Saturday, August 22, 2015

Tamasha la Kimataifa Mjini Faribault Limefana

Nimerejea alasiri hii kutoka mjini Faribault, ambako nilishiriki tamasha la kimataifa. Mambo ya kusimulia ni mengi mno. Nategemea kusimulia kidogo kidogo siku zijazo.

Hata hivi, napenda niseme kuwa siku kadhaa kabla ya tamasha, nilipomwambia mratibu kuwa mwaka huu ninayo bendera ya Tanzania, aliniambia kuwa tayari wamenunua. Nilipatwa na mshangao wenye furaha.

Kuna nchi nyingi duniani, na nchi zilizotarajiwa kuwakilishwa na bendera ni ishirini na kidogo. Sikupata wasaa wa kuulizia walifikiaje uamuzi wa kununua bendera ya Tanzania. Ninahisi ni kwa sababu nilikuwa nimejisajili kama mshiriki wa tamasha, na pia kwa kuwa nina historia ndefu ya kushiriki matamasha mjini Faribault na majukumu mengine mjini Faribault.

Ulipofika wakati wa watu kuandamana na bendera za nchi zao, name nilijumuika nao. Tulienda kwenye jukwaa kuu, na kila mtu alisema maneno machache kuhusu nchi yake. Baadhi waliimba nyimbo za mataifa yao. Nami nilifanya hivyo hivyo.

Nilielezea kifupi Tanzania iko wapi na historia yake. Nilielezea maana ya rangi za bendera ya Tanzania, kasha nikaimba wimbo wa Taifa. Naamini kuwa hii ni mara ya kwanza kwa wimbo wa Taifa wa Tanzania kusikika mbele ya kadamnasi mjini Faribault. Nitakumbuka tukio hili.

Hapa naleta baadhi ya picha nilizopiga. Zinatoa fununu fulani za hali ilivyokuwa. Katika picha mojawapo, inaonekana meza yangu, yenye vitabu na "t-shirt" za manjano, na pembeni kuna bango la filamu ya Papa's Shadow, ambalo nililipeleka kwenye tamasha ili kuwaelezea watu kuhusu filamu hiyo ambayo iko njiani kuonyeshwa kwa walimwengu.

Sehemu kubwa ya filamu hiyo ni maongezi baina yangu na Mzee Patrick Hemingway kuhusu maisha, uandishi, na falsafa ya baba yake, mwandishi Ernest Hemingway. 

Kulikuwa na upepo sana muda wote wa tamasha, na vitu vyetu vilikuwa vinarushwa huko na huko. Hii ndio sababu ya meza yangu kuwa shaghalabaghala kama inavyoonekana.

Tamasha limefana sana. Nimekutana na kuongea na watu wa mataifa mbali mbali. Nimepanua mtazamo na ufahamu wangu kwa kuwasikiliza, na mimi nimewafahamisha mambo kadha wa kadha ambayo walikuwa hawayajui.

Kama nilivyogusia, hapa nimeweka picha mbali mbali, bali nategemea kuandika taarifa na kumbukumbu siku zijazo.

No comments: