Saturday, May 26, 2018

Nimekutana na Msomaji Mpya

Jana jioni nilikutana na msomaji mpya wa kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nilikuwa mjini St. Paul kuhudhuria darasa la Nu Skool, ambayo ni jumuia ya wa-Marekani Weusi wanaokutana mara moja kwa mwezi kutafakari na kujadili masuala mbali mbali.

Kwa kawaida, kunakuwepo na mtoa mada na kunakuwepo na masuali ya watu kuyajadili. Wakati mwingine inaonyeshwa filamu ya kuelimisha, ambayo inafuatiliwa na mjadala pia. Mada ya mkutano wa jana ilikuwa "The Language of Black America."

Jana hiyo, tulipokuwa tumemaliza darasa na baadhi yetu tukawa tunaendelea kuongea na kutambulishana, mama moja aliniambia kuwa anasoma kitabu changu na kuwa kinamgusa sana. Mama huyu m-Marekani Mweusi alisema kuwa mambo ninayoelezea yanamwezesha kujitambua ni nani kiasili. Alisema anakisoma kitabu kidogo kidogo kwa makusudi ili kuupata ujumbe vizuri, bila pupa. Alisema kuwa, katika maisha yake kama m-Marekani Mweusi alikuwa na hisia mbali mbali, lakini hakuelewa chimbuko lake, ila kitabu kimemfunulia chanzo, yaani u-Afrika. Mama huyu amenigusa kwa kauli hiyo.

Nilimwuliza alisikiaje habari za kitabu hiki, kwani hiyo ni moja ya duku duku zangu. Aliniambia kuwa alihudhuria mhadhara wangu Nu Skool na ndipo alipofahamu kuhusu kitabu changu. Alikiagiza Amazon. Alisisitiza kuwa amekiweka chumbani na anasoma kidogo kidogo kwa makusudi.

Nimeshasema katika blogu hii kuwa tangu mwanzo nilipoandika na kisha kuchapisha kitabu hiki, nilikuwa na wasi wasi na duku duku kuhusu namna wa-Marekani Weusi watakavyokipokea, kwa kuwa ninagusia tofauti baina yao na wa-Afrika kwa namna ambayo huenda ikawakwaza baadhi yao. Lakini nimeshukuru kwamba hadi sasa, inaonekana kuwa hali ni shwari.

Nimeguswa na kauli za mama huyu. Nimeguswa na furaha aliyo nayo kutokana na kusoma niliyoandika. Sina namna ya kuelezea ninavyojisikia, kwani amenifanyia hisani kubwa kwa kunijulisha kuwa niliyoandika yana maana kubwa kwake, katika kujielewa na kumfariji. Ushuhuda kama huu ni motisha kwangu, niendelee kutafakari mambo na kuandika.

No comments: