Leo 28 Oktoba 2012
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Bidamu (THRD-Coalition), wadau wanaounda
mtandao huu na mwanachama mwanzilishi wa Mtandao likiwa ni shirika
lenye majukumu ya ya kutetea uhuru wa habari kusini mwa Afrika (MISA-Tan) tunaendelea kwa pamoja kuonyesha kusikitishwa kwetu kwa kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi.
Kwa
mara kadhaa sasa tunawakutanisha tena lengo likiwa ni kuendelea
kuishawishi serikali ilifungulie gazeti la Mwanahalisi. Kwa vile hoja
yetu ya kutaka kuliona gazeti la Mwanahalisi likiwa mitaani haijatimia
basi na sisi kwa upande wetu kazi yetu bado haijatimia.
Tunatambua umuhimu wa kuheshimu sheria za nchi, lakini kwa upande
mwingine tunaona kwamba ipo haja ya sisi watetezi wa haki za binadamu
kupitia kwenye vyombo vya habari na pia kwenye mashirika mengine
yanayounda mtandao huu kuishawishi serikali kuachana na sheria gandamizi
ambazo ni za kidikteta kama sheria hii ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo
hukiuka misingi ya haki za binadamu na utawala bora. Pia kwamba
maendeleo ya kiteknolojia na kisiasa hapa nchini yanaiweka rehani sheria
hiyo gandamizi.
Tumebaini kuwa kufungiwa kwa gazeti la
Mwanahalisi siyo tu kwamba kunawaathiri kwa kiwango kikubwa wasomaji
wake ndani na nje ya nchi bali pia kunaathiri uhuru wa kutafuta, kupata
na kueneza habari, kunawaathiri waajiriwa wa gazeti hilo na familia zao
na pia kunaiweka katika hati hati hata kampuni nzima ya Halihalisi
ambayo ndiyo mchapishaji wa gazeti hilo.
Tunaendelea kusisitiza
kuwa sababu walizotumia viongozi wa wizara ya habari kulifungia gazeti
la mwanahalisi sio za kweli kwani kilichoandikwa na Mwanahalisi ni
ukweli mtupu ambao hivi karibuni umethibitishwa na tamko la Dr Steven
Ulimboka.
Pia, hivi karibuni Dkt Stephen Ulimboka, kupitia kwa
wakili wake Mheshimiwa Nyaronyo Kicheere aliweka wazi kwamba Afisa wa
Usalama wa Taifa Ramadhan Ighondu alihusika katika kutekwa kwake kwa
kuwa mazingira yote kabla na baada ya tukio yanaonyesha wazi kuwa
Ramadhani Ighondu ni mdau katika tukio hili.
Kinachoshangaza
zaidi ni kwamba baadala ya serikali kutoa tamko kwamba sasa imepata
uhakika kwamba afisa wake alikiuka kanuni za ajira yake na ingeaza rasmi
kuwasaka washirika wa afisa hiyu jambo hilo halijatokea mpaka sasa huku
gazeti hili lililosidia kubainisha ushahidi likifungiwa. Zaidi,
tulitegemea serikali ingemkana afisa huyo kwamba siyo mwajiriwa wake
katika idara hiyo, kama hivyo ndivyo ilivyo, au vinginevyo tungeitarajia
serikali itangaze kwamba inachukua hatua za kisheria dhidi ya afisa
huyo ambaye ametajwa kuhusika katika makosa ya jinai kinyume cha
utaratibu wa mwajiri wake. Pia tungetemea Jeshi la polisi lingetumia
fursa hii kumkamata mshukiwa huyu wa Usalama wa Taifa na kulisadia Jeshi
la Polisi kuwapata wale waliotekeleza udhalimu huu dhidi ya Dr Steven
Ulimboka. Kwa namna yoyote vitendo vya aina hiyo vinaiabisha serikali na
haviwezi kuwa sehemu ya utawala bora ambao serikali yetu imekuwa
ikitangaza kwamba inauzingatia.
Mpaka sasa kumekuwapo na
matamko mbali mbali kutoka kwa wadau, viongozi wa kiroho, mabalozi na
hata Baraza la Habari Tanzania (MCT) likiwa peke yake na hata kwa
kushirikiana na wadau wengine wakilaani kufungiwa kwa gazeti hili lakini
serikali imeendelea kuwa kaidi katika hili.
Tunachosisitiza
1. Kwa Serikali
Tunaendelea kuwasihi viongozi wa nchi waone sasa umuhimu wa kukutana na
viongozi wa Hali Halisi na kujadili namna ya kulifungulia gazeti hili
kwani tayari Dr Steven Ulimboka ameshaweka wazi kilichoandikwa na
Mwanahalisi ni cha kweli kabisa. Serikali itambue kuwa suala hili sio
dogo katika anga za kidemokrasia na haki za binadamu kwani ubabe wa
baadhi ya viongozi serikalini leo unaweza iweka nchi pabaya siku za
usoni.
2. Vyombo vya Habari
Vyombo vya habari pamoja
na taasisi mbalimbali katika tasnia ya habari tuweke tofauti zetu
pembeni na kuungana kwa pamoja katika hili na kuhakisha kuwa
ukandamizaji wa uhuru wa habari kama huu wa wazi wazi haupati nafasi
katika enzi hizi za uwazi na ukweli. Vyombo na taasisi mbalimbali za
habari bado mna nafasi na uwezo mkubwa katika kuhakisha gazeti la
Mwanahalisi halipotei katika tasnia ya habari hapa nchini.
3. Jumuiya ya Kimataifa
Kwa kuwa mmekuwa wadau wakubwa wa maendeleo na utekelezaji wa haki za
binadamu hapa nchini, tukiwa tunaendelea kuuthamini mchango wenu,
tunawasihi muendelee kuishawishi serikali kwa njia za kidiplomasia
kuhusu suala la kuheshimu kazi za watetezi haki za binadamu na uhuru wa
habari. Nafasi zenu za kidiplomasia na uhusiano mkubwa mlionao na
nchi ya Tanzania inaweza pia kutumika kushawishi viongozi wa Tanzania
walifungulie gazeti la Mwanahalisi.
Kutokana na hali ilivyo ya
uvunjifu wa haki za watetezi wa haki za binadamu ikiwamo haki ya kutoa
habari, MISA-Tan, mwanachama wa THRD-Coalition anaehusika na uhuru wa
habari inaandaa mkutano wa siku moja utakaowakutanisha wadau
mbalimbali katika tasnia ya habari ili kujadili hatma ya gazeti la
Mwanahalisi na uhuru wa habari nchini.
Mwisho Tunawasihi
wanaharakati, watanzania wote wasichoke wala wasirudi nyuma katika
azma hii ya kutetea haki, uhuru na ulinzi kwa haki na watetezi wake.
CHANZO: KATUNEWS BLOG
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment