Showing posts with label uongozi. Show all posts
Showing posts with label uongozi. Show all posts

Tuesday, July 25, 2017

Busara za Seneta McCain Muhimu kwa Tanzania

Ninavyoona, Tanzania sio tu inaelekea kubaya katika siasa na mahusiano ya jamii, bali imeshafikia pabaya. Taifa limepasuka. Badala ya siasa za kizalendo, zinazozingatia umuhimu wa umoja wa Taifa, hata wakati wa kutofautiana mitazamo, nchi imegubikwa na uhasama. Serikali imesahau wajibu wake wa kuunganisha nguvu za umma ili kuleta maendeleo.

Tutajengaje nchi wakati kila mahali watu wanaangaliana kiuhasama kutokana na tofauti za mitazamo ya ksiasa? Ili serikali itambue wajibu wake wa kuunganisha Taifa ili kutumia uwezo wa kila mwananchi katika kuleta maendeleo, busara za Seneta John McCain wa Marekani, alizozitoa katika hotuba yake leo tarehe 25 Julai, 2017, ni muhimu.

Dakika za mwisho za hotuba hii zinawahusu zaidi wa-Marekani. Lakini, ukiachilia mbali sehemu hiyo, hotuba hii ina busara muhimu za kuinusuru Tanzania.

 

Sunday, May 21, 2017

"Contagious Success," Kitabu Muhimu

Nina furaha wakati huu kwa kuwa ninasoma kitabu kiitwacho Contagious Success: Spreading High Performance Throughout Your Organization. Nilinunua kitabu hiki siku chache zilizopita, kama nilivyoripoti katika blogu hii. Sikupoteza fedha zangu.

Mwandishi wa kitabu hiki, mwenyekiti wa Hudson Highland Center for High Performance, ni mwenye ujuzi na uzoefu mkubwa. Kitabu chake hiki ni matokeo ya utafiti ulioshirikisha watu wa sehemu mbali mbali ulimwenguni, ambao ni wafanyakazi katika sekta zinazotegemea na kuendeshwa na ujuzi na maarifa. Kwa ki-Ingereza, watu hao huitwa "knowledge workers." Hii ni dhana muhimu katika dunia ya leo na kesho, ambayo inaendelea kuwa dunia ya "knowledge economy."

Tangu mwanzo, kitabu hiki kina mafundisho muhimu kwa viongozi, mameneja, wamiliki wa biashara, watoa huduma na kadhalika. Ujumbe mahsusi ni namna ya kuyaeneza mafanikio katika shirika, kampuni, taasisi, au jamii. Mwandishi anasema: "Every company has high-performing workgroups that both make money for the business and develop new products, services, or markets. These work groups create environments in which results are achieved and people flourish."

Jambo muhimu kabisa ni kujenga mazingira ya kuwezesha ufanisi. Hata kama mtu ni hodari namna gani, hawezi kufanikiwa ipasavyo katika mazingira yasiyo muafaka. Mazingira ni msingi wa mafanikio, na ufanisi wa kikundikazi au vikundikazi unapata fursa ya kuenea katika kampuni au shirika zima.

Mwandishi ananukuu kauli za wataalam waliofafanua mawazo hayo: "According to Daniel Gilbert, Professor of psychology at Harvard University, 'Four decades of scientific research have shown that situations are powerful determinants of human behavior--and much more powerful determinants than most of us realize.'"

Baada ya maelezo, mwandishi analeta nukuu nyingine: "'Changing the situation and shaping the environment--that's what leadership is all about,' noted Linda Ginzel, clinical professor of managerial psychology at the University of Chicago Graduate School of Business."

