Thursday, May 26, 2011

Someni kwa Furaha

Wiki kadhaa zilizopita, nikiwa Madison, katika mkutano wa Peace Corps, niliingia katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Nilifurahi kuingia katika maktaba hii, ambayo niliizoea wakati nasoma katika chuo hicho, 1980-86.

Niliangalia vitabu vya ki-Swahili, ambavyo ni vingi katika maktaba hii, nikavutiwa na vitabu vya Someni Kwa Furaha, tulivyosoma tulipokuwa shule ya msingi.

Nilijikumbusha kuhusu Bulicheka na mke wake Lizabeta, Wagagagigikoko na mfalme wao, Makari Hodari, Kalumekenge, na Pauli mwenye mikono michafu.

Tulibahatika, enzi za utoto wetu, kuwa na vitabu vya kusisimua, vilivyotupa motisha ya kusoma. Vitabu hivi viliandikwa kuzingatia umri wetu. Walimu walikuwa makini, katika kufundisha, kwa mbinu mbali mbali, kama vile nyimbo. Tuliimba alfabeti hadi orodha. Nawasifu na kuwashukuru waalimu wale.

15 comments:

Subi said...

Nilijitahidi sana kupata nakala za vitabu hivi lakini sikufanikiwa, bali kupata vilivyochapishwa upya vyenye majina, "Someni bila shida" yaani kwa kweli hata ladha ya kusoma haifanani na ile ya "Someni kwa furaha", sifahamu kama watu walitilia maanani umuhimu wa neno "furaha" badala ya "bila shida" kwa kuwa jina tu la kitabu, linaweza kuwa na maana kubwa sana, likavutia hata msomaji. Mtu anapoambiwa soma kwa furaha, si sawa na kusema, soma bila shida, kwa maana kuwa, unapoandika kwa kukanusha, pengine unamwambia mhusika kuwa kusoma ni shida, lakini hebu soma bila shida.

Ninawashukuru waliotunga vitabu vya Someni Kwa Furaha, kama unavyoshukuru wewe Prof. kwani kwa kufanya hivyo walinijengea mazingira ya kupenda kusoma vitabu hata nje ya darasa na baada ya muda wa masomo. Nilipenda sana kujisomea vitabu hivi kama hadithi, na kila niliposoma, nilijenga taswira ya hadithi husika na nikajifunza kutokana na hadithi yenyewe.

Ama kwa hakika, ya kale dhahabu!

tz biashara said...

Ama kweli leo umenifurahisha kwa kitabu hiki ambacho nimekumbuka enzi zangu za utoto.Nikikuta sehemu itabidi nikinunue niwafundishe watoto wangu kusoma kiswahili maana nipo uingereza hujaribu kusoma kidogo kiswahili.Wakati nikisoma hichi kitabu nilikuwa nahisi kama sinema vile mtu anavyoangalia.

Mbele said...

Da Subi na tz biashara, ni kweli msemavyo, kuhusu mvuto wa vile vitabu. Aliyeviandika, yaani Padri Alfons Loogman, anaonekana alikuwa mweye ufahamu mzuri wa akili na saikolojia ya watoto.

Siamini kama mtu unaweza kukurupuka tu ukaandika kitabu, eti cha watoto, kama tunavyofanya nchini mwetu.

Lakini hivi vitabu vya Someni Kwa Furaha vilikuwa moto wa kuotea mbali. Tulikuwa tukifuatilia kwa ari visa vya Bulicheka na mke wake Lizabeta, walivyoingia kwenye nchi ya Wagagagigikoko, na jinsi Bulicheka alivyozipiga na mfalme wao Huihuihui (nadhani jina nimelipatia vizuri). Kulikuwa na picha ya mfalme huyu akitimua mbio, huku ameangalia nyuma. Ilituchekesha sana.

Sijui kama leo tuna watu nchini wanaoandika vitabu vya kuwavutia watoto kiasi hiki. Kwa upande wa ki-Ingereza, napenda nimtaje mwandishi Tololwa Mollel ambaye anaishi Canada. Anaandika vitabu vizuri vya watoto na amepata tuzo nyingi huku ughaibuni. Hadithi zake zinaongelea mambo ya kwetu.

Anonymous said...

jamani, tafadhalini sana fanyeni juu-chini tupate vitabu hivyo. Mimi nakumbuka vitabu kama vya Juma na Rosa-vilikuwa vina vionjo vya hali ya juu sana. Vilikuwa na mvuto wa ajabu!

Anonymous said...

Kwa kweli leo umenikumbusha mbali sana kwani na mimi nilivisoma na kuvifurahia sana vitabu hivi. Natamani vingerudi tena hapa kwetu na watoto na wajukuu zetu wakavisoma.

Kwa vile wewe utakuwa wa karibia umri wangu basi vitabu vyengine vilivyokuwa vya kufurahisha watoto ni vile vya English vya Oxford. Unakumbuka akina 'my name is Shokolokobangoshei', akina Juma Hamisi the Lorry driver, Abdul, Mr Mutabingwa na fatal coils? Hivyo vilikuwa vya grades tafauti lakini vikivutia sana kupenda kusoma.

Mara nyingi tulikuwa tunajitahidi usome hadithi ya mbele kabla ya mwalimu ili ukifiikia ile hadithi basi wewe unakuwa mtaalamu fulani hivi. Yote hiyo ni kutokana na interest ya kusoma vitabu.

Heee that was more than fourty years ago!

Anonymous said...

Tatizo la nchi yetu vitabu vizuri vilikuwepo lakini ukitaka kutafuta hata copy moja hakuna, nadhani kuna haja ya kuangalia uwezekano wa kutafuta vitabu hivi

Mbele said...

Wadau, nami mnanipa raha sana leo. Kwanza, niseme kuwa mdau unayeulizia namna ya kuvipata vitabu hivi, nimekuwa katika harakati ya kutafuta taarifa zake. Najua kuwa vilichapishwa na kampuni ya Thomas Nelson.

Sasa, inabidi kufuatilia kama kampuni hii bado iko Afrika Mashariki, maana kama sikosei ilikuwepo Nairobi. Na suali la pili litakuwa ni kama bado wanavichapisha.

Hata hivi, kama nilivyobainisha kwenye makala yangu, kuna uwezekano wa kupata nakala kwenye mtandao wa Amazon.

Wadau wengine, tuko pamoja katika kuzikumbuka enzi zile. Mimi nilianza shule mwaka 1959, na baada ya kuwasoma hao akina Bulicheka, tuliwasoma hao akina Abdul.

Kulikuwa na hadithi za akina Abunuwasi, bila kusahamu vitabu kama "Mashimo ya Mfalme Sulemani," ambamo tulikuwa tunasoma hadithi za akina Umslopogazi na shoka lake la hatari.

Lakini elimu ya wakati ule ilikuwa na mpangilio mzuri. Mkishamaliza kitabu fulani, mnakuwa kweli mmeandaliwa kusoma kitabu cha juu zaidi. Na hiyo haikuwa kwenye ki-Swahili tu, bali na ki-Ingereza pia, ambako ndiko tuliwakuta hao akina Mr. Mutabingwa na Kokogonza.

Yaani mimi mwenzenu ninapowasikia watani za wa-Haya wakisema "nshomile," huwa namkumbuka Mr. Mutabingwa :-)

Sikapundwa said...

Umebahatika Pr.kukuta vitabu hivyo,chabu vya ajabu kenye maktaba zetu vitabu hivyo ni nadra sana kuvikuta.Hukuwahi kuviona vitabu vya Hekaya za Abunuasi,vilikuwa vya kitoto lakini hivyo vya Wa- gagigikoko vilikuwa vinafundisha jamii.

Anonymous said...

Kweli hivyo vilikuwa ni vitabu kwa wakati ule na bila shaka tuanze kukaa kitako na kujaribu kuangalia kwa undani kabisa ili nasi tuweze kuandika katika muono huo hata kama siyo asilimia mia

Nina imani Prof. Mbele unaweza ukanza kama siyo kuendeleza nyanja hiyo ya utunzi wa vitabu

Renatus said...

Kwa kawaida fashen zinapotea na kurudi kama fashen mpya na aghlabu hupendwa tena na watu wa wakati huo bila kujua kwamba ilikuwepo enzi hizo. Si ni wakati sasa tukaangalia uwezekano wa kuvirudisha tena vitabu hivyo ambavyo kwa vyovyote vitakuwa vizuri kuliko vilivyopo? Ni kweli kwamba utafiti na umahiri mkubwa ulitumika kupata masuala yanayoweza kuvuta hisia za wasomaji na wakati huohuo kufikisha ujumbe uliokusudiwa. Na mimi nilibahatika kuvisoma! Ni raha na vinafaa sana.

Anonymous said...

vitahi hivi vina ladha yake kwa mtoto kuvisoma,unatamani uwe nawewe kamakana unavyoisoma hadithi Kulikuwa na vitabu vya kusisimua alfu uleilaulaila vyote hvyo ni katika vitabu vizuri kabisa ukisoma kitabu honi raha mpaka ukimalize na mara ingine unaona raha kukirejelea mafunzo mengi tulikuwa tukipata kutokana na vitabu hivi someni kwa furaha, oxford english hekaya za abunaws someni zsiku nyingi nilijaribu kuviulizia lakini hakuna hata anevijua katika vijana wa sasa

Mbele said...

Nadhani kilichotokea miaka iliyofuata ni umbumbumbu na ufisadi katika sekta hii. Kila mtu anajiandikia kitabu, hata kama haelewi saikolojia ya watoto na suala zima la kuwaandikia watoto, na halafu anapitisha vitabu hivi kienyeji ili viingie hadi darasani.

Hakuna uangalifu kama uliokuwa miaka ya zamani, na nimeona hata vitabu vyenye makosa kem kem vinatumika mashuleni.

Anonymous said...

Jamani ndugu zangu mmegusa moyo wangu kunikumbusha vitabu hivi vizuri kama lulu! Pamoja na kuwa hapa Tanzania bado natafuta hivyo vitabu kwa ajili ya watoto wangu havipatikani kabisa! Mwonjo wake ni wa ajabu ambao kwa kweli humvutia mtoto apende kusom na kusoma na kusoma bila kuchoka! Watunzi walikuwa mahiri kwa kuvuta hisia za watoto, na si watoto tu hata watu wazima kama mimi!!! Vitabu vya sasa ni elimu tu bila kuwaandaa watoto kisaikolojia....watu wanataka pesa na si ufahamu halisi wa watoto. Hivi tufanyeje ili kurudisha hadhi ya elimu yenye kina: yaani inyojikita katika kumfahamisha mtoto na kumwezesha kuwa na ufahamu wa kina!!??

Gina said...

Yan nimekumbuka mentioned leo baada ya wafanyakazi wenzangu kukumbushia hadithi za Bulicheka.....uwiii nimefurahi kupita maelezo kukumbuka kitabu hiki....wagagagigikoko

Mbele said...

Ndugu Gina,

Vitabu vile vilikuwa vinasisimua na vilijenga ari na utamaduni wa kusoma. Tunamkumbuka Bulicheka kama vile alikuwa jirani yetu. Wagagagigikoko ni watu wangu wa karibu sawa na watani zangu Wandengereko.