Tofauti na miaka iliyopita, maonesho ya leo yalifanyika sehemu iitwayo State Fairgraounds. Miaka iliyopita maonesho haya yalikuwa yakifanyika Minneapolis Community and Technical College, mjini Minneapolis. Miji ya St. Paul na Minneapolis inagusana, na mgeni huwezi kujua mpaka ni wapi.
Kama kawaida, watu walikuwa wengi, tangu kuanza kwa maonesho hadi kumalizika.
Kama ambavyo nimesema tena na tena, inavutia kuona jinsi wa-Marekani wanavyothamini matamasha ya vitabu. Wanaanza kufika hata kabla milango haijafunguliwa. Vijana, wazee, wake kwa waume wanahudhuria. Pia wako wanaokuja na watoto. Nimeongea na watoto kadhaa waliofika na wazazi wao kwenye meza yangu. Baba mmoja alifika na binti wawili wadogo, labda umri wa miaka kumi hivi. Baba ni mzungu, na hao mabinti ni weusi. Mmoja alisema anataka kununua kitabu changu cha Matengo Folktales. Mimi nilidhani kuwa baba yake ndiye atalipa. Lakini haikuwa hivyo. Mtoto alitoa hela yake akanipa. Nilipomwambia baba yake kuwa sikutegemea hivyo, baba alisema "ndio ana hela yake ya kulipia." Nilivyomwangalia, niliona kama ni mtoto wa miaka yapata kumi tu.
Nilichelewa kufika, dakika kama 45 hivi, lakini halikuharibika neno. Nilipanga vitabu vyangu mezani, nikaanza kuongea na wadau. Kitu kimoja cha pekee ni kuwa kwa nyakati tofauti, zilikuja familia mbili kutoka Bemidji, mji ambao uko upande wa kaskazini wa Minnesota. Nilifurahi kuwasikia wanatoka Bemidji. Niliwaeleza kuwa nimeshafika kule. Jambo la pili, ambalo liliwashangaza ni pale nilipowaeleza kuwa mimi ni mpenzi wa mwandishi Hemingway, na kwamba Bemidji ndio nyumbani kwa Mary Walsh, mke wa mwisho wa Hemingway. Niliwaeleza kuwa Hemingway na Mary Walsh walisafiri pamoja nchini Kenya na Tanganyika, baina ya mwaka 1953-hadi 1954. Pia niliwaeleza kuwa lengo langu moja ni kwenda Bemidji na kutafuta habari za mama huyu.
1 comment:
Nashukuru Profesa kwa kutushirikisha maonesho ya Vitabu, na jinsi Wamarekani wanayothamini kununua vitabu hata watoto wa miaka kumi, na kujinunulia kwa fedha zao wenyewe. Ni dhahiri kuwa wanataka kupata hekima kutoka kwa watu walio na hekima zaidi kupitia vitabu/ mawazo ya watu wajuzi zaidi. Huo ni mfano mzuri wa kuigwa na ni utamaduni ambao tunahitaji kuujenga katika jamii zetu, kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuo na kwa wananchi wa kawaida- kama ilivyo siku za nyuma hapa Tanzania ambapo kulikuwa na maktaba katika ngazi za Wilaya nk.
Aidha, nimalizie kusema kuwa nakushukuru kwa kutuhabarisha na mambo mazuri yanafaa kigwa siku zote.
Post a Comment