Tuesday, November 13, 2012

Kitabu cha Mazungumzo ya Nelson Mandela

Leo nimenunua kitabu cha Nelson Mandela, Conversations with Myself. Ingawa sijui nitakisoma lini, kutokana na utitiri wa vitabu vyangu, nimekinunua kutokana na umaarufu wa Mandela na kutokana na ukweli kwamba kumbukumbu zake na mawaidha yake ni hazina kubwa.

Idadi ya vitabu vinavyosimulia na kuchambua mchango wa Mandela vinaendelea kuchapishwa. Yeye mwenyewe pia amejitahidi kuandika. Kwa mfano, tulipokuwa vijana, tulikifahamu kitabu chake kiitwacho  Long Walk to Freedom. Haikuwa rahisi mtu usikijue kitabu hiki, kwani kilichapishwa katika mfululizo maarufu wa vitabu vya shirika la Heinemann, ambalo tulilifahamu sana kutokana na vitabu vyake ambavyo tulikuwa tunavisoma.

Miaka ya karibuni, Mandela amejikakamua akaandaa kitabu cha hadithi, Nelson Mandela's Favorite African Folktales. Ni mkusanyiko wa hadithi za asili za ki-Afrika.

Kwa kuangalia juu juu, nimeona kuwa hiki kitabu cha Conversations with Myself ni mkusanyiko wa barua mbali mbali za Mandela na maandishi mengine ambayo yanatufunulia picha ya Mandela sio tu kama mwanasiasa na mpigania ukombozi maarufu bali kama binadamu. Ni kitabu kikubwa, kurasa 454. Nitakuwa nakisoma kidogo kidogo. Isipokuwa ni kimoja kati ya vitabu vya pekee kabisa katika maktaba yangu.


2 comments:

emuthree said...

Huyu kweli ni mzee wetu na hazina ya wanamapinduzi wa kweli. Mimi nampenda huyu mzee kwa msimamo wake, kama kiongozi, unapokuwa kwenye nchi. Yeye hakujali wala kuogopa madola makubwa, kama wamekosea aliweza kutoa kauli isiyo na utata. Ndio hivyo, vya kale ni dhahabu!

Mbele said...

Ni kweli usemavyo kuhusu Mandela. Sasa basi, nimekuwa nikisoma soma sehemu mbali mbali za hiki kitabu, na kusema kweli, fikra na nasaha zake zinagusa sana. Nimeanzia na barua alizoandika akiwa kifungoni katika kisiwa cha Robben.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...