Nimesoma taarifa mtandaoni sasa hivi kuwa mwandishi Mo Yan wa China ameikwaa tuzo ya Nobel katika fasihi kwa mwaka huu.
Sikuwahi kusikia jina la mwandishi huyu. Hili si jambo la kujivunia.
Ni kweli kuwa kuna waandishi wengi sana maarufu hapa duniani. Sio rahisi kwa mtu kuwa amesoma au anasoma maandishi ya wale wote wanaopata tuzo ya Nobel.
Kwa mfano, mwaka 2006 tuzo ya Nobel katika fasihi aliitwaa Orhan Pamuz wa u-Turuki. Sidhani kama niliwahi kusikia hata jina lake kabla. Nilijisika vibaya kuwa sina hata ufahamu wa mwandishi huyu. Hatimaye nilijikakamua nikanunua kitabu chake kimojawapo. Nadhani kwa sasa ninavyo viwili, ila bado sijapata wasaa wa kuvisoma.
Inapotokea habari ya mwandishi kupata tuzo kama hii ya Nobel, nchi zingine hufanya hima kutafsiri maandishi ya washindi hao, iwapo lugha yao ni tofauti. Watatafsiri maandishi ya Mo Yan katika lugha zao.
Tanzania hatuna utamaduni huo. Tunadanganyana kuwa sisi ni mabingwa wa ki-Swahili, ambacho kwa kweli hatukitumii kwa nidhamu itakiwayo. Hatufundishi ki-China, ki-Jerumani, ki-Rusi, na kadhalika. Hata ki-Arabu, lugha ambayo imekuwemo nchini mwetu kwa miaka zaidi ya elfu, hatufundishi. Kwa hivyo, utajiri wa uandishi uliomo katika lugha hizi hautufikii.
Kamati inayotoa tuzo ya Nobel imetamka kuwa maandishi ya Mo Yan yamejengeka katika "hallucinatory realism." Kwa vile hii dhana imeandikwa ki-Ingereza, nafahamu fika inamaanisha nini. Lakini ukiniuliza niitafsiri kwa ki-Swahili, nitababaika, pamoja na kwamba ni msomi wa kiwango cha juu. Huu ni ushahidi wa tatizo nililoongelea hapa juu, linalotusibu wa-Tanzania. Tukiambiwa tuelezee dhana kama hii ya "hallucinatory realism" kwa ki-Swahili, tutabaki tunahangaika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
1 comment:
Profesa Mbele wewe kiboko. Licha ya kutufahamisha na kutuelemisha umezusha mawazo mazuri sana ndani ya misumari ya maandishi haya machache uliyoweka. Hata miye mpenzi na msomaji mkubwa wa vitabu na fasihi sikuwahi kumsikia Mo Yan. Uzuri wa tuzo kama hizi huwasaidia watu duniani kuzijua nchi na fasihi nyingine na kustaarabika kifikra. Hapa wewe umechangia kwetu kujiuliza je tunakifanyia nini Kiswahili? Ni kama mtu uliyelalia kitanda ca sukari, mto wa asali na shuka ya mandazi lakini huna habari navyo unalia kwa uchungu wa njaa, chawa na pilipili.
Post a Comment