo makubwa yaashiriayo uvunjifu wa haki na kuteteresha usalama wa nchi.

Na sisi viongozi wa dini za Kikristo, Kiislam, Kihindu na nyinginezo tuwajibike katika kufundisha, na katika majiundo ya waamini wetu, hasa vijana, ili kuwajengea uelewa na utashi wa kuvumiliana kwa upendo. Katika kushuhudia na kuadhimisha imani na ibada zetu sote tutambue , tulinde na kukuza maadili, tunu na desturi za imani za watu wengine wanazo ziheshimu na kuzitukuza. Vikundi vya imani kali na pambanishi kwa kutumia kashfa potoshaji sharti vidhibitiwe kwa weledi mkubwa wa viongozi wa dini husika wakisaidiana na usalama wa taifa. Stahamala [kustahimiliana] ni fadhila inayopaswa kufundishwa na kupenyezwa katika mifumo ya uongozi na maisha ya jamii na ihifadhiwe kwa kufuatiliwa kwa karibu sana.

Hitimisho: Kwa sasa Kanisa liko katika vita vya Kiroho, hivyo ni vyema Waamini wote wakakumbuka kuwa, katika mapambano kama hayo Mungu mwenyewe, Mwenye enzi yote ndiye mlinzi wa watu wake na Kanisa lake. JIBU LITAPATIKANA TU, KWA NJIA YA SALA, KUFUNGA NA MAOMBI!

Hivyo siku ya Jumanne tarehe 25 Desemba 2012, inatangazwa rasmi nchini kote kuwa siku ya sala na maombi kwa Wakristo wote na Makanisa yote nchini, pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuomba kwa imani, amani katika nchi yetu, na kumkabidhi Mungu ashughulikie mipango yoyote iliyopo, ya wazi na ya kisirisiri ya kutaka kuondoa amani ya taifa hili na kuyashambulia Makanisa nchini Tanzania ishindwe na kuanguka pamoja na wale wote walio nyuma ya mipango hiyo.

1. Askofu Bruno Ngonyani (TEC) - Mwenyekiti
2. Askofu Dkt. Israel Mwakyolile (CCT) - Mjumbe (Mwenyekiti Mwenza)
3. Askofu Daniel Aweti (PCT) - Mjumbe (Mwenyekiti Mwenza)
4. Askofu Oscar Mnung’a (CCT) - Mjumbe
5. Askofu Elisa Buberwa (CCT) - Mjumbe
6. Askofu Stephen Mang’ana (CCT) - Mjumbe
7. Askofu Dkt. Peter Kitula (CCT) - Mjumbe
8. Askofu Alinikisa Felick Cheyo (CCT) - Mjumbe
9. Askofu Christopher Ndege (CCT) - Mjumbe
10. Askofu Michael Hafidh (CCT) - Mjumbe
11. Askofu Charles Salala (CCT) - Mjumbe
12. Askofu Dismus Mofulu (CCT) - Mjumbe
13. Mchg. Conrad Nguvumali (CCT) - Mjumbe
14. Mchg. Ernest Sumisumi (CCT) - Mjumbe
15. Mchg. William Kopwe (CCT) - Mjumbe
16. Askofu Thaddaeus Ruwa’ichi (TEC) - Mjumbe
17. Askofu Paul Ruzoka (TEC) - Mjumbe
18. Askofu Norbert Mtega (TEC) - Mjumbe
19. Askofu Severine Niwemugizi (TEC) - Mjumbe
20. Askofu Michael Msonganzila (TEC) - Mjumbe
21. Askofu Castorl Msemwa (TEC) - Mjumbe
22. Askofu Eusebius Nzigilwa (TEC) - Mjumbe
23. Askofu Renatus Nkwande (TEC) - Mjumbe
24. Askofu Bruno Ngonyani (TEC) - Mjumbe
25. Fr. Antony Makunde (TEC) - Mjumbe
26. Fr. Sieggried Rusimbya (TEC) - Mjumbe
27. Fr. Ubaldus Kidavuri (TEC) - Mjumbe
28. Askofu Dkt. Paul Shemsanga (PCT) - Mjumbe
29. Askofu Ability Samas Emmanuel (PCT) - Mjumbe
30. Askofu Nkumbu Nazareth Mwalyego (PCT) - Mjumbe
31. Askofu Batholomew Sheggah (PCT) - Mjumbe
32. Askofu Dkt. Mgullu Kilimba (PCT) - Mjumbe
33. Askofu Renatus Tondogosso (PCT) - Mjumbe
34. Askofu Emmanuel Mhina (PCT) - Mjumbe
35. Askofu O.S. Sissy (PCT) - Mjumbe
36. Askofu Jackson Kabuga (PCT) - Mjumbe


CHANZO: Mjengwa Blog

Monday, December 24, 2012

Shaaban Robert na Nyerere: Waandishi Muhimu kwa Kila m-Tanzania

Kwa miaka michache iliyopita, wakati nimejitosa katika kusoma maandishi ya Shaaban Robert, nimejiwa na mawazo mbali mbali ambayo naona ni muhimu. Kwa bahati nzuri, nimechapisha makala mbili juu ya Shaaban Robert, moja katika Encyclopedia of African Literature, na nyingine katika CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Napenda kunukuu machache niliyoandika katika Encyclopedia of African Literature:

Shaaban Robert displayed profound awareness of the human condition; he opposed injustice, championed freedom, and extolled the dignity of labour. He was sensitive to the condition of women. He wrote poems celebrating women, and a biography of Siti Binti Saad, the famous female taarab singer, recounting the meteoric rise to fame of this woman from a humble rural background in a male-dominated world which put incredible obstacles in her path. He was proud of his Swahili language and culture, which he understood very well, appropriated, and celebrated in and through his writings. However, he deeply respected other languages and cultures and appropriated whatever he could from them. If colonialism had not limited his educational opportunities, he would have explored this dimension to the fullest. He greatly admired world writers like Shakespeare, whose artistic mind he described as a great ocean whose waves touched the shores of the whole world....[Shaaban] Robert's poetic sensibility was deep and intertwined with his moral and ethical principles. Sensitive to the condition and plight of all creatures, he held that all things moved with the rhythm of poetry: the birds, streams, the sea, the wind and the thunderstorms, the seasons....His vision of a just society was part of the shaping of the dream for an egalitarian society, which became his country's policy. (p. 463)

Katika kusoma na kutafakari maandishi ya Shaaban Robert, ilifikia wakati nikajenga wazo kuwa kuna uwiano mzito baina ya mafundisho ya Shaaban Robert na yale ya Mwalimu Nyerere. Wakati Nyerere anaongelea sana masuala ya siasa, uchumi, nadharia mbali mbali kuhusu jamii na maendeleo yake, Shaaban Robert aliongelea masuala ya aina hiyo hiyo kwa kutuingiza katika hisia na mahusiano baina ya binadamu na binadamu mwenzake.

Kama Nyerere, Shaaban Robert alikuwa mchambuzi wa jamii na mwanafalsafa, lakini aliongelea masuala kwa kutumia wahusika maalum na matendo na masahibu yao, na hivi kutugusa moja kwa moja. Ningekuwa na madaraka ya kuamua masuala ya mfumo wa elimu Tanzania, ningehakikisha kuwa Shaaban Robert na Nyerere wamekuwa nguzo ya elimu ya kila m-Tanzania.

Friday, December 21, 2012

Habari Njema: Kitabu cha "Hemingway and Africa" Kimefika

Leo nina furaha sana. Kisa? Kitabu nilichoagiza, Hemingway and Africa, kimefika leo.

Kila ninapojipatia kitabu kipya ninafurahi. Ukizingatia kuwa hadi sasa nina vitabu zaidi ya elfu tatu, utaona kuwa nimekuwa mwenye furaha, tena na tena. Huenda nitaishi miaka kadhaa ya ziada kutokana na hiyo furaha.

Pamoja na hayo yote, hiki kitabu cha Hemingway and Africa ni cha pekee. Mwanzo kukiona ni pale nilipokiazima kutoka maktaba ya Chuo Kikuu cha Minnesota, nikakisoma. Kilinigusa kwa namna ya pekee, kwa jinsi kilivyosheheni taarifa na uchambuzi mpya, nikaamua lazima niwe na nakala.

Kama unavyoniona pichani, nimekishika kitabu hiki nikiwa nimefurahi sawa na mtu aliyejishindia kreti ya bia. Ninataja bia kwa makusudi. Kitabu hiki, chenye kurasa 398, bei yake ni dola 80 ambayo kwa madafu ni zaidi ya 120,000. Ukienda baa na hela hizo, unapata kreti mbili za bia, kuku mzima, na nauli ya teksi ya kukurudisha kwenu Mbagala. Kama wewe si mtu wa baa, hizo hela ni mchango tosha wa sherehe kama vile "send-off."

Sasa inakuwaje Krismasi yote hii mtu ufurahie kitabu cha bei mbaya, badala ya kujichana na bia? Ukweli ni kwamba kila mtu ana udhaifu wake. Udhaifu wangu mojawapo ni kuvipenda sana vitabu.

Kuhusu mwandishi Hemingway, ni kwamba kwa miaka na miaka nimekuwa msomaji na shabiki mkubwa wa maandishi yake: kuanzia riwaya na hadithi fupi, hadi insha na barua. Nayapenda kwa namna ya pekee maandishi yake yanayohusu uhusiano wake na Afrika, kwani alitembelea na kuishi miezi mingi Afrika Mashariki, hasa Kenya na Tanganyika. Aliandika kuhusu mazingira ya nchi hizo, kuhusu watu na tamaduni zao, na kuhusu wanyama katika mbuga za hifadhi, kwa kiwango cha ustadi ambacho sisi wenyewe hatujakifikia. Alituachia hazina kubwa katika maandishi yake, hazina ambayo hatujafunguka macho na kuitumia.

Monday, December 17, 2012

Hongera JWTZ Kwa Kufungua Maktaba


Nimevutiwa sana na taarifa juzi kuwa Rais Kikwete, Amiri Jeshi wa Tanzania, amefungua maktaba ya kisasa kwenye chuo cha mafunzo cha Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Monduli. Ni habari njema kabisa.

Mimi ni mdau mkubwa wa maktaba na katika blogu hii ninaziongelea mara kwa mara. Mifano ni maktaba za TangaDar es SalaamSongeaLushotoMoshiIringa, na Southdale.

Kwa miaka mingi sijawahi kusikia rais au kiongozi mwingine wa kitaifa Tanzania akifungua maktaba, ukiachilia mbali tarehe 9 Desemba, 1967, ambapo Mwalimu Nyerere alifungua Maktaba Kuu ya Taifa, Dar es Salaam.

