Monday, August 29, 2016

Suluhu ya Maandamano

Ni muhimu kila mtu awe huru kutoa mawazo yake, kuliko kunyamazishwa. Wanataaluma katika saikolojia wanatufundisha kuwa ukandamizaji au unyamazishaji, kwa maana ya "repression," una madhara makubwa. Sigmund Freud, Carl Jung, na wafuasi wao ni kati ya wanataaluma hao.
Watu wakiwa huru kujieleza, wanapata ahueni kisaikolojia, na hii ni muhimu kwa afya ya mtu binafsi na kwa afya ya jamii. Kuhusu madhara ya "repression," hata wahenga walitahadharisha, waliposema "kimya kingi kina mshindo mkuu."
Wakati huu, wa-Tanzania wanapita katika kipindi kigumu sana, kutokana na mvutano uliozuka baina ya wapinzani wanaotaka kufanya maandamano nchi nzima kupinga kile wanachoita udikteta, na papo hapo, polisi, serikali, na baadhi ya raia hawataki maandamano haya yafanyike. Wengine wamesema watafanya maandamano yao ili kuyapinga yale mengine.
Ninaona hili si suala gumu. Wote wanaotaka kuandamana wapewe fursa ya kufanya hivyo, ili mradi wahakikishe kuwa maandamano yao ni ya amani, kama inavyotaka sheria. Sioni tatizo iwapo maandamano ya wapinzani yatafanyika sambamba na maandamano ya hao wengine.
Kitu rahisi ni waandaaji wa maandamano ya aina zote kukaa na polisi na kukubaliana utaratibu wa maandamano hayo. Kwenye mji kama Dar es Salaam, kwa mfano, wapinzani wanaweza kufanya maandamano yao Kinondoni, na hao wengine wakafanya maandamano yao Ilala. Sio lazima maandamano ya aina mbali mbali yafanyike katika mtaa huo huo na wakati huo huo. Jambo la msingi ni kutafuta namna ya kuwawezesha watu kuandamana kwa amani, kama katiba na sheria zinavyotamka.
Waandaaji wanaweza kujipanga kuhakikisha kuwa maandamano yao ni ya amani. Kwa mfano, waandaaji wa maandamano wanaweza kuwateua viongozi wengi wa maandamano. Kila kiongozi atakuwa na watu wake, kama vile kumi au hata ishirini, ambao ana wajibu juu yao, Hao wanakuwa pamoja wakati wa maandamano. Na kiongozi mwingine anakuwa na watu wake. Hata wakiwa waandamanaji elfu tano, hii inawezekana. Ninachopendekeza hapa ni utaratibu kama ule wa nyumba kumi kumi alioanzisha Mwalimu Nyerere, ambapo kila nyumba kumi zina kiongozi wake.
Sababu ya kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa maandamano hayaingiliwi na watu wasiohusika, kama vile vibaka. Wakati huo huo, polisi wawepo kusaidia kutoa ulinzi, kama inavyotaka katiba na sheria.
Maandamano ni haki ya wananchi wote. Ni muhimu kwamba tutafute kila njia ili kuhakikisha haki zisihujumiwe. Badala ya kuzuia maandamano na kuwatisha watu, jambo ambalo linajenga uhasama katika jamii, naona ni bora kukaa na kutafuta njia ya kuwezesha watu kutekeleza uhuru na haki zao na papo hapo kuhakikisha kuwa amani inadumishwa. Ninaamini kuwa hayo yote yanawezekana. Kwa ki-Ingereza tungesema kuwa hayo malengo mawili sio "mutually exclusive."

Sunday, August 28, 2016

Kimya (Muyaka bin Haji)

"Kimya kina mshindo mkuu," || ndivyo wambavyo wavyele.
Kimya chataka k'umbuu, || viunoni mtatile:
Kimya msikidharau, || nami sikidharawile.
             Kimya kina mambo mbele
            Tahadharini na kimya.

Kimya ni kinga kizushi || kuzukia wale wale.
Kimya kitazua moshi || mato msiyafumbule.
Kimya kina mshawishi || kwa daima na milele.
          Kimya kina mambo mbele:
          Tahadharini na kimya.

Kimya vuani maozi || vuani mato muole!
Kimya kitangusha mwanzi || mwendako msijikule.
Kimya chatunda p'um'zi || kiumbizi kiumbile!
          Kimya kina mambo mbele:
          Tahadharini na kimya.

(Muyaka bin Haji, 1776-1840)

Thursday, August 25, 2016

Ujumbe kwa Polisi wa Tanzania Kuhusu UKUTA

Kwanza napenda kusema kuwa jamii yote inatambua kazi kubwa na muhimu inayofanywa na polisi katika kulinda usalama na mali za wananchi, pamoja na mazingira magumu na uhaba wa vitendea kazi unaowakabili polisi. Raia wema tunashukuru tunapowaona polisi wakifanya doria mitaani, wakilinda sehemu muhimu kama mabenki, na kadhalika. Tunafurahi na kuwashangilia polisi wanapoweka mitego na kufanikiwa kuwanasa majambazi. Mioyo yetu inatulia tunapowaona polisi wako kwenye mikutano wakilinda amani. Wakati wa kampeni mwaka jana, kwa mfano, tuliona polisi walivyokuwa wakilinda mikutano ya vyama vyote vilivyoshiriki kampeni. Hayo yote na mengine mengi ni ya kujivunia, na ni sherti tukumbushane.
Ninapenda kuongelea hali ya sasa inayotokana na azma ya CHADEMA kutangaza kuwa itafanya mikutano na maandamano ya amani katika nchi nzima kupinga kile wanachoita udikteta. Katika mazingira haya, tunawasikia viongozi wa CCM wakitoa vitisho dhidi ya kampeni hiyo inayoitwa UKUTA. Wanadai kuwa maandamano haya yanaashiria uvunjifu wa amani. Viongozi wa CCM wamefanikiwa kuliaminisha jeshi la polisi kuwa maandamano haya hayana nia njema bali kuharibu amani.
Napenda kusema kwamba hizi kauli za viongozi wa CCM ni za kijinga. Wananchi wanafahamu umuhimu wa amani. Ni wao ndio walinzi wakuu wa amani, kwa sababu wanajua kuwa wanaihitaji. Haijalishi kama wanachi hao ni wanaCCM au wapinzani. Haijalishi kama hawana chama. Wote tunataka amani.
Kauli za viongozi wa CCM kwamba CHADEMA wanataka kuharibu amani ya nchi hazina mashiko. Mheshimiwa Freeman Mbowe, mwenyekiti wa CHADEMA, ni mfanyabiashara. Hainiingii akilini kuwa mfanyabiashara asipende amani, kwani amani ikivunjika, biashara zake hazitapona. Duniani kote, tunaona jinsi vibaka wanavyopora maduka na kuharibu biashara wakati amani inapovunjika. Hapa Marekani, kwa mfano, ikivunjika amani katika mji wowote, tunaona katika televisheni jinsi vibaka wanavyopora maduka na kuharibu biashara. Amani ikivunjika, wafanyabiashara ni waathirika wakuu.
Watanzania tunaposikia kauli za viongozi wa CCM tunapaswa kujiuliza: Je, ni kweli kwamba Mbowe anataka kuharibu amani? Kama ni kweli, basi Mbowe atakuwa ni mfanyabiashara wa ajabu, tofauti kabisa na wenzake, kama vile akina Bakhressa, Mohammed Dewji, Reginald Mengi, na wauza chipsi mayai mitaani. Muuza chipsi mayai anataka amani. Sembuse mfanyabiashara mwenye biashara kubwa na mali nyingi kama Mbowe?
Duniani kote wafanyabiashara, wawekezaji, na wajasiriamali wanaombea amani. Wawekezaji hawapeleki mitaji kwenye nchi isiyo na amani. Tanzania tunajivunia amani, na tunawaalika wawekezaji waje. Kama kuna mtu mwenye maslahi makubwa katika kuhifadhi amani, ni mwekezaji na mfanyabiashara. Propaganda za CCM kwamba Freeman Mbowe anataka kuhujumu amani ni ujinga.
Ninasikitika kwamba polisi wamerubuniwa na propaganda za kijinga za viongozi wa CCM. Matokeo yake tunayaona. Polisi wanakiuka wajibu wao wa kulinda amani katika mikutano na maandamano. Sheria ya vyama vya siasa inatamka wazi kuwa chama chochote hakiruhusiwi kutumia vyombo vya dola kuvitisha au kuvikandamiza vyama vingine. CCM inakiuka sheria hiyo, na inalitumia jeshi la polisi kinyume na sheria. Hili ni tatizo kubwa, na jeshi la polisi linawajibika kujirekebisha.

Wednesday, August 24, 2016

Sheria ya Vyama vya Siasa, Tanzania

                           TANGAZO LA SERIKALI NA. 215 la tarehe 12/10/2007

                                              SHERIA YA VYAMA VYA SIASA
                                                       (SURA YA 258)

                                                           -------------
                                                            KANUNI
                                          (Zimetungwa chini ya fungu la 22(b))

                                KANUNI ZA MAADILI YA VYAMA VYA SIASA ZA
                                                         MWAKA 2007

                                                 SEHEMU YA KWANZA
                                                         UTANGULIZI

1. Kanuni hizi zinaitwa kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa Mwaka 2007 na zitaanza kutumika mara tu baada ya kutangazwa katika Gazeti la Serikali.

2. Kanuni hizi, zitatumika Tanzania bara na vilevile Tanzania Zanzibar

3. Katika Kanuni hizi, isipokuwa pale muktadha utaelekeza vinginevyo- “chama cha siasa” maana yake ni chama cha siasa chenye usajili wa kudumu kwa mujibu wa Sheria.
“Msajili” maana yake ni Msajili wa Vyama vya Siasa aliyeteuliwa kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria pia itajumuisha Naibu Msajili na Msajili Msaidizi;
“Sheria” maana yake ni Sheria ya Vyama vya Siasa.

                                                 SEHEMU YA PILI
                                                 HAKI YA CHAMA

4.–(1) Kila chama cha siasa kitakuwa na haki zifuatazo-

(a) Kutoa elimu ya uraia na elimu ya uchaguzi kwa wananchi kwa kufuata sheria na kanuni za nchi;
(b) Kutoa maoni ya kisiasa kadri itakavyoona inafaa ili kutekeleza sera zake, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar;
(c) Kujadili na kushindanisha sera zake na zile za chama cha siasa kingine kwa lengo la kutaka kukubalika na wananchi;
(d) Kuwa na uhuru wa kutafuta kuungwa mkono na wapiga kura; na
(e) Kila Chama cha siasa kitakuwa na haki ya kufanya mikutano ya kisiasa na maandamano kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa;
(2) Wakati wa uchaguzi wowote utakaoendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi, kila chama cha siasa kitakuwa na haki na uhuru wa kushiriki na kushirikishwa na Tume ya Uchaguzi na au chombo chochote chenye mamlaka katika kufanya uchunguzi na kupata matokeo katika jambo au suala lolote linalohusu uchaguzi.

                                                     SEHEMU YA TATU
                                                    WAJIBU WA CHAMA

5.-(1) Kila Chama cha Siasa kitakuwa na wajibu wa kutunza maadili chini ya kanuni hizi kwa: -
(a) kukieleza kwa wanachama wake ili kuongeza uadilifu wa kisiasa ndani na nje ya chama cha siasa;
(b) kulaani, kuepukana kuchukua hatua zitakazofaa ili kuzuia au kuepusha vitendo vya vurugu, uvunjaji wa Amani au ukandamizaji wa aina yeyote ile;
(c) kutotumia vyombo vya dola kukandamiza na kutoa vitisho kwa chama cha siasa kingine kwa manufaa yake;
(d) kutotoa maneno yoyote au maandishi ambayo ni ya uongo na kuhusu mtu yeyote au chama cha siasa chochote;
(e) kufanya mkutano wa kisiasa na maandamano bila kufanya vurugu kwa mujibu wa sheria za nchi;
(f) kulaani na kupinga-
(i) vitendo vyenye kuashiria ukandamizaji;
(ii) matumizi ya lugha ya matusi
(iii) vitendo vya kibabe na vurugu
(iv) matumizi ya nguvu ili kujipatia umaarufu wa chama au sababu yeyote ile;
(f) Kuepuka kuteremsha bendera iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria, kuharibu kwa namna yeyote ile kitu chochote ambacho ni ishara au nembo inayotumiwa na chama kingine kama sehemu ya utambulisho wa chama hicho;
(g) Kuepuka kushawishi kwa kutoa rushwa kama kichocheo ili kupata upendeleo au heshima kwa nia ya kufanikisha malengo;
(h) Kuepuka kutumia mamlaka. Rsilimali za serikali, vyombo vya dola, au wadhifa wa kiserikali, kisiasa au ufadhili wa nje ama wa ndani kwa namna yeyote ile ili kukandamiza chama kingine.
(i) Kuepuka vitendo vya ubaguzi wa rika, kabila, jinsia, dini na mahali alipozaliwa mtu yeyote ikiwa ni jamii au asili Fulani kwa kufanikisha malengo ya siasa; na
(j) Kuheshimu maamuzi halali yaliyofanywa kwa pamoja na vyama vyote.
(2) Kwa kuzingatia Sheria, kila chama cha siasa kitakuwa na uhuru wa kushirikiana na chama cha siasa kingine kwa nia njema kwa ajili ya kupanga vikao, mikutano ya hadhara kwa pamoja au maandamano kwa wakati mmoja kama kwamba mambo hayo yamefanywa na chama cha siasa kimoja au bila kuvunja sheria za nchi.

                                                         SEHMU YA NNE
                                                     WAJIBU WA MSAJILI

6.-(1) ili kuhakikisha kwamba Kanuni hizi zinatekelezwa, Msajili atakuwa na wajibu wa-

(a) kusimamia maadili ya vyama vya siasa;
(b) kupoekea malalamiko yaliyowasilishw
a pande zote;
(c) kuzuia kitendo cha uvunjaji wa Kanuni za maadili kisiendelee na kukitaka chama au kumtaka kiongozi wa chama kujirekebisha; na
(d) kutoa onyo la maandishi kwa chama au kiongozi wa chama husika;
(2) Iwapo baada ya kutolewa onyo la kwanza kwa mujibu wa Kanuni (1)(d), chama cha siasa kitaendelea au kiongozi ataendelea kukiuka maadili hayo, Msajili atakemea hadharani ukiukwaji huo wa maadili.

7.-(1) Bila ya kuathiri masharti ya Kanuni ya 5, malalamiko dhidi ya uvunjwaji au ukiukwaji wa maadili yatapelekwa kwa maandishi kwa mtu yeyote kwa maandishi yakiwa yamesainiwa na mlalamikaji.

(2) Mara baada ya kupokea malalamiko, Msajili ataanza kufanya Uchunguzi dhidi ya chama cha siasa kinacholalamikiwa.


Imesainiwa na,                                                         EDWARD N. LOWASA
Dar es Salaam                                                                Waziri Mkuu
1 Oktoba, 2007

Monday, August 22, 2016

Tanzania: A Fake Crisis in the Making

With every passing day, Tanzanians await with bated breath, and some with apprehension, the arrival of September 1. That is the day the main opposition party, CHADEMA, has declared a day of nation-wide demonstrations against what it calls the dictatorial tendencies of the Chama cha Mapinduzi (CCM) Government. The CCM Government has threatened to deal harshly with the demonstrators, who, on their part, have pledged to go ahead with the demonstrations.
The CCM Government is fabricating a crisis where none need exist. It is not fate that is unfolding, but sheer hubris on the part of the powers that be. If the CCM Government has any sense, all it has to do is respect the Tanzanian constitution and the political parties act, which together recognize the people's right to peacefully assemble and hold demonstrations. CHADEMA has stated, repeatedly, that they are organizing peaceful demonstrations.
In view of this declaration, repeated and amplified time and again, it is patently absurd and unconscionable for the CCM Government to resort to threats and intimidation, and to prepare for confronting with violence citizens who seek to exercise their fundamental rights. The CCM Government can go ahead with its evil schemes, but, eventually, justice will prevail, as it has always done everywhere, since time immemorial.

Monday, August 15, 2016

Msomaji Wangu Mpya

Msomaji mwingine wa kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences amejitokeza mtandaoni. Tarehe 29 Julai, katika ukurasa wake wa facebook, msomaji huyu, Seena, amekisifu kitabu hiki kama ni "Beautifully well written book."

Seena ni msomi mzaliwa wa Ethiopia. Ni mwanaharakati wa masuala za haki za binadamu na hasa wanawake na watoto. Pia ni mwandishi, ambaye kitabu chake, The In Between: The Story of African-Oromo Women and the American Experience, nilikiongelea katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Katika picha hapa kushoto, ninaoneka naye, nikiwa nimeshika kitabu chake, siku alipokiongelea mjini Minneapolis.

Tangu nilipomfahamu Seena, nimevutiwa na ari yake ya kupigania haki. Ana taasisi yake ambayo aliianzisha kwa ajili ya kuhamasisha elimu ya wasichana katika eneo la Oromia, nchini Ethiopia, na aliniomba niwe mshauri mojawapo katika taasisi hiyo. Ninafurahi kushirikiana naye. Ninahisi kuwa Mungu akimjalia maisha marefu, atakuja kuwa kiongozi maarufu Afrika na ulimwenguni.

Friday, August 12, 2016

Wosia wa Nyerere: Viongozi Wafuate Katiba na Sheria

Kuna malalamiko miongoni mwa wa-Tanzania wengi kuwa watawala wa awamu hii ya tano wanakiuka katiba na sheria. Malalamiko haya hayatoki kwa wapinzani tu. Hata mimi ambaye sina chama nimekuwa nikielezea malalamiko yangu. Wanaokiuka katiba na sheria wanaiweka rehani amani ya nchi.

Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alielezea wajibu wa viongozi kufuata katiba na sheria. Labda kwa kukumbushia wosia wake, watawala wa Tanzania watatambua makosa yao na kujirekebisha.

Monday, August 8, 2016

Rais Magufuli ni Dikteta Uchwara?

Nimeona nianzishe mjadala wa suala linalovuma wakati huu nchini Tanzania, ambalo ni: Je, Rais Magufuli ni dikteta uchwara?
Tundu Lissu, mwanasheria wa CHADEMA ndiye mwanzilishi wa dhana hii ya kwamba Rais Magufuli ni dikteta uchwara. Kwa kuanzia, ninapenda kuwashutumu polisi na watawala wa CCM kwa namna walivyolishughulikia suala hili.
Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, Tundu Lissu ana haki na uhuru wa kuwa na mawazo yake kuhusu suala lolote. Ana haki na uhuru wa kuwa na mtazamo wake juu ya Rais Magufuli. Ana haki na uhuru wa kutoa mawazo yake kama alivyofanya.
Mtu mwingine yeyote naye ana haki na uhuru huo. Kwa hivi, kauli ya Tundu Lissu haikuhitaji hatua zilizochukuliwa na polisi za kwenda kumkamata na kumsafirisha kutoka Singida hadi Dar es Salaam kwa mahojiano makao makuu ya polisi.
Jambo ambalo lingeweza kufanyika, bila taabu yote hii na ufujaji wa hela za walipa kodi, ilikuwa ni kwa serikali kujibu hoja za Tundu Lissu na kuthibitisha kuwa Rais Magufuli si dikteta uchwara. Malumbano ya hoja yangetosha.
Ndio utaratibu unaotakiwa katika jamii iliyostaarabika. Ninaamini kuwa wa-Tanzania wana akili timamu, na wana uwezo wa kuchambua mambo. Wana uwezo wa kusikiliza hoja za pande mbali mbali na kutambua upande upi ni sahihi. Madai ya polisi na watawala wa Tanzania kwamba kauli ya Tundu Lissu ni uchochezi ni ya kuwadhalilisha wananchi. Ni kusema kwamba wananchi ni wajinga, wasio na uwezo wa kutathmini na kuchambua mambo.
Ni kwa nini serikali haikuchukua njia hii ya kujibu hoja kwa hoja? Inamaanisha kwamba katika serikali nzima hakuna mtu mwenye akili ya kuweza kumpinga Tundu Lissu na kuthibitisha kuwa Rais Magufuli si dikteta uchwara? Inamaanisha kuwa watendaji wote wa serikali hii ya CCM ni watendaji uchwara, au ni watendaji hewa, au ni vilaza?
Rais Magufuli, kwa mtazamo wangu, amekuwa akivuka mipaka ya katiba kwa baadhi ya kauli zake. Hana mamlaka kikatiba wala kwa mujibu wa sheria za vyama vya siasa, kuweka vizuizi juu ya mikutano na maandamano ya vyama vya siasa. Taratibu zote zimeelezwa katika katiba ya Tanzania na katika sheria ya vyama vya siasa.
Kwa bahati nzuri, katiba ninayo na nimeisoma, na sheria ya vyama vya siasa, ambayo imewekwa kwenye tovuti ya ofisi ya msajili wa vyama, nimeisoma pia: http://www.orpp.go.tz/en/rules/. Kwa kupitia katiba na sheria, ni wazi kuwa Rais Magufuli anakiuka katiba na sheria, na kwa hivyo, kauli ya Tundu Lissu kwamba Rais Magufuli ni dikteta uchwara ni sahihi.
Vyama vya siasa vinawajibika kufanya mikutano na maandamo kwa amani, ili kutangaza sera zao, kutafuta wanachama wapya, na kadhalika. Rais Magufuli, au mtu mwingine yeyote hana wadhifa wa kuwawekea zuio kama alivyofanya. Hana mamlaka ya kusema kwamba watu wafanye siasa katika maeneo yao tu. Hana mamlaka ya kutangaza, hata kwa kisingizio cha "hapa kazi tu," shughuli zipi za kisiasa zisitishwe hadi mwaka 2020. Huu ni udikteta.
Mimi ni raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Ninachotaka ni kuona nchi inaendeshwa kwa mujibu wa katiba na sheria zilizopo. Ninataka utawala wa sheria, unaozingatia haki za binadamu.

Thursday, August 4, 2016

Nimempata Msomaji na Mpiga Debe Mpya

Siku chache zilizopita nimefahamiana na mama mmoja mzee m-Marekani ambaye amekuja kuishi hapa mjini Northfield. Ilikuwa bahati tu kuwa tulisalimiana na tukaongea nakuanza kufahamiana. Katika maongezi na kutambulishana, tuligundua kuwa kazi ambayo tumeipenda maishani ni ya ualimu. Yeye amestaafu ila mimi ninaendelea kufundisha katika Chuo cha St. Olaf.

Katika kuongea zaidi, tuligundua kwamba mitazamo yetu kuhusu elimu, ufundishaji, na mahitaji ya wanafunzi, hasa wenye matatizo inafanana. Tangu hapo tumekuwa tunangea kila siku, kwani tunazidi kugundua jinsi tunavyopenda ualimu na tunavyopenda kuwalea wanafunzi kitaaluma na kimaadili.

Katika maongezi yetu hayo, suala la mimi kama mwandishi lilijitokeza. Nilimtajia vitabu vyangu viwili: Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na Matengo Folktales, akavinunua hima. Tangu alipovipata, alianza kusoma Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na kila tunapokutana amekuwa akinielezea mambo anayojifunza humo, na jinsi yanavyofanana na utamaduni wa Wa-Marekani wa Asili ("Native Americans"). Papo hapo amekuwa akinieleza anavyofananisha tamaduni hizi na utamaduni wa wa-Marekani wazungu.
Huyu mama amenishangaza kwa jinsi anavyolichukulia suala hili kwa dhati. Anasoma kitabu changu kwa makini sawa na mwanafunzi anayejiandaa kwa mtihani. Katika nakala yake, amechora mistari chini ya sentensi na vifungu vingi karibu katika kila ukurasa. Vifungu vingine amevizungushia mduara kwa msisitizo. Kurasa karibu zote amezipamba namna hiyo.

Zaidi ya hayo, amekuwa akiandika katika karatasi tofauti dondoo mbali mbali za kufananisha au kupambanua vipengele vya utamaduni wa wa-Afrika, wa-Marekani wa Asili, na Wamarekani Wazungu. Leo amenipa karatasi tatu alizoandika, ambazo nimezipiga picha zinazoonekana hapa.

Pamoja na juhudi yake hiyo ya kutafakari yaliyomo na yatokanayo katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, mama huyu amekuwa akinunua nakala za kuwapelekea ndugu na marafiki zake. Ingawa Krismasi bado iko mbali, ameshaniambia kuwa atahitaji kununua vitabu hivi kama zawadi za sikukuu. Hapo amenikumbusha makala niliyowahi kuhusu utamaduni wa kununua vitabu kama zawadi ya sikukuu. Ni utamaduni uliojengeka hapa Marekani.

Nimeona niandike habari hii kuhusu mdau wa vitabu vyangu, kama ilivyo desturi katika blogu hii. Kwa kuwa mdau huyu mpya anafuatilia habari zangu katika Facebook and blogu yangu ya ki-Ingereza, ninapangia kumwomba tupige picha ili wadau wangu wengine wapate kumwona mtandaoni.