TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA(THBUB) YATOA TAARIFA YAKE YA KIFO CHA DAUDI MWANGOSI
Mwenyekiti
wa Tume Ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Jaji Kiongozi (Mstaafu)
Amiri Ramadhan Manento (katikati) akiongea na waandishi wa habari
hawapo pichani jijini Dar es Salaam Oktoba 10,2012 wakati akitoa
muhtasari wa taarifa ya Uchunguzi wa Tume yake kuhusu tukio
lililopelekea kifo cha Daudi Mwangosi kilichokea Septemba 2, 2012
kijijini Nyololo. Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa.Kushoto ni Makamu
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mahfoudha.A.
Hamid na kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Tume
hiyo Florida Kazora.
Mwenyekiti
wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Jaji Kiongozi
(Mstaafu) Amiri Ramadhan Manento akionyesha taarifa kwa waandishi wa
habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuhusu Muhtasari wa wa
Taarifa ya tume yake ya Uchunguzi wa tukio lililopelekea kifo cha
Mwandishi wa habari wa kituo cha Chanel Ten Daudi Mwangosi kilichotokea
Septemba 2, 2012 kijijini Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani Iringa,.
Makamu
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mahfoudha.A.
Hamid akijibu moja ya Swali kutoka kwa Mwandishi wa Habari (hayupo
pichani) leo jijini Dar es Salaam kuhusu Muhtasari wa wa Taarifa ya
tume yake
ya Uchunguzi wa tukio lililopelekea kifo cha Mwandishi wa habari wa
kituo cha Chanel Ten Daudi Mwangosi kilichotokea Septemba 2, 2012
kijijini Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani Iringa.
Waandishi
wa Habari wakiwa kwenye ukumbi wa mkutano wa ofisi ya Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa Muhtasari
wa wa Taarifa ya tume yake
ya Uchunguzi wa tukio lililopelekea kifo cha Mwandishi wa habari wa
kituo cha Chanel Ten Daudi Mwangosi kilichotokea Septemba 2, 2012
kijijini Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani Iringa.Picha na Mwanakombo
Jumaa - MAELEZO.
2.2 Ukiukwaji wa Misingi ya Utawala Bora
3.0 MAONI NA MAPENDEKEZO
MUHTASARI
WA TAARIFA YA TUME YA HAKI ZA BINADAMU
NA UTAWALA BORA YA UCHUNGUZI WA TUKIO LILILOPELEKEA KIFO CHA DAUDI
MWANGOSI KILICHOTOKEA SEPTEMBA 2, 2012 KIJIJINI NYOLOLO, WILAYA YA MUFINDI,
MKOANI IRINGA
- UTANGULIZI
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ni idara huru ya serikali iliyoundwa kwa mujibu wa Kifungu
cha 129(1)(c) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka
1977 na Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Na. 7
ya mwaka 2001. Jukumu kubwa la Tume ni kulinda, kutetea na kuhifadhi
haki za binadamu nchini. Katika kutekeleza jukumu hilo Tume imepewa
mamlaka ya kupokea malalamiko (kwa njia mbalimbali) kutoka kwa mtu yeyote
au kuanzisha uchunguzi wake yenyewe endapo itaona kuna uvunjifu wa haki
za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Kwa kuzingatia majukumu hayo, Tume ilianzisha uchunguzi wake yenyewe
baada ya vyombo vya habari kutoa taarifa ya tukio la kifo cha Daudi
Mwangosi. Tume iliunda timu ya watu watatu iliyoongozwa na Mhe. Kamishna
Bernadeta Gambishi akisaidiwa na maafisa wawili, Bwana Gabriel Lubyagila
na Bwana Yohana Mcharo. Timu hiyo ilifanya uchunguzi wake kuanzia tarehe
13-19 Septemba, 2012.
Katika uchunguzi uliofanywa, Tume ilizingatia zaidi masuala
ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala
bora. Hivyo basi, Tume ilitilia maanani Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, sheria mbalimbali za nchi na mikataba ya kimataifa
na ya kikanda inayohusu haki za binadamu ambayo Tanzania imeridhia.
Kwa kuzingatia matakwa ya sheria ya Tume Na. 7 ya
mwaka 2001, baada ya uchunguzi huo kukamilika, Tume imeandaa taarifa
yake na kuiwasilisha kwenye mamlaka husika kwa hatua zaidi.
Taarifa ya uchunguzi wa Tume imegawanyika katika sehemu kuu nne, ambazo
ni:
- Maelezo ya viongozi, watendaji na wananchi waliohojiwa
- Uchambuzi wa taarifa/vielelezo vilivyopokelewa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinazohusiana na masuala ya haki za binadamu
- Matokeo ya uchunguzi
- Maoni na mapendekezo.
