Showing posts with label gazeti. Show all posts
Showing posts with label gazeti. Show all posts

Wednesday, December 14, 2016

Wosia wa Rabindranath Tagore Kuhusu Uhuru wa Kutoa Maoni

Rabindranath Tagore ni mmoja wa waandishi maarufu kabisa waliowahi kuishi. Alizaliwa mwaka 1861 Calcutta na kufariki 1941. Aliheshimika duniani kote wakati wa uhai wake na bado anaheshimika. Aliandika mashairi, tamthilia, insha, riwaya, hadithi fupi, na pia maelfu ya barua. Niliwahi kufundisha utungo wake maarufu Gitanjali, hapa chuoni St. Olaf.

Tagore alikuwa mwalimu aliyetukuka, kioo cha ubinadamu wa kweli ("humanism"), mwenye fikra pevu na nzito juu ya maisha na maadili. Watu maarufu kama W.B. Yeats, Mahatma Gandhi na Albert Einstein, walimmwenzi sana. Mwaka 1913 alipata tuzo ya Nobel katika fasihi. Nina vitabu vyake vitatu, kimojawapo kikiwa Rabindranath Tagore: An Anthology.

Kutoka katika kitabu hiki nimenukuu sehemu ya ujumbe wa tarehe 25 Septemba, 1930, kwa gazeti la Izvestia la Urusi. Ni ujumbe unaopaswa kutafakariwa na kuzingatiwa, tunaposhuhudia ukandamizaji wa uhuru wa watu kujieleza. Ili kuufikisha ujumbe kwa watu wasiojua ki-Ingereza, nimejaribu kuutafsiri.

     There must be disagreement where minds are allowed to be free. It would not only be an uninteresting but sterile world of mechanical regularity if all our opinions were forcibly made alike. If you have a mission which includes all humanity, you must, for the sake of that living humanity, acknowledge the existence of differences of opinion. Opinions are constantly changed and re-changed only through the free circulation of intellectual forces and moral persuasion. Violence begets violence and blind stupidity. Freedom of mind is needed for the reception of truth; terror hopelessly kills it. The brute cannot subdue the brute. It is only the man who can do it.

Tafsiri

     Lazima pawepo na kutokubaliana mahali ambapo akili zinaruhusiwa kuwa huru. Dunia itakuwa sio tu haipendezi bali tasa yenye kwenda kwa mwendo ule ule kama mashine, iwapo maoni yetu yote yatalazimishwa kufanana. Kama watu mna malengo yanayowahusu wanadamu kwa ujumla wao, sherti, kwa manufaa ya uhai wa jamii hiyo ya wanadamu, kutambua uwepo wa tofauti za maoni. Maoni hubadilishwa bila ukomo pale tu panapokuwa na mzunguko huru wa nguvu za akili na ushawishi wa mwenendo wa kimaadili. Mabavu huzaa mabavu na ujinga mithili ya upofu. Uhuru wa akili unahitajika ili ukweli upokelewe, na vitisho huua kabisa ukweli huo. Hayawani hawezi kumdhibiti hayawani. Ni binadamu tu ndiye anaweza.

Friday, September 4, 2015

Gazeti la "MwanaHalisi" Lafunguliwa

Nimefurahi kuona taarifa kuwa mahakama kuu ya Tanzania imeamuru kufunguliwa kwa gazeti la MwanaHalisi ambalo serikali ya CCM ililifungia mwaka 2012. Ni ushindi kwa mmiliki wa MwanaHalisi, Saed Kubenea, na timu yake. Ni ushindi kwa watetezi wa uhuru wa vyombo vya habari.

Nilikuwa mmojawapo wa watu waliopinga wazi wazi hatua ya serikali ya kulifungia gazeti la MwanaHalisi. Ninasimamia uhuru wa kutoa mawazo, uhuru wa waandishi, kama ilivyofafanuliwa katika tangazo la kimataifa la haki za binadamu.

Taarifa tulizozipata leo ni kwamba mahakama imetamka kwamba ni juu ya Saed Kubenea kuamua kuendelea kuchapisha gazeti lake au kutoendelea. Vile vile, mahakama imeacha mlango wazi kwa Saeed Kubenea kuishtaki serikali na kudai fidia kwa kipindi chote ambapo gazeti lake lilikuwa limezuiwa.

Ni wazi kwamba, endapo Saed Kubenea atadai fidia, ambayo ni haki yake, walipa kodi wa Tanzania watabeba mzigo mkubwa. Labda watajifunza hasara ya kuiweka madarakani serikali isiyo makini, isiyoheshimu haki za binadamu ipasavyo, au kuwaweka madarakani watu wasio makini, wasioheshimu haki za binadamu ipasavyo. Tusifiche ukweli: kulifungia gazeti la MwanaHalisi, sawa na vitendo vingine vya uvunjwaji wa haki za binadamu, kumechafua jina la Tanzania.

 

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...