Saturday, September 12, 2015

Wazo Kuhusu Kuchagua Kiongozi

Tunavyoelekea kwenye uchaguzi, mwezi ujao, nchini Tanzania, tunaona malumbano yanashamiri. Tunataka kujua nani anafaa kuwa kiongozi. Napenda kuchangia kifupi malumbano haya. Mchango wangu unasimama katika taaluma na utafiti.

Suala la uongozi linaingia moja kwa moja katika utafiti juu ya akili na saikolojia. Miaka yetu hii, watafiti wamekuwa wakituambia kuwa kuna aina nyingi za akili. Kuna maandishi mengi juu ya suala hilo, ambalo kwa ki-Ingereza linajulikana kama "multiple intelligence" au "multiple intelligences."

Kwa mujibu wa utafiti huo, uongozi unahitaji aina ya akili iitwayo "emotional intelligence." Ni akili inayomfanya mtu awe na mvuto kwa watu kwa haiba na mwenendo wake, uwezo wa kuunganisha watu, uwezo wa kuwafanya wafuate njia fulani kwa kutumia ushawishi, si vinginevyo. Mtu mwenye "emotional intelligence" kubwa ndiye anayefaa kuwa kiongozi.

Katika malumbano yanayoendelea miongoni mwa wa-Tanzania wakati huu wa kuelekea uchaguzi, sijaona dhana hii ya "emotional intelligence" ikitajwa. Sijaona kigezo hiki kikitajwa. Watu wanaongelea vitu kama uchapa kazi kama kigezo, lakini si "emotional intelligence." Watu wanaongelea uwezo wa kutoa hotuba ndefu, au uwezo wa kutembea kwa ukakamavu. Lakini hawaongelei "emotional intelligence."

Kwani kutoa hotuba ndefu ndio nini? Mtu unaweza kuongea kwa masaa lakini ukawa unasema umbea na upupu. Mtu mwingine anaweza kuongea kifupi, lakini akawa anatoa hoja thabiti.

Kwani nguvu za mwili na kifua kama cha mpiga ndondi ndio nini? Inahusiana vipi na uongozi? Lakini hivyo ndivyo vigezo vinavyoshabikiwa katika malumbano ya wa-Tanzania.

Hii haishangazi. Tanzania ni nchi ya watu wasio na utamaduni wa kusoma vitabu vya kuelimisha. Watanzania ni wavivu kutafuta elimu. Ndivyo walivyo, na ndivyo wanavyojiandaa kwa uchaguzi.

1 comment:

NN Mhango said...

Ndugu Mbele
Hujatutendea haki watanzania katika mjumlisho wako kuwa hatuna utamaduni wa kusoma vitabu wakati wapo ambao achia mbali kusoma bali wanaandika vitabu. Japo nakubaliana nawe kuwa watu wetu wengi hawana utamaduni wa kujisomea, si vizuri kuwajumlisha wote. Pia ufahamu kuwa kiongozi wa Tanzania mara nyingi hutegemea vigezo tofauti na unavyopendekeza. Hii dhana ya emotional intelligence kama ilivyotafitiwa na kuibuliwa na Daniel Goleman inaweza kuwa ngeni si kwa watanzania bali kwa watu wengi hasa ikizingatiwa kuwa ni dhana ngeni na mpya. Nadhani badala ya kuwalaumu watanzania tufahamu kuwa kila jamii hutoa kiongozi anayefanana na jamii iliyomchagua. Inanikumbusha falsafa ya Plato ya the good society and the good soul. Hivyo, kwa ufupi ni kwamba wanachotafuta watanzania japo si wote kinaweza kuwa si kile kinachotakiwa bali wanachokitaka. Utashangaa kwa mfano ukiangalia wagombea wao wenye ushawishi yaani Dk John Magufuli na Edward Lowassa. Wote wamezaliwa na kulelewa na CCM. Wameshiriki kwenye uoza wanaosema wanataka kuundoa. Je wanakuwa wakweli kwa watanzania? Huwezi kuilaumu CCM kwa mabaya ambayo mengi licha ya kuyashiriki umeyasimamia kama alivyokaririwa akisema waziri mkuu mstaafu Joseph Warioba kuwa wanoatumia kauli za marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere wanakosea wanaposema CCM haijfanya kitu wakati ndiye aliyeiunda na kumpa umaarufu wengi wanaotaka kudandia.