Mwandishi anaelezea zaidi wazo hilo, na halafu analeta mawazo ya ziada. Kwanza, nyakati zimebadilika. Dunia ya leo si ile ya wakati mapinduzi ya viwanda ("Industrial Age") ambapo wafanyakazi walisimama katika mstari na uzalishaji wa bidhaa ulikuwa unatiririka kama mnyororo ("assembly line"). Wakati ule maamuzi ya namna kuendesha kiwanda yalikuwa mepesi na wazi kuliko sasa. Ushindani haukuwa mkubwa kama leo. Amri zilikuwa zinatoka juu kwa viongozi na kwenda chini, bila matatizo. Wafanya kazi waliwajibika kutii walichoambiwa. Hawakuhitaji kuwa wabunifu.

Leo mambo yamebadilika. Wafanyakazi hawatakiwi wawe watu wa kufuata tu maelekezo. Lazima watumie akili na ubunifu, kukabiliana na mazingira ya leo. Mazingira haya yanahitaji pia mabadiliko ya mtindo wa uongozi: "The strategies that worked in the Industrial Age are no longer effective. Leaders need to be honest about their own strengths and weaknesses. They must recognize that they can't be or do everything and, therefore, should make sure the people around them have complementary strengths."

Anaendelea kufafanua, kwa kunukuu kauli ya Carol Hymowitz katika Wall Street Journal:  "Arrogance is out of fashion in the executive suite. So are autocratic executives who rule by intimidation, think they have all the answers and don't believe they need to be accountable to anyone."

Kuhitimisha suala hili la uongozi mpya, mwandishi anasema kuwa uongozi ni lazima uwe unawathamini watu, unathamini ubunifu na uthubutu, na uwe mwepesi kuzitambua na kuzikamata fursa zinazojitokeza.

Nilivyokuwa ninasoma haya mawazo, nimejikuta nikiwazia Tanzania na malengo ya serikali ya kujenga nchi ya viwanda. Nimeona wazi kuwa ili tufanikiwe, lazima tujiweke sawa kwa mambo mengi, kama haya ya kuwathamini watu, kuweka mazingira muafaka na kuzingatia rasilimali watu, ambayo inakwenda sambamba na kuwapa watu uhuru wa kufikiri, kuwa wabunifu na watundu, hata kama kwa utundu wao wanaishia kufanya makosa. Watu wakiwa na uoga wa kufanya makosa, mafanikio yanaweza kuwa shida kupatikana.

Kitabu hiki cha Contagious Success nimekifurahia sio tu kwa sababu kinaelimisha sana, bali pia, kwa kiasi kikubwa, kwa sababu kimenikumbusha kitabu kingine, Leading Beyond the Walls, ambacho ninacho na nilikiongelea katika blogu hii.

Saturday, May 13, 2017

Msikilize Raia wa Marekani Anavyomrarua Kiongozi

Jambo moja linalonivutia kuhusu Marekani ni uhuru wa kujieleza. Katiba ya Marekani inalinda uhuru huo kikamilifu. Kwa mfano, kulikuwa na kesi dhidi ya mtu aliyechoma moto bendera ya Taifa, lakini mahakama kuu iliamua na imeendelea kusisitiza kuwa kuchoma moto bendera ya Taifa ni sehemu ya uhuru wa kujieleza, ambao unalindwa na katiba. Mahakama kuu inasisitiza kuwa kauli tata, za kukera, au za kuwakosoa watawala ndizo hasa katiba ilikusudiwa kuzilinda.

Serikali ya Marekani inafahamu kuwa raia ana uhuru na haki kamili ya kuikosoa. Viongozi wa Marekani wanajua hilo. Ninaleta video hapa, inayomwonyesha mwananchi akimfokea kiongozi bila kumung'unya maneno. Mwone kiongozi huyu kutoka chama tawala cha Rais Donald Trump alivyonywea, wakati kipigo kinaendelea.

Saturday, April 8, 2017

Mwaliko Chuo Kikuu cha Winona

Tangu mwaka uanze, nimetoa mihadhara au kufanyiwa mahojiano nje ya chuo ninapofundisha, mara nyingi kuliko kawaida. Nilitegemea kuwa kuanzia mwezi huu wa Aprili, hali ingebadilika. Lakini dalili hazionyeshi mabadiliko.

