Sunday, August 28, 2016

Kimya (Muyaka bin Haji)

"Kimya kina mshindo mkuu," || ndivyo wambavyo wavyele.
Kimya chataka k'umbuu, || viunoni mtatile:
Kimya msikidharau, || nami sikidharawile.
             Kimya kina mambo mbele
            Tahadharini na kimya.

Kimya ni kinga kizushi || kuzukia wale wale.
Kimya kitazua moshi || mato msiyafumbule.
Kimya kina mshawishi || kwa daima na milele.
          Kimya kina mambo mbele:
          Tahadharini na kimya.

Kimya vuani maozi || vuani mato muole!
Kimya kitangusha mwanzi || mwendako msijikule.
Kimya chatunda p'um'zi || kiumbizi kiumbile!
          Kimya kina mambo mbele:
          Tahadharini na kimya.

(Muyaka bin Haji, 1776-1840)

3 comments:

Subi Nukta said...

Shukria Mwalimu Mbele kwa kutunukulia utendi huu.

Mbele said...

Asante, Dada Subi Nukta, kwa ujumbe wako. Huu utungo wa Muyaka, mshairi wa kale wa Mombasa, ni kati ya tungo zake maarufu kabisa. Mwalimu Nyerere aliunukuu wote katika kitabu chake, "Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania." Nimekuwa nikitafsiri mashairi ya aina hiyo ya ki-Swahili kwenda ki-Ingereza, na ninataka kutafsiri baadhi ya mashairi ya Muyaka.

Napenda kumalizia ujumbe wangu huu kwa kukushukuru kwa kunisaidia kusambaza fikra zangu katika blogu ya wavuti.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kunyamaza ni dhahabu

Wahenga walituasa, kunyamaa ni dhahabu,
Tuuache ububusa, kila tunachojaribu,
Tujipgeni msasa, kabla ya kuhutubu,
Ukimya una darasa, kunyamaa ni dhahabu.

Watakuona galasa, wengine wakusulubu,
Ukitumia fursa, fikra ukaharibu,
Kaa kimya na kuasa, kuliko mambo haribu
Ukimya una darasa, kunyamaa ni dhahabu.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...