Mwalimu Nyerere na Elimu
Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mwalimu. Naamini ni sahihi kusema kuwa silika ya ualimu iliathiri siasa na matendo ya Mwalimu Nyerere kama kiongozi wa Tanganyika na hatimaye Tanzania. Aliiona nchi yake kama darasa, na daima alikuwa anafundisha. Ninachotaka kuongelea hapa ni mchango wa Mwalimu Nyerere katika uwanja wa elimu. Elimu ni suala mojawapo ambalo Mwalimu Nyerere alilishughulikia sana. Katika kuelezea suala la elimu, Mwalimu aliweka na kufuata misingi kadhaa muhimu. Tanganyika ilipopata Uhuru, Mwalimu Nyerere alikuwa ameshajizatiti kubadilisha mfumo wa elimu uliokuwepo wakati wa ukoloni, ambao ulikuwa mfumo wa kibaguzi. Kulikuwa na shule za wazungu, za Wahindi, na za watu weusi. Mara tulipopata Uhuru, Nyerere alifuta ubaguzi na kuwachanganya wanafunzi mashuleni. Tangu mwanzo, Mwalimu Nyerere aliamini dhana ya usawa wa binadamu. Mwalimu Nyerere aliamini kuwa elimu ni haki ya kila mtu. Alifanya kila juhudi kutoa elimu kwa watu wote, kuanzia watoto hadi watu wazima. Mwalimu alij