Sunday, May 8, 2011

Kikombe cha Mwenyekiti Maggid

Kama sote tunavyojua, wa-Tanzania tuko kwenye awamu ya vikombe. Waganga wamejitokeza nchini mwetu, wakiwa na vikombe vya kuponyesha magonjwa mbali mbali. Wateja wengi wanatoa ushuhuda kuhusu uponyaji wao.

Nami napenda kutoa ushuhuda kuhusu kikombe cha Mwenyekiti Maggid Mjengwa.

Nianze kwa kusema kuwa Mwenyekiti Maggid ni mwalimu, mwandishi na mwanablogu. Hajawa mganga wa kienyeji. Isipokuwa, kikombe ameninywesha. Tega sikio nikuhadithie.

Mwaka 2009 mwanzoni, Mwenyekiti Maggid alianzisha gazeti la Kwanza Jamii, akaniomba niwe mchangiaji. Nilikubali. Sikutambua kuwa nilijipalia mkaa, maana nilijikuta nahangaika kuandika hizo makala na kuzituma kwa muda uliotakiwa.

Ilikuwa ni kazi ya kuumiza kichwa. Kwanza kabisa, wakati mwingine nilikuwa sijui niandike kuhusu nini. Huku siku na saa za kuwasilisha makala zinaendelea kusogea, nami bila kujua mada ya kuandikia, nilibaki nimekodoa macho na jasho linanitoka. Mara kwa mara Mwenyekiti Maggid alikuwa ananiletea ujumbe usiku kwenye saa sita za hapa Marekani ya kati, iwapo nilichelewa.

Tatizo jingine nililopambana nalo ni kuandika kwa ki-Swahili. Nilizoea kuandika kwa ki-Ingereza, lakini kuandika ki-Swahili sanifu ulikuwa ni mtihani wa kuumiza kichwa.

Sisi wa-Katoliki, katika falsafa ya dini yetu, tunatumia dhana ya kikombe kuelezea magumu ya maisha au mateso ambayo Mungu anatuletea tuyakabili. Ni kama tunavyotumia dhana ya msalaba. Mungu ana malengo yake anapotutwisha msalaba maishani.

Napenda niendelee kufafanua falsafa za kidini zinazohusiana na mada yangu. Babu wa Loliondo ametueleza tena na tena kuwa kikombe si kikombe tu bali ni suala la imani, na uwezo wa kutibu ni wa Mungu, si binadamu.

Mungu anaweza kumtumia binadamu yoyote kuleta ujumbe au uponyaji duniani. Kwa imani yangu, ndivyo ilivyokuwa kuhusiana na hiki kikombe cha Mwenyekiti Maggid. Naamini kilipangwa na Mungu. Matokeo ya magumu niliyopitia, ambayo nayaita kikombe cha Mwenyekiti Maggid, yamekuwa mazuri. Makala nilizoandika zilisomwa na bado zinasomwa na watu wengi.

Makala mojawapo, baada ya mimi kuitafsiri kwa ki-Ingereza, ikachapishwa huku Marekani, ilimvutia Chad Brobst, mhariri wa jarida la Monday Developments. Aliiomba, nami nikairekebisha kidogo, akaichapisha. Kila toleo la Monday Developments huteua makala moja kama makala ya mfano. Kwa mwezi Aprili, iliteuliwa makala yangu. Watu wengi sana duniani wataiona.

Vile vile, makala nilizoandika katika Kwanza Jamii nilizikusanya nikazichapisha kama kitabu, CHANGAMOTO, ambacho watu waliokisoma wamekipenda. Ninajivunia kitabu hiki kwa vile ni kitabu changu cha kwanza kwa ki-Swahili.

Nimeshawahi kuandika kuwa wito wa Mwenyekiti Maggid kunitaka niandike makala za ki-Swahili ulisaidia kuniondolea kasumba tuliyo nayo wasomi wengi, ya kutoweza au kutotaka kutumia ki-Swahli ipasavyo. Nilifanya bidii kujiongezea ufahamu wa ki-Swahili. Nilisoma vitabu vya mabingwa kama Shaaban Robert na kujijengea nidhamu ya matumizi ya lugha.

Sisiti kukiri kuwa kikombe alichoninywesha Mwenyekiti Maggid kimechangia kunitibu ugonjwa sugu unaowaathiri wasomi wengi, mbali ya kuwaneemesha walimwengu kama nilivyoelezea.

2 comments:

Mwanasosholojia said...

Profesa, hakika kikombe cha Mwenyekiti Maggid hakikupaswa kukuepuka, unakistahili haswa. Nimekuwa nikifuatilia maandiko yako kwa muda mrefu sasa. Kwa mara ya kwanza nimeamua kukutolea "siri" niliyoihifadhi moyoni kwa muda mrefu...maandiko yako na maudhui yaliyomo ndani yake yamechangia kwa kiasi kikubwa ari yangu uandishi niliyonayo leo. Mwenyekiti Maggid amekunywesha wewe Profesa Mbele kikombe, ukakinywa pamoja na maumivu makubwa, ukapata nguvu za kukaa na kuzidi kuandika, sisi wengine tukazidi kunufaika na kazi zangu na kuongeza ari..Shukrani sana Profesa Mbele!

SIMON KITURURU said...

Kikombe cha Mwenyekiti Maggid OYEEH!