Siku za hivi karibuni kumekuwa na zogo kubwa Tanzania kutokana na wanafunzi kushindwa mtihani wa dini yao. Sikufuatilia vizuri undani wa kisa hicho na siwezi kukiongelea. Badala yake, napenda tu kuongelea suala la kinadharia la mtu kushindwa mtihani kuhusu dini yake.
Tunapokuwa kanisani au msikitini, kwenye mihadhara ya dini au madrassa ya dini, tunafundishwa dini yetu kwa maana ya kwamba tunaelekezwa tuelewe dini inasema nini ili tuwe waumini bora. Suala ni kutujenga kiimani na kimaisha kwa mujibu wa dini yetu, kutokana na yale anayofundisha padri, imam au sheikh.
Mambo ni tofauti tunapokuwa shuleni au chuoni. Mimi ni mwalimu, na ingawa sifundishi dini, napenda kusema kuwa darasani hatufundishi kwa lengo la kujenga imani ya watu kwenye dini yao. Labda kabla sijaenda mbali, nifafanue kuwa naongelea kiwango cha chuo. Kwenye madarasa ya mwanzo, ambako tunawafundisha watoto, naamini tunategemewa kuwafundisha dini kwa lengo la kuwafanya wawe waumini bora.
Lakini, lengo langu hapa ni kuongelea ufundishaji wa dini vyuoni. Kwenye chuo, kazi yetu ni kutafakari na kuchambua dini, kuhoji na kudadisi. Tunawajibika kutafakari historia ya dini husika, mafundisho yake, mwelekeo wake, athari zake katika jamii na kadhalika.
Chuoni tunapaswa sio tu kusoma na kuongelea yaliyomo katika misahafu na yaliyosemwa na watetezi wa dini husika, bali tunapaswa pia kusoma na kutafakari yaliyosemwa na wapinzani wa dini. Kwa mfano, ni wajibu kutafakari kauli kama zile za Karl Marx kwamba dini ni kama bangi ya jamii yenye matatizo. Darasani tunapaswa kujadili kauli za aina hiyo kwa makini, na kila mwanafunzi anawajibika kutumia akili yake ili kujenga hoja zake.
Kwa hivyo, hata kama mtu ni muumini bora wa dini yako, mtu ambaye umeelewa na kukubali kila kinachosemwa kanisani au msikitini, ukija kwenye mtihani unaweza kufeli. Kwa msingi huo huo, kwa vile darasani ni mahali pa kuchambua na kutafakari masuala, kama mtihani ni wa dini ya u-Islam, muislam anaweza kufeli na m-Kristu akafaulu. Vile vile, kwenye mtihani wa dini ya u-Kristu, mu-Islam anaweza akafaulu na m-Kristu akafeli.
Napenda kutoa mfano ambao unaweza kufafanua hoja yangu. Nakumbuka tulipokuwa shuleni, mkoani Ruvuma, mbali kabisa na pwani, tulikuwa tunajiamini kwamba pamoja na kuwa ki-Swahili si lugha yetu ya kwanza, tuna uwezo wa kufaulu mitihani ya ki-Swahili kuliko vijana wa pwani ambako ki-Swahili ni lugha yao ya kwanza. Kama nakumbuka vizuri, matokeo ya mitihani yalidhihirisha jambo hilo, nasi tukawa tunawacheka vijana wa pwani.
Basi, katika mitihani ya dini mambo ni hayo hayo. Watu tusijiaminishe kuwa kwa vile sisi ni waumini wa dini fulani, basi ni lazima tufaulu mtihani wa dini hiyo. Ukweli ni kuwa kwa vile shuleni au chuoni somo la dini linakuwa katika mkabala wa ki-taaluma, hata mtu asiye na dini anaweza kufaulu mtihani wa dini na sisi waumini tukafeli.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
2 comments:
nikweli Profesa wangu wengine wanafikiri mtihani wa dini ni kuongea hadithi za mtume au kuongea mambo ya miujiza ya yesu kumbe unatakiwa uchambuzi wa kina haswa wa kama mambo uliyoyaongea
Shukrani kwa kutembelea "hapakwetu" na kuweka ujumbe. Niliona nitoe hiyo tahadhari kwani naamini wengi tuko usingizini.
Post a Comment