Tarehe 6, nilipata mwaliko kutoka kwa Alex Hines, mkuu wa idara ya Inclusion and Diversity katika Chuo Kikuu cha Winona, wa kwenda kutoa mhadhara:

We would like to extend an invitation for you to attend HOPE Academic & Leadership Academy during the week of June 26th through June 29th and conduct a two hour presentation from 7-9 p.m. on Embracing African and African American Culture.

Hii itakuwa ni mara ya tatu mimi kwenda kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Winona. Mara ya kwanza, niliongelea masuala ya utamaduni kama nilivyoyaeleza katika kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Mara ya pili, niliongelea mahusiano ya binadamu na uongozi, kwa kutumia kitabu cha Matengo Folktales, kama nilivyoandika katika blogu hii

Mwaliko huu wa sasa, kama ilivyoelezwa katika barua niliyonukuu hapa juu, msingi wake ni kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Alex Hines, tangu tulipofahamiana, miaka mingi iliyopita, amekuwa ni mmoja wa wale wanaonitegemea katika programu zao. Ninafurahi kwa imani ya wadau juu yangu, nami ninahamasika kufanya makubwa zaidi kwa ajili yao.

Blogu hii ni mahali ninapohifadhi kumbukumbu zangu, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii. Labda kuna siku nitapata wazo la kuandika kitabu kuhusu shughuli zangu. Ikitokea hivyo, kumbukumbu hizi zitanifaa.

Monday, September 28, 2015

Kampeni za CCM Mwaka Huu

Najaribu kutafakari picha hii iliyopigwa katika moja ya mikutano ya kampeni za uchaguzi zinazoendelea Tanzania. Ina maana kwamba mwenye uwezo wa kupiga "push-up" nyingi ndio anafaa kuwa kiongozi? Je, ili uukwae ubunge, unatakiwa upige angalau "push-up" ngapi? Udiwani je? Na ili uwe waziri, unahitaji "push-up" ngapi? Na kwa uwaziri, ni sahihi tuwe na "push-up" tu au na kuruka viunzi pia? Na kwa kuzingatia uzito wa cheo cha uwaziri, kwa nini tusiongezee pia uwezo wa kunyanyua matofali angalau manne ya zege? Kwa kweli, tukifanya hivyo, tutapata serikali imara kabisa.

Saturday, September 12, 2015

Wazo Kuhusu Kuchagua Kiongozi

Tunavyoelekea kwenye uchaguzi, mwezi ujao, nchini Tanzania, tunaona malumbano yanashamiri. Tunataka kujua nani anafaa kuwa kiongozi. Napenda kuchangia kifupi malumbano haya. Mchango wangu unasimama katika taaluma na utafiti.

Suala la uongozi linaingia moja kwa moja katika utafiti juu ya akili na saikolojia. Miaka yetu hii, watafiti wamekuwa wakituambia kuwa kuna aina nyingi za akili. Kuna maandishi mengi juu ya suala hilo, ambalo kwa ki-Ingereza linajulikana kama "multiple intelligence" au "multiple intelligences."

Kwa mujibu wa utafiti huo, uongozi unahitaji aina ya akili iitwayo "emotional intelligence." Ni akili inayomfanya mtu awe na mvuto kwa watu kwa haiba na mwenendo wake, uwezo wa kuunganisha watu, uwezo wa kuwafanya wafuate njia fulani kwa kutumia ushawishi, si vinginevyo. Mtu mwenye "emotional intelligence" kubwa ndiye anayefaa kuwa kiongozi.