Kwa kuwa tukio la kifo cha Daudi Mwangosi liligusa hisia
za jamii, Tume imeona ni vyema kukutana na wawakilishi wa vyombo vya
habari ili kutoa taarifa yake.
2.0 MATOKEO YA UCHUNGUZI
Katika uchunguzi wake Tume imebaini kuwa:
- Tarehe 02/09/2012 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliruhusiwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mufindi (OCD) kufanya mikutano ya ndani na kuzindua matawi mapya. Lakini jioni ya tarehe 01/09/2012 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa (RPC), alizuia CHADEMA kufanya mikutano iliyoruhusiwa na OCD ambaye ni “Officer In-charge” wa polisi wa eneo husika kama sheria inavyotaka.
- Viongozi wa CHADEMA walikuwa na mazungumzo na Mkuu wa Polisi Mkoa Upelelezi (RCO) na kuruhusiwa kufungua matawi yao bila ya kuwa na mikutano ya hadhara.
- Msajili wa vyama vya siasa aliwaandikia barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha shughuli zao kwa sababu ya sensa.
- Wakati shughuli za uzinduzi wa tawi la Nyololo ukiendelea, RPC alifika katika eneo hilo na kuamuru viongozi wa CHADEMA wakamatwe; na kuwa wafuasi wa CHADEMA walipinga kukamatwa kwa viongozi wao.
- RPC aliamuru kupigwa kwa mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi waliokusanyika katika ofisi za tawi hilo la CHADEMA.
- Baada ya mabomu ya machozi kupigwa, wananchi walitawanyika na kukimbia ovyo; na kuwa marehemu Daudi Mwangosi alizingirwa na askari, aliteswa na hatimaye inadaiwa alipigwa bomu na kufa hapo hapo.
- Daudi Mwangosi aliuwawa umbali wa takriban mita 100 kutoka ilipo Ofisi ya CHADEMA tawi la Nyololo.
- Katika tukio hilo wananchi kadhaa walijeruhiwa kwa mabomu, wakiwemo Mwandishi wa Habari wa Nipashe, Bwana Godfrey Mushi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake CHADEMA Wilaya ya Mufindi, Bibi Winnie Sanga na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mufindi, Asseli Mwampamba aliyekuwa akifanya jitihada za kumuokoa marehemu Daudi Mwangosi.
Kutokana na hayo yote, Tume imejiridhisha kuwa tukio lililopelekea
kifo cha Daudi Mwangosi limegubikwa na uvunjwaji wa haki za binadamu
na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
2.1 Uvunjwaji wa Haki za Binadamu
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania 1977, sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Azimio la Kimataifa
la Haki za Binadamu (Universal Declaration of Human Rights of 1948), Mkataba wa Kimataifa kuhusu haki za kiraia na kisiasa (International
Covenant on Civil and Political Rights of 1966) na Mkataba wa mataifa
ya Afrika kuhusu Haki za Binadamu na Watu (African Charter on Human
and Peoples Rights of 1981), Tume imejiridhisha kuwa Jeshi la Polisi
limevunja haki zifuatazo:
- Haki ya kuishi,
- Haki ya kutoteswa na kupigwa,
- Haki ya usawa mbele ya sheria na
- Haki ya kukusanyika na kutoa maoni.
CHADEMA ni chama cha siasa ambacho kina usajili
wa kudumu. Chini ya sheria ya vyama vya siasa (Cap. 258
RE. 2002), vyama vya siasa vyenye usajili vimeruhusiwa
kufanya maandamano na kuwa na mikutano ya kujitangaza baada ya kutoa
taarifa kwa “Afisa wa Polisi” wa eneo husika. Baada ya taarifa
kutolewa chama husika kinatakiwa kipewe ulinzi na “security agencies”
(mawakala wa usalama).
2.2 Ukiukwaji wa Misingi ya Utawala Bora
Ili pawepo utawala bora mamlaka zote za serikali ni lazima
zifuate utawala wa sheria. Uchunguzi umebaini kuwa kamanda wa
Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda tarehe 02/09/2012 katika utekelezaji
wa majukumu yake alikiuka Sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002)
kifungu cha 11(a) na (b) na sheria ya Polisi (Sura ya 322) kwa kuingilia
kazi za OCD wa Mufindi na kutoa amri ya kuzuia shughuli za CHADEMA wakati
yeye hakuwa “Officer In-charge” wa polisi wa eneo husika. Kwa maana
hiyo amri aliyoitoa haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na mtu ambaye
hakuwa na mamlaka kisheria kutoa amri hiyo. Haya ni matumizi mabaya
ya mamlaka, hivyo ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Aidha, hatua ya Msajili wa vyama vya siasa, Mhe. John Tendwa kuwaandikia
barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha shughuli zao kwa
sababu ya sensa ilikiuka misingi ya utawala bora kwani maelekezo yaliyotolewa
ndani ya barua hizo yanakinzana na sheria ya takwimu Na. 1 ya mwaka
2002 inayotoa fursa kwa wananchi kuendelea na kazi zao wakati wa sensa
pia ni kinyume na sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002) Kifungu
cha 11(a) na (b) inayotoa fursa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli
zake bila ya kuingiliwa.
