
Hivi karibuni, nimeona andiko la Filipo Lubua katika ukurasa wake wa facebook kuhusu kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Huyu anafundisha ki-Swahili katika Chuo Kikuu cha Pittsburgh hapa Marekani. Anasema kwamba anakitumia kitabu hiki katika kozi juu ya Afrika Mashariki, na anasema ni kitabu kinachovutia sana. Ananishukuru kwa kukiandika kitabu hiki rahisi kusomeka juu ya mitazamo yetu, yaani sisi wa-Afrika na wenzetu wa-Marekani. Anasema kuwa wanafunzi wake wamo katika program ya masomo ambayo watasoma Tanzania. Watakuwa Dar es Salaam na Iringa kwa wiki yapata tano.
Katika mawasiliano ya ziada, mwalimu Lubua amesisitiza kuwa hiki kitabu muhimu sana hasa katika kufundishia utamaduni wa Kiswahili. Kauli yake hiyo imenikumbusha maelezo ya Leonce Rushubirwa, m-Tanzania mwingine mwalimu wa ki-Swahili Marekani, kuhusu matumizi ya kitabu hiki katika kufundishia ki-Swahili. Kuongea na wataalam wa aina hiyo ni fursa ya kujithibitishia ile dhana kwamba lugha imefungamana na utamaduni.
No comments:
Post a Comment