Tuesday, June 22, 2010

Kitabu cha CHANGAMOTO Kimetua Msoga, Bagamoyo

Tarehe 11 Juni, ndani ya basi kutoka Dar es Salaam kwenda Tanga, alikuja mtu moja akakaa kiti cha pembeni yangu. Kama kawaida yangu, nilikuwa na vitabu mkononi. Kimoja kilikuwa kitabu change kipya cha CHANGAMOTO. Sikujua kuwa wakati nasoma kitabu kingine, huyu jamaa alikuwa amekiangalia hicho cha CHANGAMOTO. Hatimaye aliomba kukiangalia, nami nilimpa.


Baada ya muda aliniambia kuwa amekipenda sana kitabu hiki, akataja mambo kadhaa yaliyomvutia, kwamba ni changamoto. Akauliza kama anaweza kununua kitabu kile. Nilivutiwa na jambo hili, kwani, kwa uzoefu wangu, jambo hili la kununua vitabu ni nadra katika Tanzania. Nilimwambia kuwa anaweza kukichukua. Nilimwambia kuwa nimefarijika na kufurahi kumkuta Mtanzania anayependa vitabu.


Hapo alisimama, akaenda mbele na kufungua begi lake ambalo alikuwa ametundika kwenye sehemu ya kuwekea mizigo. Akarudi na vitabu kadhaa, akanionyesha. Kitabu kimojawapo kilikuwa Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania cha Mwalimu Nyerere. Tena ilikuwa kitabu chenyewe asilia si nakala ya kurudufiwa.


Nilivutiwa sana, nikamwambia kuwa nimeshangaa kuona anacho kitabu hiki cha Mwalimu Nyerere, ambacho naamini hakiwapendezi watawala wa Tanzania, kwa jinsi kinavyowaponda. Nikamwelezea hisia zangu kuwa viongozi wetu hawazipendi fikra za Mwalimu Nyerere kuhusu masuala mbali mbali ya siasa, uchumi, na jamii.


Katika maongezi yetu, tulitambulishana majina pia. NIlimpa namba ya simu yangu. Huyu ndugu aliniambia kuwa anaitwa Gilbert Mahenge, na kuwa alikuwa akifanya shughuli kijijini Msoga. Tuliongelea masuala mengi ya maendeleo Tanzania, tukawa tunasikitikia hali ya umaskini katika nchi yetu yenye ardhi na rasilimali nyingi.


Baada ya siku mbili, nikiwa Tanga, huyu ndugu alinipigia simu. Aliongelea kitabu cha CHANGAMOTO, kuwa kimemfungua macho na kimeandikwa kwa mtiririko mzuri. Akasema ameshamwazimisha rafiki yake asome.


Nimeleta taarifa hii kwa sababu huyu ndiye mtu wa kwanza nchini Tanzania kukinunua na kukisoma kitabu changu. Nimeona niandike habari zake hapa, kwani ameweka historia, vile vile amenigusa kwa kuwa anatofautiana mno na waTanzania wengi, kwenye hili suala la vitabu.

6 comments:

Fadhy Mtanga said...

ndugu Mbele nami nampongeza huyu ndugu Mahenge. nami nakisubiri kwa hamu kubwa tarehe 24 pale Diamond kama ulivyoeleza. tafadhali usimalize nakala zote. nakutakia kila la kheri.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

interesting, ila angalau hata mimi ni msomaji wa blogu yako pia!!!!

Sam said...

Mimi kama mTanzania ninadhani ni msomaji mzuri ila si wa vitabu, ninasoma sana articles kwenye internet, magazeti (mf. Zamani za kina Ulimwengu nilisoma sana Rai, sasa Raia Mwema, Mwanahalisi, jamii forums, mzalendo, CNN, BBC n.k lakini nisichoelewa ni kuwa ni kwa nini sina tabia ya kusoma vitabu! Ni tabia ambayo sikujengwa nayo toka utotoni au sababu ni nini, na mara nyingine huwa najiuliza je labda nikinunua nitasoma hilo silijui, ila najua napenda kujenga tabia ya kusoma, ni tabia ambayo pia ningependa kuwajengea watoto wangu. Swali linabaki, naanzaje?

SN said...

Samuel, ni kujitahidi kuperuzi tu unapoona vitabu. Mara nyingi ukishajua unavutiwa na nini hasa kwenye vitabu vya aina fulani, basi ndio ujue itakuwa tabia yako.

Kwahiyo usichoke kutafuta vitabu au kujaribu kusoma hata utangulizi tu utakapobahatika kupata nakala mbili tatu. Mara nyingi - kama kitabu kina mtiririko mzuri - ukishaanza kusoma ndio hutakiacha mpaka umalize.

Kama unapenda siasa, hadithi fupi, tamthilia, historia za watu maarufu n.k. itakuwa sio mbaya ukianzia kwenye mambo unayopenda.

Mimi mama yangu alikuwa analeta vitabu vya kila aina nyumbani na nilikuwa mvivu kuvisoma. Lakini kuna siku akaleta "Gifted Hands". Dah! Nikakisoma mara tatu mfululizo (nilikuwa kidato cha nne). Nikaomba anitelee "Think Big"... Kilichofuata ni historia na sasa hivi ninajua napendelea vitabu vya aina gani.

Nimesoma vitabu vya Mandela (kwasababu hakuna filamu itakayokupa picha halisi ya maisha yake akiwa gerezani), Obama, Jackal, vitabu vya hadithi fupi kutoka Latin America n.k. Na napenda michezo, kwahiyo vitabu vya kina Bechkam, Roy Keane na Fergie...

Lakini mpaka sasa hivi ni kitabu kimoja tu ambacho sitakisahau na ninakushauri ukitafute. Kinaitwa "Disgrace" cha J. Cotzee. Anatumia hadithi za watu wa kawaida kuakisi yaliyokuwa yanaendelea Afrika Kusini:

http://www.gradesaver.com/disgrace/study-guide/about/

Yaani unajifunza historia ya Afrika Kusini na matatizo watu wa kawaida waliyoyapata kwa mpigo.

Pia, waandishi maarufu wanafanya utafiti kabla ya kuandika. Kwa mtazamo wangu, zile makala kwenye vyombo maarufu vya habari zinakuwa zimechujwa sana. Hakuna mtu atakayekupa picha halisi ya mambo yanayoendelea Rwanda au Congo kwenye makala zilizopo kwenye mtandao. Sijui umeona bloggers, reporters au columnists wangapi ambao wanaeleza kwa kina facial expressions, body language nk. za wahusika kwenye makala zao?

Mbele said...

Niko hapa Tanzania bado, nikizunguka huko na huko. Leo nimepata fursa ya kupitia tena ukurasa huu, na nawashukuru wadau kewa maoni yenu.

Baadhi ya vitabu vya J.M. Coetzee, kama vile "Disgrace," nimesoma na kufundisha pia. Ni mwandishi mahiri, aliyepata tuzo ya Nobel. Anatoka Afrika Kusini, ila sasa anaishi Australia.

Mbele said...

Kabla sijaondoka Tanzania, mteja huyu wa Msoga alinipigia tena simu, akishukuru kwa kitabu hiki.

Ni faraja kuwa m-Tanzania anarudi na kushukuru kwa yale aliyojifunza katika kitabu. Wala hakuongelea pesa aliyotoa. Hii kwangu ni faraja, nikizingatia jinsi pesa ilivyo ngumu kwa wananchi wa kawaida kama yeye.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...