Thursday, July 15, 2010

Ninasoma "Siku ya Watenzi Wote"

Kwa siku kadhaa sasa nimekuwa nikisomaa Siku ya Watenzi Wote, kitabu cha Shaaban Robert, ambacho nilikinunua tarehe 8 Julai pale Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu Dar es Salaam, kwa bei ya shilingi 5,000 tu.

Ninapenda kusoma vitabu muhimu kama hivi vya Shaaban Robert, kama nilivyoandika katika blogu hii na katika kitabu cha CHANGAMOTO. Nimeamua kujielimisha ili niweze kuandika kwa ki-Swahili vizuri iwezekanavyo. Ni jitihada binafsi ya kujikomboa kutokana na kasumba na fikra potofu tulizo nazo wengi, hasa wasomi, kuhusu lugha ya ki-Swahili. Ninataka kuonyesha heshima kwa lugha hii kwa kuiandika kwa usahihi.

Mambo mengi yaliyomo katika Siku ya Watenzi Wote yanatokea Dar es Salaam. Tunawaona wahusika wakiwa katika mitaa kama Kichwele, Ilala, Mnazi Moja, Kariakoo, na Msasani. Hii inafurahisha, kwani mwandishi anauenzi mji huu kwa kuuweka kitabuni namna hii. Inanikumbusha hadithi za mwandishi Moyez Vassanji, kama vile Uhuru Street, ambaye naye aliandika sana kuhusu Dar es Salaam.

Katika Siku ya Watenzi Wote, ambacho kinasemekana kuwa ni kitabu chake cha mwisho, Shaaban Robert anarejea katika masuala ambayo alikuwa ameyashughulikia katika maandishi yake yaliyotangulia, kwa miaka mingi. Shaaban Robert anaongelea na kutafakari masuala muhimu ya jamii, kama vile tofauti za matabaka, tabaka la maskini na tajiri, hali ya wanawake. Tunamsikia Shaaban Robert mwanafalsafa, mchambuzi wa masuala ya jamii, mwenye hisia nzito kuhusu maana ya maisha, mahusiano baina ya wanadamu, haki, na utu. Shaaban Robert anawakosoa walimwengu kwa ufinyu wa mawazo ambao tunauendekeza kwa kisingizio cha dini.

Kitabu kama Siku ya Watenzi Wote ni hazina kubwa. Kila ukurasa una mambo ya kugusa akili na hisia, kupanua mawazo na ufahamu wa lugha. Thamani ya kitabu kama hiki ni kubwa mno, wala haipimiki kwa fedha, hata kama kingeuzwa kwa shilingi 50,000.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...