Kila siku naviangalia vitabu vyangu nilivyo navyo hapa ughaibuni. Ni vingi sana. Jana nilikichomoa kitabu kimojawapo, Lord of the Flies, kilichotungwa na William Golding, ili nikiongelee hapa katika blogu yangu.
Lord of the Flies ni moja ya vitabu vilivyonigusa sana nilipokisoma nikiwa sekondari. Kilikuwa ni kitabu kimojawapo cha lazima katika somo la "Literature." Kilituvutia sana vijana wa wakati ule.
Ni kitabu cha hadithi ya kubuniwa, yenye ujumbe mzito kuhusu tabia ya binadamu. Tunawaona vijana wadogo kutoka U-Ingereza wakiwa wamepata ajali ya meli na kuachwa katika kisiwa peke yao. Hakuna mtu mzima. Wanawajibika kujipanga ili waweze kuendelea kuishi, kwa kutegemea uwindaji humo kisiwani, na wanawajibika kujitungia utaratibu wa kuendesha jamii yao.
Hao ni watoto waliolelewa katika maadili mazuri huko kwao u-Ingereza, lakini katika mazingira ya kupotelea humo kisiwani, tunawaona wakididimia kimaadili, na hatimaye tunashuhudia wanavyoanza kuwa wabaya kabisa, na hii jamii yao inagubikwa na ukatili.
Hatimaye, kwa bahati kabisa, meli inaonekana kwenye upeo wa macho baharini. Insogea hadi kufika hapa kisiwani. Vijana wanaikaribia na nahodha anapowaona anashangaa kuona walivyoathirika katika kuishi wenyewe bila watu wazima. Anaposikiliza masimulizi yao, anashindwa kuamini jinsi walivyopoteza ustaarabu waliolelewa nao.
Hayo ndiyo ninayokumbuka kuhusu dhamira ya riwaya hii. Tangu wakati ule tulipoisoma riwaya hii nilifahamu kuwa ni riwaya ambayo imewapa changamoto kubwa wanasaikolojia na wanafalsafa wa tabia ya binadamu, kwa maana kwamba inazua masuala mazito. Je, watoto ni malaika kama tunavyodhani au wana silika ya ubaya wa kupindukia kama wabaya wengine wowote? Je, hayo tunayoyaita maadili yana mshiko kiasi gani, au yanategemea tu mazingira, na kwamba mazingira yasipokuwepo, maadili yanaweza kutoweka kabisa?
Lakini kuna pia suala la sanaa ya mwandishi Golding, ambayo imetukuka sana. Ana ubunifu wa hali ya juu, wa kumgusa sana msomaji, jinsi anavyoelezea maisha na mahusiano ya hao watoto humo kisiwani. Matumizi yake ya lugha yalikuwa ni kivutio kimoja kikubwa sana kwangu. Niliguswa na jinsi anavyoelezea mazingira, kwa mfano.
Nilipokuwa mwanafunzi Mkwawa High School, niliendeleza juhudi zangu za uandishi ambazo nilianza miaka iliyotangulia. Niliandika hadithi iitwayo "A Girl in the Bus," ambayo ilichapishwa katika jarida la BUSARA, lilokuwa maarufu katika vyuo vikuu vya Afrika Mashariki. Hii ilikuwa ni hadithi yangu ya kwanza kuchapishwa katika jarida la kimataifa. Nakumbuka jinsi nilivyofurahi kuisoma hadithi yangu katika jarida maarufu namna hii, ambamo walikuwa wanaandika waandishi maarufu wa Afrika Mashariki, na mimi nikiwa ni kijana wa "High School" tu. Nilikuwa na furaha isiyoelezeka, wakati napitapita mjini Iringa. Katika hadithi hii niliiga kwa kiasi fulani mtindo wa William Golding katika kuelezea mazingira.
Mwaka huu, nikiwa katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nililitafuta jarida BUSARA nikaisoma hadithi yangu, kwa furaha na mshangao kuwa niliweza kuandika vizuri namna ile wakati wa ujana wangu. Lakini, William Golding alichangia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment