Thursday, December 29, 2011

Mahojiano na Profesa Mbele, "Kombolela Show"

Nimeona niwaletee wadau mahojiano niliyofanyiwa katika "Kombolela Show," Oktoba 2, 2010. Mwendesha mahojiano alikuwa Metty Nyang'oro. Kwa jinsi mtandaoni kunavyofurika taarifa, nimeona si vibaya kuyaleta tena mahojiano haya, ili wadau wayasikie na kuyatafakari na kuchangia, endapo watajisikia kufanya hivyo, kwani elimu haina mwisho, wala haina mwenyewe.

Tuesday, December 27, 2011

Hadithi za wa-Matengo Zatamba Ughaibuni

Hivi karibuni, nilipata ujumbe kutoka kwa Profesa Paschal Kyoore wa Chuo cha Gustavus Adolphus kuwa anatunga kozi mpya, "The African Trickster," akaomba ushauri wangu, kwani mada hiyo ya "trickster" nimeifanyia utafiti na kuandika makala kwa miaka mingi.

Hatimaye, Profesa Kyoore ameniletea ujumbe kuwa ameshaagiza nakala za kitabu cha Matengo Folktales kwa ajili ya darasa hilo. Kisha angependa siku moja niende kuongea na wanafunzi wake, nami nimekubali.

Ninafurahi sana ninapoona watu wa ughaibuni wakipata fursa ya kujifunza mambo ya kwetu, na hadithi za jadi ni hazina mojawapo kubwa, kama nilivyoelezea hapa. Ni fursa kwetu na kwa walimwengu kutambua mchango wa wahenga wetu kwa utamaduni wa dunia, kwani katika hadithi zao, wahenga waliongelea na kutafakari kila aina ya suala linalomkabili binadamu, sawa na watu walivyofanya watu wa mataifa mengine.

Hadithi za wa-Matengo zinatumika katika vyuo mbali mbali hapa Marekani, kama nilivyoelezea hapa. Yapata miaka miwili iliyopita, nilipata pia ujumbe kutoka kwa mwalimu mmoja Uingereza, ambaye alikuwa anatafuta nakala ya Matengo Folktales kwa ajili ya kufundishia. Nilimpelekea.

Tunawajibika kuzirekodi hadithi hizi na masimulizi mengine, kwani vijana wa leo hawazielewi, na wanatekwa na tamaduni za nje, zinazoenezwa kwetu hasa kwa njia ya machapisho, televisheni, na mtandao wa kompyuta. Mimi nilirekodi hadithi za wa-Matengo nilipokuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, miaka yapata 40 iliyopita. Halafu nilitumia miaka yapata 23 kuzishughulikia hadithi zilizomo katika Matengo Folktales, kwa maana ya kuzitafsiri na kuziandikia uchambuzi, ndipo nikachapisha kitabu. Lakini, shughuli hii haina mwisho, na kitabu kimoja hakitoshi. Ni kama changamoto tu. Kwa walioko Tanzania, kitabu kinapatikana Dar es Salaam, simu namba 0754 888 647 na 0717 413 073.

Friday, December 23, 2011

Maongezi na Wanafunzi Waendao Tanzania

Profesa Barbara Zust, wa Chuo cha Gustavus Adolphus, amenialika kwenda kuongea na wanafunzi anaowaandaa kwa safari ya Tanzania. Anafundisha masomo ya uuguzi, na mwezi Januari anawapeleka wanafunzi Tanzania kujifunza masuala ya afya na matibabu katika utamaduni tofauti na ule wa Marekani.

Profesa Zust ameshawapeleka wanafunzi Tanzania mara kadhaa. Katika kuwaandaa, hutumia kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na pia hunialika nikaongee nao. Anajisikia vizuri sana ninapokutana na wanafunzi wake kujibu masuali yao na kuwapa maelezo mbali mbali, nami huwa nafurahi kukutana na wanafunzi hao wanaosomea taaluma ambayo sikusomea, ila ni wazi kuwa wanafaidika na mawazo yangu kuhusu jinsi tofauti za tamaduni zinavyohusika katika taaluma yao.

Hapa kushoto ni picha tuliyopiga na wanafunzi waliokuwa wanaenda Tanzania mwaka 2009. Tulikuwa kwenye chumba cha mkutano cha kanisa la Shepherd of the Valley, mjini Apple Valley. Habari za mkutano wetu niliziandika hapa.
Hapa kushoto ni picha tuliyopiga na wanafunzi waliokuwa wanakwenda Tanzania mwaka 2010. Tulikutana Mount Olivet Retreat Center, mjini Lakeville. Habari zaidi niliziandika hapa.

Wanafunzi hao na profesa wao wanapata fursa ya kuona sehemu mbali mbali za Tanzania, kama vile hospitali ya Ilula, kijiji cha Tungamalenga, na hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Sehemu zote tatu ziko Iringa. Wanafunzi hao wanaguswa sana na ziara yao Tanzania. Nimeshasoma baadhi ya maoni yao.

Mwaliko wa sasa ni wa kuongea na wanafunzi tarehe 2 Januari. Insh'Allah, nitaleta picha na taarifa.

Tuesday, December 20, 2011

Mdau Mwingine, Mwanafunzi, Kaja

Mara kwa mara naandika habari za wasomaji wa maandishi yangu wanaonitembelea, au ninaokutana nao sehemu mbali mbali.

Jana, baada ya kumaliza kufanya mtihani wa mwisho wa somo langu la fasihi ya Afrika Kusini, kaja ofisini mwanafunzi Logan. Alikuja na nakala ya kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ili nikisaini. Nilisaini, tukaendelea na michapo. Logan alisoma somo langu jingine mwaka jana.

Chuo Cha St. Olaf kinaamini kuwa ni muhimu wanafunzi waufahamu ulimwengu nje ya Marekani. Kilinileta hapa, mwaka 1991, kuanzisha masomo katika idara ya ki-Ingereza juu ya uandishi wa ki-Ingereza kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Wanafunzi wanavutiwa na fursa hii ya kupanua upeo wao, kuzifahamu jamii na tamaduni mbali mbali.

Monday, December 19, 2011

Makari Hodari

Kwa sisi tuliosoma shule ya msingi zamani, Makari Hodari ni jina tunalolikumbuka sana. Tulisoma habari zake zilizotungwa na Padri Alfons Loogman, mwandishi wa vitabu vya Someni Bila Shida na Someni Kwa Furaha. Kwa kweli, padri huyu aliziteka nyoyo zetu watoto, akatufanya tupende kusoma. Aliandika vitabu kadhaa vya masomo ya ki-Swahili na hata mwongozo kwa walimu kuhusu kufundisha kusoma.

Nakumbuka kuwa katika shule yangu ya msingi ya Litembo, tulikuwa tunasoma hadithi ya Makari Hodari kwa kuiimba. Watoto wote darasani tulikuwa tunaimba kwa pamoja, kwa furaha. Hadi leo naweza kuimba tulivyoimba. Na mwalimu alikuwa akiimba nasi. Pamoja na utamu wa hadithi, tulivutiwa na picha.

Nikiitafakari hadithi ya Makari Hodari, naona kuwa ilijengeka katika mfumo wa zile hadithi za kale za mashujaa, ambazo zinasimuliwa katika tamaduni mbali mbali. Kwa mfano, Wa-Haya wana hadithi za mashujaa kama Mugasha, Rukiza, na Kilenzi. Wa-Chagga wana hadithi ya Mrile, wa-Swahili hadithi ya Liongo Fumo. Hadithi ya Makari Hodari imerahisisha na kufupisha masimulizi ili yawavutie watoto kwa umri wao. Lakini inataja vitendo vya ushujaa, majigambo, na nafasi ya mama katika maisha ya shujaa.

Leo ni mara ya pili kwangu kuandika kuhusu vitabu hivi vya Padri Loogman katika blogu hii. Nilipoandika mara ya kwanza, ujumbe wangu uliwafikia watu wengi, hasa baada ya kutokea katika blogu ya Michuzi. Leo nimeona niwaletee wadau hadithi ya Makari Hodari, waione pia picha yake na picha ya mama yake.

Saturday, December 17, 2011

Wanafunzi Wangu Wameondoka Tanzania

Mapema leo, wanafunzi niliowaleta Tanzania mwaka huu wameondoka nchini, baada ya kumaliza masomo ya miezi kadhaa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Wanafunzi hao nami tunaonekana katika picha hapa kushoto, tuliyopiga kwenye hoteli ya Wilolesi, mjini Iringa, tarehe 10 Agosti.

Kama nilivyoelezea mara kadhaa katika blogu zangu, tulizunguka sehemu mbali mbali, kama vile Kalenga, Matema Beach, Lyulilo na Bagamoyo. Baada ya mizunguko hiyo niliwafikisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nami nikarejea Marekani kwani muhula wa masomo ulikuwa unaanza.

Ni faraja kuona wameondoka salama, kwani nilikuwa na wasi wasi kutokana na taarifa za migomo, vurugu na mabomu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa miaka yote niliyofundisha hapa Marekani nimekuwa mshauri katika programu kadhaa zinazopeleka wanafunzi Tanzania na nchi zingine za Afrika, kama nilivoelezea hapa. Huwa tunawaambia hao wanafunzi kuwa wasishiriki maandamano au migomo katika nchi husika. Kwa upande wa Tanzania, nimekuwa mwepesi kuwaeleza jinsi tulivyo nchi ya amani na utulivu.

Programu hizi zina manufaa mengi sio tu kwa hao wanafunzi, bali kwa wa-Tanzania humo mitaani. Kwa upande wa mahusiano baina ya nchi na nchi, programu hizi zinachangia maelewano baina ya Tanzania na Marekani. Marekani yenyewe kwa miaka mingi imewapokea na kuwaelimisha wa-Tanzania wengi, na wengi wao sasa ni watu wenye madaraka serikalini, katika taasisi mbali mbali, na katika jamii kwa ujumla. Hata kwa upande wa uchumi, mwanafunzi wa kigeni anayesoma Tanzania analiingizia Taifa hela nyingi za kigeni, kumzidi mtalii mara dufu.

Lazima niseme ukweli na kuelezea duku duku yangu. Kutokana na haya mabomu ya polisi ambayo yamekuwa jambo la kawaida vyuoni na mitaani nchini Tanzania, najiuliza kama inawezekana kuendelea kuipigia debe Tanzania kama nilivyozoea. Jambo la kufariji ni kuwa kwa ujumla, wanafunzi wa ki-Marekani wanaoenda Afrika wanaporudi Marekani wanasema kuwa pamoja na matatizo yote, wanakuwa wamejijengea upendo kwa Bara hili. Hii inatokana na ukarimu wanaoupata miongoni mwa watu vijijini, mitaani na mijini.

Friday, December 16, 2011

Vitabu Kama Zawadi ya Idd el Fitr na Krismasi

Hebu fikiria: sikukuu ya Idd el Fitr au Krismasi imewadia na unataka kuwapa zawadi ndugu na marafiki zako, wa-Tanzania wenzako. Unaamua kwenda kwenye duka la vitabu, na unawanunulia nakala za kitabu kama Kufikirika cha Shaaban Robert, au Binadamu na Maendeleo cha Mwalimu Nyerere, au kwa wanaojua ki-Ingereza, The Tempest cha Shakespeare. Unawafungia vizuri, kisha unawapelekea. Je, watajisikiaje hao wa-Islam na wa-Kristu wa Tanzania?

Miaka ya tisini na kitu, katika jumuia ya mawasiliano ya mtandaoni iitwayo Tanzanet, ambayo wanachama wake ni wa-Tanzania na marafiki wa Tanzania, niliwahi kuandika, kiutani, kwamba siku za usoni huenda nikaamua kwamba, kwenye mialiko ya arusi nisipeleke kreti ya bia, bali kreti ya vitabu. Ingawa ulikuwa ni mchapo, nilikuwa na jambo muhimu kichwani, kwani ni kweli kuwa vitabu ni hazina, na ni bora kuliko bia.

Hapa Marekani, ni kawaida watu kutoa au kupokea zawadi ya vitabu. Msimu kama huu wa Krismasi, watu wengi wananunua vitabu ili kuwapa zawadi wenzao. Hata kwenye arusi, mtu unaweza kutoa zawadi ya kitabu.

Je, ukimpa m-Tanzania zawadi ya kitabu wakati wa Idd el Fitr au Krismasi, itakuwaje? Tafakari hilo.