Pita katika maktaba yoyote Tanzania, utaona kuwa maktaba ni kitu ambacho wa-Tanzania hawakithamini sana, isipokuwa labda wanafunzi. Na hao wanafunzi wanaonekana maktabani endapo wamebanwa sana na mwalimu au wanakabiliwa na mitihani.

Wakaazi wa Tanga, kwa mfano, wamekuwa na bahati ya kuwa na maktaba tangu mwaka 1958, kabla ya Uhuru. Ingebidi wawe juu kabisa kitaifa kwenye suala la elimu. Lakini wapi, ukiingia katika maktaba ile, hutawaona. Je, unadhani kuwa ukimwuliza mkaazi wa Arusha au Songea akuonyeshe maktaba iko wapi, ataweza kukuambia? Jaribu uone.

Tanzania tumezoea kusikia kuhusu ufunguzi wa baa, sio maktaba. Kama unafungua baa maarufu, unaweza kabisa kumleta waziri akawa mgeni rasmi. Kutokana na utamaduni huo, kitendo cha JWTZ cha kufungua maktaba ya kisasa ni cha pekee. Ni kitendo kinacholeta matumaini kuwa labda tutashtuka na kuelewa umuhimu wa maktaba. Natoa pongezi kwa JWTZ.

Sunday, December 16, 2012

Serikali Yapongeza Kuanzishwa Kitivo cha Udaktari Songea

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Said Mwambungu akisalimia wananchi baada ya kuwasili Peramiho. Kushoto kwake ni ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Norbert Mtega akifuatiwa na Mratibu wa Kitivo cha Udaktari Peramiho Chuo cha Mt Augustino Tawi la Songea Padre Dunstan M. Mbano
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Said Mwambungu akikagua maeneo ya kitivo cha udaktari Peramiho. Kushoto kwake ni Joseph Joseph Mkirikiti na kulia kwake ni ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Norbert Mtega akifuatiwa na Mratibu wa Kitivo cha Udaktari Peramiho Padre Dunstan MbanoMkuu wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Said Mwambungu akielekezwa jambo na ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Norbert Mtega.

Jengo la utawala ambalo bado halijaanza kutumika
Jengo la hosteli ya wanafunzi ambalo bado halijaanza kutumika
Jengo la Maabara Kitivo cha Udaktari Peramiho baada ya ukarabati ambalo bado halijaanza kufanya kazi kutokana na ukosefu wa vifaa vya kufundishia

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Said Mwambungu akihutubia wananchi wa Peramiho
Serikali imepongeza uamuzi wa Chuo Kikuu cha Mt Augostino Tanzania kuanzisha kitivo cha udaktari katika kituo chake cha Songea. Hayo yalisemwa jana tarehe 15.12.2012 na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma ndugu Said Thabit Mwambungu alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya chuo hicho kilicho katika eneo la Peramiho.  Amesema kuanzishwa chuo hicho ni ukombozi kwa Mkoa wa Ruvuma ambao awali haukuwa na vyuo vya elimu ya juu.

“Kuanzishwa kwa chuo cha Tiba ni lulu kwa mkoa wa Ruvuma kwa vile kitapunguza usumbufu kwa wananchi wa ukanda huu ”alisema Mwambungu.

Aidha, akijibu risala ya chuo kuhusu tatizo la ardhi kwa ajili ya upanuzi wa eneo la chuo, Mwambungu amewataka watendaji walio chini yake wakae na uongozi wa chuo kwa ufumbuzi. Alisisitiza kuwa anaamini liko ndani ya uwezo wao.

“Watendaji kuanzia kijiji kaeni na viongozi wa chuo kupata ufumbuzi wa tatizo hili nanaamini hata likiwashinda, ofisi ya Mkuu wa Wilaya itawasaidia” alisema ndugu Mwambungu.

Akizungumzia tatizo la maji, amekemea tabia ya wananchi kuharibu mazingira na vyanzo vya maji na kusababisha tatizo la maji. Amewataka wananchi waache tabia hii mara moja. Akifafanua zaidi amewataka viongozi wa dini waisaidie serikali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tatizo la uharibifu wa mazingira na athari zake.

“Nawaomba viongozi wa dini mzungumze na waumini wenu kuhusu tatizo hili wakati serikali inasimamia sheria kuhusu waharibifu na uharibifu mazingira” Alisema Mwambungu.

Kwa upande wa umeme alisema watakaa na pande zote zinazohusika ili kupata ufumbuzi kwa vile linaigusa serikali pia.

Awali mratibu wa Kitivo cha Udaktari Peramiho Chuo cha Mtakatifu Agustino Tawi la Songea Padre Dunstan M. Mbano alisema Padre Mbano alisema chuo kina wanafunzi 39 wa mwaka wa kwanza wanaosoma masomo ya udaktari ambao wamelazimika kupelekwa kwa muda katika Chuo cha Ifakara-Morogoro kilicho chini ya Chuo Mama cha Mtakatifu Augustino wakisubiri kukamilika kwa miundo mbinu. Alisema, hata hivyo, wanafunzi hawa kiutawala bado wako chini ya Chuo Kikuu cha Mt Augustino Kituo cha Songea. Alisema Kituo cha Songea kilizinduliwa Novemba mwaka 2011 na kina jumla ya wanafunzi 631. Wanafunzi wa shahada ya kwanza ualimu kwa mwaka wa kwanza na wa pili ni 592 na wanaosoma udaktari ni 39.


Padre Mbano alisema ujenzi wa chuo umegawanyika katika awamu tatu. Awamu ya kwanza ilihusu ukarabati wa majengo ya iliyokuwa hospitali ya wakoma, nyumba ya Mkuu wa Chuo, jengo la utawala na hostel kwa ajili ya wanafunzi. Awamu ya pili na tatu zitahusisha ujenzi wa hostel mbili, ukumbi, maktaba, ,adarasa na nyumba za walimu.

Padre Mbano alisema chuo kinakabiliwa na changamoto za ukosefu wa umeme, maji na samani na vifaa vya kufundishia. Kuhusu umeme, alisema zinahitajika shilingi za Kitanzania milioni 178.3 kuufikisha umeme katika eneo hilo na kwa upande wa samani na vifaa vya kufundishia zinahitajika shilingi za Kitanzania milioni 57.3.

Habari na mwanablog CHANZO: Azimioletu Blog

Tuesday, December 11, 2012

Mungu ni Mmoja: Anaitwa Allah, Brahman, Chiuta, Ruwa na Kadhalika

Uzuri wa kuwa na blogu yako ni kuwa hutawaliwi na mtu katika kuamua nini cha kuandika. Uamuzi wote ni wako. Nimesema kabla kuwa katika blogu yangu hii, masuala ambayo yanasemwa kuwa ni nyeti, kama dini, ni ruksa kujadiliwa. Tena sio tu ruksa, bali muhimu kujadiliwa.

Leo napenda kutoa hoja kuwa Mungu ni mmoja: anaitwa Allah, Brahman, Chiuta, Ruwa, na kadhalika, kutokana na kuwepo kwa lugha nyingi hapa duniani. Huyu ndiye aliye juu ya yote, mwenye uwezo wote, kama inavyosemwa katika ki-Arabu, "Allahu akbar." Ni dhana ya msingi katika dini zetu.

Kama wewe ni mu-Islam, halafu unasema kuwa Allah ni tofauti na Mungu wanayemwabudu wa-Kristu, au Mungu wanayemwabudu wa-Hindu, jichunguze upya, kwani utakuwa unasema kuna miungu zaidi ya mmoja. Utakuwa unaongelea kuwepo kwa mungu mwingine zaidi ya Allah. U-Islam hautambui kuwepo kwa Mungu mwingine zaidi ya Allah.

Kama wewe ni m-Kristu, halafu unasema kuwa Mungu unayemwabudu ni tofauti na Allah, basi inabidi ujichunguze, kwa misingi hiyo hiyo. U-Kristu hautambui kuwepo kwa mungu zaidi ya huyu ambaye sisi wa-Kristu tunayemwabudu, ambaye kwa ki-Arabu huitwa Allah. Usishangazwe na jina Allah. Wa-Kristu ambao ni wa-Arabu nao hutumia jina Allah, wakimaanisha Mungu, kama nilivyowahi kusema katika blogu hii.

Huyu Mungu mmoja anatajwa kwa majina mbali mbali kufuatana na lugha. Wa-Tumbuka wa Malawi na Zambia humwita Chiuta. Wa-Hindu humwita Brahman. Wa-Kamba na wa-Kikuyu humwita Ngai. Wachagga humwita Ruwa.

Hoja yangu ni kuwa majina yote hayo yanamtaja Mungu huyu huyu. Muumini anayeamini kuwa kuna Mungu mmoja tu, sherti akubali na azingatie hilo. Ni ushahidi kuwa Mungu alijitambulisha kwa wanadamu duniani kote tangu mwanzo kabisa.

Nimeona nitoe mawazo yangu, kwa uhuru kabisa, kwani ni haki yangu. Kama kuna anayetaka kuyajadili au kuyapinga, namkaribisha kwa mikono miwili kufanya hivyo.

Monday, December 10, 2012

Baridi Kali Minnesota

Jimbo la Minnesota ni moja ya sehemu zinazopata baridi kali kuliko zote Marekani, wakati wa miezi ya baridi. Jana imeanguka theluji nyingi, kama inavyoonekana pichani, katika eneo la Chuo cha St. Olaf.

Wakati kama huo ni hatari kuendesha magari, na ajali huwa nyingi, yaani magari kugongana barabarani, au kuteleza na kutumbukia mitaroni.

Baridi hii haizoeleki hata kama mtu umepambana nayo miaka na miaka. Inapokuja, ni bora kubaki nyumbani, kama huna sababu ya lazima ya kwenda nje, na kama unakwenda nje, ni lazima kujizatiti kwa mavazi yatakiwayo. Vinginevyo, baridi hii itakuletea madhara. Kuna watu wanaokufa kutokana na kuwa nje kwenye baridi hii.

Katikati ya picha hapa kushoto linaonekana gari maalum ambalo kazi yake ni kusafisha njia na barabara kutokana na kufunikwa na theluji.

Saturday, December 8, 2012

Simba wa Tsavo

Leo napenda kuongelea habari ya simba wa Tsavo. Ni habari iliyokuwa inatusisimua sana tulipokuwa shuleni, baina ya darasa la tano na la nane. Kulikuwa na kitabu, Simba wa Tsavo, ambacho kilichapishwa mwaka 1966. Ni tafsiri ya kitabu cha J.H. Patterson kilichoitwa The Man Eaters of Tsavo.

Kitabu hiki kilielezea matukio ya kutisha wakati ujenzi wa daraja la reli kwenye mto Tsavo, nchini Kenya, miaka mia na kitu iliyopita. Kilielezea namna simba walivyokuwa wakiwavizia, kuwadaka na kuwaua wafanya kazi kwenye eneo la hili daraja wakawaua watu zaidi ya mia, hadi, hatimaye, Patterson alipofanikiwa kuwaua, mwezi Desemba 1898. Hiyo ndio habari tuliyosoma tukiwa shuleni, miaka hiyo ya sitini na kitu.

Lakini, kwa miaka hii ya karibuni, yapata miaka kumi, nimekutana na taarifa nyingine nyingi kuhusu simba wa Tsavo. Je, unajua wale simba waliishia wapi? Katika kusoma habari za mwandishi Ernest Hemingway, ambaye alizaliwa mwaka 1899 eneo la jirani na Chicago, nimegundua kuwa alipokuwa mtoto alipelekwa na baba yake katika hifadhi ya Field Museum of Natural History mjini Chicago. Hapo alipata kuziona maiti za wanyama mbali mbali kutoka Afrika ambazo zilikuwa zimehifadhiwa kitaalam ili zionekane kama vile ni wanyama hai.

Kati ya wanyama hao ni wale simba wa Tsavo, ambao picha yao inaonekana hapa juu. Habari hii ilinishtua sana, kwani sikujua kabisa kuwa simba wa Tsavo wamehifadhiwa na kwamba wako Chicago. Hiyo ni faida ya wazi ya kusoma vitabu, kwamba mtu unagundua mambo ambayo hukuyajua. Pamoja na kuangalia wanyama hao waliohifadhiwa, mtoto Hemingway alisoma kitabu cha The Man Eaters of Tsavo. Hayo yote yalichangia katika kumjengea Hemingway mapenzi makubwa aliyokuwa nayo juu ya Afrika kwa maisha yake yote.

Mwaka 1933, Hemingway na mke wake Pauline walifunga safari wakitokea Ulaya, wakaja Afrika Mashariki. Walishuka meli Mombasa, wakapanda treni kuelekea Nairobi. Walipita Tsavo, wakaenda hadi Machakos, kisha Tanganyika. Kuhusu safari yake ya Tanganyika, Hemingway aliandika kitabu maarufu kiitwacho Green Hills of Africa, ambacho ni kimoja ya vitabu vyake ambavyo nimevisoma na kuwafundisha wanafunzi.

Wednesday, December 5, 2012

Barua za Ernest Hemingway, 1907-1922

Leo nimekipata kitabu cha barua za Hemingway ambacho nilikitaja katika blogu hii siku chache zilizopita. Kama nilivyoandika, nilikiona kwa mara ya kwanza katika duka la vitabu hapa Chuoni St. Olaf. Lakini nakala ile ilinunuliwa hima, ikabidi niagize.

Hemingway alikuwa mwandishi makini wa barua. Hata mwanae, Mzee Patrick Hemingway, amethibitisha hivyo. Kwa ujumla, Hemingway hakutaka wala kutarajia kuwa barua zake zichapishwe. Alikuwa na mazoea ya kuandika barua zake kwa uwazi na hata kutumia lugha ambayo inaonekana kali au yenye kukiuka maadili.

Baada ya Hemingway kufariki, mwaka 1961, suala la kuchapisha au kutochapisha maandishi ya Hemingway ambayo alikuwa hajayachapisha lilijitokeza na kuwa kubwa. Maandishi yake mengine alikuwa hajamaliza kuyarekebisha. Barua zake alikuwa hajaazimia zichapishwe. Suala likawa nini kifanyike.

Wasomaji wa maandishi ya Hemingway walisukumwa na kiu ya kutaka kusoma maandishi yake yote. Wahariri na watafiti walitaka hivyo pia. Familia yake ilikuwa katika mtihani mgumu. Lakini hatimaye, iliamuliwa kuwa bora kuchapisha maandishi hayo, hata barua zake. Ndivyo tulivyovipata vitabu vya Hemingway kama vile The Garden of Eden, Islands in the Stream, A Moveable Feast, na Under Kilimanjaro. Ni matokeo ya maamuzi magumu, na juhudi za wahariri kuhariri miswada aliyoicha Hemingway ikiwa haijakamilika, wakiongozwa na wazo kwamba bila shaka Hemingway mwenyewe angeafiki uhariri huo.

Tunaposoma vitabu hivi bado tunajiuliza iwapo kama Hemingway angeishi zaidi, angerekebisha vipi maandishi haya, hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa mwandishi mwenye nidhamu ya hali isiyo ya kawaida katika kusahihisha na kuboresha maandishi yake. Alitaka kila neno liwe mahali pake na liwe kweli ni neno hilo, si jingine, na kila sentensi iwe imekamilika kwa kiwango cha juu kabisa.

Leo nilitaka nikumbushie pia kitabu cha barua za Shaaban Robert, ambacho niliandika habari zake katika blogu hii. Nilitaka nivijadili vitabu hivi vya barua kwa pamoja, kuelezea umuhimu wa vitabu vya aina hii, ambamo tunapata kuwafahamu waandishi hao maarufu kupitia njia ya barua walizoandika. Barua hizi ni kioo muhimu cha kutuwezesha kuyafahamu mambo ambayo pengine hatungeyafahamu kwa kuangalia tu vitabu vyao vingine. Nangojea nipate wasaa wa kuandika na kuzihusianisha barua za Hemingway na zile za Shaaban Robert.

Tuesday, December 4, 2012

Wa-Kristu Wasilimu; Wa-Islam Waingia u-Kristu

Dini ni moja ya mada ambazo nazizungumzia sana katika blogu yangu. Leo napenda kugusia tena mada ya mtu kubadili dini. Niliwahi kuandika kuhusu mada hiyo, nikatamka kuwa kubadili dini ni haki ya mtu, kwa mujibu wa dhamiri yake. Soma hapa.

 Dini ni safari ambayo binadamu anasafiri. Kwa wengine ni safari ngumu yenye vikwazo vingi. Kwa wengine ni safari nyepesi, kwa maana kwamba wametulia kabisa katika imani yao. Namshukuru Muumba kwamba mimi ni mmoja wa hao waliotulia, ingawa nilipokuwa kijana nilihangaika na kutetereka kiasi fulani.

Ukiangalia mtandaoni, kama vile YouTube, utaona taarifa nyingi za watu wanaobadili dini, kutoka u-Islam kuingia u-Kristu, kutoka u-Kristu kuingia u-Islam, na kadhalika. Maelfu ya watu wanafanya hivyo muda wote. Katika YouTube utawaona wengi wakitoa ushuhuda kuhusu walivyohamia dini nyingine na nini kiliwafanya wahame.  Kwa mtazamo wangu, hayo ni mambo yao binafsi, baina yao na Muumba. Hayaongezi wala kuteteresha imani yangu.

Hapa chini ni taarifa ya watu kuingia u-Islam hivi karibuni nchini Burundi. Hakuna mwenye haki ya kuwazuia, iwapo watu hao wanajisikia ndani ya moyo wao kuwa kwa kubadili dini wanakuwa karibu zaidi na Muumba. Nawatakia mema katika safari hii ya kiroho.
.

Hapa chini ni taarifa ya wa-Islam kuingia u-Kristu nchini Pakistan. Hakuna mwenye haki ya kuwazuia, iwapo watu hao wanajisikia ndani ya moyo wao kuwa kwa kubadili dini wanakuwa karibu zaidi na Muumba. Nawatakia mema katika safari hii ya kiroho.

Nimekutana na Kobina Aidoo

Siku chache zilizopita, Kobina Aidoo kutoka Ghana alitembelea hapa Chuoni St Olaf kutoa mhadhara kama sehemu ya maazimisho ya Africa Weeks. Maazimisho hayo huandaliwa kila mwaka na jumuia ya wanafunzi iitwayo Karibu.

Sikuwa nimesikia jina la Kobina Aidoo, ila nilihudhuria mhadhara wake. Ni kijana mwenye kipaji anayeinukia katika nyanja za filamu na uanaharakati katika kuelimisha jamii.

Aliongelea suala la nani ni mw-Amerika Mweusi, akaleta changamoto nyingi zinazowakabili watu weusi wanaoishi hapa Marekani katika kujitambua na kujitambulisha. Baada ya kusema machache, alituonyesha DVD yake ambayo imajaa kauli na mitazamo ya watu weusi wanaoishi Marekani, wakiwa wametokea nchi mbali mbali za Afrika na bara la Marekani.

Ni mitazamo inayofikirisha na kuchangamsha akili. Inatupanua mawazo kuhusu utata wa suala hilo la nani ni m-Marekani Mweusi, na kwa ambaye hakufahamu, inashtua kuona migogoro baina ya waMarekani weusi wa asili na watu weusi ambao ni wahamiaji wa miaka ya karibuni nchini Marekani.

Katika picha hapo juu ninaonekana na Kobina, baada ya mhadhara wake. Tulipiga picha hii mara baada ya mimi kumkabidhi nakala ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambayo anaonekana ameishika, na yeye akawa amenikabidhi nakala ya DVD yake.

Sunday, December 2, 2012

Naiwazia Songea

Nyumbani ni nyumbani. Leo nimeikumbuka Songea, nikaamua kuleta picha mbili tatu nilizopiga mwaka huu. Hapa kushoto ni barabara itokayo stendi kuu kuelekea bomani, hatua chache tu kutoka duka la vitabu la Kanisa Katoliki. Nyuma ya haya majengo ndipo kilipo Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki.Hapa ni taswira ya uwanja wa Maji Maji, kutoka juu. Nilipiga picha hii kutoka ghorofa ya tatu ya hoteli niliyofikia, ng'ambo ya barabara kutoka kituo kikuu cha polisi. Kule ng'ambo ni kitongoji cha Lizaboni, njiani kuelekea Peramiho, Mbinga, na Mbamba Bay.
Hapa kushoto ni stendi kuu nikiwa na dada yangu na mdogo wangu.

Saturday, December 1, 2012

Mwandishi Hemingway: Vitabu Vipya

Ernest Hemingway ni kati ya waandishi maarufu kabisa duniani. Alizaliwa mwaka 1899 karibu na mji wa Chicago, akafa kwa kujipiga risasi nyumbani kwake kwenye jimbo la Idaho mwaka 1961. Katika maisha yake, aliandika sana, akianzia kama ripota wa gazeti la Kansas City Star. Maandishi yake ni pamoja na riwaya, hadithi fupi, insha, masimulizi ya safari zake, barua magazetini, mashairi, na maelfu ya barua. Tangu wakati wa uhai wake hadi leo, watu wengi sana wamechambua maandishi yake na kuelezea maisha yake.


Vitabu kumhusu Hemingway vinaendelea kuchapishwa. Miezi ya karibuni, vimechapishwa vitabu kama Hemingway and Africa, Hemingway's Boat, na The Letters of Ernest Hemingway: Volume 1,1907-1922.

Kitabu cha The Letters of Ernest Hemingway: Volume 1, 1907-1922 nilikiona kwa mara ya kwanza miezi michache iliyopita katika duka la vitabu la Chuo cha St. Olaf. Ni kitabu muhimu sana kwa jinsi kinavyojumlisha kila barua ya Hemingway inayojulikana kwa kipindi cha miaka iliyotajwa. Ninapangia kujipatia nakala.

Ninayo nakala ya kitabu cha mwanzo cha barua za Hemingway, kiitwacho Ernest Hemingway: Selected Letters: 1917-1961. Lakini hiki cha sasa kinafunika kila kitu. Ni juzuu la kwanza, na inategemewa kwamba kutachapishwa majuzuu mengine, hadi kukamilisha maisha yote ya Hemingway.

Wakati wa maonesho ya vitabu yaliyofanyika wiki chache zilizopita mjini Minneapolis, mzee mmoja alifika kwenye meza yangu, na katika mazungumzo yetu nilimtaja Hemingway. Hapo hapo mzee akaniuliza kama nimeshasoma Hemingway's Boat.

Niligutuka kuona mzee huyu keshasoma kitabu hiki ambacho kimetoka karibuni tu. Lakini papo hapo nikakumbuka kuwa hapa ni Marekani, sio Tanzania. Usomaji wa vitabu hapa ni jambo la kawaida kabisa. Nilimwambia kuwa kitabu hicho nimekiona katika duka la vitabu Chuoni St. Olaf, na kwamba nimekiangalia angalia, ila sijakisoma. Hata hivi, tuliendelea na mazungumzo kuhusu mambo ya aina hiyo.

Kitabu cha Hemingway and Africa nilikiazima kutoka maktaba ya Chuo Kikuu cha Minnesota nikakisoma. Niko njiani kujipatia nakala. Hiki ni kimoja kati ya vitabu muhimu sana vinavyochambua uhusiano wa Hemingway na Afrika. 

Najihesabu kama mmoja wa wapenzi na wafuatiliaji wakubwa wa Hemingway. Nimefanya na naendelea kufanya utafiti juu yake na maandishi yake, hasa uhusiano wake na Afrika. Imekuwa ni furaha kwangu kuwapeleka wanafunzi Tanzania, kwa somo hilo.

Tuesday, November 27, 2012

Tanzania: Nchi ya Mavuvuzela

Kama ilivyo kawaida yake, Kipanya hakosi neno. Kwenye katuni hapa kushoto katoboa ukweli: Tanzania ni nchi ya mavuvuzela. Tukubaliane kwa hilo.

Monday, November 26, 2012

Wanafunzi Wangu wa ki-Ingereza Muhula Huu

Leo nimepiga picha na baadhi ya wanafunzi wangu ambao nimekuwa nikiwafundisha muhula huu somo la uandishi wa lugha ya ki-Ingereza.

Wanafunzi wote wanaosoma hapa chuoni St. Olaf wanatakiwa kusoma somo hilo kama msingi wa masomo ya chuo. Kwa vile wanafunzi ni wengi, tunawagawa katika madarasa madogo, yasiyozidi wanafunzi 18 kila darasa. Uchache huu unamwezesha mwalimu kumsaidia kila mwanafunzi ipasavyo, kwa kuhakiki uandishi wake na kumpa mawaidha.


Ninapenda kufundisha masomo yote ninayofundisha. Ninawapenda wanafunzi. Lakini kwa vile mimi ni mwandishi, ninapenda kwa namna ya pekee kufundisha uandishi wa lugha ya ki-Ingereza.

Kutumia ki-Ingereza vizuri kabisa ni mtihani mkubwa, kama mwandishi maarufu Ernest Hemingway alivyokiri na kutukumbusha. Hata huku ughaibuni kwa wenye lugha hii, wengi hujiandikia tu na kuamini kuwa wameandika ki-Ingereza vizuri. Kukaa nao na kuwaonyesha njia nzuri ni bahati na baraka ambayo ninaifurahia.

Sunday, November 25, 2012

Rais Obama Anunua Vitabu

Jana Rais Obama aliripotiwa akinunua vitabu kwenye duka dogo, kwa lengo la kuchangia mapato ya wafanya biashara wadogo. Alitanguzana na binti zake, akanunua vitabu 15 vya watoto, kwa ajili ya kuwagawia ndugu. Picha ionekanayo hapa ni ya J. Scott Applewhite, Associated Press.

Niliposoma taarifa hii, nilijiuliza je, ni lini tumewahi kuwaona vigogo wa Bongo wakinunua vitabu? Ni lini umewahi kumwona kigogo wa Bongo akiwa na wanawe katika duka la vitabu? Pia nilikumbuka kuwa niliwahi kuuliza katika blogu hii kama unaweza kumpa m-Tanzania kitabu kama zawadi ya Krismasi au Idd el Fitri. Soma hapa.

 Kama vigogo wa Bongo wangekuwa na utamaduni wa kuvithamini vitabu, wangeweza kuleta mabadiliko makubwa nchini. Wangeweza kuanzisha maktaba vijijini. Wangeweza kuanzisha klabu za usomaji wa vitabu.

Vigogo hao husafiri sana nje ya nchi. Kwenye viwanja vya ndege, iwe ni O'Hare, Schippol, Heathrow, Johannesburg, au Istanbul, kuna maduka ya vitabu. Vigogo hao wangeweza kununua vitabu kila wanaposafiri na kuvipeleka kwenye maktaba za mkoa, shule na vyuo. Hebu fikiria, ukimpelekea hata tu kamusi ya ki-Ingereza mwalimu wa shule kule Lindi au Kalenga, unakuwa umeleta mapinduzi fulani katika ufundishaji kwenye shule hiyo.

Sisemi tu kwa kujifurahisha au kuwalaumu wengine. Mimi mwenyewe nanunua sana vitabu, na hadi sasa ninavyo zaidi ya elfu tatu. Niliposoma Marekani, 1980-86 nilinunua vitabu vingi sana, nikarejea navyo Tanzania. Ingawa watu walinishangaa kwa kuleta vitabu badala ya gari, vitabu hivyo vimewafaidia wanafunzi na wasomi wengi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Baada ya kuja kufundisha Marekani, 1991, nimenunua vitabu vingi zaidi. Nikifanikiwa kuvisafirisha nitakaporudi Tanzania, itakuwa ni hazina kubwa kwa wapenda elimu. Ila sina hakika kama nitaweza kuvisafirisha, kwani ni vingi mno. Itabidi wa-Tanzania wafanye mchango waniletee hela za kusafirishia vitabu hivyo. Uwezo wanao sana, kama inavyothibitika katika michango ya sherehe mbali mbali. Vinginevyo huenda nikaamua kuviuza hapa hapa Marekani nipate hela za kununulia angalau bajaji. Itanisaidia baada ya kustaafu Tanzania.

Thursday, November 22, 2012

Kanisa Katoliki Mjini New Prague, Minnesota

Jana nilifika mjini New Prague hapa Minnesota, kwa shughuli binafsi. Nilishawahi kupita kwenye mji huu mara kadhaa, na kitu kimoja kilichonivutia tangu mwanzo ni kanisa Katoliki ambalo liko katikati ya mji, pembeni mwa barabara.

Watu waliniambia tangu zamani kuwa kanisa hili lilijengwa na wahamiaji kutoka Czechoslovakia, na kwamba madirisha yake ya vioo (stained glass) yanavutia sana. Nilikuwa na hamu ya siku moja kwenda kusali hapo na pia kuangalia hayo madirisha. Mimi hupenda nyumba za ibada za dini mbali mbali kama nilivyoeleza hapa na hapa.
Jana, kwa vile nilikuwa mjini hapo, nilihakikisha nimepiga picha ya kanisa hilo, ingawaje ni kwa nje tu. Nilipata fursa ya kuona kuwa pembeni mwa kanisa kuna shule. Huu ni utamaduni wa kanisa Katoliki, kwamba panapojengwa kanisa, na huduma zingine ziwepo, hasa shule na hospitali. Nilivyoliangalia hilo kanisa na hiyo shule, nilikumbuka kijijini kwangu, kwani kule nako hali ni hiyo hiyo.

Monday, November 19, 2012

Kwa wa-Luteri wa Tungamalenga, Iringa

Makanisa mengi ya ki-Luteri Marekani, ELCA, yana ushirikiano na makanisa ya ki-Luteri ya Tanzania na nchi zingine. Kanisa la Shepherd of the Valley, ambalo liko hapa Minnesota, lina uhusiano na kanisa la Tungamalenga, mkoani Iringa. Kwa taarifa zaidi, soma hapa.

Nimewahi kutembelea Shepherd of the Valley kuongea na wanafunzi wa Chuo cha Gustavus Adolphus ambao walikuwa hapo kufanya maandalizi ya safari ya Tanzania, kama nilivyoelezea hapa.

Kwa miaka mingi kiasi nilifahamu kuhusu uhusiano baina ya Shepherd of the Valley na Tungamalenga.  Kila ninapoliwazia kanisa la Shepherd of the Valley, au ninapoliona, naiwazia Tungamalenga, ingawa mimi si m-Luteri. Kwa vile liko pembeni mwa barabara, ninaliona kanisa hilo kila ninapoenda kutoa mihadhara katika Chuo cha Mazingira.

Sikuwahi kufika Tungamalenga, hadi mwaka jana, niliposafiri na wanafunzi wa ki-Marekani kutoka Iringa kwenda hifadhi ya Ruaha. Ghafla tulipita sehemu iitwayo Tungamalenga. Nilishtuka, kwa sababu sikuwa hata najua kama Tungamalenga iko katika njia hiyo, karibu kabisa na hifadhi ya Ruaha.

Picha inayoonekana hapa juu nilipiga tarehe 13 Novemba, nilipokuwa narudi kutoka kwenye Chuo cha Mazingira. Kwa miaka miwili au zaidi nilitaka niweke picha ya Shepherd of the Valley hapa katika blogu yangu, nikiwawazia wa-Luteri wa Tungamalenga.

Saturday, November 17, 2012

Mdau Wangu Mpya, Mhadhiri wa Mankato

Nimempata mdau mpya, mhadhiri katika chuo cha North Central, mjini Mankato, Minnesota. Natumia neno mdau au wadau kwa maana ya wasomaji wa vitabu vyangu ambao wanajitokeza na kujitambulisha kwangu. Nina kawaida ya kuwataja wadau hao katika hii blogu yangu, kama unavyoweza kusoma hapa na hapa.

Leo napenda nimwongelee huyu mdau mpya, Mhadhiri Davis. Wiki kadhaa zilizopita, nilipigiwa simu na Profesa Scott Fee wa Chuo Kikuu cha Minnesota, Mankato, akisema kuwa wakati anapiga simu, yuko katika mazungumzo na Mhadhiri Becky Davis, wakiongelea kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Alinipa fursa nikasalimiana na Mhadhiri Davis, ambaye anaonekana pichani hapa kushoto.

Waalimu hao walikuwa katika maandalizi ya kupeleka wanafunzi Afrika Kusini. Pamoja na kuongelea upatikanaji rahisi wa nakala za kitabu hiki, walikuwa wananialika Mankato kuongea na wanafunzi. Bila kusita, niliupokea mwaliko wao. Falsafa yangu ni kuwa Mungu kanipa fursa ya kuelimika sio ili nimwage mbwembwe bali niwafaidie wanadamu.

 Profesa Scott Fee tulifahamiana miaka kadhaa iliyopita, wakati anaandaa msafara wa wanafunzi wa kwenda Afrika Kusini. Katika maandalizi hayo, aliamua kutumia kitabu changu hicho. Kama sehemu ya maandalizi ya safari, alinialika chuoni kwake kuongea na wanafunzi kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni, kama nilivyoelezea kitabuni. Nilienda, nikaongea na wanafunzi, ambao walikuwa wengi, kama ninavyokumbuka.

Baada ya kutajiwa jina la Mhadhiri Davis, niliingia mtandaoni kutafuta taarifa zake. Yeye ni mwandishi makini, kama ilivyoelezwa hapa. Nafurahi kuunganishwa na mwandishi mwenzagu, kwani kutakuwa na fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu.

Nashukuru kwamba kazi yangu ya kutafakari na kuandika kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni inawagusa na kuwafaidia wengine. Insh'Allah, siku itakapowadia, nitaenda Mankato na kutoa mchango wa kiwango cha juu kwa kadiri ya uwezo wangu.

Tuesday, November 13, 2012

Kitabu cha Mazungumzo ya Nelson Mandela

Leo nimenunua kitabu cha Nelson Mandela, Conversations with Myself. Ingawa sijui nitakisoma lini, kutokana na utitiri wa vitabu vyangu, nimekinunua kutokana na umaarufu wa Mandela na kutokana na ukweli kwamba kumbukumbu zake na mawaidha yake ni hazina kubwa.

Idadi ya vitabu vinavyosimulia na kuchambua mchango wa Mandela vinaendelea kuchapishwa. Yeye mwenyewe pia amejitahidi kuandika. Kwa mfano, tulipokuwa vijana, tulikifahamu kitabu chake kiitwacho  Long Walk to Freedom. Haikuwa rahisi mtu usikijue kitabu hiki, kwani kilichapishwa katika mfululizo maarufu wa vitabu vya shirika la Heinemann, ambalo tulilifahamu sana kutokana na vitabu vyake ambavyo tulikuwa tunavisoma.

Miaka ya karibuni, Mandela amejikakamua akaandaa kitabu cha hadithi, Nelson Mandela's Favorite African Folktales. Ni mkusanyiko wa hadithi za asili za ki-Afrika.

Kwa kuangalia juu juu, nimeona kuwa hiki kitabu cha Conversations with Myself ni mkusanyiko wa barua mbali mbali za Mandela na maandishi mengine ambayo yanatufunulia picha ya Mandela sio tu kama mwanasiasa na mpigania ukombozi maarufu bali kama binadamu. Ni kitabu kikubwa, kurasa 454. Nitakuwa nakisoma kidogo kidogo. Isipokuwa ni kimoja kati ya vitabu vya pekee kabisa katika maktaba yangu.


Nimeenda Tena Chuo Cha Mazingira, Minnesota

Leo nilitembelea tena Chuo cha Mazingira, mjini Apple Valley. Kama alivyofanya mwaka hadi mwaka, Mwalimu Todd Carlson alinialika kwenda kuongea na wanafunzi wake kuhusu uwiano baina ya masimulizi ya jadi na mazingira. Mwalimu Todd Carlson, anaonekana pichani kushoto kabisa


Mwalimu Carlson huwaeleza wanafunzi kuhusu masimulizi ya jamii mbali mbali za asili, kama vile wa-Marekani Wekundu, wenyeji wa asili wa Australia, na pia wa-Khoisan wa pande za kusini mwa Afrika.

Anatumia pia kitabu changu cha Matengo Folktales. Kila ninapoenda kuongea na wanafunzi hao, nawakuta wamesoma angalau sehemu fulani muhimu za kitabu hicho. 


Kutokana na maandalizi hayo anayofanya Mwalimu Carlson, mazungumzo yangu na wanafunzi pamoja na masuali yao huwa ya kiwango cha juu.


Kama ilivyokuwa safari zilizopita, sote tumefurahia ziara yangu ya leo.

Friday, November 9, 2012

U-Islam Watekwa Nyara

Leo nimejipatia kitabu kiitwacho The Great Theft: Wrestling Islam From the Extremists. Mwandishi ni Khaled Abou El Fadl, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha California, Los Angeles, ambaye kwenye jalada nyuma ya kitabu, ametajwa kuwa "one of the world's preeminent Islamic scholars and an accomplished Islamic jurist."

Nikitafsiri kwa ki-Swahili, ni kwamba mwandishi huyu ni mmoja wa wataalam wa u-Islam ambao wanaongoza hapa duniani na pia ni mwanasheria mahiri wa sheria za ki-Islam. Nimeanza kukisoma kitabu hiki leo hii. Tayari ninaona kuwa hiki kitabu ni moto wa kuotea mbali, kwa jinsi kinavyouelezea na kuutafsiri u-Islam kwa mujibu wa misahafu yake, na kwa jinsi kinavyowabomoa hao wanaoitwa wa-Islam wenye siasa kali. Mwandishi anawabainisha kuwa ni wapotoshaji, kwenye masuala kama nafasi ya wanawake katika u-Islam, jihad, haki za binadamu, ugaidi, na vita.

Kitabu hiki kinanikumbusha kitabu changu kingine, kiitwacho Muhammad: A Biography of the Prophet, ambacho nilikifurahia sana, nikakitaja katika blogu hii. Yeyote anayetaka kujielimisha kuhusu Mtume Muhammad ni vema akasoma kitabu hiki, ambacho gazeti la Muslim News lilikisifu kwamba kinaondoa umbumbumbu uliopo, na ni kitabu muhimu kwa wasio wa-Islam na wa-Islam pia.

Basi nimeona kuwa kitabu cha The Great Theft ni kimoja kati ya hivi vitabu vinavyofafanua kwa umahiri mkubwa ukweli kuhusu u-Islam, tofauti na yale yanayosemwa na hao wanaoitwa wa-Islam wenye siasa kali, ambao wameuteka nyara na wanaupotosha u-Islam. Ushauri wangu ni kuwa tuvisome vitabu hivi. Lakini je, kwa wa-Tanzania, ambao kwwa ujumla ni wavivu wa kujifunza lugha mbali mbali na ni wavivu wa kusoma vitabu, elimu hii itawafikia?

Thursday, November 1, 2012

Lord of the Flies: Riwaya ya William Golding

Kila siku naviangalia vitabu vyangu nilivyo navyo hapa ughaibuni. Ni vingi sana. Jana nilikichomoa kitabu kimojawapo, Lord of the Flies, kilichotungwa na William Golding, ili nikiongelee hapa katika blogu yangu. Lord of the Flies ni moja ya vitabu vilivyonigusa sana nilipokisoma nikiwa sekondari. Kilikuwa ni kitabu kimojawapo cha lazima katika somo la "Literature." Kilituvutia sana vijana wa wakati ule.

Ni kitabu cha hadithi ya kubuniwa, yenye ujumbe mzito kuhusu tabia ya binadamu. Tunawaona vijana wadogo kutoka U-Ingereza wakiwa wamepata ajali ya meli na kuachwa katika kisiwa peke yao. Hakuna mtu mzima. Wanawajibika kujipanga ili waweze kuendelea kuishi, kwa kutegemea uwindaji humo kisiwani, na wanawajibika kujitungia utaratibu wa kuendesha jamii yao.

Hao ni watoto waliolelewa katika maadili mazuri huko kwao u-Ingereza, lakini katika mazingira ya kupotelea humo kisiwani, tunawaona wakididimia kimaadili, na hatimaye tunashuhudia wanavyoanza kuwa wabaya kabisa, na hii jamii yao inagubikwa na ukatili.

Hatimaye, kwa bahati kabisa, meli inaonekana kwenye upeo wa macho baharini. Insogea hadi kufika hapa kisiwani. Vijana wanaikaribia na nahodha anapowaona anashangaa kuona walivyoathirika katika kuishi wenyewe bila watu wazima. Anaposikiliza masimulizi yao, anashindwa kuamini jinsi walivyopoteza ustaarabu waliolelewa nao.

Hayo ndiyo ninayokumbuka kuhusu dhamira ya riwaya hii. Tangu wakati ule tulipoisoma riwaya hii nilifahamu kuwa ni riwaya ambayo imewapa changamoto kubwa wanasaikolojia na wanafalsafa wa tabia ya binadamu, kwa maana kwamba inazua masuala mazito. Je, watoto ni malaika kama tunavyodhani au wana silika ya ubaya wa kupindukia kama wabaya wengine wowote? Je, hayo tunayoyaita maadili yana mshiko kiasi gani, au yanategemea tu mazingira, na kwamba mazingira yasipokuwepo, maadili yanaweza kutoweka kabisa?

Lakini kuna pia suala la sanaa ya mwandishi Golding, ambayo imetukuka sana. Ana ubunifu wa hali ya juu, wa kumgusa sana msomaji, jinsi anavyoelezea maisha na mahusiano ya hao watoto humo kisiwani. Matumizi yake ya lugha yalikuwa ni kivutio kimoja kikubwa sana kwangu. Niliguswa na jinsi anavyoelezea mazingira, kwa mfano.

Nilipokuwa mwanafunzi Mkwawa High School, niliendeleza juhudi zangu za uandishi ambazo nilianza miaka iliyotangulia. Niliandika hadithi iitwayo "A Girl in the Bus," ambayo ilichapishwa katika jarida la BUSARA, lilokuwa maarufu katika vyuo vikuu vya Afrika Mashariki. Hii ilikuwa ni hadithi yangu ya kwanza kuchapishwa katika jarida la kimataifa. Nakumbuka jinsi nilivyofurahi kuisoma hadithi yangu katika jarida maarufu namna hii, ambamo walikuwa wanaandika waandishi maarufu wa Afrika Mashariki, na mimi nikiwa ni kijana wa "High School" tu. Nilikuwa na furaha isiyoelezeka, wakati napitapita mjini Iringa. Katika hadithi hii niliiga kwa kiasi fulani mtindo wa William Golding katika kuelezea mazingira.

Mwaka huu, nikiwa katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nililitafuta jarida BUSARA nikaisoma hadithi yangu, kwa furaha na mshangao kuwa niliweza kuandika vizuri namna ile wakati wa ujana wangu. Lakini, William Golding alichangia.

Sunday, October 28, 2012

Taarifa kwa Umma Kuhusu Hatma ya MwanaHalisi

Leo 28 Oktoba 2012

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Bidamu (THRD-Coalition), wadau wanaounda mtandao huu na mwanachama mwanzilishi wa Mtandao likiwa ni shirika lenye majukumu ya ya kutetea uhuru wa habari kusini mwa Afrika (MISA-Tan) tunaendelea kwa pamoja kuonyesha kusikitishwa kwetu kwa kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi.

Kwa mara kadhaa sasa tunawakutanisha tena lengo likiwa ni kuendelea kuishawishi serikali ilifungulie gazeti la Mwanahalisi. Kwa vile hoja yetu ya kutaka kuliona gazeti la Mwanahalisi likiwa mitaani haijatimia basi na sisi kwa upande wetu kazi yetu bado haijatimia.

Tunatambua umuhimu wa kuheshimu sheria za nchi, lakini kwa upande mwingine tunaona kwamba ipo haja ya sisi watetezi wa haki za binadamu kupitia kwenye vyombo vya habari na pia kwenye mashirika mengine yanayounda mtandao huu kuishawishi serikali kuachana na sheria gandamizi ambazo ni za kidikteta kama sheria hii ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo hukiuka misingi ya haki za binadamu na utawala bora. Pia kwamba maendeleo ya kiteknolojia na kisiasa hapa nchini yanaiweka rehani sheria hiyo gandamizi.

Tumebaini kuwa kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi siyo tu kwamba kunawaathiri kwa kiwango kikubwa wasomaji wake ndani na nje ya nchi bali pia kunaathiri uhuru wa kutafuta, kupata na kueneza habari, kunawaathiri waajiriwa wa gazeti hilo na familia zao na pia kunaiweka katika hati hati hata kampuni nzima ya Halihalisi ambayo ndiyo mchapishaji wa gazeti hilo.

Tunaendelea kusisitiza kuwa sababu walizotumia viongozi wa wizara ya habari kulifungia gazeti la mwanahalisi sio za kweli kwani kilichoandikwa na Mwanahalisi ni ukweli mtupu ambao hivi karibuni umethibitishwa na tamko la Dr Steven Ulimboka.

Pia, hivi karibuni Dkt Stephen Ulimboka, kupitia kwa wakili wake Mheshimiwa Nyaronyo Kicheere aliweka wazi kwamba Afisa wa Usalama wa Taifa Ramadhan Ighondu alihusika katika kutekwa kwake kwa kuwa mazingira yote kabla na baada ya tukio yanaonyesha wazi kuwa Ramadhani Ighondu ni mdau katika tukio hili.

Kinachoshangaza zaidi ni kwamba baadala ya serikali kutoa tamko kwamba sasa imepata uhakika kwamba afisa wake alikiuka kanuni za ajira yake na ingeaza rasmi kuwasaka washirika wa afisa hiyu jambo hilo halijatokea mpaka sasa huku gazeti hili lililosidia kubainisha ushahidi likifungiwa. Zaidi, tulitegemea serikali ingemkana afisa huyo kwamba siyo mwajiriwa wake katika idara hiyo, kama hivyo ndivyo ilivyo, au vinginevyo tungeitarajia serikali itangaze kwamba inachukua hatua za kisheria dhidi ya afisa huyo ambaye ametajwa kuhusika katika makosa ya jinai kinyume cha utaratibu wa mwajiri wake. Pia tungetemea Jeshi la polisi lingetumia fursa hii kumkamata mshukiwa huyu wa Usalama wa Taifa na kulisadia Jeshi la Polisi kuwapata wale waliotekeleza udhalimu huu dhidi ya Dr Steven Ulimboka. Kwa namna yoyote vitendo vya aina hiyo vinaiabisha serikali na haviwezi kuwa sehemu ya utawala bora ambao serikali yetu imekuwa ikitangaza kwamba inauzingatia.

Mpaka sasa kumekuwapo na matamko mbali mbali kutoka kwa wadau, viongozi wa kiroho, mabalozi na hata Baraza la Habari Tanzania (MCT) likiwa peke yake na hata kwa kushirikiana na wadau wengine wakilaani kufungiwa kwa gazeti hili lakini serikali imeendelea kuwa kaidi katika hili.

Tunachosisitiza
1. Kwa Serikali
Tunaendelea kuwasihi viongozi wa nchi waone sasa umuhimu wa kukutana na viongozi wa Hali Halisi na kujadili namna ya kulifungulia gazeti hili kwani tayari Dr Steven Ulimboka ameshaweka wazi kilichoandikwa na Mwanahalisi ni cha kweli kabisa. Serikali itambue kuwa suala hili sio dogo katika anga za kidemokrasia na haki za binadamu kwani ubabe wa baadhi ya viongozi serikalini leo unaweza iweka nchi pabaya siku za usoni.

2. Vyombo vya Habari
Vyombo vya habari pamoja na taasisi mbalimbali katika tasnia ya habari tuweke tofauti zetu pembeni na kuungana kwa pamoja katika hili na kuhakisha kuwa ukandamizaji wa uhuru wa habari kama huu wa wazi wazi haupati nafasi katika enzi hizi za uwazi na ukweli. Vyombo na taasisi mbalimbali za habari bado mna nafasi na uwezo mkubwa katika kuhakisha gazeti la Mwanahalisi halipotei katika tasnia ya habari hapa nchini.

3. Jumuiya ya Kimataifa
Kwa kuwa mmekuwa wadau wakubwa wa maendeleo na utekelezaji wa haki za binadamu hapa nchini, tukiwa tunaendelea kuuthamini mchango wenu, tunawasihi muendelee kuishawishi serikali kwa njia za kidiplomasia kuhusu suala la kuheshimu kazi za watetezi haki za binadamu na uhuru wa habari. Nafasi zenu za kidiplomasia na uhusiano mkubwa mlionao na nchi ya Tanzania inaweza pia kutumika kushawishi viongozi wa Tanzania walifungulie gazeti la Mwanahalisi.

Kutokana na hali ilivyo ya uvunjifu wa haki za watetezi wa haki za binadamu ikiwamo haki ya kutoa habari, MISA-Tan, mwanachama wa THRD-Coalition anaehusika na uhuru wa habari inaandaa mkutano wa siku moja utakaowakutanisha wadau mbalimbali katika tasnia ya habari ili kujadili hatma ya gazeti la Mwanahalisi na uhuru wa habari nchini.

Mwisho Tunawasihi wanaharakati, watanzania wote wasichoke wala wasirudi nyuma katika azma hii ya kutetea haki, uhuru na ulinzi kwa haki na watetezi wake.

CHANZO: KATUNEWS BLOG

Thursday, October 25, 2012

Mdau Profesa Aliyenihamasisha Kuandika Kitabu

Leo nimekutana na rafiki yangu wa siku nyingi, Profesa John Greenler wa Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Alikuja hapa Chuoni St. Olaf na binti yake. Kama umesoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, utaona nimemtaja Profesa Greenler kwenye ukurasa wa "Acknowledgements."

Profesa huyu tulifahamiana miaka yapata kumi iliyopita kwenye mikutano ya washauri wa programu ya Associated Colleges of the Midwest (ACM) ambayo hupeleka wanafunzi Tanzania. Miaka ile yeye alikuwa anafundisha Chuo cha Beloit. Wakati wa kupanga na kutathmini hali ya program kila mwaka, nachangia kwa namna ya pekee masuala yanayohusu tofauti za tamaduni, ambayo ni changamoto kwa wa-Marekani na wa-Tanzania.Kwenye mikutano yetu hiyo, nilikuwa, na bado niko, mstari wa mbele kufafanua matukio mbali mbali na mambo mengine wanayokumbana nayo wanafunzi katika kuishi na wa-Tanzania.

Profesa Greenler alipochukua fursa ya kupeleka wanafunzi Tanzania, aliniomba niandike mwongozo angalau kurasa hata tatu tu, wa masuala hayo, ili yamsaidie katika safari yake. Nililitafakari ombi lake, hatimaye nikaanza kuandika.

Wakati muswada ukiwa bado katika hali duni, bila marekebisho ya kutosha, watu mbali mbali hapa Marekani wanaopeleka wageni Tanzania waliuchangamkia, wakawa wanautumia. Nilipogundua hivyo, nilifadhaika, kwa sababu muswada haukuwa umekamilika,  na haukufanana na hadhi na ujuzi wangu. Niliona ni sherti nifanye juhudi kuurekebisha bila kuchelewa. Baada ya kazi ngumu ya miezi kadhaa nilichapisha kitabu, Februari 2005.
Leo nimemkumbusha Profesa Greenler alivyonihamasisha katika suala hili, na nikamsisitizia binti yake kuwa habari ndio hiyo. Tumefurahi sana kukutana na kukumbushana mambo ya Bongo. Ameniambia tena kuwa yeye na familia yake wanaikumbuka sana Tanzania na wanaipenda.

Amenielezea pia kuhusu wanafunzi wa ACM aliowapeleka Tanzania miaka ile, na ambao wanaendelea kuwa na uhusiano na Tanzania. Hili ni jambo la kawaida, na sisi tunaohusika na programu hizi tunafarijika tunapoona kuwa zimechangia kujenga mahusiano baina ya watu wa nchi hizi mbili.

Hata hivi, kwa kuzingatia kuwa profesa huyu ni kati ya wa-Marekani wengi sana ambao ni wapenzi wa Tanzania, ilibidi nimwambie kuhusu maandamano na vurugu Zanzibar na Dar es Salaam, ambayo yanachafua jina la Tanzania. Miaka yote iliyopita ilikuwa rahisi na heshima kuinadi Tanzania kama nchi ya amani na utulivu, lakini ni sherti kusema ukweli unaojitokeza sasa.

Monday, October 22, 2012

Ngoma Nzito Marekani: Tanzania Je?

Pamoja na mapungufu yake yote, siasa Marekani ina mambo kadhaa ya kupigiwa mfano. Kinachonivutia zaidi ni mijadala inyofanyika baina ya wagombea kabla ya uchaguzi. Leo, kwa mfano, tumeshuhudia pambano la tatu baina ya Obama na Romney

Mijadala ya namna hii inawapa wapiga kura fursa ya kuwasikiliza wagombea. Vile vile naiona kama namna ya kuwaheshimu wapiga kura.

Mfumo wa Marekani unatambua kuwa wapiga kura wana haki ya kuwasikia wagombea wakiongelea masuala kadha wa kadha katika kupambanishwa na wapinzani wao.

Ninakerwa ninapokumbuka mambo yalivyo kwetu Tanzania. Ninakerwa nikikumbuka jinsi CCM ilivyotoroka midahalo mwaka 2010. Ni dharau kwa wapiga kura. Tatizo ni jinsi wapiga kura wengi walivyo mbumbumbu, wasitambue kuwa hili lilikuwa dharau. Walipiga kura kama vile hawajadharauliwa.

Hebu fikiria mambo yangekuwaje ule mwaka 2010 iwapo Kikwete angepambana na Slaa katika midahalo mitatu hivi, ambayo ingeonekana katika televisheni na kusikika redioni. Lakini tulinyimwa fursa hii, kutokana na maaumzi muflisi ya CCM.

Hakuna sababu yoyote kwa nini siku zijazo tusifanye kama wa-Marekani wafanyavyo. Watangazaji makini wa redio na televisheni tunao, ambao wanaweza wakaendesha mahojiano nasi tukapata fursa nzuri ya kuwabaini wababaishaji na kuwatupilia mbali.

Saturday, October 20, 2012

Mtume Hatetewi kwa Dhulma na Ujinga

Mtume Hatetewi Kwa Dhulma Na Ujinga

Uislamu Na Shari'ah Zake

Imekusanywa Na: ‘Uthmaan Beecher

Imefasiriwa Na: Abu Suhayl

Shukrani njema zinamstahili Allaah, rahmah na amani zimuendee Mtume wetu Muhammad, na aali zake na maswahaba zake na Waislamu wote. Ama baada ya hayo

Hakuna Muislamu ambaye anaweza kukubaliana na kutukanwa, kudhalilishwa, kudhauruliwa na kusingiziwa mambo mabaya Mtume wetu mpendwa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ma-Imaam wa Ahlus-Sunnah kama Imam Maalik, al-Layth, Ahmad, na Ash-Shaafi’iy, wamekubaliana kwa pamoja kwamba yeyote atakayemvunjia heshima, kumtukana au kumdhalilisha au kumtia ila Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atakuwa amekufuru, na adhabu inayomstahili kwa yule anayeishi katika dola ya Kiislamu na akafanya hivyo ni kifo, adhabu ambayo itakuwa katika mikono ya mtawala wa Kiislamu.

Hapana shaka kwamba mashambulizi ya aina hii kwa Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yatasababisha hasira na kukata matumbo ya kila Muislamu kutokana na mapenzi yao kwa Allaah, Mtume wake na Dini yake. Lakini Muislamu aliye mkweli, muadilifu na muaminifu hawezi kuruhusu kuchukuliwa na hasira na jazba na kujibu mashambulizi haya kwa matendo ya kihuni ambayo yanakusanya matendo ambayo Allaah na Mtume wake wameyakataza. Zaidi atakuwa kama katika matendo mengine na subra, kisha anayarejesha mambo hayo katika Qur-aan na Sunnah na ufahamu wa Maswahaba na Ma’ulamaa walioshikana barabara na elimu. Hivyo Muislamu anakuwa na subira na anaithibitisha miguu yake kwa elimu na anajisalimisha kwa hukumu za Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah anasema:

“Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya ‘Aakhirah. Hivyo ni (njia) bora na matokeo mazuri zaidi.” [An-Nisaa 4: 59].

Al-Haafidhw Ibin Kathiyr ametaja kuwa maana ya “wenye madaraka katika nyinyi.” kwa mujibu wa Ibn ‘Abbaas, Mujaahid na ‘Atwaa na wengine katika Salaf, inakusudiwa “Maulamaa”. Na Ibn Kathiyr amesema inakusudiwa Ma’ulamaa na watawala na hapa inakusudiwa Ma’ulamaa wa Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah.

Ambacho kimetokea siku chache zilizopita katika ardhi za Waislamu na sehemu nyingine kama hatua za kupinga filamu inayoshambulia Uislamu na kumtukana Mtume wetu mpendwa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yanapingana na muongozo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tunatakiwa tukumbuke kuwa mashambulizi haya si mapya. Allaah Ametaja katika Qur-aan kuwa Mitume Wake (‘Alayhimus Salaam) walishambuliwa na kutukanwa, watu wao waliwaita vichaaa, wendawazimu na hata kuwaita wachawi. Allaah Anasema:

“Basi ndio hivyo hivyo, hakuwajia kabla yao Mtume ila walisema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu.” [Adh-Dhaariyaat 51: 52].

Na haya yametokea kwa Mitume kuanzia Nuwh (‘Alayhis Salaam) mpaka kwa Mtume wa mwisho Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Katika kipindi cha maisha ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuna ambao walikuwa wakimtusi na kumkashfu hadharani. Ka’ab bin Ashraf Al-Yahuwdiy aliyekuwa Madiynah alikuwa akiimba mashairi ya kumkashifu Mtume na kuimba mashairi mabaya kuhusu wanawake wa Kiislamu. Na Makkah alikuwepo ‘Abdullaah bin Khatal ambaye alikuwa na waimbaji wawili wa kike ambao walikuwa wakiimba mashairi ya kumkejeli Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

Aliporudi toka safari ya Makkah kuja Madiynah Ka’ab bin Al-Ashraf akaanza kuimba mashairi ya kumtukana. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwauliza Maswahaba zake, “Nani atakayemdhibiti Ka’ab bin Al-Ashraf? Kwani amemdhuru Allaah na Mtume Wake.” Na hapa ni pale Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa katika dola yake na yeye alikuwa ndiye kiongozi na Ka’ab alikuwa akiishi chini ya mamlaka yake hapo Madiynah. Lakini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwaambia Maswahaba zake kwenda kuwaadhibu majirani zake, rafiki zake au familia yake kwa yale aliyokuwa akifanya Ka’ab bin Al-Ashraf. Wala hakuuadhibu ukoo wake wa Banu Nadhwiyr au kuwaadhibu Mayahudi wengine wa Madiynah.

Yeyote mwenye akili iliyosalimika hawezi kukubaliana na hili kwani halikubaliani na mantiki achilia mbali maandiko ya Kitabu na Sunnah.

Alichofanya kama mtawala Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuadhibu Ka’ab ambaye ndiye aliyekuwa anafanya kosa hilo.

‘Abdullaah bin Khatal alikuwa Makkah na alikuwa na waimbaji wawili wa kike aliowafundisha kuimba nyimbo za kumkejeli na kumkashifu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na wakati huo Mtume alikuwa ni kiongozi na hakuwahi kamwe kuwashambulia makafiri wa Madiynah au miji au vijijiji vingine kama malipo ya matusi ya ‘Abdullaah bin Khatal kwake yeye. Pia hakuwaamrisha Maswahaba zake kuishambulia Makkah au watu wa Makkah kwa sababu ya ‘Abdullaah bin Khatal.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na subira na hakuwakandamiza watu au kuchupa mipaka. Alikuwa na subira na alikuwa muadilifu. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoiteka Makkah na jeshi lake, akaamrisha asidhuriwe yeyote ambaye hatopigana nao, isipokuwa kikundi kidogo cha watu ambao aliwataja kwa majina.

Hapa Mtume alikuwa na nguvu, ameiteka Makkah na alikuwa na nguvu na miongoni mwa aliowataja ni ‘Abdullaah bin Khatal na waimbaji wake wawili wa kike. Hakuamrisha majirani zake wala familia yake kuadhibiwa. Hakuamrisha mali za ukoo wake kuharibiwa. Alichoamrisha ni kuuawa ‘Abdullaah bin Khatal na waimbaji wake wawili wa kike.

Hii ni mifano miwili tu ya jinsi Mtume alivyofanya na watu waliomtukana akiwa hai. Alikuwa ni muadilifu na subira. Hakumkandamiza mtu wala kumdhulumu na hawa watu walimlaani, wakamtukana, wakamdhalilisha na kumkashifu akiwa hai (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Sasa matendo haya ya haya makundi na wajinga wengine walioathiriwa na hayo makundi wameyapata wapi kwa kutazama mwenendo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?

Mmeona wapi kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake walikwenda katika miji mingine na kuandamana, na kuua watu wasiokuwa na hatia, kuharibu mali zao kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyafanya Ibn al-Ashraf na Ibn Al-Khatal wakiwa Makkah na Madiynah?

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na subira na uadilifu. Na uadilifu ni kukiweka kila kitu mahali pake. Na haya tunayayona toka kwa watu Misr, Yemen, Libya na nchi zingine katika mashariki ya kati ni ukandamizaji, dhulma na kuvunja Sunnah. Allaah Anasema:

“Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake (Mtume Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), isije kuwasibu fitnah au ikawasibu adhabu iumizayo.” [An-Nuwr 24: 63].

Kinachofafanua zaidi tofauti katika muongozo wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wale Waislamu ambao wanachukuliwa na jazba na upotevu ni Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) ambayo imesimuliwa na Al-Bukhaariy, Muslim, Ahmad na wengineo, walipokuja kundi la Mayahudi kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia “As-Saamu ‘Alaykum” (kifo kiwe juu yako). ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alielewa walichosema hivyo akawajibu “Wa ‘alaykum As-Saam wa la‘ana.” (Na kifo na laana ziwe juu yenu). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “Taratibu ee ‘Aaishah, bila shaka Allaah Anapenda upole katika mambo yote.” ‘Aaishah akasema “Ee Mtume wa Allaah! Hukuwasikia waliyoyasema?” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “Nimeshawajibu (kwa kusema) “Wa ‘Alaykum.” (Na juu yenu pia.” Na Dini yetu haiendi kwa hisia na jazba. Muislamu ambaye anampenda kiukweli Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atafuata muongozo na Sunnah zake.

“Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni, Atakupendeni Allaah na Atakughufurieni dhambi zenu. Na Allaah ni Ghafuwrur-Rahiym (Mwingi wa Kughufiria - Mwenye Kurehemu.” [Al-‘Imraan 3: 31].

Tuzizingatie nukta zifuatazo:

- Maandamano haya ambayo yameenea katika ardhi za Waislamu na yameeingia mpaka Kuwait ni bida’a kama walivyosema wanachuoni wa Ahlus Sunnah waljama’a kama Shaykh Ibn Baaz, Shaykh al-Albaani, Shaykh Ibn ‘Uthaymini na walivyoyafafanua. Ni matendo ya kuwapinga na kupambana na viongozi wa Kiislamu na ni katika njia za Makhawaariji. Makundi ya kisiasa wanayaruhusu na kuyatetea kwani ni njia ya kupambana na watawala wa Kiislamu na ndio njia ya kuchukua madaraka.

Tumeona jinsi vijana waliojawa na hamasa walivyochukua hatua kuingia mitaani katika maandamano haya na kupambana na polisi na kusababisha uharibifu kwa mali na si mali za balozi -ambacho pia kitendo hichi ni ukandamizaji lakini mali za Waislamu pia!! Na hii ndio inaitwa kumlinda Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)? Haiwezekani kwa Muislamu kumtetea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ukandamizaji wakati Allaah Ametuamrisha kuwa waadilifu:

“Enyi mlioamini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Allaah mkitoa ushahidi kwa uadilifu. Na wala chuki ya watu isikuchocheeni kutokufanya uadilifu. Fanyeni uadilifu; hivyo ni karibu zaidi na taqwa. Na mcheni Allaah; hakika Allaah Khabiyr (Mjuzi wa undani na ukina wa mambo) kwa myatendayo.” [Al-Maaidah 5: 8].

Al-Haafidhw Ibn Kathir amesema: “Usiache chuki zako kwa watu zikufanye ukaacha kuwafanyia uadilifu. Fanya uadilifu kwa kila mtu akiwa ni rafiki au adui.”

Shaykh wa Uislamu Ibn Taymiyyah amesema:

“Kwani watu hawakutofautiana kuhusiana na ukweli kwamba mwisho wa dhulma ni mbaya na una madhara na mwisho wa uadilifu ni mzuri wenye kupendeza.” Kwa ajili hiyo pamesemwa: Allaah atalisaidia taifa ambalo linafanya uadilifu hata kama watakuwa ni makafiri na hatolisaidia taifa litakalokuwa linafanya dhulma hata kama taifa hilo litakuwa limeamini.” [Majmu’u Al-Fataawaa 28/63].

Jua kwamba kuwaadhibu watu wengine kwa makosa ya mtu mwingine sio uadilifu Allaah Anasema:

“Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Je, nitake ghairi ya Allaah kuwa ni Mola, na hali Yeye ni Mola wa kila kitu? Na wala nafsi yoyote haitachuma (ubaya) ila ni dhidi yake. Na wala hatobeba mbebaji (mzigo yake ya dhambi) mzigo (wa dhambi) wa mwengine. Kisha kwa Mola wenu Pekee ndio marejeo yenu, Atakujulisheni kwa yale mliyokuwa ndani yake mkikhitilafiana kwayo.” [Al-‘An’aam 6: 164].

Makundi ya kisiasa wanatumia maandamano haya na matukio kama haya kama jukwaa na mimbari za kuenezea mashaka na hila zao kwa watu ili watu wawageuke watawala.

- Maandamano haya ambayo Ma’ulamaa wamesema ni bid’ah yametumika kama ngao kujificha kwa wale walio katika Manhaj ya Khawaarij kuua wasio na hatia. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema “Yeyote katika Waislamu atakayeua mtu ambaye anaishi kwa mkataba au makubaliano (na Waislamu) hatoonja harufu ya pepo japokuwa harufu ya pepo inasikika umbali wa mwendo wa miaka 40.” [Al-Bukhaariy].

Na katika Hadiyth nyingine amesema:

“Mkataba wa amani kwa Waislamu ni mmoja, yeyote atakayeuvunja mkataba wa amani na usalama kwa Muislamu mwengine ni juu yake laana ya Allaah, Malaika na watu wote.”

Al-Haafidhw Ibn Hajr (Rahimahu Allaah) amefafanua:

“Maneno mkataba wa amani kwa Waislamu ni mmoja’ ina maana kuwa kumpa mtu uhakika wa usalama wa amani ni sahihi (unakuwa mkataba umefungika). Kama mmoja wao atampa mkataba wa amani kafiri ni haramu kwa yeyote yule kuuvunja.”

Makafiri wanaoishi na kufanya kazi katika nchi za Waislamu wamepewa mkataba wa amani kwa hiyo kuwashambulia ni kupambana na kuwapinga watawala wa Kiislamu na kitendo cha usaliti na dhulma.

Shaykh Twaariq As-Subay’i amesema kwamba kama Muislamu atampa amani asiyekuwa Muislamu, hata kama huyo Muislamu atakuwa ni mwanamme au mwanamke, muungwana au mtumwa, na hata akiwa amepewa amani kwa ishara tu au kama amepewa amani kwa makubaliano ya kibalozi au kwa kumpa viza kuingia katika nchi -mtu huyo atakuwa amepewa mkataba wa amani na usalama wa maisha yake. Ni haramu kwa Waislamu kumdhuru. Na Muislamu atakayemdhuru ataangukia katika laana za Allaah, na Malaika na watu wote.

- Ukitazama wanaoongoza maandamano haya utawakuta wote ni katika viongozi wa vyama vya kisiasa. Na ushahidi kuwa hakuna katika Wanachuoni wa Ahlus-Sunnah ambaye amejihusisha na haya maandamano yatosha kuwa dalili kwa mtu mwenye akili, kama ambavyo Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) alivyotumia hoja kama hii dhidi ya Makhawaarij kwamba hakuna hata Swahaba mmoja aliye pamoja nao aliposema: “Bila shaka nimekuja kwenu kutoka katika Maswahaba wa Mtume wa Allaah na hakuna hata Swahaba mmoja aliye pamoja nanyi.”

Tunaona Waislamu wakiandamana, wakipambana na polisi wakiharibu mali na mambo mengine mabaya zaidi ya yote hayo yanafanyika kwa jina la kumtetea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutokana na filamu iliyotengenezwa na mtu mmoja anayeishi Marekani. La kusataajabisha hakuna hata mmoja anayechukizwa na Misikiti yenye makaburi ndani ambapo asiyekuwa Allaah anaabudiwa kama Msikiti wa Badawi, Zaynab na Al-Husayn?! Dhambi kubwa kabisa mtu anayoweza kuifanya inafanyika katika ardhi za Waislamu na watu wanashambulia mali na haki za watu kwa kitu ambacho hawana mamlaka nacho au uwezo wa kufanya chochote kukizuia!

Allaah Anasema:

“Hakika Allaah Haghufuri kushirikishwa; na Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amebuni dhambi kuu.” [An-Nisaa 4: 48].

Kwa hiyo Waislamu hawa na makundi haya wanataka kumtetea Mtume kwa kufanya dhulma na na uonevu - lakini uko wapi utetezi wa Allaah na Tawhiyd yake kutokana na shirk zinazofanywa na Waislamu katik ardhi ya Waislamu wenyewe!

Jua kwamba Allaah Ametuamrisha kuwa na subira na uvumilivu na Ametukataza kufanya dhulma na uonevu. Na hakuna uadilifu katika matendo tunayoyaona toka kwa kaka zetu na dada zetu wa Misr, Yemen, Tunisia, Morocco, Sudan na nchi nyingine ambapo haya yanatokea. Matendo haya ni matendo ya ujinga, dhulma, upotevu na kuiacha Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Aliyetengeneza filamu hii chafu anaishi Marekani na Marekani ni nchi ambayo ina kanuni zake inazotumia kutawala raia wake. Jambo hili halipo katika mikono ya sisi watu wa kawaida na hatuna uwezo wa kufanya lolote kulihusu. Jambo muhimu kwetu na subira na kushikamana na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na hii ni njia bora zaidi ya kumtetea Mtume zaidi ya haya tunayoyaona yakifanywa na makundi haya na wafuasi wao.

Na ni muhimu kuzingatia kuwa subira yetu na uvumilivu wetu na kushikamana kwetu na Sunnah wakati wa hali kama hizi wakati hatuna uwezo wa kuzikabili si alama ya udhalili au unyonge. Makundi yaliyopotea ndiyo yamewaingiza vijana katika fikra hizi kuwa ukikosa uwezo wa kuchukua hatua ni sawa na kutochukua hatua, huu ni usaliti na upotevu.

Ibn Mas’uwd amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali katika Ka’abah na alipokuwa akisujudu mmoja kati ya wafuasi wa Abu Jahl alimuwekea matumbo ya ngamia mgongoni kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati Ibn Mas’uwd akiwa anamtazama. Ibn Mas’uwd amesema: “Nilikuwa natazama lakini sikuwa na cha kufanya. Laiti ningekuwa na nguvu na uwezo (wa kumzuia).” [Al-Bukhaariy].

Hili linatuonyesha kwamba wakati hatuna uwezo kutokana na kuwa na miili dhaifu, au kukosa uwezo au kuna kitu kinakuzuia hakuna aibu kwa hilo, kama ambavyo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyoshindwa kuwasaidia Yaasir, ‘Ammaar na mama yake ‘Ammaar (Radhiya Allaahu ‘anhum) alipowaona wakiteswa kwa sababu ya kumuamini Allaah. Hivyo akawaambia: “Fanyeni subra enyi watu wa nyumba ya Yaasir, kwani mmeahidiwa pepo.” [Al-Mastadrak Al-Haakim (3/383), Al-Hilyah (1/140), na vingine. Tazama vilevile Swahiyh Siyrat An-Nabawiyyah cha Shaykh Al-Albaanee (uk. 154-155)].

Haya tumayoyaandika hapa si kwa ajili ya kuitetea filamu hiyo. Hiyo filamu nasi tunaiona kuwa ni matusi yenye kuudhi kama watu wengine. Lakini tunafanya hivi kama njia ya kumtetea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Dini yetu dhidi ya wale wenye kuchupa mipaka, na wale wanaocheza na hisia za Waislamu na vijana na kuwaita katika njia za upotevu. Huu ni wito wa kuwa na subra na kuwa na uadilifu na kushikama na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na haya ndiyo yaliyokuwa ynahitajika kuelezewa na kufafanuliwa. Allaah ni mjuzi zaidi.

Rahmah na amani zimuendee Mtume wetu Muhammad na aali zake na Maswahaba zake wote. Na shukrani njema zinamstahili Allaah.

CHANZO: ALHIDAAYA