Katika malumbano yanayoendelea miongoni mwa wa-Tanzania wakati huu wa kuelekea uchaguzi, sijaona dhana hii ya "emotional intelligence" ikitajwa. Sijaona kigezo hiki kikitajwa. Watu wanaongelea vitu kama uchapa kazi kama kigezo, lakini si "emotional intelligence." Watu wanaongelea uwezo wa kutoa hotuba ndefu, au uwezo wa kutembea kwa ukakamavu. Lakini hawaongelei "emotional intelligence."

Kwani kutoa hotuba ndefu ndio nini? Mtu unaweza kuongea kwa masaa lakini ukawa unasema umbea na upupu. Mtu mwingine anaweza kuongea kifupi, lakini akawa anatoa hoja thabiti.

Kwani nguvu za mwili na kifua kama cha mpiga ndondi ndio nini? Inahusiana vipi na uongozi? Lakini hivyo ndivyo vigezo vinavyoshabikiwa katika malumbano ya wa-Tanzania.

Hii haishangazi. Tanzania ni nchi ya watu wasio na utamaduni wa kusoma vitabu vya kuelimisha. Watanzania ni wavivu kutafuta elimu. Ndivyo walivyo, na ndivyo wanavyojiandaa kwa uchaguzi.

Tuesday, May 26, 2015

Mwaliko Chuo Kikuu cha Winona

Nimepata mwaliko kutoka Chuo Kikuu cha Winona, Minnesota, kwenda kutoa mhadhara tarehe 23 Juni. Huu utakuwa ni mchango wangu katika semina ya mafunzo kwa wanafunzi kutoka sehemu mbali mbali itakayofanyika Juni 17-27. Kama ilivyo kawaida yangu, nimeona niweke kumbukumbu hapa.

Mafunzo haya yatalenga kuwaandaa wanafunzi hao kwa masomo ya juu, waweze kuifahamu hali halisi ya maisha ya chuoni na taratibu za taaluma, waweze kujijengea hali ya kujitambua na uwezo wa uongozi.

Mratibu wa mafunzo, Alexander Hines, ambaye anafahamu kiasi shughuli zangu,  aliniambia tuangalie ni kipi kati ya vitabu vyangu viwili kitafaa zaidi kwa semina hii: Africans and Americans: Embracing Cultural Differences au Matengo Folktales. Nilishauri kwamba hicho cha pili kingeendana vizuri zaidi na dhamira kuu ya semina.

Tumekubaliana. Tumekubaliana nikaelezee ni nini tunaweza kujifunza kutokana na tamaduni za jadi za Afrika katika masuala haya ya kujitambua, falsafa ya maisha, na uongozi katika dunia ya leo na kesho.

Kama ilivyo kawaida yangu, huwa napokea mialiko ya kutoa mchango wa mawazo kufuatana na mahitaji ya wale wanaonialika. Itabidi nitafakari na kuandaa mawazo yatakayotoa mchango unaohitajika katika semina. Wazo la kutumia kitabu cha Matengo Folktales kama msingi ni wazo muafaka, kwani masimulizi haya ya jadi yanathibitisha jinsi wahenga wetu walivyoyatafakari masuala muhimu ya maisha, mahusiano, na mengine yanatuhusu leo na yataendelea kuwa muhimu daima.
 

Tuesday, May 24, 2011

Nataka Tanzania Isitawalike Kamwe

Nataka Tanzania isitawalike kamwe. Kama hupendi kusikia hayo, shauri lako. Mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa, ila nataka Tanzania isitawalike.

Nataka Tanzania iwe na viongozi, sio watawala. Wanaotaka kutawala wasipate nafasi hiyo. Uongozi unahitaji busara na ushawishi, kukubalika na jamii husika. Kama ni kutawaliwa, tulitawaliwa na wakoloni. Masultani walikuwa wanatawala. Walikuwa wakandamizaji, sawa na wakoloni. Wazee wetu walipambana hadi Uhuru ukapatikana.

Nataka nchi yetu iimarishe misingi ya Uhuru na demokrasia. Kutawala ni suala la mabavu, kwani hakuna jamii inayokubali kutawaliwa, labda iwe ni jamii ya wajinga, au waoga, au ambao wamelishwa sana kasumba ili wasitambue haki zao.

