Monday, August 10, 2015

Bendera ya Tanzania Itapepea Faribault, Minnesota, 22 Agosti

Tarehe 22 Agosti, nitashiriki tamasha la kimataifa mjini Faribault, Minnesota. Nimeshalipia gharama. Nitakuwa na meza ambapo nitaweka vitabu vyangu na machapisho mengine.

Hapo nitaongea na watu siku nzima kuhusu shughuli zangu za ufundishaji, utafiti, uandishi, na utoaji ushauri kuhusu athari za tofauti za tamadauni, ushauri ambao ninautoa kwa wanafunzi na waalimu wa vyuo vya Marekani na watu wengine waendao Afrika, taasisi na jumuia zenye mahusiano na wa-Afrika, na kadhalika.

Nitaweka pia mabango ya filamu ya "Papa's Shadow." Filamu hiyo, ambayo ni ya maelezo ("documentary"), kwa kiasi kikubwa ni mazungumzo baina yangu na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee wa Ernest Hemingway aliyebaki. Tunajadili maisha na maandishi ya Ernest Hemingway, hasa yale yanayohusu Afrika. Filamu hii itaanza kuonyeshwa hivi karibuni katika majumba ya sinema na itakuwa inapatikana katika DVD na kadhalika. Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti ya Ramble Pictures.

Jambo jingine la pekee ni kuwa, kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa tamasha la kimataifa mjini Faribault, bendera ya Tanzania itapepea, sambamba na bendera za mataifa mengine. Siku chache zilizopita, nilipeperusha bendera hii katika tamasha la Afrifest, mjini Brooklyn Park, kama nilivyoripoti katika blogu hii.

Ninapokuwa Tanzania, ninaweza kuiangalia bendera ya Tanzania nikawa ninaguswa kwa namna fulani, lakini hisia hizo huwa za pekee zaidi huku ughaibuni. Ingekuwa natoka Dar es Salaam kwenda kushiriki tamasha Mtwara, Chake Chake au Mbeya nisingeona sababu ya kubeba bendera ya Tanzania, labda kama tamasha ni la kimataifa. Na hata ningebeba, watu hawangekuwa na duku duku nayo au mshangao. Ni kitu walichozoea.

Lakini mambo ni tofauti huku ughaibuni. Sina namna ya kuelezea vizuri ninachomaanisha. Labda kwa kuwa niko mbali, nina hisia za pekee kuhusu kijiji changu cha Lituru, kata yangu ya Litembo, wilaya yangu ya Mbinga, mkoa wangu wa Ruvuma, na nchi yangu ya Tanzania.

Isipokuwa, jambo moja ni wazi, na linaelezeka: watu watakaohudhuria tamasha mjini Faribault wataiona bendera ya Tanzania. Bendera hii itatokea katika picha mbali mbali watakazopiga siku hiyo na kuzihifadhi, kuwapelekea marafiki au kuziweka mitandaoni.

No comments: