Saturday, August 8, 2015

Maajabu Katika Siasa Tanzania, 2015

Kuna maajabu mengi katika siasa Tanzania. Mimi si bingwa wa uchambuzi wa mambo hayo, na wala siamini kama kuna bingwa. Ila kila mtu ana uhuru wa kuchambua aonavyo. Oktoba tutaona tuko wapi, na kama uchaguzi utakwenda kiustaarabu, tutawajibika kuyapokea matokeo.

Hebu nirudi kwenye mada yangu ya maajabu ya siasa Tanzania. Edward Lowassa amejitoa CCM na kuibukia CHADEMA (UKAWA). Tayari amezua zogo. Watu wanarusha makombora kwake, kwa CHADEMA, na kwa UKAWA. Wanasema kwa nini CHADEMA impokee mtu ambaye wamekuwa wakimtukana kama fisadi mkubwa.

Ajabu ni kwamba hakuna mahakama yoyote ambayo imemwona Lowassa kuwa fisadi. Amehukumiwa na hisia za watu pamoja na majungu ya magazetini, katika blogu, na vijiweni. Amekosewa haki ya msingi, kwa mujibu wa tangazo la kimataifa la haki za binadamu, haki ya kwamba mtu anayetuhumiwa au kushtakiwa kwa kosa, lazima ahesabiwe kuwa hana kosa hadi mahakama ithibitishe vinginevyo.

Kwa hivi, wote wanaomwita Lowassa fisadi, au waliomwita fisadi (wakiwemo CHADEMA) wajirekebishe. Wamtendee haki Lowassa. Hadi mahakama ithibitishe, Lowassa ana haki ya kuonekana hana kosa, na kuingia kwake CHADEMA hakuna dosari.

Kwa CHADEMA na UKAWA kumkaribisha Lowassa ni sahihi kabisa. Ni jambo la busara CHADEMA wamwombe radhi kwa kumtukana kwa miaka mingi, yaishe. Na yeye ameonyesha roho nzuri kwa kuja kwenye chama chao, bila kinyongo. Ameonyesha moyo unaoendana na mafundisho ya dini yetu ya u-Kristu ya kuwasamehe wanaotutendea mabaya.

Kwa upande wa CCM ni kwamba Lowassa muda wote wamekuwa naye bega kwa bega. Alikuwa mkuu wa idara yao ya mambo ya nje. Hata baada ya kukatwa kwenye uchaguzi wa mgombea urais, hawakumtukana. Lakini ghafla, baada ya yeye kuhamia CHADEMA (UKAWA) wameanza kumtukana, kwamba ni kapi. Vigogo wa CCM wanaohamia upinzani wanatukanwa kwamba ni makapi.

Kwa maana hiyo, hao akina Asha Rose Migiro, Bernard Membe, Mizengo Pinda, January Makamba, Hamisi Kigwangwala, Emmanuel Nchimbi, na wengine, wakae chonjo. Wakae mkao wa kula. Wakitimkia upinzani, hapo hapo watajikuta wanaitwa makapi.

Haya ni kati ya maajabu ya siasa Tanzania

6 comments:

Khalfan Abdallah Salim said...

Uchambuzi mzuri. Unajua Siasa za majitaka zina vituko vingi. Ilianza na CCM, kisha Chadema sasa waasisi wa siasa hizo wamerudi tena. Unajua kumkata mtu katika kamati ya Maadili, maana yake wale wote walikuwa hawana maadili isipokuwa watano tu. Si kweli, lakini ndio picha iliyopo. Leo kuitwa makapi eti kwa kutoka CCM ni afadhali sana kuliko kuvunjiwa heshima ya kukosa maadili kisha ukakubali, radhi kabisa na kubaki CCM. Inataka moyo wa chuma kama si wehu wa kisiasa kubaki CCM na watu wengi namna hiyo wasiokuwa na maadili.

Mbele said...

Mkuu Khalfan Abdallah Salim,

Shukrani sana kwa mchango wako murua. Naona umegonga nyundo barabara kwenye kichwa cha msumari.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kaka Mbele angalia vizuri unachotetea. Kwenye mahakama za kisiasa hakuna cha mahakama kumkuta mtu na hatia. Nadhani hata akina James Rugemalira na Singasinga wa Escrow, Rostam Aziz wa Kagoda na EPA, Andrew Chenge wa Vijisenti na mafisadi wengine wengi hawajahukumiwa na mahakama. Kama tutakuwa wakweli, kuna ukweli mwingine haupaswi kuingojea mahakama bali common sense hasa kwenye uchumaji mali. Hivi kwa mfano kesho ukisikia Ridhwan Kikwete ni bilionea utangoja mahakama imkute na hatia kusema alitumia urais wa baba yake kujitajirisha? Watoto wa Gaddafi hawakuwa wamepatikana na hatia ya kuibia taifa lakini bado walikuwa wezi na mafisadi sawa na watoto wa Saddam Hussein sawa na akina Lowassa watoto wa CCM. Simple.

Mbele said...

Ndugu Mhango

Msimamo wangu ni huo huo nilouelezea. Lazima zizingatiwe haki za binadamu na utawala wa sheria, kwa kiwango cha juu kabisa. Kulegeza msimamo huo kwa namna yoyote, hata kwa hiyo hoja unayosema ya "common sense" ni kukaribisha mmomonyoko na uvunjifu wa haki.

Kuhusu hiyo mifano uliyotoa, ya watoto wa wazito, ni kwamba vyombo husika vipeleke mashtaka mahakamani, pamoja na ushahidi na vielelezo na taarifa zote za mashtaka. Wenye jukumu la kufungua kesi watafanya kazi yote ya kuandaa ushahidi. Katika kesi wataitwa mashahidi. Ni jukumu la wafungua kesi, yaani walalamikaji, kuthibitisha hatia ya mtuhumiwa, yaani mshtakiwa, bila kubakiza wasi wasi.

Kama kuna wasi wasi katika ushahidi, ni faida kwa mtuhumiwa. Ni msingi wa yeye kuachiwa huru. Huu ndio utaratibu pekee wa kuhakikisha haki inatendeka. Kumwadhibu mtu kwa vile tu ni bilionea na mtoto wa mzito fulani si haki. Siafiki kwamba aadhibiwe kwa msingi huo, ingawa nitakuwa na hisia kubwa kwamba huyu ni fisadi.

Anonymous said...

Tehetete, tehetehe, siasa hasa hizi za Tanzania ni mchezo wa kuigiza tu.
Mr Mbele, Hivi unazijua mahakama zetu?.

Mbele said...

Ndugu Anonymous

Nashukuru kwa suali lako. Nakiri kuwa sikuzingatia jambo hilo unalogusia. Hata hivi, hii iwe ni changamoto, kwamba tufanye kazi ya kuleta mapinduzi katika jamii na taasisi zote, ili tuwe na mahakama bora kabisa, shule bora kabisa, hospitali bora kabisa, na kadhalika.

Tusiache mambo yalivyo. Tujiwekee viwango vya juu kabisa katika shughuli zetu, taasisi zetu, huduma zetu, na kdhalika na kujibidisha kuvifikia.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...