Lakini jamii inayojitambua, inayotambua maana ya uhuru, haki, na demokrasia, jamii inayothamini na kutetea hayo, haiwezi kutawalika, labda kwa mabavu na vitisho. Itakuwa ni jambo la kuhuzunisha iwapo Tanzania itatawalika. Nataka tuwe macho, tuwe makini, nchi yetu isitawalike, kamwe.

Tuesday, April 5, 2011

Mwalimu Nyerere Aongelea Uongozi, 1995

Suala la uongozi lilikuwa moja ya vipaumbele vya Mwalimu Nyerere maisha yake yote. Tunasikia, kwa mfano, jinsi alivyolichukulia suala hili alipokuwa kiongozi wa wanafunzi katika shule ya Tabora. Wakati wa kupigania Uhuru na baada ya Uhuru aliliongelea suala hili tena na tena, kama vile katika "Azimio la Arusha" na "Mwongozo."

Mwalimu aliliongelea suala hili tena, kwa masikitiko, katika kitabu chake cha "Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania," akiihofia hatima ya Tanzania kutokana na uongozi mbovu wa CCM. Niligusia suala hilo katika makala hii hapa. Hata baada ya kuandika kitabu hiki, Mwalimu aliendelea kuongelea suala la uongozi. Hebu msikilize katika hotuba yake hii ya mwaka 1995.

Tuesday, October 26, 2010

Mbumbumbu Waache Kugombea Uongozi

Kitu kimoja kinachonikera ni jinsi wakati wa kugombea uongozi, mbumbumbu wengi wanavyojitokeza kuwania uongozi. Halafu, kwa jinsi wapiga kura wengine walivyo mbumbumbu, wanawapigia kura hao mbumbumbu wenzao na kuwawezesha kushinda.

Baada ya hapo, kunakuwa na matatizo mengi. Tatizo moja kubwa ni jinsi hao mbumbumbu wanaoitwa viongozi wanavyojifanya miungu. Hawakubali kukosolewa.

Kwa mfano, gazeti likiwakosoa, wanalitishia au wanazuia lisichapishwe. Kama kuna kitabu kimewakosoa, wanakipiga marufuku. Msimamo wangu ni kuwa watu wasiojiamini au wasioheshimu uhuru wa watu kutoa fikra, wasigombee uongozi.

Nchi inahitaji viongozi wa kweli, ambao wanatambua kuwa wao si miungu, na ambao hawatetereki kwa kukosolewa. Kibaya zaidi ni kuwa hao mbumbumbu wanadhani kuwa wao ndio nchi. Wakikosolewa, wanasema ni hatari kwa usalama wa taifa. Ni usalama wa taifa au ni usalama wa mbumbumbu? Ni taifa gani ambalo linatetereka kwa sababu ya mbumbumbu kukosolewa?

Haya ninayosema nayasema kwa dhati. Mimi mwenyewe ninakosolewa na hata kutukanwa. Kwa mfano, soma hapa, na hapa.

Sioni sababu ya kuwazuia watu wanaofanya hivyo, hata kama ningekuwa kiongozi. Ni muhimu watu wawe huru kutoa mawazo yao. Ingawa tunasema kuwa tutumie lugha ya kuheshimiana, na mimi nakubali hivyo, lakini hatimaye nasema kuwa hata anayetukana anakuwa amepata fursa ya kujieleza. Ni bora iwe hivyo kuliko kuwafunga watu mdomo, kwani madhara ya kuwanyima watu fursa ya kujieleza yanaweza kuwa mazito. Nimefafanua zaidi msimamo wangu huo katika kitabu cha CHANGAMOTO.

Napenda kurudia, mbumbumbu waache kugombea uongozi. Nafasi hizi zinahitaji viongozi, si watu ambao hawajiamini.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...