Saturday, May 26, 2018

Nimekutana na Msomaji Mpya

Jana jioni nilikutana na msomaji mpya wa kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nilikuwa mjini St. Paul kuhudhuria darasa la Nu Skool, ambayo ni jumuia ya wa-Marekani Weusi wanaokutana mara moja kwa mwezi kutafakari na kujadili masuala mbali mbali.

Kwa kawaida, kunakuwepo na mtoa mada na kunakuwepo na masuali ya watu kuyajadili. Wakati mwingine inaonyeshwa filamu ya kuelimisha, ambayo inafuatiliwa na mjadala pia. Mada ya mkutano wa jana ilikuwa "The Language of Black America."

Jana hiyo, tulipokuwa tumemaliza darasa na baadhi yetu tukawa tunaendelea kuongea na kutambulishana, mama moja aliniambia kuwa anasoma kitabu changu na kuwa kinamgusa sana. Mama huyu m-Marekani Mweusi alisema kuwa mambo ninayoelezea yanamwezesha kujitambua ni nani kiasili. Alisema anakisoma kitabu kidogo kidogo kwa makusudi ili kuupata ujumbe vizuri, bila pupa. Alisema kuwa, katika maisha yake kama m-Marekani Mweusi alikuwa na hisia mbali mbali, lakini hakuelewa chimbuko lake, ila kitabu kimemfunulia chanzo, yaani u-Afrika. Mama huyu amenigusa kwa kauli hiyo.

Nilimwuliza alisikiaje habari za kitabu hiki, kwani hiyo ni moja ya duku duku zangu. Aliniambia kuwa alihudhuria mhadhara wangu Nu Skool na ndipo alipofahamu kuhusu kitabu changu. Alikiagiza Amazon. Alisisitiza kuwa amekiweka chumbani na anasoma kidogo kidogo kwa makusudi.

Nimeshasema katika blogu hii kuwa tangu mwanzo nilipoandika na kisha kuchapisha kitabu hiki, nilikuwa na wasi wasi na duku duku kuhusu namna wa-Marekani Weusi watakavyokipokea, kwa kuwa ninagusia tofauti baina yao na wa-Afrika kwa namna ambayo huenda ikawakwaza baadhi yao. Lakini nimeshukuru kwamba hadi sasa, inaonekana kuwa hali ni shwari.

Nimeguswa na kauli za mama huyu. Nimeguswa na furaha aliyo nayo kutokana na kusoma niliyoandika. Sina namna ya kuelezea ninavyojisikia, kwani amenifanyia hisani kubwa kwa kunijulisha kuwa niliyoandika yana maana kubwa kwake, katika kujielewa na kumfariji. Ushuhuda kama huu ni motisha kwangu, niendelee kutafakari mambo na kuandika.

Tuesday, May 15, 2018

Mtanzania Afundishaye ki-Swahili Marekani Akifurahia Kitabu

Mimi kama mwandishi ninathamini maoni ya wasomaji juu ya maandishi yangu. Msomaji anapokuwa ametumia muda wake kusoma na kutafakari nilichoandika, halafu akatumia muda wake kuandika maoni, kwangu si jambo dogo. Ninashukuru. Katika blogu hii nina jadi ya kuwatambua wadau hao.

Hivi karibuni, nimeona andiko la Filipo Lubua katika ukurasa wake wa facebook kuhusu kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Huyu anafundisha ki-Swahili katika Chuo Kikuu cha Pittsburgh hapa Marekani. Anasema kwamba anakitumia kitabu hiki katika kozi juu ya Afrika Mashariki, na anasema ni kitabu kinachovutia sana. Ananishukuru kwa kukiandika kitabu hiki rahisi kusomeka juu ya mitazamo yetu, yaani sisi wa-Afrika na wenzetu wa-Marekani. Anasema kuwa wanafunzi wake wamo katika program ya masomo ambayo watasoma Tanzania. Watakuwa Dar es Salaam na Iringa kwa wiki yapata tano.

Katika mawasiliano ya ziada, mwalimu Lubua amesisitiza kuwa hiki kitabu muhimu sana hasa katika kufundishia utamaduni wa Kiswahili. Kauli yake hiyo imenikumbusha maelezo ya Leonce Rushubirwa, m-Tanzania mwingine mwalimu wa ki-Swahili Marekani, kuhusu matumizi ya kitabu hiki katika kufundishia ki-Swahili. Kuongea na wataalam wa aina hiyo ni fursa ya kujithibitishia ile dhana kwamba lugha imefungamana na utamaduni.

Tuesday, May 8, 2018

Nimeshiriki Amani Festival 2018

Tarehe 5 nilikuwa Carlisle, Pennsylvania, kushiriki katika tamasha liitwalo Amani Festival, ambalo nilishiriki mara ya mwisho mwaka 2005. Nilipata fursa ya kuonyesha baadhi ya vitabu vyangu na kuongea na watu mbali mbali, akiwemo mama mmoja ambaye alifanya kazi Afrika Kusini kwa miaka mitatu. Nilipata pia fursa ya kuhojiwa na mwandishi wa gazeti la Carlisle liitwalo The Sentinel.



















Kama kawaida, nilipanga vitabu mezani, na hicho kikawa kivutio. Watu wanafika hapo, na inakuwa ni fursa ya kuongea mambo mengi, kuhusu vitabu na yatokanayo.









Huyu mama alipopita mezani pangu alinyooshea kidole kitabu cha Matengo Folktales akisema "I have read that book!" akimaanisha amesoma kitabu hicho. Nilishangaa, nikaanzisha mazungumzo naye. Aliniambia kuwa alinunua kitabu hiki na kusainiwa nami miaka iliyopita, nikajua kuwa ni yapata miaka kumi na tano iliyopita, ambapo nilishiriki tamasha hili. Aliniambia kuwa yeye na mumewe ni wa kanisa moja hapa ambalo lina uhusiano na dayosisi ya Konde ya Kanisa la ki-Luteri Tanzania.Hapo nilijionea kuwa kumbe dunia hii ni ndogo sana.


















Hao ni wanafunzi wakicheza muziki wa Afrika.




























































Wadau hawajifichi







Wednesday, May 2, 2018

Wadau Niliokutana Nao Wikii Hii

Katika siku saba zilizopita, nimekutana na wadau wengi wa vitabu vyangu. Kwanza, nilipata barua pepe kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni m-Marekani anayefundisha ki-Ingereza Mwanza kwa kujitolea. Ameandika kuhusu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences:

Nimemaliza kitabu chako kuhusu tofauti za tamaduni zetu na nilikifurahia sana. Ulinichekesha mara nyingi. Aidha ukanieleza mambo mengi.

Aprili tarehe 28, niliongea na wanafunzi wa somo la Global Semester ambao watasafiri na kukaa sehemu mbali mbali za dunia, ikiwemo Arusha, Tanzania, ambako watakaa kwa mwezi moja. Profesa wao aliniomba nikawaeleze masuala ya tofauti za tamaduni. Yeye mwenyewe amesoma Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Tarehe 28 Aprili, nilikuwa Rochester, Minnesota, kushiriki tamasha la kimataifa linaloandaliwa kila mwaka na Rochester International Association. Hapo nilikutana na hao ndugu wawili wanaoonekana pichani hapa juu. Huyu wa kushoto ni daktari katika hospitali maarufu ya Mayo, mwenye asili ya Uganda, na huyu wa kulia ni m-Kenya ambaye alikuwa mwanafunzi wetu chuoni St. Olaf. Tuliongea kirefu. Daktari ndiye aliyetaka tupige hiyo picha tukiwa tumeshika vitabu vyangu.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...