Showing posts with label W.B. Yeats. Show all posts
Showing posts with label W.B. Yeats. Show all posts

Wednesday, December 14, 2016

Wosia wa Rabindranath Tagore Kuhusu Uhuru wa Kutoa Maoni

Rabindranath Tagore ni mmoja wa waandishi maarufu kabisa waliowahi kuishi. Alizaliwa mwaka 1861 Calcutta na kufariki 1941. Aliheshimika duniani kote wakati wa uhai wake na bado anaheshimika. Aliandika mashairi, tamthilia, insha, riwaya, hadithi fupi, na pia maelfu ya barua. Niliwahi kufundisha utungo wake maarufu Gitanjali, hapa chuoni St. Olaf.

Tagore alikuwa mwalimu aliyetukuka, kioo cha ubinadamu wa kweli ("humanism"), mwenye fikra pevu na nzito juu ya maisha na maadili. Watu maarufu kama W.B. Yeats, Mahatma Gandhi na Albert Einstein, walimmwenzi sana. Mwaka 1913 alipata tuzo ya Nobel katika fasihi. Nina vitabu vyake vitatu, kimojawapo kikiwa Rabindranath Tagore: An Anthology.

Kutoka katika kitabu hiki nimenukuu sehemu ya ujumbe wa tarehe 25 Septemba, 1930, kwa gazeti la Izvestia la Urusi. Ni ujumbe unaopaswa kutafakariwa na kuzingatiwa, tunaposhuhudia ukandamizaji wa uhuru wa watu kujieleza. Ili kuufikisha ujumbe kwa watu wasiojua ki-Ingereza, nimejaribu kuutafsiri.

     There must be disagreement where minds are allowed to be free. It would not only be an uninteresting but sterile world of mechanical regularity if all our opinions were forcibly made alike. If you have a mission which includes all humanity, you must, for the sake of that living humanity, acknowledge the existence of differences of opinion. Opinions are constantly changed and re-changed only through the free circulation of intellectual forces and moral persuasion. Violence begets violence and blind stupidity. Freedom of mind is needed for the reception of truth; terror hopelessly kills it. The brute cannot subdue the brute. It is only the man who can do it.

Tafsiri

     Lazima pawepo na kutokubaliana mahali ambapo akili zinaruhusiwa kuwa huru. Dunia itakuwa sio tu haipendezi bali tasa yenye kwenda kwa mwendo ule ule kama mashine, iwapo maoni yetu yote yatalazimishwa kufanana. Kama watu mna malengo yanayowahusu wanadamu kwa ujumla wao, sherti, kwa manufaa ya uhai wa jamii hiyo ya wanadamu, kutambua uwepo wa tofauti za maoni. Maoni hubadilishwa bila ukomo pale tu panapokuwa na mzunguko huru wa nguvu za akili na ushawishi wa mwenendo wa kimaadili. Mabavu huzaa mabavu na ujinga mithili ya upofu. Uhuru wa akili unahitajika ili ukweli upokelewe, na vitisho huua kabisa ukweli huo. Hayawani hawezi kumdhibiti hayawani. Ni binadamu tu ndiye anaweza.

Monday, December 12, 2016

Leo Nimemaliza Kufundisha Muhula wa Kwanza

Leo nimemaliza kufundisha muhula wa kwanza. Nilikuwa ninafundisha kozi tatu: "First Year Writing," "African Literature," na "Muslim Women Writers." Nilihitimisha ufundishaji wa "First Year Writin"g wiki iliyopita, ili kuwapa wanafunzi muda wa kuandika insha kuu ya mwisho. Katika kozi hii, ninafundisha uandishi bora wa ki-Ingereza, na uangalifu unaotakiwa katika vipengele vyote , kuanzia neno, hadi sentensi, hadi insha.

Katika African Literature tumemalizia muhula tukisoma riwaya ya Mia Couto, The Tuner of Silences. Mia Couto ni mwandishi wa Msumbiji, ambaye ni maarufu sana. Amepata sifa na tuzo kem kem, ikiwemo tuzo ya Neustadt. The Tuner of Silences ni riwaya inayosisimua akili kwa jinsi ilivyosheheni ubunifu wa kisanaa na kifikra.

Kuna mengi ya kutafakari katika riwaya hii, hasa yatokanayo na dini, fasihi linganishi, historia, falsafa kama vile "existentialism," na mikondo ya falsafa ya sanaa kama vile "surrealism."  Vile vile, taaluma ya saikolojia, kama vile mkondo wa "psychoanalysis," inasaidia kutafakari dhamira zilizomo. Kuisoma na kuufaidi utajiri wa riwaya kama The Tuner of Silences kunahitaji upeo mpana wa mawazo ambao unatokana na kusoma kwingi, sio tu fasihi bali taaluma mbali mbali.

Katika kuiongelea The Tuner of Silences darasani, nimesisitiza jambo hilo, Nimefundisha wanafunzi umuhimu wa kuzingatia nadharia za usomaji kama zilivyoelezwa na Cleanth Brooks katika insha yake, "The Language of Paradox," na pia zilivyoelezwa na Roland Barthes katika kitabu chake kiitwacho S/Z: An Essay.

Katika kozi ya "Muslim Women Writers," tumemalizia muhula tukisoma riwaya ya Monica Ali, Brick Lane. Ni riwaya ndefu, inayoelezea maisha ya watu wa Bangladesh ambao wanaishi Uingereza. Ni jamii ya ki-Islam, na tunaiona inavyojitahidi kustahimili na kustawi katika mazingira ya ugenini.

Hii ni jamii kama jamii zingine, yenye watu wenye maadili mema na ari ya kuwa mfano kwa wengine, na pia wako ambao tabia zao zina walakini. Wanapenda kufuatilia habari za wenzao, na ni wapiga majungu. Tofauti baina ya utamaduni wao na ule wa wa-Ingereza zinajitokeza, na pia tofauti baina ya vijana na watu wazima au wazee. Vijana wanaonekana kuiga mambo ya vijana wa kizungu, yakiwemo ambayo si mazuri.

Kufundisha kazi ya fasihi kutoka Bangladesh imekuwa ni fursa ya kuelezea historia ya fasihi ya nchi hiyo, ukiwemo mchango mkubwa wa Rabindranath Tagore, mwandishi wa mashairi, tamthilia, riwaya, na insha, ambaye aliitwaa tuzo ya Nobel mwaka 1913. Kwa bahati nzuri, Tagore ametajwa katika Brick Lane, kwa jinsi alivyo hazina kwa watu wa Bangladesh. Lakini jambo la kuzingatia ni kuwa Tagore ni mwamba katika fasihi ya ulimwengu, aliyeheshimiwa na miamba wenzake kama vile W.B. Yeats wa Ireland, aliyekuwa na urafiki na mawasiliano na Tagore.

Leo, katika kuhitimisha kozi yetu ya "Muslim Women Writers," nimewaomba wanafunzi ushauri juu ya kuitumia tena riwaya hii siku za usoni, nitakapofundisha kozi hii. Wameniambia kuwa ni riwaya muhimu sana, ingawa inachukua muda sana kuisoma. Wameshauri kwamba nitakapofundisha tena kozi hii, Brick Lane iwe mwanzoni, wakati wanafunzi wakiwa bado hawajachoka na masomo. Riwaya zingine, ambazo ni fupi fupi, zije baadaye. Nimewashukuru kwa ushauri huo wa wanafunzi ambao wamepitia kozi yangu, nikizingatia kuwa adhabu ya kaburi aijuaye maiti.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...