Monday, August 31, 2015

Lowassa, CHADEMA na UKAWA

Kuhusu madai kwamba Lowassa ni fisadi, na kuhusu suala la CHADEMA kumkaribisha, na UKAWA kumteua kuwa mgombea wao wa urais, msimamo wangu ni kama ifuatavyo. Na napenda kuweka wazi kuwa mimi si mwanachama wala msemaji wa chama chochote cha siasa. Ni kiumbe huru, ninayetumia akili yangu na kuchambua mambo nipendavyo.
Kuna kitu kiitwacho haki za binadamu, na kuna kitu kiitwacho utawala wa sheria. Kwa mujibu wa tangazo la kimataifa la haki za binadamu, mtu yeyote anayetuhumiwa au kushtakiwa kwa kosa lolote ana haki ya kuhesabiwa kuwa hana kosa hadi mahakama ithibitishe vinginevyo.
Na hata huko mahakamani, inatakiwa uthibitisho wa hatia ya huyu mshtakiwa uwe wazi bila shaka ("reasonable doubt"). Pakiwa na hiyo "reasonable doubt," ni manufaa kwa mshtakiwa, yaani mahakama inapaswa kumwachia huru, arudi zake uraiani.
Haki hii unayo wewe, ninayo mimi, anayo Lowassa. Lowassa hajapelekwa mahakamani na kuthibitishwa ana hatia kwa vigezo nilivyotaja hapa juu.
Kwa msingi huo, CHADEMA hawajakosea kumkaribisha katika chama chao. UKAWA wamefanya jambo sahihi kumweka kama mgombea wao wa urais.
Ni kweli kuwa CHADEMA hao walikuwa wanamtukana sana Lowassa, wakamwita fisadi mkubwa, wakamweka hata kwenye orodha yao, maarufu kama "List of Shame."
Lakini nahisi CHADEMA wametambua kuwa walikosea, kwa maana kwamba hakuna mahakama iliyothibitisha kuwa Lowassa ni fisadi. Ni sahihi kwa CHADEMA kuwa na msimamo walio nao sasa juu ya Lowassa.
Wenye matatizo, wasiofuata haki, wahujumu wa haki za binadamu, ndio wanaendelea kuimba huu wimbo kuwa Lowassa ni fisadi. Wenye matatizo ni hao akina Samuel Sitta na Harrison Mwakyembe, wanaotangaza kuwa wanamtaka Lowassa aje kwenye mdahalo juu ya ufisadi wake. Akina Sitta na Mwakyembe wanafanya usanii na ulaghai. Watuhumiwa hatuwaiti kwenye mdahalo. Tunawapeleka mahakamani.
Nawashauri watu hao wajifunze kutoka kwa CHADEMA, kujirekebisha na kuzingatia utawala wa sheria na haki za binadamu.

6 comments:

NN Mhango said...

Kaka Mbele
Kinyesi ni kinyesi hata kiwe chooni chumbani au kwenye nguo. Huna haja ya kuchagua kinyesi. Heri kutopiga kura kama unachagua kati ya vinyesi. Hata hivyo, kama utasoma vizuri maneno ya Dk Slaa, sijui kama tafsiri yako ni sahihi. Kimsingi alichobainisha ni kwamba hakuna kinyesi bora kama tutakuwa wakweli na wasio na upendeleo wala mapenzi ya kibubusa.

Mbele said...


Ndugu Mhango

Tafsiri, kwa mujibu wa taaluma ya lugha, falsafa, na kadhalika, hasa maeneo ya "semantics," ina tabia ya kuleta mitazamo tofauti. Hakuna tafsiri moja ambayo ndio pekee iliyo sahihi. Katika nadharia ya fasihi ("literary theory") tunategemea tafsiri iwe "valid" sio "true" au "correct." Na hasa tukizingatia kwamba hiyo dhana ya choo ni tamathali ya usemi ("figure of speech") tunajikuta moja kwa moja katika uwanja wa fasihi, ambamo suala la tafsiri, kwa maana ya "interpretation," ni tata zaidi.

