
Hiyo jana ilikuwa ni mara ya kwanza kwa bendera ya Tanzania kupepea kwenye tamasha la Afrifest. Baada ya kushiriki matamasha na kujionea wenzetu wanavyotumia fursa kuzitangaza nchi zao, nilijiuliza kwa nini nisitafute bendera ya Tanzania, kama nilivyoeleza katika blogu hii.
Hatimaye, nilifanya uamuzi wa kununua bendera, niwe ninaipeperusha kwenye matamasha ninayoshiriki, maadam fursa zipo. Hapo kushoto naonekana na binti zangu Assumpta na Zawadi kwenye meza yetu, hiyo jana.
Sawa na kuweka vitabu mezani katika tamasha, ambavyo huwavutia watu waje kuulizia habari zake, sawa na kutundika bendera ya kampuni yangu ya Africonexion: Cultural Consultants, ambayo nayo huwavutia watu waje kuulizia maana ya Africonexion, bendera hiyo nayo ni kivutio na kianzio cha mazungumzo kuhusu Tanzania.
Kwa kuwa bendera hiyo ilipepea hapo uwanjani siku nzima, kila mtu katika umati wa waliohudhuria tamasha aliiona. Wengi wa waliohudhuria walipiga picha hapo uwanjani, na haikwepeki bendera kuonekana katika baadhi ya picha.
No comments:
Post a Comment