Safari ya Bajaji: Lushoto Hadi Irente
Agosti 6, mwaka jana, nilisafiri kutoka Lushoto kwenda Irente. Nilishawahi kusafiri hadi Irente miaka michache kabla, nikitumia teksi. Lakini mwaka jana niligundua kuwa ningeweza kusafiri kwa bajaji. Bajaji yenyewe ndio hii inayoonekana katika picha, na dreva wake. Bajai hii ilikuwa maarufu mjini Lushoto. Niliziona bajaji kwa mara ya kwanza nilipokuwa India, mwezi Aprili mwaka 1991. Wakati huo hapakuwa na bajaji Tanzania. Lakini kidogo kidogo, miaka iliyofuatia, bajaji zilianza kuonekana, na leo zimejaa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam. Sasa zinaonekana hata kwenye miji midogo kama Lushoto. Ndio mambo ya ulimwengu katika utandawazi wa leo. Safari ilikuwa murua. Bajaji ilikula milima na kukwepa mifereji na mashimo kama mchezo. Tulipofika Irente, nilianza kuwatafuta vijana wawili mapacha ambao niliwafahamu miaka iliyotangulia, wakati nafanya utafiti kuhusu masimulizi juu ya Osale Otango na Paulo Hamisi. Osale Otango na Paulo Hamisi ni maarufu katika historia ya miaka ya hamsini n