Kwa msingi huo, unakaribishwa kutoa tafsiri yako ya hotuba ya Dr. Slaa, ili mradi tuachane na dhana ya "tafsiri sahihi." Hakuna kitu kama hicho.

NN Mhango said...

Ndugu Mbele
Nakualiana nawe. Tafsiri inaweza kuwa "implied", "misled","misconstrued", "sheer bias", "biased" na hata "distorted". Hata hivyo, common sense inasema kuwa kuna uwezekano wa kuwa na tafsiri yenye kukubaliwa na wengi na tafsiri inayoweza kukataliwa na kuwashagaza wengi kama kuboresha kinyesi. Tafsiri inaweza kuwa sahihi na usahahi wake unaweza kuelezwa na mtu ambaye maneno au falsafa yake inatafsiriwa. Hivyo, kama Dk Slaa angekuwa anapita hapa na akaamua kuchambua tafsiri zetu, bila shaka tafsiri 'sahihi' inaweza kupatikana bila mshikeli. Hivyo, si kweli kuwa hakuna tafsiri sahihi. Ndugu zetu waislam wanaweza kutusaidia kwenye hadith na tafsiri za kazi za Mtume Muhammad (SAW) ambapo kuna hadith sahih na dhaifu japo mada ya hapo juu haihusiani na uislam. Naleta dhana ya usahihi katika tafsiri kwa kukopa toka kwao.

Mbele said...


Ndugu Mhango

Suala la kumtegemea msemaji au mwandishi kuwa ndiye mwenye tafsiri sahihi linapingwa sana na watafiti wa mambo haya, ambao wanatutahadharisha kuhusu "intentional fallacy." Ni kwamba ukishaandika au kusema kitu, kikawa hadhirani, huna tena namna ya kutawala au kudhibiti tafsiri zake. Kama ni andiko, kwa mfano, wewe mwandishi unakuwa ni mmoja tu wa wasomaji. Wasomaji wanaweza kukutafsiria uliyoandika kwa namna ambayo hukukusudia, na kwa kweli wanaweza kukufungua macho kuhusu ulichoandika, hadi wewe mwenyewe ukashangaa, "Lo, kumbe!"

Ukishaichapisha kazi yako, wewe mwandishi huna "control" juu ya tafsiri yake, na wala tafsiri yako haina "authority" kuliko tafsiri za wasomaji wengine. Kuna makala nzuri mojawapo inayoelezea suala hili iitwayo "The Death of the Author," iliyoanikwa na Roland Barthes. Naitaja hapa kwa vile huenda kuna wasomaji wa mjadala huu ambao watapenda kuitafuta wajisomee.

Kwa hivyo, hata tukamwita Dr. Slaa atueleze alimaanisha nini, haibadili ukweli kwamba andiko lake au hotuba yake inajieleza yenyewe. Ni jambo jema kumsikia, lakini haina maana kuwa kauli yake ni bora kuliko yetu, au ndio kauli sahihi. Ndivyo ilivyo hata kwa waandishi waliofariki, kama akina Shaaban Robert au Shakespeare. Awe hai au marehemu, awe karibu yetu au mbali asikofikika, mwandishi hana mamlaka juu ya tafsiri ya andiko.

NN Mhango said...

Ndugu Mbele,
Ili kuboresha mjadala wetu, ningewaomba wengine waje hapa wachangie lau tupate faida zaidi. Hata hivyo, nikushukuru kwa mchango wako siku zote.

Mbele said...

Ndugu Mhango

Nami, kama wewe, natamani wengine wangekuwa wanachangia mijadala hii. Masuala ni tata, na hata tukisema tusome vitabu fulani au makala fulani tutatambua kuwa kuna mitazamo tofauti, tofauti za kila aina. Kilichopo ni kama unavyosema, kwamba tunapata "faida zaidi."

Elimu haina mwisho, wala haina mwenyewe. Na hata kama tuna msimamo fulani, kwa kusoma zaidi na kutafakari zaidi tunajikuta tukibadilisha mitazamo. Hii ni ishara akili yenye afya bora.