Monday, October 1, 2012

Vitabu Nilivyonunua Leo



Leo baada ya mizunguko kwenye mji wa Apple Valley, niliingia katika duka la vitabu la Half Price Books, ambalo nimeshaliongelea kabla.

Kama ilivyo kawaida hapa Marekani, kwenye duka la vitabu, hawakosekani wateja, na mara kwa mara kunakuwa na msongamano.

Leo nilinunua vitabu vitano. Kimoja ni Three Plays cha Sean O'Casey. Huyu ni mwanatamthilia maarufu wa Ireland. Nilipokuwa nasoma Chuo Kikuu Dar es Salaam, 1973-76, tulisoma tamthilia yake mojawapo iitwayo Purple Dust. Ilituvutia sana. Ingawa nahisi kitabu cha Three Plays ninacho katika shehena ya vitabu vyangu vilivyopo Tanzania, nimeona ni vema nikawa na nakala nyingine. Sean Ocasey alikuwa mtu wa ajabu, kwa jinsi ambavyo alivyokuwa mtoto maskini wa mitaani, akajielimisha mwenyewe hadi kufikia hadhi ya kuwa mwandishi anayeheshimiwa sana duniani.

Kitabu kingine nilichonunua ni Reality, Man and Existence: Essential Works of Existentialism, kilichohaririwa na H.J. Blackham. Kitabu hiki kina maandishi ya Kierkegaard, Sartre, Nietzsche, Jaspers, Buber, na Merleau-Ponty, ambao ni wanafalsafa maarufu sana. Kati ya vitabu vyangu vilivyopo Tanzania, kuna mengi ya maandishi ya wanafalsafa hao na wengine. Hapa Marekani pia nina vitabu vyenye maandishi yao. Lakini sikuona tatizo kununua kitabu hiki cha Reality, Man and Existence, kwa sababu kimekusanya maandishi machache muhimu ya wanafalsafa waliotajwa. Mtu unaweza kusafiri na kitabu hiki, ukajisomea.

Nimenunua pia vitabu viwili vya Robert Louis Stevenson. Kimoja ni The Strange Case of Dr. Jekyll and Mr. Hyde and Other Stories. Kingine ni Treasure Island. Kwa wafuatiliaji wa fasihi ya ki-Ingereza, hadithi ya Dr. Jekyll and Mr. Hyde ni maarufu. Kwetu tuliosoma sekondari miaka ya sitini na kitu nchini Tanzania, tulisoma kwa bidii maandishi ya waandishi kama Robert Louis Stevenson. Kwa mfano, tunaikumbuka vizuri Treasure Island.

Kitabu cha tano nilichonunua leo ni A Moveable Feast, cha Ernest Hemingway. Ninayo nakala ya kitabu hiki hapa ughaibuni. Lakini, muda fulani uliopita nilianza kusoma taarifa kuwa limechapishwa toleo jipya la kitabu hiki, na walioandaa toleo hilo ni Mzee Patrick Hemingway na Sean Hemingway. Mzee Patrick Hemingway ni mtoto pekee wa Ernest Hemingway ambaye bado yuko hai. Sean Hemingway ni mjukuu wa Ernest Hemingway. Wameshirikiana kuandaa hili toleo jipya, ambalo limejumlisha baadhi ya mambo ambayo hayakuwemo katika toleo la mwanzo, lililoandaliwa na Mary Hemingway, ambaye alikuwa mke wa mwisho wa Ernest Hemingway. Mimi ni mpenzi mkubwa wa maandishi ya Hemingway, kama nilivyogusia hapa. Nina hamu ya kusoma toleo hili la A Moveable Feast, nione yaliyomo ambayo hayakuwepo katika toleo la mwanzo.

9 comments:

PBF Rungwe Pilot Project said...

Hongera Profesa kwa kutushirikisha jambo hili muhimu,kwa maana utamaduni wa kununua vitabu hapa Tanzania ni mgeni na kwa wasomi hauvitii sana, kwa vile mkazo ni katika kununua vitu mbalimbali- hata kwa wanafunzi wa vyuo.
Asante kutukumbusha kuwekeza kwenye vitabu

Mbele said...

Shukrani kwa kutembelea hapa kwetu na kuweka maoni. Ni kweli utamaduni wa kununua vitabu ni mgeni hapa Tanzania. Napenda nikupe dondoo moja tu.

Nikiwa mhadhiri Chuo Kikuu Dar, nilifika Marekani kusomea shahada ya juu mwaka 1980. Wakati ule, Nyerere alikuwa ametufundisha vizuri masuala ya uwajibikaji, tukamwelewa.

Basi mimi, katika miaka yangu ya kusoma Marekani, nilifanya kila juhudi katika masomo, na nikatumia hela zangu za ziada kununulia vitabu, kwa miaka yote sita, nikijua kuwa vitabu ndio zana itakayonifanikishia ufundishaji wangu nitakaporejea Chuo Kikuu Dar.

Mwaka 1986, baada ya kuhitimu, nilirudi chuo Kikuu Dar nikiwa na shehena kubwa ya vitabu. Kilichonishtua ni kuwa jamii ilinishangaa kwa kuleta vitabu badala ya "pick-up." Na kweli mimi sikuja na gari bali hivyo vitabu, na watu waliniona nimechamsha.

Kwa mujibu wa Profesa Mugyabuso Mulokozi, ambaye alinitunzia hivyo vitabu vyangu, vitabu vimewafaidia wa-Tanzania wengi, hasa katika masomo ya juu. Kwa vile niliacha kufundisha pale Chuo Kikuu Dar mwaka 1991, watu wanaotumia vitabu hivyo kwa ujumla huenda hawajui kuwa ni vyangu. Cha zaidi ni kuwa kwa miaka niliyokaa tena hapa ughaibuni, nimenunua vitabu vingi kuliko vile vilivyoko Tanzania.

Halafu hapa Marekani nilipo, sijawahi kuwaona wa-Tanzania kwenye maduka ya vitabu, wala kwenye matamasha ya vitabu. Utamaduni ule ule ulioko Tanzania, wa kutothamini vitabu, wanakuja nao huko ughaibuni. Nami nimeandika tena na tena kuhusu tatizo hili.

Kwa hapa Minnesota, kutakuwa na tamasha kubwa la vitabu tarehe 13 mwezi huu, kama nilivyoelezea hapa. Nitashiriki, ila nitashangaa iwapo nitamwona m-Tanzania hata mmoja.

PBF Rungwe Pilot Project said...

Nashukuru sana Profesa kwa maelezo na habari zinazohusu jinsi gani ulivyochangia kusaidia wanafunzi kupata vitabu vya kujisomea kwa gharama ya kujinyima huko ughaibuni ulipokwenda kusoma. Mara nyingi watu wanaotoka kusoma huko ughaibuni hutegemewa kuja na vitu kama magari n.k. Lakini wewe ulichagua fungu lililobora zaidi, yawezekana wengi wetu wa wanafunzi tulisoma Chuo Kikuu cha Dar-E-salaam, wamefaidika na vitabu ulivyonunua bila hata kufahamu. Kwa niaba ya hao wote, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa moyo wako mkuu uliokuwa nao

Unknown said...

Ni lazima nikiri kwamba nimekosa uhondo mkubwa kutoijua blogu hii mapema. Siku mbili tu za kuifahamu zimetosha kunithibitishia kuwa nipo kwenye darasa maridhawa.
Kwa hakika sitabanduka kwenye darasa hili.

Unknown said...

Na kuhusu desturi ya kupenda vitabu, kwa kweli bado tuna changamoto kubwa. Chuoni(UDSM)nilijijengea utaratibu wa kununua vitabu. Kwa kweli rafiki zangu(wanafunzi wa sheria) walinishangaa sana niliponunua vitabu kama ''Bad Muslim, Good Muslim: America, Cold War and the Roots of Terror'' au riwaya ya ''The Concubine'' ya Elechi Amadi. Kwa bahati mbaya, desturi ya kununua vitabu chuoni imejikita kwenye ununuzi wa vitabu vya taaluma ambayo mtu anasomea(hasa vile ambavyo vilivyo kwenye ''course outline''.
Naomba niseme kwamba Profesa Mbele umenipa mshawasha mkubwa na nitaendelea kujibinya kwa pesa ''kiduchu'' ninayopata kununua vitabu vya maarifa mbalimbali.

Mbele said...

Shukrani ndugu Ado Shaibu, kwa yote uliyosema. Nafurahi kuwa umekigundua kiblogu changu hiki, ukakipenda.

Vitabu ni moja ya mada ninayoiongelea sana, kwani mimi mwenyewe ni msomaji wa vitabu sana na pia mwandishi, na mnunuaji mkubwa wa vitabu.

Kutokana na yote hayo, nafahamu namna usomaji unavyotajirisha akili. Ninaweza kuongelea mambo mengi sana muda wowote, kutokana na usomaji. Natamani kila m-Tanzania angefanya juhudi kwa kadiri ya uwezo wake.

Ninafika Tanzania tarehe 3 Januari, na tukiwasiliana, naweza kukuleta vitabu viwili vitatu kama zawadi, kwa jinsi ulivyoikuna roho yangu kwa kujitokeza na kusema kuwa nawe ni mdau wa vitabu.

Mbele said...

Ndugu Ado Shaibu, nimeona picha yako, ukiwa na Dr. Lwaitama na Profesa Shivji. Lo, hao ndio tulikuwa wote pale UDSM. Profesa Shivji tayari alikuwa mwalimu wakati nilipanza kusoma pale mwaka 1973. Dr. Lwaitama alikuja kusoma baada yangu. Ukitaka habari zangu, waulize wao. Wananifahamu sana.

Unknown said...

Samahani kwa kuchelewa. Funzo kubwa nilililolipata toka kwako ni kwamba hakuna kitu azizi kama kitabu.
Nami ninaanza kujifunza desturi ya kukifanya kitabu kuwa zawadi iliyo bora kwa wale niwapendao. Siku nikienda kwetu Tunduru, napanga kumchukulia Mwalimu wangu aliyenifundisha pale shule ya msingi Nanjoka. Kwa vile ana hamasa na masuala ya siasa na jamii, nadhani vitabu vya Insha za Mapambano ya wanyonge cha Prof.Shivji na kitabu chako cha Changamoto vitamfaa sana. Ingawa sijakisoma bado, natumaini kitabu cha Changamoto kimejaa changamoto chungutele.

Mbele said...

Ndugu Ado Shaibu, ninafika Tanzania tarehe 3 Januari. Nitakuletea zawadi ya hiki kitabu cha CHANGAMOTO, ukisome kisha ukipeleke Tunduru. Umenikumbusha mbali, kwani Tunduru nilishafika mara kadhaa, miaka ya sabini na kitu.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...