Thursday, May 5, 2011

Mitaani Namanga, 2007

Ingawa mdogo, mji wa Namanga ni maarufu, kwa vile uko mpakani. Hapa naonekana nikiwa Namanga, upande wa Tanzania. Naelekea kwenye geti la mpaka, hatua chache mbele yangu. Kule mbali unaona Mlima Longido. Barabara inapita kulia kwake, inaingia Longido, nyuma ya mlima, na kuelekea Arusha.

Hii ni moja ya hoteli ambapo napenda kufikia, kwa Bwana Minja, kupata chakula na kinywaji. Nimeshalala hapo.
Nilipendezwa na mpangilio wa nyumba hizi na ile
milima. Hizi nyumba ziko mwanzoni mwa mji wa Namanga, kabla hujafika kwenye geti la mpaka baina ya Kenya na Tanzania.Nilikuwa Namanga na kikundi cha wanafunzi kutoka Chuo cha Colorado na mwalimu wao, ambao walifika Tanzania katika kozi niliyoiunda, kuhusu mwandishi Hemingway. Hao ni wanafunzi waanzilishi wa kozi hii. Napangia kuibadili kidogo na kuiweka katika program ya Chuo cha St. Olaf.

Hapa nipo upande wa Kenya. Kama mdau unavyoona, mapokezi hayakuwa haba. Ndio mambo ya ujirani mwema hayo.
Namanga, kama ilivyo miji mingine, ina sehemu nyingi ambapo unaweza kupumzika, na kujipatia chakula na pia kukata kiu baada ya mizunguko yako mitaani.

5 comments:

SIMON KITURURU said...

Hapa mahali sijui kwanini napaogopa hasa kwa kuwa kuna marafiki zangu wajanja tu huwa wakijituliza tu kinamna fulu kuibiwa!

Siku hizi sishauri marafiki zangu wang'aeng'ae macho hapo na nakataza kabisa wasibadilishie manoti pesa hapo.

Ila kwa kukusoma naona labda sio kila mtu atulizaye manyanga hapo wajanja humgeuza dili!

Mie na bahati sichani nywele kwahiyo watoto tundu karibu wote huwa washkaji kwa kudhania mie RASTA halafu fulu mtundu kumbe wapi!

Unanifanya nipafikirie tena kivingine hapo Prof.

sikapundwa christian said...

Si haba Profesa,kufanya ziara kama hizo,katika mitaa ya Namanga kuwepo katika miji tofauti utaona tabia za watu tofauti kulingana na mazingira tofauti na jamii tofauti za watu.

Ingawa sija fika huko lakini nimepapenda Namanga hasa kwa hekaheka zake za utafutaji wa maisha,mara nyingi watu wa mipakani wana shughuli nyingi zikiwemo na za wizi kama alivyo ogopa ndugu yangu Kitururu

Ninaimani wewe hukupata mkasa huo wa kuibiwa.Tuko pamoja nawe daima.

Mbele said...

Ndugu Kitururu na Mzee Sikapundwa, shukrani kwa mchango wenu. Nami napenda nichangie tena kidogo.

Mara ya kwanza kuiona Namanga ilikuwa mwaka 1989 nilipokuwa nakwenda Kenya. Upande wa Kenya kulikuwepo na jamaa wengi wanaobadilisha hela.

Lakini miaka hii ya karibuni, hakuna haja ya yote hayo, kwani ninatembea na kadi ya kuchukulia hela badala ya hela taslimu.

Mara ya kwanza nilipolala hapo Namanga niliona kuna ujirani mwema kweli baina ya wa-Kenya na wa-Tanzania. Ukiingia hoteli au baa za upande wa Tanzania, unawakuta wa-Kenya kibao, na wewe m-Tanzania unajivukia mpaka na kwenda kupata ulabu upande wa Kenya.

Wenyeji waliniambia kuwa kwa hapo hapo mpakani, huhitaji kibali kuingia nchi jirani. Kibali unahitaji unapoenda ndani zaidi ya nchi.

Mfanyabiashara wa kwanza niliyemfahamu hapo Namanga ni m-Chagga mmoja akiitwa Bwana Mangelepa. Alikuwa anamiliki Heshima Bar. Hii baa haiko tena, ila mwaka 1989 na 1990 nilikuwa nakata kiu hapo :-)

SIMON KITURURU said...

Ila Prof. hilo toto la Kimasai lililokuwekea mkono begani hukulipa lavu yani ! Limetoka kikujipendekeza kweli kwenye hiyo Picha Profesa Jay.


Kukiachana nahilo!


Kupitia njia hiyo ya NAMANGA mara yangu ya kwanza ni 1996 .Nampaka leo sijawahi kusumbuliwa hapo ila wadau niwajuao mpaka kwenye viofisi vya kubadili pesa pale washaliwa fweza yani!:-(

Ila nimesha farijiwa sana tu hapo kikukata kiu ingawa kuna mchezo naustukia ukionekana unakata kiu kiurahisirahisi unaanza kuletewa sana biashara kitalii hapo kitu kiwezacho kufanya uondoke umenunua bangili ambazo inabidi utunge umpe nani kama zawadi!:-(

NN Mhango said...

Kaka usemayo ni kweli. Nimepita Namanga zaidi ya mara hamsini hivi. Ni pazuri sema kuna uwezekano pakawa mazalio mazuri ya ukimwi, ujambazi, biashara haramu, madawa ya kulewa hata kupitisha magaidi. Kitu cha kusikitisha ni ufisadi wa maafisa wa mpakani pale. Nilishuhudia mara nyingi wakiwanyanyasa na kuwatoa rushwa akina mama wafanyao vijibiashara za kuvusha vitu adimu. Pia kuna wasomali wengi wanaofanya biashara ya kubadili fedha kinamna.
Kwa ujumla Namanga ni pazuri hasa upande wa Tanzania ambapo kuna vivutio vingi kuliko upande wa Kenya. Namanga ni pazuri kuliko Holoholo ambako kuna umbali mrefu baina ya posts mpakani.