Nilikuwa mmojawapo wa watu waliopinga wazi wazi hatua ya serikali ya kulifungia gazeti la MwanaHalisi. Ninasimamia uhuru wa kutoa mawazo, uhuru wa waandishi, kama ilivyofafanuliwa katika tangazo la kimataifa la haki za binadamu.
Taarifa tulizozipata leo ni kwamba mahakama imetamka kwamba ni juu ya Saed Kubenea kuamua kuendelea kuchapisha gazeti lake au kutoendelea. Vile vile, mahakama imeacha mlango wazi kwa Saeed Kubenea kuishtaki serikali na kudai fidia kwa kipindi chote ambapo gazeti lake lilikuwa limezuiwa.
Ni wazi kwamba, endapo Saed Kubenea atadai fidia, ambayo ni haki yake, walipa kodi wa Tanzania watabeba mzigo mkubwa. Labda watajifunza hasara ya kuiweka madarakani serikali isiyo makini, isiyoheshimu haki za binadamu ipasavyo, au kuwaweka madarakani watu wasio makini, wasioheshimu haki za binadamu ipasavyo. Tusifiche ukweli: kulifungia gazeti la MwanaHalisi, sawa na vitendo vingine vya uvunjwaji wa haki za binadamu, kumechafua jina la Tanzania.
No comments:
Post a Comment