Thursday, December 15, 2011

Hatimaye Itabidi Nielezee Nilivyotoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam

Mwaka 1991 niliondoka Chuo Kikuu Dar es Salaam, nikaja kufundisha Chuo cha St. Olaf hapa Marekani. Kulikuwa na mlolongo wa masuala yaliyonifanya nikaondoka, baada ya kuwa mwalimu pale kuanzia mwaka 1976. Sijaelezea masuala hayo, ingawa yamo katika maandishi kwenye makabrasha, ambayo yalikuwa mawasiliano rasmi baina ya wahusika.

Mwaka jana, nikiwa maeneo ya Mwenge, Dar es Salaam, na marafiki zangu, nilikutana na Profesa Sam Maghimbi wa Chuo cha Elimu cha Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Nilishangaa alivyokumbushia nilivyotoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na marafiki zangu wakasikia. Nilifarijika kuona kuwa kumbukumbu bado zipo kiasi hiki.

Wako wengi wanaokumbuka nilivyofundisha Chuo Kikuu Dar es Salaam, na jinsi nilivyoondoka. Lakini, kwa jinsi miaka inavyopita, wanafikia umri wa kustaafu, na wengine wamefariki. Nami natatizwa na fikra ya wa-Tanzania wengi za kudhani kila m-Tanzania anayeenda kufanya kazi nje hana sababu nyingine bali kufuata maslahi binafsi. Hata mafisadi waliozagaa nchini nao wanaimba wimbo huo huo waonekane wazalendo. Jambo hili linanikera, na ndio maana naona itabidi niandike habari zangu.

Tuesday, December 13, 2011

Leo Nimekuwa Marley Katika Hadithi ya Charles Dickens

Leo katika idara yetu ya ki-Ingereza tulifanya onesho la tamthilia kutokana na hadithi ya A Christmas Carol iliyotungwa na mwandishi maarufu Charles Dickens.

Watu tuliosoma shule zamani tunakumbuka sana vitabu vya Charles Dickens, hasa Oliver Twist. Ni nani asiyekumbuka wahusika wa hadithi hii, kama vile Oliver Twist mwenyewe, The Artful Dodger, na Fagin m-Yahudi? Ilikuwa raha kusoma miaka ile, na tulikuwa tunapenda hata kukariri baadhi ya kauli za hao wahusika.

Basi katika kipindi hiki cha kuelekea Krismasi, idara yetu ina jadi ya kufanya jambo la kumbukumbu na burudani. Kwa miaka kadhaa, tumekuwa tukiigiza mchezo huu unaotokana na riwaya hii ya Dickens. Katika A Christmas Carol kuna wahusika wakuu kadhaa, na Scrooge ndio kinara. Huyu ni mfanyabiashara bahili, ambaye zamani alikuwa na mshiriki wake wa kibiashara aliyeitwa Jacob Marley.

Wakati hadithi inapotokea, tunaambiwa kuwa Jacob Marley alifariki miaka saba iliyopita. Tunachoona ni mzimu tu wa Marley, ambao unamtokea Scrooge kwa namna ya kumfanya afadhaike. Ila mzimu wa Marley unamwachia maaagizo muhimu. Basi, nilipewa jukumu la kuigiza kama mzimu wa Marley. Nilishafanya hivyo pia mwaka juzi.

Tuliamua kuwa niwe Marley kwa namna ya mwanamuziki wa reggae Bob Marley, ili kuleta usasa na kunogesha hadithi. Nilivaa kofia iliyoshonewa rasta, ambayo ilinunuliwa Jamaica na profesa mstaafu wa idara yetu, Jonathan Hill. Nilionekana kama m-Jamaica kabisa. Wakati wote wa onesho nilijitahidi kuongea kama m-Jamaica, na watazamaji wa onesho letu walibaki hawana mbavu. Picha tuliyopiga leo baada ya onesho nimeiweka hapa. Kuna picha ambayo tulipiga mwaka juzi ila sijapata nafasi ya kuitafuta. Ningeiweka hapa pia.

Hadithi hii ya Dickens, kama hadithi zake zingine, inavutia na ina maadili mema, kwani, hatimaye Scrooge anabadilika. Mwanzoni alikuwa bahili na katili asiye na huruma kwa yeyote, na wala hataki hata kusikia maneno kama "Heri ya Krismas." Kwake zote hizo zilikuwa ni kero na upuuzi. Hatimaye, kutokana na mambo ya ajabu yanayomtokea, anabadilika na kuwa mtu mwenye roho njema ya kuvutia.

Posho za Wabunge Hazitoshi

Yapata mwaka 1997 nilipokuwa katika utafiti Mwanza, mimi na washiriki wa utafiti tulikutana na mbunge katika hoteli ya Ramada. Sikumbuki alikuwa ni mbunge wa sehemu gani nchini. Katika maongezi yetu, alilalamika kwa masikitiko kuwa wa-Tanzania wanaamini kuwa mbunge ni mtu mwenye hela sana. Akatoa mfano wa maisha yake mwenyewe, kwamba nyumbani kwake, watu wamejaa kwenye makochi muda wote. Mchana wako hapo, na usiku wanalala hapo. Na yeye anawajibika kuwalisha na kuwanywesha siku zote.

Wakati huu ambapo wa-Tanzania wanalumbana kuhusu kuongeza posho za wabunge, mimi nakumbuka kilio cha yule mbunge. Nasita kuwalaumu wabunge wanapodai kuongezewa posho. Naamini kuwa posho zao hazitoshi.

Tatizo ni sisi wa-Tanzania, sio wabunge. Mtu akishapata ubunge, tunamtegemea atufanyie mambo mengi sana yanayohitaji hela. Mbunge akiingia baa, tunategemea ofa zake, tena za uhakika, sio soda za reja reja. Tunamtegemea achangie hela nyingi kwenye vikao vya "send-off," kipaimara, arusi, na kadhalika. Asipochangia hela nyingi, hatutamhurumia. Na kama ana ndoto ya kugombea tena, anafanya bahati nasibu.

Mbunge asipotembelea eneo lake la uwakilishi, akaweza kujionea kila sehemu na kukutana na watu wote, tutamwona hafai. Bila hela nyingi, mbunge hawezi kutekeleza hayo. Na ukizingatia kuwa kila apitapo, anatakiwa kuchangia misiba, sherehe, na harambee, ni wazi kuwa hata akipewa posho ya laki tatu kwa siku, haitatosha.

Kwa kifupi, kitu cha kwanza kinachotakiwa ni kwa sisi wananchi kubadilika. Tusiwe mzigo kwa mbunge. Tukitekeleza hilo, tutakuwa na haki ya kuhoji ongezeko la posho za wabunge. Lakini kama tabia zetu ndio hizo nilizoelezea, za kutegemea mbunge achangie hela nzito kila shughuli, na utitiri wa watu kuhamia nyumbani kwa mbunge, malalamiko yetu kuhusu ongezeko la posho za wabunge ni unafiki.

Zaidi ya hayo niliyosema, wa-Tanzania wengi ni mbumbumbu. Wakati wa kampeni, tulijionea jinsi wagombea wa chama fulani walivyokuwa wanawahonga wapiga kura kwa khanga, ubwabwa, na kadhalika. Hao wa-Tanzania mbumbumbu wanaafiki na wanategemea hayo. Sasa basi, wabunge wa aina hii wakisema wanahitaji posho ziongezwe, huenda wanafanya maandalizi ya uchaguzi ujao, kwani wapiga kura mbumbumbu watategemea tena hizo khanga, ubwabwa na bia.

Hoja yangu inarudi pale pale, kwamba tatizo linaanzia kwa wananchi.

Saturday, December 10, 2011

Miaka 50 Baada ya Uhuru, Mtoto Albino Anaogopa Kwenda Shule

Jana ilikuwa ni kumbukumbu ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika. Nilijaribu sana kuandaa makala kuhusu siku hiyo ya jana, lakini nilipata kigugumizi. Kwa upande moja, ninafahamu kuwa ndoto ya uhuru aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere, ya kuleta ukombozi wa kweli katika nyanja mbali mbali na kujenga taifa linalojitegemea, imezimishwa na sera zilizopo, ambazo zinaimarisha ukoloni mamboleo. Kama ningeandika makala jana kuhusu kumbukumbu za uhuru wa Tanganyika, pangekuwa hapatoshi.

Lakini jambo jingine lililonipa kigugumizi ni kuwa mawazo yangu yalikuwa yanarudi tena na tena kwenye taarifa niliyosoma wiki kadhaa zilizopita, kuhusu mtoto albino wa Ludewa ambaye anaogopa kwenda shule asije akauawa na watu wenye imani za kishirikina. Habari hii niliiweka hapa.

Siku nzima ya jana nilikuwa najiuliza, inakuwaje miaka 50 baada ya uhuru, mtoto huyu anaishi katika hofu ya kuuawa? Tumepiga hatua mbele au nyuma? Enzi za Mwalimu Nyerere, mtoto huyu angekuwa anaenda shule sawa na watoto wengine. Ndoto ya Mwalimu, wakati Tanganyika inapata uhuru, ilikuwa kwamba tupambane na maadui wakuu watatu: ujinga, umaskini, na maradhi. Leo, kushamiri kwa ujinga katika jamii yetu kunatishia maisha ya mtoto huyu albino.

Nimekuja ofisini asubuhi hii nikaona kwenye blogu ya Mtwara Kumekucha taarifa kuhusu mauaji ya albino. Inakuwa kama vile mawazo yetu yamefanana wakati huu. Naileta hiyo taarifa hapa.


Wednesday, December 7, 2011

Hifadhi za Historia Bagamoyo

Bagamoyo ni mji maarufu katika historia ya nchi yetu na dunia. Kwa mtu anayetaka kujifunza historia hiyo, napendekeza ziara Bagamoyo kuangalia hifadhi zilizopo. Mwaka huu, nilitembelea Bagamoyo, na wanafunzi kutoka Marekani, kama nilivyoelezea hapa. Mahali pamoja tulipotembelea ni Caravan Serai, hifadhi mojawapo ya historia. Hapa kushoto ninaonekana mbele ya mlango wa kuingilia Caravan Serai. Kuna sanamu ya mtumwa aliyebeba pembe ya ndovu.


Hapa kushoto tunaonekana katika eneo la Caravan Serai, tukiwa na mfanyakazi wa hifadhi hiyo, ambaye alikuwa anatuonyesha na kutuelezea yaliyomo.Hapa anaonekana mtaalam wetu akitoa maelezo ya historia ya Caravan Serai.
Humo ndani kuna nyaraka, picha na vitu mbali mbali, kama vile vyombo vya nyumbani, na maelezo kuhusu vitu hivyo. Hapa kushoto, katika picha ya katikati, anaonekana Tippu Tip.


Hapa kushoto ni picha ya watumwa.

Hapa kushoto ni picha ya "bangili," kwa mujibu wa bandiko la maelezo, ambazo walikuwa wakivalishwa watumwa shingoni na kuunganishwa na watumwa wengine kwa mnyororo.


Hapa kushoto ni baadhi ya vitu vya nyumbani.

Vitu ni vingi katika hifadhi hii, na maandishi. Mtu ukiingia hapo, ukaangalia na kusoma yaliyomo, na kusikiliza maelezo, utajikuta umeelimika kutosha.

Hii Caravan Serai ni hifadhi mojawapo tu; kuna nyingine, kama vile ya Kanisa Katoliki, ambayo nimeisikia kwa miaka mingi, na niliiona kwa nje mwaka juzi. Napangia kuingia ndani yake na kuangalia siku za usoni.

Sunday, December 4, 2011

Barua za Shaaban Robert

Kitabu cha Barua za Shaaban Robert ni mkusanyiko wa barua alizoandika Shaaban Robert kwa mdogo wake Yusuf Ulenge baina ya mwaka 1931 na 1958. Yusuf Ulenge alifanya busara ya kuzihifadhi na sasa zimechapishwa kama kitabu, na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mhariri Profesa Mugyabuso Mulokozi amefanya kazi kubwa na watafiti wenzake katika kuzichapisha na kuziwekea maelezo.

Nilikinunua kitabu cha Barua za Shaaban Robert mwaka 2008 katika duka la Taasisi. Nilifurahi na pia kushtuka kugundua kuwa Yusuf Ulenge alikuwa mdogo wa Shaaban Robert. Jina la Yusuf Ulenge nililifahamu tangu kwenye mwaka 1964, nilipokuwa darasa la sita. Nilinunua kitabu kiitwacho Nguzo ya Maji na Hadithi Nyingine, kilichotungwa na Yusuf Ulenge. Miaka yote sikuwa na wazo hata kidogo kuwa huyu alikuwa mdogo wa Shaaban Robert.

