Walikuwa wakijadili utendi wa Hamziya, nami nilikaribishwa kuongelea tendi kwa ujumla.
Wazo moja ambalo lilionekana kuwasisimua wanafunzi ni mchango wa wanawake katika tendi, suala ambalo nililiongelea kwa kirefu kiasi, nikatoa mifano ya utafiti na uandishi wangu kuhusu suala hili. Mfano moja niliotoa ni utafiti wangu juu ya Gindu Nkima, shujaa katika masimulizi ya wa-Sukuma.
Maongezi haya yalikuwa ni changamoto kwangu, kwa sababu daima nimeongelea masuala haya ya tendi kwa ki-Ingereza, iwe ni kwa maandishi au kwa mihadhara. Niliwahi kuandika makala moja tu kwa ki-Swahili kuhusu tendi, “Ushujaa Katika Ras il Ghuli.”
Kutokana na hali hiyo, mara kadhaa katika mhandara wangu niliwajibika kuuliza tafsiri ya ki-Swahili ya dhana kadhaa za ki-Ingereza. Kwa mfano, nilipowauliza tafsiri ya “destiny,” nilifurahi kuambiwa kuwa tafsiri ni hatima.
Niliulizwa masuali mengi ya kufikirisha, baadhi yakiwa yamejengeka katika falsafa. Suali moja ninalolikumbuka lilikuwa maana ya kifo cha shujaa. Suali hili nililiona lenye upana na kina, kwani dhana ya kifo cha shujaa hujitokeza au kutojitokeza kwa namna mbali mbali katika tendi za tamaduni mbali mbali. Dhana ya kifo cha shujaa imefungamana na falsafa, imani, na hisia za jamii husika.
2 comments:
Prof umenikumbusha mbali sana...Nilipokuwa mdogo baba yangu alikuwa akininunulia vitabu vingi sana vya hadithi. Nakumbuka vitabu vya akina Alif lela ulela, Mashimo ya mfalme Suleiman,Hadithi za kiyunani, Hekaya za Abunuasi, Visa na Haidithi na Hadithi za Esopo...Achilia mbali Hadithi za kina Elistabrus Elvis Musiba,Adam Shafi,na wengineo.Hadithi ya Liongo uliyoitaja ndiyo imenikumbusha haya yote...kiasi kwamba naiona picha yake akipiga tawi la mti kwa upinde wake...Hadithi hiyo jinsi ilivyokuwa maarufu mtu mmoja aliwahi kuitaja katika shairi lake alilotunga kumponda nduli Iddi Amini. Shairi hilo bado nalikumbuka mpaka leo " Eti wewe ulisema, u wmenye nguvu za liongo. Ona sasa unapigwa, hata kurambishwa nyongo...." Ninachotaka kusema ni kwamba usomaji vitabu ni kitu muhimu sana na WAZAZI tunao wajibu wa kuwazoeza watoto wetu tabia ya kusoma vitabu. Hongera sana Prof Mbele. (Mwana dikala)
Professor shukrani kubwa sana kwa habari nzuri za kusisimua. Mimi ni mfuatiliaji wa karibu wa blog na habari zako. Tunakusikia vyema huku New Haven na Yale University. Nilitaka pia kukushirikisha kwenye blog yetu ya utamaduni, lugha, na ushairi wa Kiswahili. Tungefurahi sana kupata maoni na rai zako www.radiomrima.org shukrani sana.
Post a Comment