Profesa huyu tulifahamiana miaka yapata kumi iliyopita kwenye mikutano ya washauri wa programu ya Associated Colleges of the Midwest (ACM) ambayo hupeleka wanafunzi Tanzania. Miaka ile yeye alikuwa anafundisha Chuo cha Beloit. Wakati wa kupanga na kutathmini hali ya program kila mwaka, nachangia kwa namna ya pekee masuala yanayohusu tofauti za tamaduni, ambayo ni changamoto kwa wa-Marekani na wa-Tanzania.

Kwenye mikutano yetu hiyo, nilikuwa, na bado niko, mstari wa mbele kufafanua matukio mbali mbali na mambo mengine wanayokumbana nayo wanafunzi katika kuishi na wa-Tanzania.
Profesa Greenler alipochukua fursa ya kupeleka wanafunzi Tanzania, aliniomba niandike mwongozo angalau kurasa hata tatu tu, wa masuala hayo, ili yamsaidie katika safari yake. Nililitafakari ombi lake, hatimaye nikaanza kuandika.
Leo nimemkumbusha Profesa Greenler alivyonihamasisha katika suala hili, na nikamsisitizia binti yake kuwa habari ndio hiyo. Tumefurahi sana kukutana na kukumbushana mambo ya Bongo. Ameniambia tena kuwa yeye na familia yake wanaikumbuka sana Tanzania na wanaipenda.
Amenielezea pia kuhusu wanafunzi wa ACM aliowapeleka Tanzania miaka ile, na ambao wanaendelea kuwa na uhusiano na Tanzania. Hili ni jambo la kawaida, na sisi tunaohusika na programu hizi tunafarijika tunapoona kuwa zimechangia kujenga mahusiano baina ya watu wa nchi hizi mbili.
Hata hivi, kwa kuzingatia kuwa profesa huyu ni kati ya wa-Marekani wengi sana ambao ni wapenzi wa Tanzania, ilibidi nimwambie kuhusu maandamano na vurugu Zanzibar na Dar es Salaam, ambayo yanachafua jina la Tanzania. Miaka yote iliyopita ilikuwa rahisi na heshima kuinadi Tanzania kama nchi ya amani na utulivu, lakini ni sherti kusema ukweli unaojitokeza sasa.
1 comment:
Duu kweli elimu ni kiboko. Kwa kweli mwl usingekazania elimu leo hii ungefamahamiana wapi na hao hao watu mashuhuri? duu
Post a Comment