Sasa, hizi barua zimenifungua macho kabisa, kwani nimejionea jinsi uhusiano wa hao ndugu wawili ulivyokuwa mkubwa na jinsi Yusuf Ulenge naye alivyokuwa mwandishi mahiri. Katika kitabu hiki kuna taarifa za maandishi mengi ya Yusuf Ulenge, vikiwemo vitabu alivyochapisha na vingine alivyopangia kuchapisha. Mzee Yusuf Ulenge alifariki tarehe 16 Desemba, 2002.

Shaaban Robert ni mfano wa mlezi bora, kwa jinsi alivyokuwa anamshauri na kumwongoza mdogo wake Yusuf katika masuala mbali mbali ya maisha, kama vile elimu. Siwezi kuelezea kwa ufasaha jinsi Shaaban Robert alivyothamini elimu na maadili mema, akawa anamwongoza Yusuf katika njia hiyo. Shaaban Robert alikuwa tayari kutoa gharama zozote zilizohitajika kumlipia Yusuf katika masomo yake, kuanzia daftari hadi usafiri. Ni mfano mzuri sana kwetu wazazi na walezi wa watoto.

Kitabu hiki kinaelimisha sana. Kinautikisa kabisa moyo wangu kwa undani na uzito wa maudhui yake. Kitabu hiki kinafaa kuwemo katika kila nyumba ya wa-Tanzania, ili kisomwe na wazazi na watoto. Hakuna kisingizio cha kutokuwa na kitabu kama hiki, na vitabu vingine vya Shaaban Robert, ambaye ndiye gwiji wa uandishi wa ki-Swahili, mwanafalsafa na mwalimu wa jamii. Hayo nimeyaelezea katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, uk. 30-41

Ingekuwa ni hapa Marekani, tukio la kuchapishwa kitabu kama hiki lingekuwa na kishindo, na watu wangepanga foleni kwenye maduka ya vitabu kukinunua. Kingezungumziwa magazetini na vyombo vingine vya habari. Wa-Tanzania tunapaswa kujiuliza iweje hatuna utamaduni wa aina hiyo. Iweje hatuna hata habari wala hamu ya kujua mwandishi kama Shaaban Robert alizaliwa wapi na aliishi wapi na mchango wake katika jamii na ulimwengu ni upi. Tuko wa-Tanzania yapata milioni arobaini. Ni nyumba ipi katika Tanzania, kuanzia nyumba za walalahoi hadi za hao tunaowaita viongozi, yenye vitabu vya mwandishi muhimu kama huyu?

Kwenye mtandao wa Facebook kuna ukumbi wa wadau na wapenzi wa Shaaban Robert, uitwao Ukumbusho wa Shaaban Robert. Walioanzisha ukumbi huu si wa-Tanzania, bali wa-Kenya. Hii ndio hali halisi, kwamba nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake. Kuthibitisha zaidi jambo hili, jionee jinsi mwanafunzi m-Marekani alivyokichangamkia kitabu hiki cha Barua za Shaaban Robert, akakiandikia uchambuzi huu hapa.

Friday, December 2, 2011

Wadau Wamekuja Ofisini Kwangu

Leo, bila kutegemea, nimetembelewa na akina mama wawili ofisini kwangu. Walijitambulisha, wakasema wamekuja ili nisaini nakala za vitabu vyangu. Anayeonekana kushoto ni Mama Kay wa Lanesboro, Minnesota, na huyu wa kulia ni Mama Sandy wa maeneo ya St. Louis, Missouri.

Nimesaini nakala tatu za Matengo Folktales na moja ya Africans and Americans: Embracing Cultural Differences ambazo wamezinunua leo hapa Chuoni St. Olaf. Tumeongelea vitabu hivi na masuala mengine ya aina hiyo.

Kumbe, Mama Kay, tulishaonana miaka kadhaa iliyopita hapa St. Olaf, alipokuja na mumewe, ambaye ni marehemu sasa, pamoja na Mchungaji Gabriel Nduye, Mchungaji Mengele (ambaye sasa ni askofu) na mkewe, wote kutoka Njombe. Mama Kay ameshafika Tanzania.

Nimewaambia kuwa nimeguswa na ujio wao. Ninaguswa na namna wadau wanavyoyafuatilia maandishi yangu, na falsafa yangu ni kumshukuru Mungu kwa yote. Kama inavyoonekana katika picha, tumefurahi kukutana.