Ibara ya 8(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inaelezea kwamba Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na
Haki ya Kijamii, aidha ibara 18(b) na (c) ya Katiba inaeleza kuwa kila
mtu anayo haki ya kufanya mawasiliano (kutoa maoni/habari) na haki ya
kutoingiliwa katika mawasiliano yake. Haki hii imekiukwa kwa kiasi
kikubwa na Jeshi la Polisi katika tukio la Nyololo Mufindi kwa kuwa
waandishi wa habari na wafuasi wa CHADEMA walizuiwa na Polisi kufanya
shughuli zao za kupata habari na za kisiasa. Huu ni ukiukwaji
wa misingi ya utawala bora kwa kuwa hali hiyo inazorotesha au inafifisha
uhuru wa habari.
3.0 MAONI NA MAPENDEKEZO
Kwa kuzingatia Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Na. 7 ya mwaka 2001 Kifungu cha 15(2)(c)
na 28 Tume inapendekeza yafuatayo:
- Kamati za ulinzi na usalama za Mkoa na Wilaya ziwe makini na vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utalawa bora vinavyofanywa na mamlaka mbalimbali kwenye maeneo yao. Aidha, kamati hizo zihusike moja kwa moja na usalama wa wananchi na mali zao kwa kujadili masuala yote ya kiusalama kabla hatua hazijachukuliwa na vyombo vinavyotekeleza sheria.
- Viongozi wa CHADEMA na wafuasi wao waepuke malumbano na vyombo vya dola kwa kutii maagizo yanayotolewa na vyombo hivyo bila shuruti. Pale wanapogundua kuwa pana uonevu au upendeleo ni vyema busara ikatumika ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea.
- Jeshi la Polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa waepuke kufanya maamuzi au matendo yanayoibua hisia za ubaguzi au upendeleo miongoni mwa jamii wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria. Mfano, Jeshi la Polisi lilizuia mikutano ya CHADEMA kwa sababu ya sensa wakati huo huo Chama cha Mapinduzi (CCM) walikuwa wakifanya uzinduzi wa Kampeni huko Zanzibar. Aidha, rai ya Msajili wa vyama vya siasa haikuzingatiwa kwa upande wa CCM Zanzibar huku CHADEMA walishurutishwa na Polisi kutii rai hiyo.
- Demokrasia ya mfumo vya vyama vingi iheshimiwe na kulindwa.
- Elimu ya vyama vya siasa na sheria ya Polisi kuhusu vyama vya siasa itolewe kwa askari polisi ambao wanaonekana kutozifahamu kabisa.
4.0 HITIMISHO
Jukumu la kulinda amani na utulivu ni wajibu
wa kila mtanzania, mkulima na mfanyakazi, viongozi wa serikali na watumishi
wa umma wote wanapaswa kuwa wazalendo wa kweli wakati wanapotekeleza
majukumu yao ya kila siku. Tume inatoa wito kwa watanzania wote
kuheshimu haki za binadamu na kutekeleza kwa vitendo misingi ya utalawa
bora. Kwa kufanya hivi Taifa letu litaendelea kuwa na amani na
utulivu. Tume inatoa rai kwa jeshi la polisi kutekeleza wajibu
wake mkuu wa ulinzi na usalama wa raia bila kutumia jazba.
Kuwepo kwa vyama vya siasa ionekane kuwa ni kukuwa kwa demokrasia
na sio kuwa ni upinzani kwa chama tawala.
.............................. ......................
Jaji Kiongozi (Mstaafu) Amiri R. Manento
MWENYEKITI
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA
BORA
OKTOBA 10, 2012
CHANZO: MICHUZI-MATUKIO
2 comments:
Ni hatua nzuri sana kama kweli watatufanyia haya lakini nawaomba waangalie upya na yale ya waisilamu ya mwembe chai na Zanzibar mwaka 2001 chini ya uongozi wa Mkapa.Ni lazima uwepo mfano katika mifano ili serikali iliyokuwepo madarakani pamoja na serikali zijazo iwe ni fundisho kwa viongozi kuonea raia.
Shukrani kwa ujumbe wako. Mimi pia ni mmoja wa wale wenye msimamo kwamba haki ni haki, na kila mtu anastahili kutimiziwa haki yake, bila ubaguzi wowote.
Post a Comment