Monday, October 22, 2012

Ngoma Nzito Marekani: Tanzania Je?

Pamoja na mapungufu yake yote, siasa Marekani ina mambo kadhaa ya kupigiwa mfano. Kinachonivutia zaidi ni mijadala inyofanyika baina ya wagombea kabla ya uchaguzi. Leo, kwa mfano, tumeshuhudia pambano la tatu baina ya Obama na Romney

Mijadala ya namna hii inawapa wapiga kura fursa ya kuwasikiliza wagombea. Vile vile naiona kama namna ya kuwaheshimu wapiga kura.

Mfumo wa Marekani unatambua kuwa wapiga kura wana haki ya kuwasikia wagombea wakiongelea masuala kadha wa kadha katika kupambanishwa na wapinzani wao.

Ninakerwa ninapokumbuka mambo yalivyo kwetu Tanzania. Ninakerwa nikikumbuka jinsi CCM ilivyotoroka midahalo mwaka 2010. Ni dharau kwa wapiga kura. Tatizo ni jinsi wapiga kura wengi walivyo mbumbumbu, wasitambue kuwa hili lilikuwa dharau. Walipiga kura kama vile hawajadharauliwa.

Hebu fikiria mambo yangekuwaje ule mwaka 2010 iwapo Kikwete angepambana na Slaa katika midahalo mitatu hivi, ambayo ingeonekana katika televisheni na kusikika redioni. Lakini tulinyimwa fursa hii, kutokana na maaumzi muflisi ya CCM.

Hakuna sababu yoyote kwa nini siku zijazo tusifanye kama wa-Marekani wafanyavyo. Watangazaji makini wa redio na televisheni tunao, ambao wanaweza wakaendesha mahojiano nasi tukapata fursa nzuri ya kuwabaini wababaishaji na kuwatupilia mbali.

2 comments:

Anonymous said...

Mimi ni mfuatiliaji mzuri wa chaguzi za Marekani.Naamini suala la midahalo ni sehemu ya utamaduni wa Wamarekani wa kujinadi kwa hoja katika masuala muhimu ya kijamii. Lakini suala la midahalo linaenda sambamba pia na umuhimu wa kuendesha kura za maoni.
Hapa kwetu hata kura za maoni zikiendeshwa, wadau wakuu (hasa wanapoona kuwa kura hizo haziwapendezi) huzipuuza na hata kuziponda, japo kama zina ukweli wa hali halisi.
Tatizo kubwa hapa kwetu ni pia ukosefu wa waendeshaji makini na waliojiimarisha katika shughuli hizo za uendeshaji midahalo na kura za maoni. Napenda nimtoe ndugu Mbele hofu kuwa ifikapo mwaka 2015 tutakuwa na waendeshaji wa haja wa mambo hayo. Kwa upande wa midahalo, watu kama Rose Mwakitwange, Kitila Mkumbo na wengineo wanaweza kuwa chachu muhimu.
Bado sina hakika kama Synovate wamejipanga vema kujiaminisha mbele za umma juu ya uendeshaji wa kura za maoni. Nadhani kuna haja ya kujisajili kwa chombo maalum kama The Commission on Presidential Debates (CPD)ya Marekani.
Hatujachelewa kwani hata kamisheni hii Marekani imeanzishwa mwaka 1987 na vyama viwili vikuu vya siasa, Democratic na Republican (sehemu ya utamaduni komavu wa kisiasa).
Je, tuamini kuwa kwa Tanzania ni wakati wake tuwe na chombo kama hiki??

Anonymous said...

Sio rahisi kukubali midahalo kwasababu wanajijua kama hawawezi kujitetea miaka 50 ya uongozi.Ikiwa naibu waziri wa elimu anahutubia mkutano nje ya Tanzania na kusema "muungano wa visiwa vya Zimbabwe na Pemba"Na kutojistukia kabisa kama amekosea ili kurekebisha,unadhani mdahalo utaongeleka?Kingereza ndio usiseme kama "zecomedy"

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...