Tuesday, June 1, 2010

Nataka Kuandika Vitabu Bora Zaidi

Mimi ni mwandishi. Naweza kusema ninaendelea vizuri katika uwanja huo, kwani watu wanavitumia vitabu nilivyoandika, kama vile Africans and Americans, na Matengo Folktales, wakiwemo walimu vyuoni, katika masomo mbali mbali, hasa huku Marekani. Hata kijitabu kidogo cha Notes on Achebe's Things Fall Apart kimewahi kupendekezwa katika Chuo Kikuu cha Cornell, ambacho kinajulikana kwa masomo mengi, likiwemo somo la ki-Ingereza.

Kutokana na mafanikio hayo, ningeweza kusema niendelee kuandika kama ninavyoandika. Lakini mimi nataka kuandika vitabu bora zaidi, na ningependa kila kitabu ninachoandika kiwe bora kuliko vile vilivyotangulia.

Bado kuna fursa ya kufanya vizuri zaidi, na ni wajibu kuitumia fursa hiyo. Ninajua kuwa nikifanya juhudi, nitaandika vitabu bora zaidi. Ingawa naandika ki-Ingereza kiasi cha kuwaridhisha wale tunaowaita wenye lugha yao, na ingawa nakifahamu ki-Ingereza kiasi cha kuweza kuwafundisha hao watu, sijafikia kiwango cha Shakespeare. Kwa nini niridhike? Kuridhika kwa namna hii ni jambo baya. Kilichobaki ni kufanya bidii ili niandike vizuri zaidi.

Ningependa hili liwe somo kwa waandishi chipukizi. Wasiridhike na uandishi wao, bali wajitahidi muda wote kufanya vizuri zaidi.

4 comments:

Fadhy Mtanga said...

Ama kwa hakika hili ni somo muhimu sana kwetu sisi tunaochipukia katika fani ya uandishi. Ni wazi tunapaswa kufanya jitihada za makusudi. Sisi hatupaswi kuridhika hata kidogo ili kuwapa nafasi watakaozisoma kazi zetu kupima ubora wetu.

Prof Mbele, daima nachota maarifa ya thamani kila niingiapo hum. Lakini leo nimejifunza kitu kikubwa zaidi. Ahsante sana kwa somo la leo.

Mbele said...

Ndugu Mtanga, shukrani kwa ujumbe wako. Tungeweza kujifunza mengi kutoka kwa wana riadha maarufu. Utamkuta mtu kavunja rekodi ya dunia katika mbio za labda marathon au masafa mengine.

Ukimsikiliza anapohojiwa, utamsikia anasema anafanya mazoezi makali ili avunje rekodi yake mwenyewe.

Moyo huu tungekuwa nao sisi wote katika yale tunayoyafanya, tungekuwa haturidhiki na mafanikio yetu, wala hatupumziki, na matokeo yake yangekuwa mazuri sana.

kigonzile kwetu said...

Prof Mbele nachukua nafasi hii kutambua uwepo wako na kwamba naomba niwe na mawasiliano nawe ili nipate skill kidogo ya kuandika maandiko mbalimbali.

Mbele said...

Ndugu Kigonzile Kwetu, shukrani kwa ujumbe wako. Samahani sikuwa nimepita kwenye mada hii miezi mingi, na leo ndio napita. Vinginevyo ningekuwa nimekujibu kabla.

Sasa basi, nitakutafuta mtandaoni tuwasiliane zaidi kutimiza haya malengo uliyoelezea.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...