Wednesday, September 2, 2015

Hotuba ya Dr. Wilbroad Slaa Kuacha Siasa

Kuhusu hotuba ya Dr. Slaa kwa waandishi wa habari akitangaza kuondokana na siasa, mengi muhimu yamesemwa na wenye upeo na tafakari nzito kunizidi. Ila nami kama raia mwingine yeyote, nina uhuru kamili wa kuongelea suala hili, kama mwananchi anavyoongea mtaani, ambayo ni haki yake.

Napenda nianze kwa kujikumbusha kwamba kwa miaka mingi, CCM wamekuwa wakimbeza Dr. Slaa, kwamba ni mzushi na mropokaji. Alipoanza kusema kuna ufisadi, CCM walimkatalia katakata, wakasema ni mzushi. Baadaye, vijana wa UVCCM wakawa wanafanya kibarua cha kumtukana Dr. Slaa.

Sasa, baada ya huyu mzushi na mropokaji kutema cheche juzi, mbele ya waandishi wa habari, nasubiri kuwasikia CCM wanasemaje. Wakisema tumpuuze kwa vile ni mzushi na mropokaji, basi ina maana kuwa UKAWA hawana sababu ya kukosa usingizi wala kujibishana naye. Kwa nini mtu ukose usingizi kwa sababu ya maneno ya mtu anayefahamika wazi kuwa ni mzushi na mropokaji?

Nitawashangaa CCM iwapo watashangilia mashambulizi ya Dr. Slaa dhidi ya Lowassa na UKAWA. Nitawashangaa.

Dr. Slaa amewaponda kabisa CCM. Sio tu kwa jinsi alivyoifananisha CCM na choo kichafu, bali kwa kauli yake kwamba serikali ya CCM ni waoga wa kuwachukulia hatua watuhumiwa wa ufisadi. Amesema kuwa CCM ni mfumo unaofuga mafisadi. Sio hivyo tu, bali amewaumbua pia wabunge wa CCM, kwamba hawasomi wanayopaswa kusoma.

Alivyosema hayo kuhusu wabunge wa CCM, nimekubaliana naye kabisa, kwani nami nilishaandika kuhusu wabunge hao nikiwaita mbumbumbu. Ushahidi ulikuwa jinsi walivyotoroka midahalo wakati wa uchaguzi wa mwaka 2010. Midahalo inaheshimiwa na watu wote wenye akili, lakini mbumbumbu hawaelewi umuhimu wake.

Umbumbumbu wa wabunge wa CCM umejidhihirisha tena na tena kwa tabia yao ya kuzomea Bungeni, na tabia ya kuunga mkono chochote kinachosemwa na serikali ya CCM. Kwa hayo yote, ninaichukulia kwa uzito upasao kauli ya Dr. Slaa kuwa wabunge wa CCM hawasomi.

Dr. Slaa hajawaonea CCM kwa hilo. Nakumbuka ule mwaka Mwalimu Nyerere alipojiandaa kung'atuka uenyekiti wa CCM, alizunguka nchi nzima akikagua uhai wa chama hicho. Inaonekana hakuridhika, kwani kuna siku alisema kuwa wako watu katika CCM ambao hata mtihani kuhusu "Azimio la Arusha" hawawezi kupasi. Kwa hivyo Mwalimu alishabaini umbumbumbu katika CCM tangu miaka ile ya katikati ya themanini na kitu.

Sasa, nikijumlisha hayo yote, nakuta kwamba Dr. Slaa ametuambia kuwa Tanzania inaendeshwa na mbumbumbu wasiosoma. Inaendeshwa na vipofu. Hilo ni janga kwa Taifa. Halafu ukiongezea na lile wazo la kuwa CCM ni kama choo kichafu, unaona wazi kuwa Dr. Slaa amemwaga hadharani mambo mazito dhidi ya CCM.

Sasa katika hali hii, nikiangalia wagombea wawili wa urais, yaani Magufuli na Lowassa, naona kuwa tafsiri ya kauli za Dr. Slaa ni kuwa UKAWA wamemtoa Lowassa chooni, lakini Magufuli ameng'ang'ania kubaki chooni. Ningekuwa mpiga kura, kura yangu ningempa huyu Lowassa aliyelopolewa kutoka chooni kuliko huyu Magufuli ambaye amepania kufia humo chooni.

No comments: