Saturday, October 6, 2012

Nimejipatia iPad

Pamoja na kuwa mimi ni mmoja wa wale watu wa zamani tuliozaliwa na kukulia kijijini na ambao tunababaishwa na hizi tekinolojia zinazofumuka kwa kasi, nimejipatia kifaa kiitwacho iPad siku chache zilizopita. Nimenunua iPad Wi-Fi+3G. Nilishinikizwa na binti yangu Zawadi. Ndiye anayenisukuma niende na wakati.

Tangu ninunue kifaa hiki, yapata wiki mbili zilizopita, nimekuwa katika kujifunza namna ya kukitumia, maana kina mambo mengi sana. Angalau naweza kutembelea mitandao, kutuma na kupokea barua pepe, na kupiga picha na kisha kuziangalia. Hata video najua namna ya kupiga.

Kitu ninachotaka kukifanya hima ni kuingiza vitabu pepe kwenye hii iPad, nikianzia na kitabu changu kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho wadau wanakipata mtandaoni, pamoja na vitabu vyangu vingine, kwa njia hiyo.





Kidogo najisikia vibaya kwamba nilikiweka kitabu hiki katika muundo wa kitabu pepe na wadau wanakinunua, wakati mimi mwenyewe sikuwa na kifaa cha kuingizia vitabu pepe wala sikuwahi hata kuona kinakuwaje katika umbo la kitabu pepe. Nimejisikia kama mpishi ambaye anawapikia wengine lakini yeye mwenyewe hata kuonja haonji. Sasa, na hii iPad yangu, ngoja nikae mkao wa kula, kwa vitabu vyangu na vya wengine.

5 comments:

Jeff Msangi said...

Prof.
Hongera sana kwa kujisogeza hatua kadhaa mbele hususani katika kitu kinachoitwa tekinolojia.Kama ulivyogusia,tekinolojia hizi zinakua kwa kasi sana na ni wazi kwamba hatuwezi kwenda nazo sambamba kila wakati.Hata hivyo,inapowezekana(kama ilivyowezekana kwako),basi hatuna budi kuzitumia ipasavyo.

Katika iPad napenda mambo matatu;kwanza ni vitabu.Ukiingia katika iTunes unaweza kujipatia vitabu vizuri sana.Kitu cha pili ninachopenda ni kuperuzi mtandao kwa kutumia iPad.Flawless wanasema wenyewe.Cha tatu napenda kutizama filamu au video mbalimbali kupitia YouTube nk(napenda zaidi kutizama documentaries).

Nisema karibu na endelea kufurahia tekinolojia.

Mbele said...

Shukrani sana ndugu Msangi. Kwanza napenda nijikumbushe jinsi wewe na Freddy Macha mlivyonihamasisha hadi nikawa mwanablogu. Sijasahau, na nawashukuru.

Na huyu binti yangu anavunjika mbavu ninapomhadithia jinsi nilivyozaliwa kijijini nikakulia nikiwa nachunga mbuzi na ng'ombe. Kwa hivyo, anajitahidi kunisogeza hatua mbele kutoka katika fikra za kichunga mbuzi na kuniingiza katika huu ulimwengu wa sasa.

Kama ulivyofanya, naye ananielezea mambo mengi yaliyomo katika hii iPad. Ni maajabu kabisa, hasa kwa sisi watoto wa wakulima.

Asante sana kwa ujumbe wako.

Filipo Lubua said...

Nyinyi vijana wa zamani mnakuwa wakaidi kufuatana na mambo ya vijana wa sasa, ila mtalazimika maana kila kitu kimeshabadilika. Mmepata fursa ya kuishi katika vipindi viwili visifyofanana. Hata hivyo niwape pongezi maana mmeweza kuvitangamanisha vipingi hivi viwili na kwa hakika vijana wa sasa tupigapo hatua moja, twawaona nanyi mko pembeni yetu tukisonga pamoja.

Kama alivyofanya binti yako, vijana wa sasa hatutaki tuwaache nyuma maana tukiwaacha nyuma, bila shaka, hamtatumegea yale ya enzi zenu, ambayo nasi twatamani tungeyaonja pia.

Twatambua kuwa "fagio jipya linafagia vyema, bali la zamani linajua kona zote". Sisi ni mafagio mapya, twaweza kufagia vyema sana; bali ni lazima tuwatumie nyie mlio mafagio ya zamani, maana mwazijua kona zote. Kwa sababu sisi twafagia vyema, na kwa sababu nyinyi mwazijua kona zote, basi inakuwa vyema kuwa nyinyi mwatuongoza katika kona zote na kutuonyesha wapi pa kufagia. Mara mtuonyeshapo, nasi twafagia vyema kweli :)

Anonymous said...

je huyo binti yako anakucheka kama utani au nikwanini ulisomea vijijni?je hujawahi kumletanyumbani kupaona?mimi pamoja ninaishi hapa dsm nimelazimika wanangu wasomee hukohuko kijijini ilikusudi waishi maisha ambayo ni halisi

Mbele said...

Ndugu anonymous, shukrani kwa kutembelea hapa na kuleta suali. Ukweli ni kwamba anacheka kwa sababu ninaongelea suala la kuchunga mbuzi kwa namna ya kuchekesha. Anawaheshimu watu wa kijijini. Alishafika kule, na huwa ananisukuma nifanye mipango ya yeye na dada zake kwenda kuwaona ndugu kijijini. Kwa hilo hana tatizo kabisa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...