Thursday, July 15, 2010

Ninasoma "Siku ya Watenzi Wote"

Kwa siku kadhaa sasa nimekuwa nikisomaa Siku ya Watenzi Wote, kitabu cha Shaaban Robert, ambacho nilikinunua tarehe 8 Julai pale Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu Dar es Salaam, kwa bei ya shilingi 5,000 tu.

Ninapenda kusoma vitabu muhimu kama hivi vya Shaaban Robert, kama nilivyoandika katika blogu hii na katika kitabu cha CHANGAMOTO. Nimeamua kujielimisha ili niweze kuandika kwa ki-Swahili vizuri iwezekanavyo. Ni jitihada binafsi ya kujikomboa kutokana na kasumba na fikra potofu tulizo nazo wengi, hasa wasomi, kuhusu lugha ya ki-Swahili. Ninataka kuonyesha heshima kwa lugha hii kwa kuiandika kwa usahihi.

Mambo mengi yaliyomo katika Siku ya Watenzi Wote yanatokea Dar es Salaam. Tunawaona wahusika wakiwa katika mitaa kama Kichwele, Ilala, Mnazi Moja, Kariakoo, na Msasani. Hii inafurahisha, kwani mwandishi anauenzi mji huu kwa kuuweka kitabuni namna hii. Inanikumbusha hadithi za mwandishi Moyez Vassanji, kama vile Uhuru Street, ambaye naye aliandika sana kuhusu Dar es Salaam.

Katika Siku ya Watenzi Wote, ambacho kinasemekana kuwa ni kitabu chake cha mwisho, Shaaban Robert anarejea katika masuala ambayo alikuwa ameyashughulikia katika maandishi yake yaliyotangulia, kwa miaka mingi. Shaaban Robert anaongelea na kutafakari masuala muhimu ya jamii, kama vile tofauti za matabaka, tabaka la maskini na tajiri, hali ya wanawake. Tunamsikia Shaaban Robert mwanafalsafa, mchambuzi wa masuala ya jamii, mwenye hisia nzito kuhusu maana ya maisha, mahusiano baina ya wanadamu, haki, na utu. Shaaban Robert anawakosoa walimwengu kwa ufinyu wa mawazo ambao tunauendekeza kwa kisingizio cha dini.

Kitabu kama Siku ya Watenzi Wote ni hazina kubwa. Kila ukurasa una mambo ya kugusa akili na hisia, kupanua mawazo na ufahamu wa lugha. Thamani ya kitabu kama hiki ni kubwa mno, wala haipimiki kwa fedha, hata kama kingeuzwa kwa shilingi 50,000.

4 comments:

Fadhy Mtanga said...

Ndugu Mbele nafurahi sana kwani kila nikifika hapa huchota maarifa mengi sana. Sikufahamu kama mwanafalsafa na kielelezo cha fasihi ya Kiswahili hayati Shaaban Robert aliandika pia kitabu hicho. Nitakitafuta.

Juzi nimepita pale duka la vitabu la Tanzania Publishing House mtaa wa Samora na kukuta vitabu vyake kadhaa kama Mapenzi Bora, Kusadikika, Kufikirika, Wasifu Wa Siti, Maisha yangu na Baada ya Miaka Hamsini.

Hakika Shaaban Robert ndiye fasihi ya Kiswahili. Kwenye kitabu cha mapenzi bora nimefurahi kuona ameandika utenzi wenye beti zaidi ya elfu moja. Jana yote nimejaribu kufanya kama yeye lakini nimeishia kuandika beti mia moja. Hii ina maana viatu vyake ni vikubwa mno maana pamoja na kujaza makaratasi bado havinitoshi.

Napenda kujifunza sana kutoka kwenu. Ulifundisha umuhimu wa kujifunza uandishi mzuri.

bibi Alesha said...

Kaka Joseph, Pole na likizo na nafurahi umeweza kutembelea vitabu hasa vya kiswahili.

Naoomba sana tena sana unikusanyie nakala mbali mbali za Shaaban Robert, riwaya alizoandika Banzi, Kiu na naomba unitafutie kitabu cha Ujamaa by J.K Nyerere. Kama utakuwa mzigo nijulishe ili tuone kama mtaniwekea kwenye Fedex.

Kile kitabu kila anayekisoma anakitamani. Ukirudi nitakuwa nimeshaona ni akina nani wanakihitaji kiuhakika ili niweke oda yangu.

Furahia likizo yenye shughuli nyingi.

emuthree said...

Kama kuna kitu ambacho tunaweza kujivunia kwa nguvu zote kuwa ni chetu ni lugha yetu ya Kiswahili.
Wasiwasi wangu ni kuwa huenda huko mbelenii tukahangaika kutafuta wafadhili wa kuja kutusaidia kukiweka hiki kiswahili kiwe fasaha.
Nasema hivi kwasababu watu hawataki kujifunza vyema lugh yetu hii kwa kuwasoma wakongwe wa lugha kama akina Shaban Robert. Hawa wenzetu wapo hai mpaka leo kutokana na michango yao waliyoitoa kwa lugha hii. Nafikiri kuna haja ya waigizaji wa tamithilia na michezo mbalimbali wakawa wanachukua hadithi za hawa wakongwe ili watu wazione, na kuifunza kwa njia hiyo kwani nasikitika kusema wengi hawataki kusoma vitabu wanapenda kuangalia.
Kwa kuthibisha hili, angalia hata hizi blogi tunazojitahidi kuzianzisha watu wanapenda zaidi blogi za picha na sio za kusoma habari ndefu nk.
Tunataka akina Shaban Robert wengi wazidi kukifanya kiswahili kuwa moja ya lugha za kimataifa.
emu-three

Unknown said...

Hakika kazi nzuri sana , shukrani Shabaan ni fahari ya fasihi na gwiji wa lugha pendwa ya kiswahili

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...